Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kisukuku Bandia
‘Kwa miaka 116, mifupa ya mnyama-mwindaji mwenye miaka milioni 200 aliyeishi baharini katika kipindi cha Mesozoiki ilipamba Jumba la Makumbusho la Kitaifa la Wales huko Cardiff,’ lasema gazeti la The Guardian la Uingereza. “Kisha maafisa-wakuu wa jumba hilo huko Cardiff waliamua kuboresha mabaki ya mnyama huyo mla-nyama aliyeitwa ichthyosaurus—na wakatambua kwamba walidanganywa.” Mhifadhi Caroline Buttler alisema hivi: “Tulipoondoa matabaka matano ya rangi tulipata kwamba mifupa hiyo ilikuwa kazi ya udanganyifu iliyofanywa kwa uangalifu sana. Mifupa hiyo ilikuwa mchanganyiko wa aina mbili za ichthyosaurus na sehemu bandia zilizotengenezwa kwa ujanja.” Badala ya kutupwa, mifupa hiyo itahifadhiwa katika jumba la makumbusho iwe mfano wa kisukuku bandia.
Maziwa ya Milimani Yaliyochafuliwa
Maziwa ya milimani si safi kama inavyodhaniwa. “Hata yale maziwa yaliyo juu kabisa, kama Schwarzsee juu ya mji wa Sölden [Austria], yamechafuliwa sana,” laripoti gazeti la natur & kosmos la Ujerumani. Samaki wanaopatikana katika maziwa yaliyo kwenye nyanda za juu wana kiwango kikubwa cha kemikali ya DDT ambacho ni mara 1,000 zaidi ya kile kilicho katika samaki walio kwenye nyanda za chini. Kwa nini? Katika nchi za kitropiki, kemikali hiyo yenye sumu huingia hewani inapovukizwa na husafirishwa kwa mikondo ya hewa kwenye sehemu nyingine za ulimwengu. Chembe za DDT zinapokuwa juu ya sehemu zenye baridi—kama vile maziwa ya milimani—hizo huungana, kisha hunyesha kama mvua. Gazeti hilo lasema kwamba ‘maziwa ya milimani yaliyo baridi kama barafu huvuta hewa yenye DDT kutoka kwenye anga.’ DDT—dawa ya kuua wadudu ambayo ni sumu kwa wanadamu na wanyama—imepigwa marufuku huko Ulaya kwa zaidi ya miaka 20, lakini ingali inatumiwa katika nchi zinazositawi.
Makaburi Yenye Alama
Gazeti la Ufaransa la L’Express lasema hivi: “Makaburi ya kiajabu-ajabu ndio mtindo wa kisasa kwenye mazishi.” Wachimba-kaburi wanatoa huduma za kujenga sanamu za ukumbusho za rangi tofauti-tofauti 25, zenye mitindo mipya, na sanamu zilizojengwa kwa kutumia vifaa kama kioo kilichotiwa rangi au metali. Sanamu za ukumbusho zilizotengenezwa zatia ndani parachuti, mbwa na ng’ombe, gari moshi lililovunjika, na pipa kubwa la divai—lililoagizwa na mfanya-biashara wa kuuza divai. Kampuni moja kubwa yasema kwamba inatengeneza angalau sanamu 80 za pikipiki kwa mwaka kwa minajili ya kurembesha makaburi. Kwa mujibu wa makala hiyo, sheria za sehemu hiyo huruhusu watu waweke jiwe la kaburi na bamba tu, lakini sheria ya Ufaransa huunga mkono imani za kibinafsi na hutoa “uhuru wa kujenga” kwa wanaomiliki viwanja vya makaburi.
Tahadhari Kuhusu Vito Vyenye Madini ya Risasi
Ripoti moja ya Afya ya Kanada yashauri hivi: “Iwapo kuna uwezekano kwamba mtoto wako atatafuna au kumumunya vito vyenye madini ya risasi, tupa vito hivyo mara moja.” Majaribio ya maabara kuhusu vito bandia vya bei rahisi ambavyo hununuliwa kwa ajili ya watoto, ulifunua kwamba vito vingi vilikuwa na kati ya asilimia 50 na asilimia 100 ya madini ya risasi. “Hata kumeza kiasi kidogo cha madini ya risasi kwaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa ukuzi wa kiakili na wa kitabia wa vitoto na watoto,” yasema ripoti hiyo. Kwa wazi, ni vigumu kugundua madini ya risasi bila kutumia vifaa vya kupimia. Basi kwa kuwa vito vya watoto huuzwa kwa bei nafuu, njia bora yaweza kuwa ile iliyopendekezwa na gazeti la National Post: “Ukiwa na shaka, vitupe.”
