Kutembelea Majiji Yenye Kuvutia ya Milan na Turin
Kutembelea Majiji Yenye Kuvutia ya Milan na Turin
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA
YAMKINI ungefurahia sana kutembelea Italia. Chakula, divai, mandhari, historia, utamaduni, muziki, lugha—zote zafanya nchi hii isiweze kusahaulika. Huenda ikawa mwaka huu ndio wakati unaofaa kutembelea majiji hayo, hasa kwa wale walioalikwa kuhudhuria mojawapo ya mikusanyiko ya Mashahidi wa Yehova ambayo itafanywa huko. Acheni tutalii kifupi kwenye majiji mawili ya pekee ya Italia na maeneo yake.
Je, Milan Ndilo Jiji Kuu la Italia?
Kwa habari ya biashara na shughuli za viwanda Milan huhesabiwa mara nyingi kuwa jiji kuu la Italia. Milan halijulikani sana kwa vitu vya kale au sanaa kama majiji mengine ya Italia. Mambo ya kisasa yatokeza zaidi jijini Milan kuliko mambo ya kale. Hata hivyo, kuna majengo na sanaa za kale kadha wa kadha zinazoonyesha kwamba Milan ni jiji la kale.
Mnamo mwaka wa 600 K.W.K., watu wa Gaul walianza kuishi katika eneo hilo, nao walikuwa Waselti waliotoka sehemu ambayo leo ni Ufaransa. Waroma waliteka jiji hilo mwaka wa 222 K.W.K., na kulipa jina la Kilatini la Mediolanum, nalo siku hizi linaitwa Milan. Nchi ya Italia ilikuwa ikigawanywa na kutekwa kwa muda wa mamia ya miaka, na hatimaye ilipata uhuru ikielekea mwisho wa karne ya 19. Kwa hiyo, Milan lilivamiwa na wavamizi wengi tofauti-tofauti. Miongoni mwa wale waliotwaa eneo hilo walikuwa watu wa Lombard, ambao yamkini walikuwa watu wa Skandinavia. Eneo la Lombardy liliitwa kwa jina lao, na Milan ndilo jiji kuu la eneo hilo.
Njoo Tukatembelee Milan
Historia ya Milan inahusiana sana na Kanisa Katoliki, kama vile historia ya sehemu nyingine za Italia. Basi, si ajabu kwamba kanisa kuu la Milan, au duomo, ni kanisa la tatu kwa ukubwa huko Ulaya, nalo ni mojawapo ya makanisa makubwa ulimwenguni ya aina ya Gothic. Kanisa hilo lina urefu wa meta 150 hivi, na lina vijimnara vingi sana na sanamu na nguzo zaidi ya 3,000 zenye maumbo ya ajabu. Ujenzi ulianza katika mwaka wa 1385 na ilichukua miaka 500 kumaliza kujenga kanisa hilo. Siku hizi, Waitalia wanapotaja kazi inayochukua muda mrefu mno kumaliza, wanasema ni kama “kujenga lile kanisa kuu.”
Wasomaji wa Biblia watapendezwa kuona jina la Mungu, ambalo limeandikwa kwa muundo wa “Jahve,” huko juu katika dirisha kwenye ukuta wa mbele wa kanisa hilo. Ukuta wa mbele umepambwa kwa michoro kadhaa ya matukio yanayosimuliwa katika Biblia.
Jumba la Kifalme la Castello Sforzesco ni mojawapo ya majengo yanayowakilisha mji huu. Lilijengwa katika karne ya 15 na jamaa ya Sforza, watawala wa Milan. Leo kuna vyumba mbalimbali vya vitu vya kale humo ndani. Kuna michoro ya ukutani katika chumba kimoja maarufu, ambayo baadhi ya watu hudhani ilichorwa na Leonardo da Vinci, msanii mashuhuri aliyekuwa pia mwanasayansi.
