Je, Ndoto Ni Ujumbe Kutoka kwa Mungu?
Maoni ya Biblia
Je, Ndoto Ni Ujumbe Kutoka kwa Mungu?
YASEMEKANA kwamba mvumbuzi Elias Howe alipata wazo la kuunda cherehani katika ndoto. Mtungaji wa muziki aitwaye Mozart alisema kwamba sauti za nyimbo zake nyingi zilimjia katika ndoto. Hali kadhalika, mwanakemia Friedrich August Kekule von Stradonitz alidai kwamba aligundua umbo la molekuli ya benzene alipoota ndoto. Matukio kama hayo ni ya kawaida. Muda wote watu wa utamaduni mbalimbali wameamini kwamba ndoto hutokana na chanzo kisicho cha kibinadamu. Watu wa utamaduni fulani huamini kwamba kile kinachootwa ni matukio halisi ya maisha.
Katika Biblia kuna masimulizi kadhaa yaonyeshayo ndoto kuwa chanzo muhimu cha habari—mawasiliano kutoka kwa Mungu. (Waamuzi 7:13, 14; 1 Wafalme 3:5) Kwa mfano, Mungu aliwasiliana na Abrahamu, Yakobo, na Yusufu kwa njia ya ndoto. (Mwanzo 28:10-19; 31:10-13; 37:5-11) Mfalme Nebukadneza wa Babiloni alipokea ndoto za kiunabii kutoka kwa Mungu. (Danieli 2:1, 28-45) Kwa hiyo, je, kuna sababu nzuri kuamini kwamba hata leo baadhi ya ndoto ni ujumbe kutoka kwa Mungu?
Ndoto Kutoka kwa Mungu
Katika Biblia, ndoto zilizotoka kwa Mungu sikuzote zilikuwa na kusudi hususa. Ni kweli kwamba nyakati nyingine mwenye kupokea ndoto hakuelewa mara moja maana ya ndoto hiyo. Hata hivyo, katika visa vingi ‘Afunuaye siri’ mwenyewe alitoa ufafanuzi ili kusiwe na mashaka yoyote juu ya maana ya ndoto. (Danieli 2:28, 29; Amosi 3:7) Ndoto zilizotoka kwa Mungu hazikuwa zenye maana isiyo dhahiri kama vile ndoto za kawaida.
Mara kwa mara, Mungu alitumia ndoto kuwalinda watu waliohusika kwa njia kubwa katika utimizo wa kusudi lake. Si watumishi wa Mungu tu waliopokea ndoto hizo. Kwa mfano, wanajimu waliotembelea mtoto Yesu hawakurudi kwa Herode, aliyetaka kumwua Yesu kama alivyokuwa amewaomba. Kwa nini? Walipokea onyo katika ndoto. (Mathayo ) Jambo hilo lilimpa Yosefu, baba wa kambo wa Yesu, fursa ya kukimbia Misri pamoja na jamaa yake, kwa kufuata mwelekezo ambao hata yeye alikuwa amepokea katika ndoto. Hilo liliokoa maisha ya mtoto Yesu.— 2:7-12Mathayo 2:13-15.
Karne nyingi mapema, farao mmoja wa Misri aliota ndoto kuhusu masuke saba mema yaliyolinganishwa na masuke saba dhaifu, na ng’ombe saba wanono waliolinganishwa na ng’ombe saba waliokonda. Mungu alimsaidia Yusufu kufasiri ndoto hizo kwa usahihi: Miaka saba ya shibe nchini Misri ingefuatwa na miaka saba ya njaa. Kujua mapema jambo hilo kuliwapa Wamisri fursa ya kutayarisha chakula na kukiweka akiba. Hiyo ilikuwa njia ya Mungu ya kuhifadhi wazao wa Abrahamu na kuwapeleka Misri.—Mwanzo, sura ya 41; 45:5-8.
Mfalme Nebukadneza wa Babiloni pia aliota ndoto. Ndoto hiyo ilitabiri kutokea na kuanguka kwa tawala za ulimwengu za wakati ujao, ambazo zingeathiri moja kwa moja watu wa Mungu. (Danieli 2:31-43) Baadaye aliota ndoto nyingine iliyotabiri kichaa na kupona kwake. Ndoto hiyo ya kiunabii ilikuwa na utimizo mkubwa zaidi, ilionyesha kimbele kusimamishwa kwa Ufalme wa Kimesiya, ambao ungetumiwa na Mungu kutimiza mapenzi yake.—Danieli 4:10-37.
Vipi Siku Hizi?
Naam, Mungu aliwasiliana na baadhi ya watu kwa njia ya ndoto. Lakini Biblia huonyesha kwamba matukio hayo yalikuwa machache sana. Mungu hakuwasiliana kupitia ndoto kwa ukawaida. Watumishi wengi waaminifu wa Mungu hawakupokea kamwe ujumbe kutoka kwa Mungu kwa njia ya ndoto. Mawasiliano kati ya Mungu na wanadamu kwa njia ya ndoto yanaweza kulinganishwa na kutenganishwa kwa maji ya Bahari Nyekundu. Ingawa alifanya hivyo mara moja, tunajua kwamba hiyo si njia yake ya kawaida ya kushughulika na watu wake.—Kutoka 14:21.
Mtume Paulo alitambua kwamba katika siku zake Mungu alitumia roho yake kuwapa watumishi wake vipawa vingi vya ajabu. Paulo alisema hivi: “Mmoja hupewa usemi wa hekima kupitia ile roho, mwingine usemi wa ujuzi kulingana na roho ileile, mwingine imani kwa roho ileile, mwingine zawadi za maponyo kwa roho moja hiyo, mwingine bado utendaji wa kazi zenye nguvu, mwingine kutoa unabii, mwingine ufahamu wa matamko yaliyopuliziwa, mwingine lugha tofauti, na mwingine fasiri ya lugha.” (1 Wakorintho 12:8-10) Ijapokuwa ndoto kutoka kwa Mungu hazitajwi mahususi, ni wazi kwamba ndoto kutoka kwa Mungu zilikuwa mojawapo ya zawadi za roho ambazo zilitabiriwa katika Yoeli 2:28 ambazo Wakristo kadhaa walipokea.—Matendo 16:9, 10.
Hata hivyo, mtume huyo alisema kuhusu vipawa hivyo vya kipekee: “Kama kuna zawadi za kutoa unabii, zitaondolewa mbali; kama kuna lugha, zitaacha kuwako; kama kuna ujuzi, utaondolewa mbali.” (1 Wakorintho 13:8) Ni dhahiri kwamba zawadi ambazo “zingeondolewa mbali” zilitia ndani njia mbalimbali za mawasiliano kutoka kwa Mungu. Baada ya kifo cha mitume, Mungu hakuwapa tena watumishi wake vipawa hivyo vya kipekee.
Leo, wataalamu bado wanajaribu kuelewa mambo yote yanayohusiana na kuota ndoto na ikiwa hunufaisha kwa njia yoyote. Biblia haina maelezo yoyote kuhusu manufaa ya kuota ndoto. Hata hivyo, kuna onyo katika Biblia kwa wale wanaosisitiza kwamba ndoto zao ni mawasiliano kutoka kwa Mungu. Andiko la Zekaria 10:2 lasema hivi: “Waaguzi, . . . wameleta habari za ndoto za uongo.” Mungu huonya pia dhidi ya kubashiri. (Kumbukumbu la Torati 18:10-12) Kwa kufikiria maonyo hayo, siku hizi Wakristo hawatarajii kupokea mwongozo wa kimungu katika ndoto zao. Badala yake, wanaona ndoto kuwa hali inayotukia usingizini tu.