Kutambua Dalili
Kutambua Dalili
“Huzuni ni hisia ya kawaida na inayofaa; mshuko wa moyo ni ugonjwa. Tatizo ni kuelewa na kutambua tofauti.”—Dakt. David G. Fassler.
KAMA ilivyo na magonjwa mengine mengi, mshuko wa moyo una dalili zilizo wazi. Lakini si rahisi sana kutambua dalili hizo. Kwa nini? Kwa sababu karibu matineja wote huhuzunika mara kwa mara, kama watu wazima. Kuna tofauti gani kati ya kuhuzunika tu na kushuka moyo? Tofauti kubwa hasa yahusu kiwango na kipindi cha hali hiyo.
Kiwango huhusisha kadiri ambavyo kijana ameathiriwa na hisia za huzuni. Mshuko wa moyo ni ugonjwa mbaya sana wa kihisia-moyo ambao hudhoofisha uwezo wa tineja wa kufanya mambo kama kawaida, na huumiza sana kuliko kuvunjika moyo tu kwa muda mfupi. Dakt. Andrew Slaby afafanua maumivu ya hali hiyo hivi: “Hebu wazia maumivu makali zaidi uliyowahi kupata—mfupa uliovunjika, maumivu ya jino, au maumivu ya kujifungua—ongeza maumivu hayo mara kumi na ujifanye hujui kisababishi cha maumivu hayo; basi huenda ukajua kwa kadiri fulani maumivu ya kushuka moyo.”
Kipindi humaanisha muda wa kuwa katika hali hiyo ya kulegea kabisa. Kulingana na maprofesa wa tiba Leon Cytryn na Donald H. McKnew, Jr., “mtoto asiyechangamka au asiyerudia hali yake ya kawaida katika muda wa juma moja baada ya kuhuzunika (kwa sababu yoyote ile)—au katika muda wa miezi sita baada ya kupata hasara kubwa sana—anakabili hatari ya kupata ugonjwa wa mshuko wa moyo.”
Dalili za Kawaida
Kijana husemwa kuwa ameshuka moyo baada ya kuwa na dalili kadhaa kwa saa nyingi kila siku, kwa angalau majuma mawili. Kipindi kifupi cha kushuka moyo huitwa tukio la kushuka moyo (depressive episode). Aina fulani ya ugonjwa wa kushuka moyo ambao huendelea kwa muda mrefu zaidi, hubainishwa wakati dalili zaendelea kuonekana kwa angalau mwaka mmoja bila kuacha kwa zaidi ya miezi miwili. Katika visa vyote hivyo, ni zipi baadhi ya dalili za kawaida za kushuka moyo? *
Badiliko la ghafula la hisia na tabia. Tineja aliyekuwa mtiifu abadilika ghafula na kuwa mkali. Vijana walioshuka moyo kwa kawaida huasi au hata kutoroka nyumbani.
Kujitenga. Kijana aliyeshuka moyo hujitenga na rafikize. Au huenda ikawa kijana aliyeshuka
moyo akahepwa na rafikize wanapotambua badiliko fulani lisilopendeza katika mtazamo na tabia yake.Kutopendezwa sana na karibu mambo yote. Kwa kustaajabisha, tineja hawi chapuchapu. Mambo aliyopenda kufanya kwa furaha hivi majuzi, sasa yamchosha.
Badiliko la ulaji linaloonekana wazi. Wataalamu wengi huonelea kwamba matatizo ya kula kama kukosa hamu ya kula, kuwa na hamu nyingi ya kula isiyo ya kawaida, na kula kupita kiasi, huonekana katika kipindi cha (na huenda nyakati nyingine yakasababishwa na) mshuko wa moyo.
Matatizo ya kulala. Tineja hulala ama kwa muda mfupi sana au kwa muda mrefu sana. Wengine hupata matatizo ya kulala yasiyo ya kawaida. Wao hukesha usiku kucha kisha hulala mchana kutwa.
Matatizo shuleni. Kijana aliyeshuka moyo hapatani vyema na walimu na vijana wenzake, na maksi zake huanza kushuka. Punde si punde tineja hukataa katakata kwenda shuleni.
Kufanya mambo yanayomhatarisha. Kijana anapozoea kufanya mambo yanayomhatarisha, hiyo yaweza kuonyesha kwamba hataki kuishi. Kujikatakata (kama vile kujikatakata ngozini) kwaweza kuwa dalili.
Kujihisi hafai au kujilaumu isivyofaa. Tineja ajichambua isivyofaa na kuhisi kuwa hawezi kufaulu maishani, hata ikiwa jambo hilo si kweli.
Shida zinazotokana na matatizo ya akili. Wakati kisababishi cha matatizo kama maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, maumivu ya tumbo, na maumivu mengine hakipatikani mwilini, hiyo yaweza kuwa dalili ya kushuka moyo.
Kufikiria mara kwa mara kuhusu kifo au kujiua. Kuzungumza sana kuhusu mambo yanayoogopesha kwaweza kuwa dalili ya kushuka moyo. Ndivyo ilivyo pia na vitisho vya kujiua.—Ona sanduku lililo chini.