Mojawapo ya michoro maarufu ya da Vinci ni mchoro mmoja wa ukutani katika nyumba ya watawa ya Santa Maria delle Grazie—nyumba hiyo ilijengwa katika karne ya 15 kwa kufuatana na mtindo wa Mwamko (Renaissance). Mchoro huo unaonyesha Yesu anapokula kile ambacho kimeitwa Chakula cha Mwisho na huo wasemekana kuwa mchoro maarufu kushinda michoro yote mingine ya Kipindi cha Mwamko. Mojawapo ya mkusanyo mkubwa zaidi wa michoro ya wasanii mashuhuri kama Bellini, Raphael, Tintoretto, na Caravaggio nchini Italia unapatikana katika sehemu inayoitwa Pinacoteca di Brera.
Wanafunzi wa Biblia watapendezwa na Pinacoteca Ambrosiana, ambalo ni jengo lenye maktaba na vitu vya sanaa, na hapo unaweza kuona kipande cha hati-kunjo kiitwacho Muratorian Fragment. Hati-kunjo hiyo ni orodha ya Kilatini ya Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo ya mwishomwisho wa karne ya pili W.K. Orodha hiyo yasaidia kuthibitisha kwamba vitabu vya “Agano Jipya,” ni sehemu ya Maandiko Matakatifu. *
Katika maktaba hiyo pia kuna hati-kunjo inayoitwa Ambrosian O 39 sup., ya mwisho-mwisho wa karne ya tisa W.K., ambamo jina la Mungu limeandikwa kwa herufi za Kiebrania, kama vile inavyoonyeshwa katika Biblia ya New World Translation of the Holy Scriptures—With References. * Kuna Biblia nyingine za kale pia katika maktaba hiyo na vilevile hati-kunjo zinazoitwa Atlantic Codex, ambazo ni mikusanyo ya michoro 2,000 na maandishi ya kisayansi ya Leonardo da Vinci.
Inafaa kukumbuka kwamba maktaba nyingi na vyumba vingi vya vitu vya kale vimo katika majengo ya kale yenye fahari, lakini pia mara nyingi
watalii wanaoendelea kuongezeka wanasongamana sana humo. Ni lazima kupanga kimbele ili kutembelea sehemu kadhaa, na baadhi ya nyumba za ukumbusho zinaweza kutembelewa kwa muda uliowekwa tu.Kabla ya kuondoka kwenye jiji la kale, wale wanaopenda muziki huenda wakataka kuona jengo la La Scala, ambalo ni mojawapo ya nyumba maarufu za opera ulimwenguni. Hata kama mgeni hawezi kuhudhuria maonyesho ya opera, yamkini angependa kutalii nyumba ya ukumbusho, ambamo mna maonyesho ya vitu vya ukumbusho vya wanamuziki na waimbaji mashuhuri. *
Unapotalii sehemu ya kisasa ya Milan, ambalo ni mojawapo ya majiji tajiri sana huko Ulaya, utaona majengo ya orofa na uwanja wa michezo, na utakuwa umeona mambo muhimu ya Milan. Utaweza kufurahia mambo tofauti-tofauti mengi, umaridadi, na mambo ya kale ya Milan. Watalii wanaopenda kununua vitu na kutazama mambo mbalimbali bila shaka wangependa kutembelea jengo kubwa sana linaloitwa Galleria Vittorio Emanuele II lenye dari na paa la duara la kioo.
Utafurahia kutembelea Milan! Lakini sasa hebu tusafiri kwenda magharibi tutembelee jiji lingine kubwa la Italia lililo tofauti kabisa na Milan.
