Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Rafiki Mkubwa wa Wanadamu?
Watoto wadogo wanaoachwa peke yao na mbwa wamo hatarini kuumwa, kulingana na ripoti katika gazeti la El Universal la Mexico City. “Karibu sikuzote mashambulio husababishwa na mtoto, na mbwa hujitetea tu,” ripoti hiyo yasema. Katika miaka mitano iliyopita, watoto 426 walioumwa na mbwa wametibiwa katika hospitali moja nchini Mexico. Asilimia 12 ya watoto hao walipata madhara ya kudumu au kuharibiwa sura. Ripoti hiyo yasihi wazazi wafundishe watoto sheria za msingi zinazohusu mbwa wote: Usichukue vichezeo vyao, au vyombo vyao vya kulia, usiingie katika nyumba yao; usimkaribie mbwa anapokula au kulala; usivute mkia wake au kujaribu kumpanda.
Kujiua Japani
Wajapani wengi wasema kwamba, “Yaelekea Wajapani wamepoteza kusudi” na “hawana kusudi maishani.” Tokeo ni kwamba “wengi wamejiua katika miaka kumi iliyopita,” lasema gazeti la The New York Times. “Katika jumuiya ambamo kuogopa kuaibishwa huathiri watu sana, ukosefu wa kazi umefanya wanaume wengi wavunjike moyo, nao huzurura mtaani mchana wote ili kufanya wengine wafikirie kwamba wako kazini.” Wanapokumbwa na wasiwasi na aibu, baadhi yao hufikiria kujiua. “Hawana tumaini,” asema Dakt. Yukio Saito. “Watu hawana miradi ya wakati ujao, na mambo yote yaonekana kuharibika. . . . Kujiua kumekuwa kwingi kupindukia.” Yaonekana kwamba kujiua kwa kujirusha mbele ya garimoshi kwapendwa na wengi. Katika jitihada ya kuzuia watu wasijiue kwa kujirusha mbele ya garimoshi, kampuni moja ya reli imepaka rangi ya kijani kibichi kivukoni cha reli ili kujaribu kubadili hali ya akili ya yule atakaye kujiua, na kuweka vioo pande zote za reli kufanya mwenye kutaka kujirusha mbele ya garimoshi kutua na kubadili fikira. Kampuni hiyo pia imekata matawi ya miti ili watu wasiweze kujirusha kwenye reli bila kuonekana na wengine. Hata hivyo, wataalamu wasema kwamba jitihada hizo hazitafaulu, uchumi usipoimarika.
Ugomvi na Ndoa
Uchunguzi mpya uliofanywa na Andrew Christensen wa Chuo Kikuu cha California jijini Los Angeles waonyesha kwamba “wenzi wa ndoa wasio wachambuzi sana na walio tayari kukubali utu tofauti wa wenzao, wana ndoa zinazofanikiwa,” lasema gazeti la Time. Kwa upande mwingine, kugombana huzidisha ugomvi.
Kupata Usingizi wa Kutosha
“Jumuiya yetu hukosa usingizi kiasi cha kutokeza hatari,” asema mwanasaikolojia Stanley Coren wa Chuo Kikuu cha British Columbia. Kisababishi kimoja cha aksidenti ya nyuklia kwenye Three Mile Island na umwagikaji wa mafuta wa meli ya Exxon Valdez kilikuwa ukosefu wa usingizi. Kila mwaka kusinzia husababisha aksidenti 100,000 za magari huko Amerika Kaskazini, laripoti gazeti la Maclean’s la Kanada. Mtaalamu wa usingizi wa Chuo Kikuu cha Stanford, Dakt. William Dement aonya hivi: “Watu huwa hawajui kiasi cha usingizi wanachohitaji.” Ili upate usingizi wa kutosha, watafiti wapendekeza: Kula chakula cha jioni muda wa saa tatu kabla ya kulala. Kwenda kulala saa ileile na kuamka saa ileile kila siku. Usiweke televisheni au kompyuta katika chumba cha kulala. Epuka kafeini, vileo, na tumbaku. Vaa soksi kitandani ili nyayo zako zisiwe baridi. Oga maji ya moto kabla ya kulala. Fanya mazoezi kila siku—lakini si kabla tu ya kwenda kulala. Mwishowe, gazeti la Maclean’s lasema: “Ukikosa kupata usingizi, inuka na ufanye jambo fulani. Rudi kitandani tu unaposikia umechoka, kisha amka saa yako ya kawaida.”
