Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Takataka Baharini
Chupa iliyotupwa baharini huoza na kutokomea kabisa baada ya miaka elfu moja. Karatasi ya shashi huoza kwa muda wa miezi mitatu, na vijiti vya kiberiti huchukua miezi sita. Vichungi vya sigareti huchafua bahari kwa muda wa mwaka mmoja hadi 5; mifuko ya plastiki, miaka 10 hadi 20; vifaa vya nailoni, miaka 30 hadi 40; mikebe, miaka 500; na polistirini, miaka 1,000. Makadirio hayo ni baadhi tu ya habari iliyotolewa na Legambiente, shirika la mazingira la Italia, ili kuwatia moyo waogeleaji wajali mazingira na viumbe wanapoenda ufuoni. “Je, mapendekezo hayo yamepita kiasi?” lauliza gazeti la Corriere della Sera. Lajibu hivi: “Tani 605 za takataka zilizokusanywa kwenye fuo za Italia kuanzia mwaka wa 1990 hadi leo na wajitoleaji wa kikundi cha Clean Beaches zaonyesha jawabu ni la.”
Watoto na Mambo ya Mizungu
“Watoto wanakabili hatari ya mambo ya Kishetani na ya mizungu yaliyowekwa kwenye Internet,” chasema chama kimoja cha walimu, kwa mujibu wa gazeti la The Independent la London. Uchunguzi uliofanywa Uingereza na Shirika la Walimu na Wahadhiri (ATL) ulifunua kwamba zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 11 na 16 “walipendezwa na mambo ya mizungu na yale ya kishetani,” takriban robo “walipendezwa sana,” na 1 kati ya 6 walidai kwamba “walitishwa” walipochunguza mambo ya mizungu. Peter Smith, katibu mkuu wa ATL, aonya hivi: “Vijana wanaweza kwa urahisi kufungua mamia ya vituo mbalimbali kwenye Internet vinavyohusu mbinu za uchawi, ulogi na utoaji wa damu, bila mtu yeyote mzima kukagua habari wanazosoma. . . . Hilo ladhihirisha mwelekeo wenye kutia hofu sana miongoni mwa vijana. Wazazi na walimu watajitahidi kuelimisha watoto na vijana kuhusu hatari za kujihusisha na mambo ya mizungu kabla hawajatumbukia ndani kabisa.”
Usikawie Kuhifadhi Vyakula Moto Katika Friji
Ni kosa kuacha vyakula moto mezani ili vipoe kabla ya kuvihifadhi katika friji, asema Bessie Berry, meneja wa Idara ya Agriculture Meat and Poultry Hotline ya Marekani. “Hata vyakula vilivyotolewa tu jikoni au vilivyo moto sana” vyapasa kuhifadhiwa katika friji mara moja ikiwa haviliwi. Kama inavyoelezwa kwenye kijarida cha Tufts University Health & Nutrition Letter, “unapohifadhi vyakula vilivyopikwa katika friji upesi iwezekanavyo, ndivyo bakteria zozote zenye kudhuru zilizomo zinavyokoma kuongezeka.” Je, hilo halitaharibu friji au kulemea mota? La, ajibu Bi. Berry. Friji za kisasa zimebuniwa ili kuweza kuhifadhi vyakula moto. Wazo la kwamba friji haziwezi kuhifadhi vyakula moto huenda lilitokana na matumizi ya visanduku vya barafu, ambamo joto lingeweza kuyeyusha barafu hiyo. Hata hivyo, tahadhari mbili zahitaji kuzingatiwa: Iwapo unahifadhi kiasi kikubwa cha chakula—kama vile kuku mzima, sufuria yenye supu, au chakula kilichotiwa katika bakuli kubwa—chapasa kutiwa kwenye vyombo vingine vidogo kwanza, la sivyo havitapoa ndani haraka vya kutosha na kuzuia bakteria kusitawi. Na vyakula moto vyapasa kuwa mbali kidogo na vyakula vingine katika friji ili hewa iweze kusambaa na kupoza vyakula hivyo upesi.
Sauti za Kompyuta Zenye Kugusa Hisia
Katika jitihada ya kufanya sauti za kompyuta ziwe za kirafiki, wanasayansi wamekuwa wakitafuta njia za kufanya sauti hizo ziwe na hisia. Kwa mujibu wa gazeti la Gießener Allgemeine, la Ujerumani, kikundi cha watafiti katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Berlin kilichunguza jinsi ambavyo sauti hubadilika kupatana na hisia mbalimbali. Waigizaji walisoma sentensi za kawaida kwa njia mbalimbali—kwa hasira, huzuni, uchoshi, shangwe, hofu, au kwa kuudhika. Halafu sentensi hizo zilichanganuliwa—silabi kwa silabi—kuhusiana na uzito, kasi, frikwensi, kiasi, na ufasaha. Matokeo yalionyesha kwamba shangwe au hasira iliongeza kasi na kiasi cha sauti. Silabi zilikaziwa, na ufasaha ulikuwa mzuri. Usemi uliosemwa kwa uchoshi, hofu, au huzuni, ulikuwa wa pole na wenye kukokotezwa na uzito ulibadilika. Hofu iliongeza kiasi cha sauti kwa kipimo cha nane hivi. Nyuzi za sauti zilitikisika taratibu na sauti kuwa nzito na yenye kukwaruza wakati wa huzuni. Sifa hizo zilijaribiwa kwa kutumia sauti bandia ili kuona iwapo wasikilizaji wangeweza “kutambua hisia inayofaa.” Wale wanaoshughulikia uunganishaji wa maneno kielektroni na utambuzi wa haraka wa usemi wamependezwa hasa na utafiti huo.