Turin—Jiji Lingine Muhimu la Italia
Turin ni jiji lenye wakazi milioni moja hivi, ambalo liko kwenye sehemu nyembamba zaidi ya Bonde
la Mto Po, chini ya milima ya Alps, na umbali usiozidi kilometa 100 kutoka mpaka wa Ufaransa. Jiji hilo linazungukwa na milima ya Alps kila upande na unaweza kuiona mbali sana. Karibu nusu ya mkoa wa Turin ni milima, misitu, na mabonde. Safari isiyozidi muda wa saa nzima inakufikisha kwenye makao ya starehe ya watalii huko milimani. Safari isiyozidi muda wa saa mbili, itakufikisha pwani ya Liguria.Jiji la Turin lilikuwapo kabla ya Waroma kuishi humo. Awali lilikuwa makao ya watu wa Taurini, na baadaye lilitwaliwa na Waroma. Vifusi vya makao ya Waroma vinapatikana katika eneo la kale. Kuna majengo ya enzi za kati, lakini majengo mengi ya jiji hilo yalijengwa katika karne ya 17 na 18, na majengo mengi yaliyoko katikati ya jiji yalijengwa kwa kupatana na mtindo wenye mapambo mengi wa baroque.
Huko Turin kuna nyumba ya ukumbusho yenye mkusanyo wa pekee wa vitu vya Misri. Ni jijini Cairo tu ambako kuna mkusanyo mkubwa zaidi wa vitu vya utamaduni wa kale uliositawi kwenye Mto Nile kuliko huko Turin.
Katika ziara ya muda wa saa chache utaweza kutazama na kuvutiwa na kitovu cha Turin cha historia na sanaa, Madama Palace, Royal Palace na jengo lingine liitwalo Mole Antonelliana. Mole Antonelliana lina urefu wa meta 170, nalo mpaka hivi majuzi lilikuwa mojawapo ya majengo marefu yaliyojengwa kwa mawe huko Ulaya. Kwa kuwa jengo hilo linatokeza sana mara nyingine limeitwa Mnara wa Eiffel wa Turin. Huko pia kuna Bustani ya Valentino yenye bustani mbalimbali za mimea, na vilevile uwanja wa nyasi, vijia, na chemchemi mbalimbali, na pia kuna ngome moja ya enzi za kati—kijiji chenye kuvutia cha Piedmontese ambacho kimejengwa upya jinsi kilivyokuwa kabisa katika karne ya 15.
Turin ni mojawapo ya majiji yenye viwanda muhimu nchini Italia. Kiwanda cha gari la FIAT (Fabbrica Italiana Automobili Torino) kipo hapo. Ikiwa unapendezwa na magari bora ya zamani, na magari ya pekee, kuna magari kama hayo 150, kutia ndani magari aina ya Bugatti, Maserati, na Lancia, katika nyumba ya ukumbusho ya magari inayoitwa Museo dell’Automobile, umbali wa kilometa tatu kutoka jijini. Nusu ya wakazi wa kisasa wa Turin wanapata mapato yao kutokana na viwanda vya magari.
Mashahidi wa Yehova Huko Turin na Milan
Wazawa wa wahubiri waliosafiri wa Marekebisho ya Kidini ya Kiprotestanti, walioitwa Waldenses, wameishi katika mabonde ya eneo la Turin tangu zamani. Kwa hiyo, si ajabu kwamba Charles Taze Russell, aliyeongoza kazi ya Wanafunzi wa Biblia (kama Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo), alifahamiana na padri wa dini ya Waldenses, Daniele Rivoir, katika safari yake huko Ulaya mwaka wa 1891. Russell alipanga na huyo padri ili vichapo kadhaa vya Biblia vitafsiriwe katika Kiitalia. Kikundi cha kwanza cha Wanafunzi wa Biblia kilianzishwa katika eneo hilo mwaka wa 1903. Russell aliporudi Italia mwaka wa 1912, watu 40 hivi walihudhuria mikutano ya Kikristo kwa kawaida katika jengo moja huko Pinerolo, karibu na Turin. Na huko Pinerolo ndipo mkusanyiko wao wa kwanza ulipofanywa nchini Italia mwaka wa 1925.
