Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Dini Ilivyoshambuliwa na Sovieti

Jinsi Dini Ilivyoshambuliwa na Sovieti

Jinsi Dini Ilivyoshambuliwa na Sovieti

MUUNGANO wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti ulianzishwa mwaka wa 1922, na Urusi ndiyo iliyokuwa jamhuri kubwa na maarufu zaidi kati ya jamhuri nne za kwanza za muungano huo. Baadaye muungano huo ulipanuka na kuwa na jamhuri 15 na kumiliki takriban sehemu moja kwa sita ya dunia yote. Lakini Muungano wa Sovieti ulivunjika ghafula mwaka wa 1991. * Muungano huo ulikuwa Serikali ya kwanza kujaribu kuzuia watu kumwamini Mungu.

Vladimir Lenin, kiongozi wa kwanza wa Muungano wa Sovieti, alikuwa mfuasi wa Karl Marx. Karl Marx aliona kwamba Ukristo ulitumiwa kuwakandamiza watu. Marx alisema dini huwapumbaza watu, naye Lenin akasema hivi baadaye: “Wazo lolote la kidini, wazo lolote juu ya mungu awaye yote, . . . ni uovu usiowazika.”

Kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Urusi, Tikhon, alipokufa katika mwaka wa 1925, kanisa halikuruhusiwa kuteua kiongozi mwingine. Dini ilishambuliwa na majengo mengi ya kanisa yakaharibiwa ama kutumiwa kwa makusudi mengine. Makasisi walipelekwa kwenye kambi za kazi ngumu, ambamo wengi walifia. Kichapo Encyclopædia Britannica chaeleza kwamba “kanisa lilinyanyaswa kinyama na maelfu wakauawa wakati wa utawala wa Joseph Stalin mwishoni mwa miaka ya 1920 na 1930. Kufikia mwaka wa 1939 ni maaskofu watatu au wanne tu wa Kanisa Othodoksi ambao walisalia na makanisa 100 ndiyo yaliyokuwa yakitumiwa kwa ibada.”

Lakini, badiliko kubwa sana lilitokea ghafula.

Vita ya Ulimwengu ya Pili na Dini

Vita ya Ulimwengu ya Pili ilizuka mwaka wa 1939, wakati Ujerumani ya Nazi, iliyokuwa rafiki ya Muungano wa Sovieti wakati huo, ilipovamia Poland. Baada ya mwaka mmoja, Muungano wa Sovieti ulikuwa umenyakua jamhuri 4 za mwisho kati ya jamhuri zake 15—Latvia, Lithuania, Estonia, na Moldavia. Hata hivyo, Ujerumani ilishambulia vikali Muungano wa Sovieti mnamo Juni 1941, jambo hilo lilimshtua sana Stalin. Mwishoni mwa mwaka huo, wanajeshi Wajerumani walikuwa wamefikia vitongoji vya Moscow, na Muungano wa Sovieti ulielekea kushindwa.

Stalin alijitahidi kwa hofu kutayarisha taifa lake kwa pambano ambalo Warusi waliliita Vita Kuu ya Kizalendo. Mamilioni ya watu bado walikuwa wafuasi wa dini. Kwa hiyo Stalin aling’amua kwamba alihitaji kulirudishia kanisa mapendeleo fulani ili wafuasi wamwunge mkono katika vita hiyo. Kubadilika kabisa kwa maoni ya Stalin kuelekea dini kulikuwa na matokeo gani?

Kwa kushirikiana na kanisa, Warusi waliunga mkono vita, na Sovieti ikashinda kabisa Wajerumani kufikia mwaka wa 1945. Sovieti ilipoacha kushambulia kanisa kwa muda, idadi ya makanisa ya Othodoksi iliongezeka hadi 25,000, na idadi ya makasisi ikafikia 33,000.

Mashambulizi Yaendelea

Hata hivyo, viongozi wa Sovieti bado walikuwa na lengo la kuwazuia watu kumwamini Mungu. Kichapo The Encyclopædia Britannica chaeleza hivi: “Waziri Mkuu Nikita Khrushchev alianzisha mbinu mpya ya kukomesha dini mwaka wa 1959-1964, akiruhusu tu makanisa yasiyozidi 10,000. Pimen aliteuliwa kuwa Kiongozi wa Kanisa mwaka wa 1971 baada ya kifo cha Alexis, lakini kanisa lilielekea kutokomea lijapokuwa na mamilioni ya wafuasi.” *

Baadaye tutazungumzia jinsi Kanisa Othodoksi la Urusi lilivyookoka shambulizi hilo jipya la Sovieti. Lakini dini nyingine katika Muungano wa Sovieti zilikabilianaje na hali hiyo? Kati ya dini hizo, ni ipi iliyokuwa shabaha hasa ya mashambulizi, na kwa nini? Maswali hayo yatazungumziwa katika makala ifuatayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Nchi 15 zifuatazo zilizo huru zilikuwa jamhuri za Sovieti hapo awali: Armenia, Azerbaijan, Belarus, Estonia, Georgia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Latvia, Lithuania, Moldova, Tajikistan, Turkmenistan, Ukrainia, Urusi, na Uzbekistan.

^ fu. 11 Nyakati nyingine majina ya Alexis wa Kwanza, kiongozi wa Kanisa Othodoksi la Urusi kutoka mwaka wa 1945 hadi 1970, na Alexis wa Pili, ambaye ameongoza tangu 1990 hadi leo, hutamkwa Alexy, Aleksi, Aleksei, na Alexei.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Lenin alisema ‘wazo lolote juu ya Mungu ni uovu usiowazika’

[Hisani]

Musée d’Histoire Contemporaine—BDIC