Makao ya Asili—Njia ya Kuwahifadhi
“Kulinda makao ya wanyama [ndio] njia ya kuwahifadhi wanyama-pori,” lasema gazeti la Times of Zambia. Ripoti hiyo yasema kwamba jambo kuu linalosababisha kupungua kwa idadi ya wanyama-pori ni uharibifu wa makao yao. “Kulisha mifugo sehemu moja ya malisho kupita kiasi, moto, mmomonyoko wa udongo, [na] kilimo” husababisha tatizo hilo pia. Makala hiyo yaeleza hivi: “Hapana shaka kwamba ukulima ni muhimu na hatuwezi kuukomesha.” Lakini katika sehemu ambazo ukulima “haufaidi sana kwa sababu ya udongo usio na rutuba,” makao ya asili ya wanyama yaweza kuhifadhiwa, lasema gazeti la Times. Wanyama wa kufugwa wanapoletwa kwenye sehemu hizo, wao hutaabishwa na wadudu
kama kupe na wanyama wadogo waharibifu, lakini “wanyama-pori hukabiliana na wadudu hao kwa urahisi,” kwa kugaagaa matopeni, kujibingirisha mavumbini, na kuondolewa wadudu na ndege.Mashahidi Washinda Kesi Nchini Urusi
Gazeti la The New York Times la Februari 24, 2001, liliripoti hivi: “Mashahidi wa Yehova walipata ushindi mkubwa leo [Februari 23] katika mahakama moja ya Moscow dhidi ya waendesha-mashtaka ambao walitaka kikundi hicho kipigwe marufuku kwa kutumia sheria ya mwaka wa 1997 iliyokataza madhehebu ya kidini yanayochochea chuki au upinzani.” Kesi hiyo ilisimamishwa Machi 12, 1999, na wataalamu watano waliteuliwa ili kuchunguza imani za Mashahidi. Kesi hiyo ilisimamishwa kwa karibu miaka miwili. Kesi ilipoendelea tena Februari 6, 2001, mahakama ilitumia majuma matatu tu kugundua kwamba mashtaka hayo hayakuwa na msingi wowote. Hata hivyo, waendesha-mashtaka waliomba Mahakama ya Jiji ya Moscow iamuru kesi isikizwe upya. Mnamo Mei 30, ombi hilo lilikubaliwa na kesi ikarudishwa mahakamani ili isikizwe upya. Gazeti la Los Angeles Times lilisema hivi: “Kanisa la Kiothodoksi la Urusi, linalopinga vikali shughuli za wamishonari, lilikuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa ile sheria ya kidini ya mwaka wa 1997, ambayo ilishurutisha dini nyingi zikabili kibarua kigumu cha kusajiliwa.
Wajifaidi Kutokana na Nguo za Msaada
“Ni idadi ndogo tu” ya nguo za msaada inayowafikia watu wenye uhitaji kabisa, lasema gazeti la Südwest Presse la Ujerumani. Katika Ujerumani, zaidi ya tani 500,000 za nguo hutolewa kila mwaka ili kuwasaidia maskini. Lakini kwa kawaida, mashirika yanayokusanya nguo hizo huziuza kwa mashirika ya kibiashara, hivyo wanapata mamia ya mamilioni ya maki za Kijerumani kutokana na biashara ya kuuza nguo za msaada. Mara nyingi mashirika yanayokusanya nguo za msaada hayajui nguo hizo huenda wapi. Makala hiyo yataarifu hivi: “Ukitaka kuhakikisha kwamba nguo zako zinawanufaisha maskini kabisa, itakubidi wewe mwenyewe uwapelekee maskini au uwatumie watu wanaoaminika katika maeneo yenye taabu.”
Kwa Nini Watoto Huwa na Matatizo ya Kuwasiliana
Kwa mujibu wa gazeti la Berliner Morgenpost, msemaji wa shirika moja la wataalamu wa magonjwa ya watoto huko Berlin asema kwamba kutazama sana televisheni na kutumia sana kompyuta husababisha matatizo ya mawasiliano. Alisema kwamba watoto, hasa wale ambao hawajaanza kwenda shule, hawapaswi kutumia muda mwingi kutazama televisheni au kutumia kompyuta na wapaswa kutumia muda mwingi zaidi kuwasiliana na kufurahishwa na watu ana kwa ana. Kwa kuongezea, gazeti la The Sunday Times la Uingereza lasema kuwa uchunguzi mpya wadokeza kwamba “idadi inayoongezeka ya watu walio katika miaka ya 20 au 30 wanasahau mambo sana” na hawawezi “kupambanua kati ya mambo ya maana na yasiyo ya maana” kwa sababu ya “kutegemea sana tekinolojia ya kompyuta.”
Lugha Zinazotokomea
Mradi wa pamoja wa Brazili na Ujerumani wapanga kurekodi lugha za kienyeji za Brazili ambazo ziko karibu kutokomea, laripoti gazeti la Brazili la Folha de S. Paulo. Wachunguzi watumai kuhifadhi lugha za Trumai, Aweti, na Cuicuro kwa kukusanya habari katika kompyuta kuhusu maandishi na matamshi ya lugha hizo. Kulingana na mwana-isimu Aryon Rodrigues, kati ya lugha 1,200 za Brazili zilizokuwepo mwanzoni, ni 180 tu zilizopo sasa. Kati ya lugha hizo, 50 hivi huzungumzwa na watu wasiozidi 100. Kwa habari ya lugha moja, Makú, ni mjane mmoja tu wa miaka 70 anayeishi kaskazini mwa Brazili anayezungumza lugha hiyo. Rodrigues asema kwamba kuhifadhi lugha za kienyeji ni muhimu ili kuendeleza utamaduni wa jamii.
Tatizo la Takataka Huko Mexico City
Ripoti moja ya hivi majuzi katika gazeti la El Universal la Mexico City ilisema kwamba asilimia 30 ya takataka za Mexico City hubaki barabarani na kusababisha madhara ya uchafuzi. Aarón Mastache Mondragón, waziri wa mazingira, alionyesha kwamba ni asilimia 10 tu ya takataka za Mexico City zinazotengenezwa upya na asilimia 48 hivi haziwezi kuoza. Kwa mujibu wa habari za Shirika la Kitaifa la Urejelezaji, kadi ya kitambulishi huoza baada ya mwezi; tawi la mwanzi huoza baada ya mwezi hadi miezi mitatu; taulo ya pamba huoza baada ya mwezi hadi miezi mitano; soksi ya sufu huoza baada ya mwaka; ubao uliopakwa rangi huoza baada ya muda unaozidi mwaka mmoja; mkebe wa kuhifadhia chakula huoza baada ya miezi 100; mkebe wa alumina huoza baada ya miaka 200 hadi 500; na chupa ya kioo huoza baada ya zaidi ya miaka milioni moja.