Ugonjwa wa Hisia Zinazobadilika-badilika
Ugonjwa mwingine unaotatanisha huwa na baadhi ya dalili hizohizo—ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika. Kulingana na Dakt. Barbara D. Ingersoll na Dakt. Sam Goldstein, ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika (unaoitwa pia manic-depressive disorder) ni ‘hali inayotambuliwa kwa matukio ya kushuka moyo yanayofuatwa na vipindi vya kusisimuka kupita kiasi
na kupata nguvu nyingi sana. Kusisimuka huko huzidi hali ya kawaida ya kuchangamka.’Hali hiyo isiyo ya kawaida huitwa mania. Dalili zake zatia ndani kuruka ghafula kutoka wazo moja hadi lingine, kuzungumza kupita kiasi, na kutokuwa na usingizi. Kwa hakika, mgonjwa aweza kukosa usingizi kwa siku nyingi bila kuonyesha dalili zozote za uchovu. Dalili nyingine ya ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika ni tabia ya kufanya mambo hima-hima bila kufikiria matokeo. Ripoti moja ya Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili yasema hivi: “Mara nyingi hali hiyo ya mania huathiri fikira, maamuzi, na njia ya kushughulika na wengine na hivyo kutokeza matatizo makubwa na aibu.” Hali hiyo hudumu kwa muda gani? Nyakati nyingine kwa siku chache tu; katika visa vingine, hali hiyo hudumu kwa miezi kadhaa kabla ya ugonjwa wa mshuko wa moyo kuanza.
Wale wanaokabili hatari kubwa zaidi ya kupatwa na ugonjwa huo watia ndani watu wenye washiriki wa familia walio na ugonjwa huo. Jambo la kupendeza ni kwamba kuna tumaini kwa watu wanaougua ugonjwa huo. Kitabu The Bipolar Child chasema hivi: “Ugonjwa huo unapobainishwa mapema na kutibiwa vizuri, watoto hao na familia zao waweza kuishi maisha mazuri sana yaliyotulia zaidi.”
Ni muhimu kung’amua kwamba dalili moja tu haitoshi kuonyesha kwamba mtu ameshuka moyo au ana ugonjwa wa hisia zinazobadilika-badilika. Mara nyingi, mshuko wa moyo hubainishwa baada ya dalili nyingi kuonekana katika kipindi fulani cha wakati. Hata hivyo, bado kuna swali, Kwa nini matineja hukumbwa na tatizo hili linalotatanisha?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 7 Dalili zinazoonyeshwa hapa zakusudiwa kuandaa muhtasari tu wala si kuandaa njia ya kubainisha mshuko wa moyo.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Mtoto Anapotaka Kufa
Kwa mujibu wa Vituo vya Marekani vya Kudhibiti Magonjwa, katika mwaka mmoja hivi karibuni, idadi ya vijana waliojiua ilizidi jumla ya idadi ya wale waliokufa kutokana na kansa, ugonjwa wa moyo, UKIMWI, kasoro za maumbile, kiharusi, homa ya vichomi, mafua makali, na ugonjwa wa kudumu wa mapafu. Jambo jingine linalosikitisha ni kwamba: Visa vya kujiua vilivyoripotiwa vya watu walio kati ya umri wa miaka 10 na 14 vimeongezeka sana.
Je, vijana wanaobalehe wanaweza kuzuiwa wasijiue? Ndiyo, katika hali fulani. “Takwimu zaonyesha kwamba visa vingi vya kujiua huanza kwa majaribio au maneno na maonyo yanayodokeza kujiua,” aandika Dakt. Kathleen McCoy. “Tineja wako anapodokeza tu kwamba anafikiria kujiua, huo ni wakati wa kulizingatia jambo hilo na hata labda kutafuta msaada wa wataalamu.”
Kuongezeka kwa matineja wanaoshuka moyo huonyesha wazi uhitaji wa wazazi na watu wengine wazima kuchukua kwa uzito mambo yoyote yanayodokeza kwamba kijana ataka kujiua. “Katika karibu visa vyote vya kujiua nilivyopata kuchunguza, ishara zozote zilizoonyesha mipango ya kijana zilipuuzwa au hazikutiliwa maanani,” aandika Dakt. Andrew Slaby katika kitabu chake No One Saw My Pain. “Washiriki wa familia na marafiki hawakuelewa uzito wa mabadiliko waliyokuwa wakiona katika kijana. Walikazia fikira matokeo badala ya tatizo lenyewe, hivi kwamba wakakata kauli kwamba tatizo lilikuwa ‘matatizo ya familia’ au ‘kutumia dawa za kulevya’ au ‘kukosa hamu ya kula.’ Nyakati nyingine, badala ya kutibu mshuko wa moyo, jambo lililoshughulikiwa hasa ni ile hali ya kukasirika, kuchanganyikiwa, na kuudhika upesi. Tatizo lenyewe liliendelea kusababisha mateso na uchungu.”
Ujumbe u wazi: Chukua kwa uzito ishara zozote zinazodokeza nia ya kujiua!
[Picha katika ukurasa wa 7]
Nyakati nyingine, uasi ni ishara ya kushuka moyo
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mara nyingi, matineja walioshuka moyo hawapendezwi tena na mambo yaliyowafurahisha zamani