Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Majiji Mbona Yamo Taabani?

Majiji Mbona Yamo Taabani?

Majiji Mbona Yamo Taabani?

“Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni,. . . ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.”—Mwanzo 11:4.

MANENO hayo, yaliyonenwa zaidi ya miaka 4,000 iliyopita, yalitangaza ujenzi wa jiji kuu la Babeli.

Babeli, ambalo baadaye liliitwa Babiloni, lilikuwa kwenye nyanda zenye rutuba za Shinari huko Mesopotamia. Hata hivyo, tofauti na maoni ya wengi, halikuwa jiji la kwanza kutajwa katika Biblia. Kwa kweli, majiji yalianza kujengwa kabla ya Furiko la siku ya Noa. Kaini yule mwuaji alijenga mji wa kwanza kurekodiwa. (Mwanzo 4:17) Mji huo, ulioitwa Henoko, huenda ulikuwa makazi yenye ngome au kijiji tu. Kwa upande mwingine, Babeli lilikuwa jiji kubwa—kituo maarufu cha ibada bandia chenye mnara mkuu wa kidini. Hata hivyo, Babeli na mnara wake wenye sifa mbaya haukupatana kabisa na mapenzi ya Mungu. (Mwanzo 9:7) Kwa hiyo kulingana na Biblia, Mungu aliingilia kati na kuvuruga lugha ya wajenzi, na hivyo kukomesha mradi wao wa kidini wa kujitafutia umaarufu. Mungu ‘aliwatawanya waende usoni pa nchi yote,’ yasema Mwanzo 11:5-9.

Si ajabu kwamba hatua hiyo ilifanya majiji yasambae. Majiji yaliandaa ulinzi kutokana na mashambulizi ya maadui. Majiji yalikuwa vituo vya kuhifadhi na kuuzia mazao ya wakulima. Kuibuka kwa masoko pia kuliwawezesha wakazi wajiruzuku kwa njia nyingine mbali na kilimo. Kichapo The Rise of Cities chasema hivi: “Badala ya kuishi maisha magumu, wakazi wa majijini wangeweza kufanya kazi mbalimbali maalum: usukaji wa vikapu, ufinyanzi, usokotaji, ufumaji, utengenezaji wa bidhaa za ngozi, useremala na uashi—kazi yoyote ya kibiashara iliyofua dafu.”

Majiji yalikuwa vituo bora vya kuuzia bidhaa hizo. Fikiria simulizi la Biblia la njaa kali iliyokumba Misri. Waziri mkuu, Yosefu, aliona kuwa inafaa kuwahamisha watu hadi mijini. Kwa nini? Kwa wazi ni kwa sababu kufanya hivyo kulirahisisha ugawanyaji wa chakula kilichosalia.—Mwanzo 47:21.

Majiji pia yaliboresha mawasiliano na ushirikiano wa watu wakati ambapo hali ya usafiri ilikuwa duni na ya polepole. Jambo hilo lilileta mabadiliko makubwa ya kijamii na kitamaduni. Majiji yakawa vituo vya uvumbuzi ambavyo vilisitawisha ukuzi wa kitekinolojia. Kuenea upesi kwa mawazo mapya kulitokeza uvumbuzi wa dhana za kisayansi, kidini, na kifalsafa.

Matumaini Yasiyotimizwa

Majiji ya kisasa bado yana manufaa mengi kama hayo. Si ajabu kwamba yangali yanavutia mamilioni ya watu—hasa katika nchi ambamo maisha ya mashambani yamekuwa magumu sana. Lakini, matumaini ya watu wengi wanaohamia majijini ili kuwa na maisha bora hayatimizwi. Kitabu Vital Signs 1998 chasema hivi: “Kulingana na uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Baraza la Idadi ya Watu, kuna umaskini zaidi katika majiji mengi ya nchi zinazositawi leo kuliko sehemu za mashambani.” Kwa nini?

