Wamaya Walivyokuwa na Walivyo Leo
Wamaya Walivyokuwa na Walivyo Leo
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO
YASEMEKANA kwamba ustaarabu wao ulikuwa miongoni mwa staarabu maarufu zaidi katika Kizio cha Magharibi. Si ajabu kwa sababu wenyeji hao wa kale wa Belize, El Salvador, Guatemala, Honduras, na Mexico walibuni usanifu-majengo, uchoraji, ufinyanzi, na uchongaji wa pekee sana! Walibuni mfumo bora wa maandishi na kufanya maendeleo makubwa katika taaluma ya hesabu. Hata walibuni kalenda inayotegemea kipindi ambacho dunia inazunguka jua. Wamaya walikuwa nani? Wamaya walikuwa wajenzi wa mojawapo ya staarabu za kale sana zenye ufanisi zaidi na maarufu sana huko Amerika.
Mambo mengi tunayojua kuhusu Wamaya yalitokana na maandishi na picha zilizochongwa kwenye mawe. Wamaya waliandika historia na desturi zao kwenye ngazi, kwenye miimo ya milango, kwenye mabamba ya mawe au nguzo kwa kutumia mfumo wa maandishi wenye herufi 800, herufi nyingi ziliwakilishwa na michoro. Waliandika pia kwenye karatasi zilizotengenezwa kutokana na magamba ya ndani ya mitini ya mwitu. Walikunja karatasi hizo na kutengeneza vitabu (vilivyoitwa kodeksi), kisha wakafunika vitabu hivyo kwa ngozi ya chui wa Amerika. Mabuku mengi yaliharibiwa wakati Wahispania waliposhinda Wamaya mwaka wa 1540 W.K., lakini mabuku machache yangalipo leo.
Yaelekea wakulima wa kwanza Wamaya walihamia kwenye nyanda za chini za kaskazini mwa Guatemala miaka 1,000 hivi kabla ya Kristo. Lakini ustaarabu wa Wamaya ulifikia kilele kati ya mwaka wa 250 W.K. na 900 W.K.—kwa kawaida kipindi hicho huitwa Kipindi Bora cha Ufanisi. Acheni tuchunguze kwa ufupi mambo ambayo yamejulikana kuhusu Wamaya hao wa kale.
Wajenzi na Wasanifu-Majengo Stadi Sana
Wamaya walikuwa wachongaji stadi sana wa mawe, nao walijenga piramidi na mahekalu makubwa kwa kutumia mawe ya chokaa na mchanganyiko wa saruji na mchanga. Piramidi hizo zinafanana sana na piramidi za Misri. Hapo kale, piramidi hizo zilifanya watu fulani wafikiri kimakosa kwamba Wamaya walikuwa wazao wa Wamisri.
Magofu ya majiji ya Wamaya yaliyojengwa kwa mawe yamepatikana nchini Guatemala, Honduras na Yucatán, kusini mwa Mexico. Milki ya Wamaya ilipofikia kilele cha ufanisi na maendeleo, ilikuwa na zaidi ya majiji 40 kama hayo, kila jiji lilikuwa na wakazi wapatao 5,000 hadi 50,000. Kichapo The New Encyclopædia Britannica, chasema kwamba “huenda kilele cha idadi ya wakazi Wamaya kilifikia 2,000,000, wengi wao waliishi katika nyanda za chini za nchi inayoitwa leo Guatemala.”
Ujenzi wa majiji hayo pamoja na majengo yake maridadi sana ya mawe ulifaulu tu kwa sababu ya jitihada kubwa sana za wakulima Wamaya waliokuza mahindi. Mbali na kukuza chakula kwa ajili ya familia zao, wanaume hao wenye bidii walitarajiwa kusaidia pia katika kazi ya ujenzi. Isitoshe, walilazimika kukuza chakula kwa ajili ya watu wenye vyeo vya juu na makasisi, ambao, ilisemekana kwamba walikuwa na kazi muhimu zaidi ya kufanya.
Maisha ya Familia za Wamaya
Familia za Wamaya zilikuwa na uhusiano wa karibu sana. Kwa kawaida, babu na nyanya,
wazazi, na watoto waliishi pamoja. Kazi nyingi za kilimo zilifanywa na wanaume na wavulana wenye umri mkubwa. Wasichana walijifunza kupika, kushona nguo, na kulea ndugu na dada zao wachanga.Wakulima Wamaya walikuza parachichi, pilipili, na viazi vitamu. Lakini chakula kikuu cha Wamaya kilikuwa mahindi. Wanawake na wasichana walipika mahindi kwa njia mbalimbali. Walipika keki yenye umbo la chapati, inayoitwa leo tortilla. Hata pombe inayoitwa balche ilitengenezwa pia kutokana na mahindi. Inakadiriwa kwamba leo asilimia 75 hivi ya chakula cha Wamaya kina kiasi fulani cha mahindi, na huenda walitumia kiasi kikubwa zaidi cha mahindi nyakati zilizopita.
