Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Kutoka kwa Wasomaji Wetu

Bahari Leo nilisoma ule mfululizo wenye kichwa “Bahari Zafunua Siri Zake za Ndani.” (Novemba 22, 2000) Ninapenda mambo ya asili, lakini sikujua habari zozote kuhusu makorongo ya bahari. Kwa hakika, unapojifunza zaidi kuhusu dunia na maajabu yake, ndivyo unavyoithamini zaidi na kuthamini Muumba wake mwenye hekima isiyo na kikomo.

C. F., Italia

Asanteni kwa makala hizo zenye kusisimua. Nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini Yehova aliumba viumbe kama tube worm, ilhali wanadamu wengi hawajui kuwa kuna viumbe kama hao. Nilipendezwa na ile hoja kwamba kuwapo kwa viumbe hao huonyesha kwamba Yehova huhangaikia usafi wa dunia. Twapaswa kuwa na hangaiko hilo pia.

H. S., Uingereza

Niliposoma makala hizo ilikuwa ni kana kwamba nimeingia ndani ya bahari na kutazama maajabu yake huku nikielezwa mambo kinaganaga. Maelezo yenu yalinisaidia kuona sifa za Mungu waziwazi kama zinavyoonekana kupitia uumbaji wake.

J.M.M., Zambia

Huo ulikuwa mojawapo ya mifululizo yenye kusisimua ambayo nimewahi kusoma katika gazeti la Amkeni! Mfululizo huo ulithibitisha zaidi kwamba Mtu mwenye akili tu ndiye angaliweza kuumba dunia na vitu vyote vilivyomo. Makala kama hizo huongeza tamaa yetu ya kumtumikia Muumba wetu Mtukufu.

S. G., Brazili

Akina Baba Waliotoweka Nyumbani Baba yangu alitoweka nyumbani nilipokuwa na umri wa miaka sita. Sasa nina umri wa miaka 20 na sijawahi kumwona tangu alipoondoka. Sikuzote nimehisi kuwa mimi ndiye niliyefanya aondoke na kwamba hakunipenda. Makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Baba Alituacha?” (Novemba 22, 2000) ilijibu maswali yangu yote waziwazi. Asanteni kwa kuelewa hisia za watoto wasio na baba.

K. M., Japani

Zaidi ya miaka miwili iliyopita, tulitalikiana na mume wangu. Nimejaribu kufanya yote niwezayo ili mwanangu anieleze jinsi anavyohisi kuhusu kuvunjika kwa familia yetu, lakini sijafua dafu. Sasa, kwa mara ya kwanza mwanangu amekubali kwamba aliathiriwa na talaka hiyo. Hayo yalikuwa maendeleo makubwa sana katika mawasiliano yetu. Pole kwa pole, anajieleza kwa uhuru zaidi. Nashukuru sana kwa ajili ya misaada mingi mnayotoa kwa ajili ya vijana wanaoteseka.

D. H., Marekani

Makala hiyo ilisema kwamba akina baba hutoweka nyumbani kwa sababu ya ukosefu wao wa adili. Ni taarifa moja fupi tu iliyosema tofauti. Hata hivyo, yaonekana kuna ongezeko katika idadi ya wanawake wanaoacha waume zao. Baada ya miaka 18 ya ndoa, mke wangu alianza kujihusisha na ukosefu wa adili. Nililazimika kutoka nyumbani kwangu. Ninaona ni lazima nitaje jambo hili linalochangia tatizo hilo.

L. G., Marekani

Kama unavyosema, twakubali kwamba akina baba fulani hutoweka nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa adili wa wake zao. Kanuni nyingi zilizoelezwa katika makala hiyo zaweza kutumika pia katika hali kama hii.—Mhariri.

Unusukaputi Katika makala “Kutoka Maumivu Makali Hadi Unusukaputi” (Novemba 22, 2000), mlisema kuwa hakukuwa na unusukaputi kabla ya miaka ya 1840. Katika Japani, Seishu Hanaoka alikuwa akifanya upasuaji kwa mafanikio hata kabla ya miaka ya 1840.

S. A., Japani

Kwa ujumla, wataalamu wa tiba hawakutumia unusukaputi kabla ya miaka ya 1840. Hata hivyo, kichapo “Kodansha Encyclopedia of Japan” chasema kwamba Seishu Hanaoka (1760-1835) alitayarisha aina ya nusukaputi iliyoitwa “mafutsusan” kwa kuchanganya “mitishamba sita.” ‘Aliitumia katika upasuaji wa kutibu kansa ya matiti mnamo mwaka wa 1805, miaka 40 hivi kabla ya etha kutumiwa kwa mara ya kwanza kwenye Hospitali Kuu ya Massachusetts, huko Boston.’ Baadaye, Seishu alitumia nusukaputi yake katika upasuaji mbalimbali.Mhariri.