Henry G. Cisneros aandika hivi katika kichapo The Human Face of the Urban Environment: “Watu maskini wanapojazana kwenye maeneo fulani hususa, matatizo yao huongezeka sana. . . . Kuongezeka kwa watu maskini, hasa wa vikundi duni kumesababisha uhaba mkubwa wa kazi ya kuajiriwa, kuongezeka kwa watu wanaotegemea msaada wa umma kwa muda mrefu, kuzorota sana kwa afya ya umma, na jambo lenye kushtua zaidi, ongezeko la uhalifu.” Vivyo hivyo, kitabu Mega-city Growth and the Future chasema hivi: “Kufurika kwa watu mara nyingi husababisha uhaba mkubwa wa kazi za kuajiriwa na kufanya kazi zisizotosheleza kwa sababu hakuna nafasi za kazi kwa wote wanaotafuta kazi.”

Idadi inayoongezeka ya watoto wa mitaani ni jambo la kuhuzunisha linaloonyesha umaskini mkubwa unaokumba majiji ya nchi zinazositawi. Kulingana na makadirio fulani, kuna takriban watoto wa mitaani milioni 30 ulimwenguni pote! Kitabu Mega-city Growth and the Future chasema: “Umaskini na matatizo mengine yamedhoofisha vifungo vya familia hivi kwamba watoto wa mitaani wamelazimika kujitafutia riziki.” Watoto hao huishi maisha magumu sana kwa kuchokora takataka, kuombaomba, au kufanya kazi duni kwenye masoko ya umma.

Mambo Mengine Yenye Kuogofya

Umaskini waweza kusababisha uhalifu. Katika jiji moja la Amerika Kusini lenye majengo ya kisasa yenye kuvutia sana, uhalifu umeenea sana kiasi cha kwamba majengo mengi yana madirisha na nyua za vyuma. Wakazi wote, matajiri kwa maskini wanajenga nyua za vyuma ili kujilinda na kulinda mali yao. Kwa kweli, wanaishi vizimbani. Wengine hata hujenga nyua za vyuma kabla ya ujenzi wa nyumba yao kumalizika.

Idadi kubwa ya watu hufanya iwe vigumu kwa jiji kuandaa huduma muhimu kama vile maji na usafi. Yakadiriwa kwamba jiji moja la Asia linahitaji vyoo vya umma vipatavyo 500,000. Lakini uchunguzi mmoja wa hivi majuzi ulionyesha kwamba ni vyoo 200 tu vinavyotumika!

Jambo jingine la kufikiria ni uharibifu wa mazingira unaosababishwa na idadi kubwa zaidi ya watu. Mashamba yaliyo karibu hutokomea wakati majiji yanapopanuka. Aliyekuwa msimamizi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa Federico Mayor asema: “Majiji hutumia kiasi kikubwa mno cha nishati, maji, vyakula na bidhaa. . . . Mazingira ya asili huchakaa kwa sababu hayawezi kuandaa wala kutimiza mahitaji.”

Matatizo ya Majiji Makubwa Katika Nchi za Magharibi

Huenda hali si mbaya sana katika nchi za Magharibi, hata hivyo bado majiji yamo taabani. Kwa mfano, kitabu The Crisis of America’s Cities chasema: “Majiji ya Amerika leo yanakumbwa na jeuri nyingi isivyo kawaida. . . . Jeuri imeenea sana katika majiji ya Amerika kiasi cha kwamba majarida ya kitiba yameanza kuandika makala nyingi kuhusu jeuri ikiwa suala muhimu kwa afya ya umma leo.” Bila shaka, jeuri imeenea sana katika majiji makubwa kotekote ulimwenguni.

Kuzorota kwa maisha katika majiji ni mojawapo ya sababu zinazofanya waajiri waepuke majiji mengi. Kitabu The Human Face of the Urban Environment chasema hivi: “Biashara zimehamia vitongojini au nchi za ng’ambo, viwanda vimefungwa, na kinachosalia ni ‘ardhi iliyoharibiwa’—majengo yaliyohamwa yaliyo kwenye ardhi iliyochafuliwa, huku kemikali zenye sumu zikiwa zimezikwa ardhini, na kufanya ardhi hiyo isiweze kabisa kusitawishwa.” Tokeo ni kwamba watu maskini hujazana kwenye maeneo ya majiji ambamo “matatizo ya mazingira hupuuzwa—mifumo ya maji machafu huziba; maji hayasafishwi vya kutosha; wanyama-waharibifu hutapakaa kwenye marundo ya takataka na kuingia nyumbani; watoto wadogo hula rangi zenye madini ya risasi zinazobabuka kutoka kwa kuta za majengo ya makazi yanayochakaa . . . na yaonekana hakuna mtu anayejali.” Uhalifu, jeuri, na kukata tamaa huenea katika mazingira hayo.