Kudumisha Usafi Jikoni
“Dawa [ya kawaida] ya kung’arisha nguo (klorini) ni kinga bora” dhidi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa vinavyojificha katika jikoni lenye shughuli nyingi, lasema gazeti la habari la Vancouver Sun la Kanada. Ripoti hiyo yapendekeza yafuatayo: Kila siku weka mililita 10 za klorini katika lita nne ya maji yasiyo ya moto sana. Maji ya moto mno huvukisha klorini. Panguza sehemu za juu za meza na kabati za jikoni ukitumia maji hayo na kitambaa safi. Acha pakauke. Unaporuhusu pakauke penyewe vijidudu vingi zaidi vitakufa. Osha vyombo
kwa maji ya moto yenye sabuni, halafu uvitumbukize katika maji yenye klorini kwa muda wa dakika chache. Dawa hiyo haitabaki kwenye vyombo baada ya kukauka. Kila siku, fua sponji, vitambaa, na brashi katika maji yenye klorini. Na ili kupunguza uwezekano wa kuchafua chakula kwa vijidudu vilivyopo mikononi, nawa mikono vizuri, hasa kucha.Lugha Zilizo Hatarini Kutoweka
Nchini Mexico kuna lugha nyingi za kienyeji kuliko katika nchi nyingine za Amerika. Zaidi ya hayo, ulimwenguni ni nchi za India na China tu ambazo zina idadi kubwa ya lugha za kienyeji ambazo bado hutumiwa kuliko nchi ya Mexico. Lugha nyingi kati ya hizo zinaendelea kutoweka, laripoti gazeti la habari la Kiingereza la Mexico, The News. Rafael Tovar de Teresa, mkurugenzi wa Baraza la Utamaduni na Sanaa, aeleza kwamba, kati ya lugha za kienyeji 100 zilizokuwapo mwishoni mwa karne ya 19 ni 62 tu zinazosalia. Na kila moja ya lugha 16 kati ya hizo zatumiwa na watu chini ya 1,000. Hangaiko moja ni kwamba lugha zinapotoweka, majina ya kienyeji ya mimea hupotea pamoja na ujuzi wa jinsi mimea hiyo ilivyotumiwa kutibu magonjwa.
Usiogelee Ukiwa Umelewa
Katika mwaka mmoja wa karibuni, watu wengi waliokufa maji Ujerumani walikuwa “wamekunywa kileo kupindukia,” asema Dakt. Klaus Wilkens, msimamizi wa Shirika la Ujerumani la Kuokoa Uhai. Kulingana na jarida la habari ya afya la Apotheken Umschau, watu 477 walikufa maji katika mito, vijito na maziwa ya Ujerumani katika mwaka wa 1998. Kuogelea baada ya kunywa kileo ni hatari kwa kuwa kileo chaweza kuzuia misuli ya mwili isifanye kazi kwa upatano na kufanya ujikadirie uwezo usio nao. Kwa hiyo, waokoaji waonya: ‘Usiogelee ukiwa umelewa!’
Walipwa Waue Wadudu
Idara ya msitu ya Jimbo la Uttar Pradesh nchini India imeanza kampeni ya kuzuia mdudu mwenye urefu wa sentimeta mbili na nusu aitwaye hoplo asiharibu kabisa msitu wenye miti 650,000 ya sal, laripoti gazeti la The Times of India. Kwa kuwa wadudu hao wameongezeka hivi karibuni, mti huo umo hatarini kutoweka. Wadudu huingia katika maganda na mashina, na kusababisha kunyauka na kufa kwa miti. Idara ya msitu yatumia mbinu ya “mti-mtego” kuwakamata wadudu hao. Vipande vya maganda a miti ya sal hutawanywa katika eneo walipo wadudu. Umajimaji utokao katika vipande hivyo huvutia na kulewesha wadudu hao, na hilo hufanya iwe rahisi kuwakamata. Wavulana wa hapo huajiriwa kufanya kazi hiyo, nao hulipwa paisa 75 (senti mbili za Marekani) kwa kila mdudu mmoja.
Huzuni Kutokana na Kustaafu
Kustaafu mapema kwaweza kuwa na manufaa fulani, lakini pia kwaweza kuhuzunisha. Gazeti la Brazili la Diário de Pernambuco laripoti kwamba waliokuwa wameajiriwa na serikali hapo zamani walipatwa na matatizo kama vile ‘kutoridhika, kukasirika haraka, kutohisi salama, kutojijua, kukata tamaa, na kuona kana kwamba maisha yao yameharibika. Kulingana na mtaalamu wa uzee Guido Schachnik, “ni jambo la kawaida kwa wanaume waliostaafu mapema kuanza kunywa na wanawake kuzoea dawa.” Wanaopanga kustaafu wapaswa kuepuka “kuwa na deni, kuwa tayari kutumia stadi zao katika shughuli tofauti, na kuomba ushauri ili wasipate deni ambayo hawataweza kulipa,” asema mwanasaikolojia Graça Santos.
UKIMWI na Ukulima Nchini Zambia
Mazao ya ukulima yanapungua nchini Zambia kwa sababu ya ongezeko la haraka la UKIMWI. Gazeti la habari la Zambia Daily Mail lasema kwamba mojawapo ya mambo muhimu zaidi ya ukulima ni kazi inayofanywa na wakulima na vibarua wao. Hata hivyo, wengi wa wafanyakazi hao wanakufa UKIMWI. “Wakulima wafapo, kazi shambani hupunguka na ili mazao pia hupunguka. Jambo hilo lamaanisha kwamba huenda familia mojamoja wasiwe na chakula cha kutosha, na hilo huzidisha umaskini,” laripoti gazeti la Daily Mail. Kulingana na Daniel Mbepa, msimamizi wa wilaya ya Mansa ya Zambia, suluhisho ni wakulima kuwa na uhusiano wa ngono na wenzi wao pekee. Alisema hivi: “Kwa kuendeleza maadili mazuri, tatizo la UKIMWI laweza kudhibitiwa.”