Kwa hiyo, utendaji wa Wanafunzi wa Biblia jijini Turin ulianza katika miaka ya 1920. Lakini wamishonari wa kwanza wa Mashahidi wa Yehova walitumwa Italia katika mwaka wa 1946. Walisaidia kuimarisha kazi ya Mashahidi. Katika miaka ya 1940 na 1950, makutaniko ya kwanza yalianzishwa jijini Turin. Sasa kuna Mashahidi wa Yehova 13,000 hivi huko Turin na katika mkoa wake. Vipi Milan?
Ofisi ya tawi ya Italia ya Mashahidi wa Yehova ilikuwako Milan kwa muda unaozidi kidogo mwaka mmoja. Ilihamishwa Roma mwaka wa 1948. Mkusanyiko wa kwanza baada ya Vita ya Pili ya Ulimwengu huko Milan ulifanywa katika jumba la maonyesho katika mwaka wa 1947. Watu 700 kutoka sehemu zote za nchi walihudhuria. Mkusanyiko wa Kimataifa wa “Habari Njema za Milele” ulifanywa, katika mwaka wa 1963, kwenye uwanja wa Vigorelli Velodrome huko Milan, ambao huenda wakati huo ulikuwa uwanja maarufu zaidi kuliko nyanja nyingine za mashindano ya mbio ya baiskeli huko Ulaya.
Kazi ya kuhubiri ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova imefanikiwa kwelikweli jijini Milan. Sasa kuna watangazaji wa Injili zaidi ya 4,000 na makutaniko 57 katika jiji hilo, na vilevile kuna Jumba moja la Mkusanyiko, ambalo awali lilikuwa Jumba la maonyesho la jiji.
Kutembelea Milan na Turin kwaweza kufurahisha kwelikweli. Wakati wowote utakapotembelea huko, yamkini utakaribishwa kwa uchangamfu na kuona mambo ambayo hutasahau kamwe.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Soma kitabu “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa,” ukurasa wa 303-305, kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
^ fu. 13 Nyongeza 1C, ukurasa 1564, iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.
^ fu. 15 Soma toleo la Amkeni! la Julai 8, 1994, ukurasa wa 24, “Usiku Mmoja Kwenye Opera.”
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
Je, Sanda ya Turin Ni ya Kweli?
Huenda mojawapo ya mambo yanayojulikana sana kuhusu jiji la Turin ni sanda ambayo wengi hufikiri ilitumiwa kuufunga mwili wa Kristo. Kitabu kimoja cha kuongoza wasafiri chasema hivi: “Salio takatifu lililo maarufu sana—na linalotiliwa shaka sana—limehifadhiwa katika kanisa kuu la jiji la Turin.” Sanda hiyo yaendelea kuonyeshwa kwa umma katika mojawapo ya makanisa madogo ya kanisa hilo kuu na imefungiwa kabisa ndani ya kasha thabiti la kioo lisiloweza kupenywa na risasi ambalo lina gesi isiyotenda. Kitabu hicho chaendelea kusema hivi: ‘Hata hivyo, mnamo mwaka wa 1988, uwongo kuhusu sanda hiyo ulifunuliwa. Jaribio lililofanywa ili kubainisha sanda hiyo ni ya wakati gani, lilionyesha kwamba ni ya karne ya 12 wala si ya kabla ya hapo.’ *
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 36 Ona gazeti la Amkeni! la Desemba 22, 1998, ukurasa wa 23, “Sanda ya Turin—Je, Ni Nguo ya Yesu ya Maziko?”
[Ramani katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MILAN
TURIN
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kanisa kuu la Milan
[Picha katika ukurasa wa 24]
Majengo ya kisasa ni mengi kuliko ya kale jijini Milan
[Picha katika ukurasa wa 25]
La Scala (juu) na Galleria Vittorio Emanuele II (kulia), jijini Milan
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mchoro “Chakula cha Mwisho” uliochorwa na Leonardo da Vinci
[Hisani]
Scala/Art Resource, NY
[PPicha katika ukurasa wa 26]
Daraja la kushusha na kupandisha la kijiji cha enzi za kati cha Turin
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mole Antonelliana huko Turin; mnara wake una urefu wa meta 170
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mto Po hupitia Turin