Isitoshe, majiji ya nchi za Magharibi yanashindwa kuandaa huduma muhimu. Huko nyuma katika mwaka wa 1981, waandishi Pat Choate na Susan Walter waliandika kitabu chenye kichwa kinachoshtua America in Ruins—The Decaying Infrastructure. Waliandika hivi: “Vifaa vya umma vya Amerika vinaharibika haraka zaidi lakini havirekebishwi haraka.” Waandishi hao walieleza wasiwasi mkubwa uliopo kwa sababu ya idadi ya madaraja yanayoharibika, barabara zinazoharibika, na mifumo ya maji machafu inayoharibika katika majiji makubwa.

Miaka ishirini baadaye, majiji kama vile New York City bado yana miundo ya msingi iliyoharibika. Makala moja katika New York Magazine ilizungumzia mradi wa Third Water Tunnel. Mradi huo umekuwa ukijengwa kwa miaka 30 sasa na unaitwa “mradi pekee wa muundo wa msingi ulio mkubwa zaidi katika Kizio cha Magharibi.” Utagharimu takriban dola bilioni tano za Marekani. Utakapokamilika, mfereji huo utasambaza lita zipatazo bilioni nne za maji safi kila siku katika New York City. “Lakini lengo la kazi hiyo yote ya kuchimba,” asema mwandishi, “ni kwamba mfereji huo uchukue mahali pa mabomba yaliyopo, ili yaweze kurekebishwa kwa mara ya kwanza tangu yalipowekwa mwanzoni mwa karne ya 20.” Kwa mujibu wa makala moja katika gazeti la The New York Times, kurekebisha miundo mingineyo ya msingi ya jiji hilo inayosambaratika—reli za chini ya ardhi, mabomba makuu ya maji, barabara, na madaraja kutagharimu takriban dola bilioni 90 za Marekani.

New York si jiji pekee linaloshindwa kuandaa huduma muhimu. Kwa kweli, majiji kadhaa makubwa yamekumbwa na matatizo mbalimbali. Mnamo Februari 1998, jiji la Auckland, New Zealand, lilikumbwa na tatizo kubwa sana umeme ulipokatika kwa zaidi ya majuma mawili. Wakazi wa Melbourne, Australia, walikosa maji moto kwa muda wa siku 13 wakati usambazaji wa gesi uliposimamishwa kufuatia aksidenti iliyotukia kwenye kiwanda cha gesi.

Kisha kuna tatizo linalokumba karibu majiji yote—msongamano wa magari. Msanifu-ujenzi Moshe Safdie asema hivi: “Kuna tofauti kubwa sana—pengo kubwa—kati ya ukubwa wa majiji na mifumo ya usafiri inayoyahudumia. . . . Majiji ya kale yamelazimika kubadili maeneo yake ya kibiashara ili kukabiliana na misongamano mikubwa ya magari ambayo haikutarajiwa kuwapo yalipojengwa.” Kulingana na gazeti la The New York Times, misongamano ya magari katika majiji kama vile Cairo, Bangkok, na São Paulo ni “jambo la kawaida.”

Licha ya matatizo hayo, yaonekana watu bado wanafurika majijini. Ni kama makala moja katika kichapo cha The UNESCO Courier ilivyosema, “haidhuru itakavyokuwa, wengi huvutiwa sana kuhamia jijini wakitumaini kupata maisha bora na uhuru, fursa ya kujiendeleza.” Lakini kuna tumaini gani kwa majiji makubwa ya ulimwengu? Je, kuna masuluhisho yoyote halisi kwa matatizo yanayokabili majiji hayo?

[Blabu katika ukurasa wa 5]

“Kufurika kwa watu mara nyingi husababisha uhaba mkubwa wa kazi na kufanya kazi zisizotosheleza”

[Picha katika ukurasa wa 7]

Majiji mengi hukumbwa na misongamano ya magari

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mamilioni ya watoto wa mitaani hujitafutia riziki

[Picha katika ukurasa wa 7]

Matumaini ya wakazi wengi wa majiji ya kuwa na maisha bora hayatimizwi