Miaka 500 ya Uharibifu
Brazili imepoteza asilimia 37 ya mifumo yake mitatu mikuu ya ikolojia tangu ukoloni ulipoanza miaka 500 hivi iliyopita. Ndivyo unavyosema uchunguzi mmoja wa shirika la World Wide Fund for Nature (WWF). Kufikia sasa, “asilimia 93 ya msitu wa Atlantiki, asilimia 50 ya eneo la savanna na asilimia 5 ya eneo la Amazoni imeharibiwa,” lasema gazeti la O Estado de S. Paulo. Garo Batmanian, mkurugenzi mkuu wa shirika la WWF nchini Brazili asema hivi: “Wareno walipowasili hapa, walikuta msitu mkubwa na maji mengi ambayo hawakuwahi kuona. Hilo lilizua ngano ya kwamba kila mmea unaopandwa hapa husitawi tu na kwamba hakuna haja ya kutumia tekinolojia ya Ulaya katika mazingira hayo.” Alisema kwamba dhana hiyo ilichochea uharibifu mkubwa wa msitu wa Atlantiki nchini Brazili.
Usafiri Safi wa Wakati Ujao
“Tekinolojia ya fueli ya betri inayonuia kutokeza mabadiliko makubwa katika biashara ya magari ulimwenguni itaanza kutumiwa karibuni,” laripoti gazeti la The Australian. Tekinolojia ya fueli ya betri inafaa hasa mabasi ya jijini kwa sababu haina kelele nyingi wala moshi unaochafua. Mabasi hayo yaweza kusafiri umbali wa kilometa 300, na kasi ya juu ya kilometa 80 kwa saa, na yataweza kubeba abiria 70. Mabasi hayo yatauziwa makampuni ya usafiri kote Ulaya kwa kiasi cha zaidi ya dola milioni moja za Marekani kwa kila basi, na inatarajiwa kwamba yataanza kutumiwa mwishoni mwa mwaka wa 2002. Fueli za betri huenda zikatumiwa sana wakati ujao katika magari, lakini kwa sasa hazijafikia hatua ya kutengenezwa kwa wingi. “Lazima tupunguze gharama, ukubwa na uzito wa mifumo ya fueli za betri ili tuweze kushindana na injini zinazotumia petroli,” asema Profesa Ferdinand Panik.
“Stempu za Ubatili”
“Stempu za ubatili, bidhaa za kisasa kwa kizazi chenye ubinafsi, zilitengenezwa kwa mara ya kwanza huko Kanada,” laripoti gazeti la The New York Times. Sasa watu wanaweza kutengeneza stempu zao binafsi “zikiwa na picha ya mtoto mchanga, mhitimu mpya, wenzi wawili wenye furaha au mbwa mwaminifu.” Wateja hutuma malipo pamoja na fomu iliyoambatanishwa na picha. Kisha wanapokea karatasi yenye fremu 25 zenye vibandiko, vilivyochapwa kwa rangi ya dhahabu na vilivyoandikwa jina “Canada” na gharama ya posta na karatasi ya pili yenye nakala za picha, ambazo zinaweza kutiwa kwenye fremu hizo. Lakini, gharama yake ni zaidi ya maradufu ya gharama ya kawaida ya posta. Kwa kuongezea, vibandiko vya salamu ambavyo “vitawaruhusu wateja wapatanishe barua zao na hali au ujumbe uliomo,” vinauzwa pia, akasema Micheline Montreuil, mkurugenzi wa bidhaa za stempu katika Posta ya Kanada. Isitoshe, Australia, Singapore, Uingereza, na Uswisi zimebuni pia stempu za ubatili. Stempu hizo mbalimbali zaweza kuwakanganya wakusanyaji wa stempu.
Magonjwa na Misiba
Ijapokuwa misiba, kama vile mafuriko na matetemeko ya dunia, hutangazwa sana, magonjwa ya kuambukizwa huangamiza watu wengi zaidi, yasema ripoti moja ya shirika la Msalaba Mwekundu. Likizungumzia habari hiyo, gazeti la The New York Times lasema hivi: “Idadi ya watu waliokufa kutokana na magonjwa ya kuambukizwa kama vile UKIMWI, kifua kikuu na malaria ni mara 160 zaidi ya idadi ya watu waliokufa mwaka uliopita kutokana na matetemeko ya dunia huko Uturuki, vimbunga huko India na mafuriko nchini Venezuela. . . Takriban watu milioni 150 wamekufa kutokana na hayo magonjwa matatu pekee tangu mwaka wa 1945 ikilinganishwa na milioni 23 waliouawa vitani katika kipindi hichohicho.” Kulingana na Peter Walker, mwandishi wa ripoti hiyo, afya mbaya ya umma ndiyo chanzo cha tatizo hilo. “Katika karibu kila nchi, kuna mifumo ya afya ya kiwango cha chini mijini, lakini sehemu za mashambani hazina mfumo wowote wa afya,” akasema. Watu milioni 13 waliokufa mwaka uliopita kutokana na magonjwa ya kuambukizwa hawangekufa endapo dola tano tu za Marekani zingetumiwa kwa minajili ya kutunza afya ya kila mmoja wao. Makala hiyo yamalizia kwa kusema: “Fedha zinazotumiwa katika harakati za kubadili mazoea ya watu huokoa uhai wa wengi kuliko fedha zinazotumiwa kwa ajili ya majengo yenye gharama kama vile hospitali na vifaa vya kisasa zaidi.”