Miungu Mingi ya Kiume na ya Kike
Dini ilikuwa muhimu sana katika maisha ya Wamaya. Waliabudu miungu mingi, kichapo kimoja kinataja miungu 160. Kwa mfano, kulikuwa na mungu muumbaji, mungu wa mahindi, mungu wa mvua, na mungu-jua. Wanawake walisafiri hadi kwenye hekalu la mungu-mke Ixchel kwenye kisiwa cha
Cozumel na kusali ili kuwa na uwezo wa kuzaa au, endapo walikuwa wajawazito, walimsihi awasaidie wajifungue bila matatizo.Kwa Wamaya, kila siku ilikuwa na umuhimu fulani wa kidini, na kila mwezi kwenye kalenda ya Wamaya ulikuwa na sherehe hususa. Sherehe maalumu zilifanywa pia kuhusiana na mazishi ya wafu. Miili ilipakwa rangi nyekundu, kisha miili hiyo pamoja na vyombo fulani vya kibinafsi ilifungwa ndani ya mikeka ya majani makavu. Halafu ilizikwa chini ya sakafu ya nyumba ambamo watu hao walikuwa wakiishi. Watawala walizikwa kwa njia tofauti kidogo, walizikwa ndani ya piramidi, chini ya mahekalu. Watumishi wao waliuawa na kuzikwa pamoja nao, pamoja na vyombo fulani ambavyo Wamaya waliamini kwamba vingewasaidia watu hao katika maisha yao ya baada ya kifo.
Nyakati nyingine Wamaya walitoboa ndewe zao za masikio au miguu na nyayo zao kwa sababu ya desturi za kidini. Hata walitoboa ulimi wao. Sanamu za kuchongwa na picha zilizo ukutani na kwenye vyungu zinaonyesha waziwazi kwamba Wamaya walitoa dhabihu katika ibada yao. “Mara nyingi walidhabihu wanyama mbalimbali, lakini dhabihu bora zaidi ilikuwa dhabihu ya wanadamu. Wale waliotolewa dhabihu walikuwa askari maadui na watumwa, lakini pia watoto wachanga wa kiume na wa kike,” aandika Dakt. Max Shein katika kitabu chake The Precolumbian Child. Wanahistoria fulani wamesema kwamba pindi moja wasichana wadogo walitolewa kuwa mabibi-arusi wa mungu wa mvua kwa kutupwa wakiwa hai katika kidimbwi kitakatifu katika jiji la Chichén Itzá. Ikiwa msichana alipatikana angali hai jioni, waliona hiyo kuwa ishara ya kwamba mungu wa mvua alikuwa ameridhika na bibi-arusi aliyetupwa kidimbwini mapema. Kwa hiyo, msichana huyo alitolewa kwenye kidimbwi hicho.
Wamaya Walivyo Leo
Kichapo The New Encyclopædia Britannica chasema kwamba baada ya mwaka wa 900 W.K., “ustaarabu bora wa Wamaya ulididimia ghafula. Yale majiji yao makubwa na vituo vya kisherehe vilibaki ukiwa na vikafunikwa na vichaka.” Hakuna mtu anayejua kikweli kilichosababisha kutokomea kwa Wamaya. Baadhi ya watu husema kwamba mashamba yao yalikosa rutuba kwa sababu ya kutumiwa sana. Wengine hudokeza kwamba wakulima walianza kutumia mbinu zisizofaa za kilimo kwa sababu ya upungufu wa chakula, ilhali wengine walikimbilia majiji maskini ambayo tayari yalikuwa yamesongamana watu maskini. Vyovyote iwavyo, Wamaya hawakutokomea kabisa. Kuna Wamaya 2,000,000 leo, wanaishi hasa kaskazini mwa Yucatán na huko Guatemala.
Dini kuu ya Wamaya leo ni Katoliki, na imejitahidi kuwavutia wenyeji hao. Kwa mfano, ripoti moja ya shirika la habari la Associated Press inasema kwamba “katika mwaka wa 1992, ambao ulikuwa mwadhimisho wa 500 wa ushindi wa Hispania dhidi ya Guatemala, Kanisa Katoliki la Guatemala liliomba msamaha hadharani kwa ajili ya kuwatesa Wahindi Wamarekani wakati lilipokuwa likieneza injili nchini Guatemala.”
Lakini kuenea kwa Ukatoliki hakumaanishi kwamba Wamaya wameacha dini ya mababu wao wa kale. Badala yake, makasisi wengi Wakatoliki hukubali kuchanganya desturi za wenyeji hao na mazoea na mafundisho ya kanisa. Kwa mfano, kwa muda mrefu Wamaya wamekuwa na imani ya kwamba vitu vyote vilivyo hai na visivyo hai vina kani ya uhai, kwa hivyo vyapasa kuabudiwa. Dhana hiyo imekubaliwa na kanisa na ingawa imefanywa kuwa sehemu ya mafundisho ya Kikatoliki, jambo hilo limewafanya viongozi fulani waulize kanisa hilo litakubali mambo mengi kadiri gani ya kipagani na huku likidai kuwa la Kikristo? *
Wamaya na Mashahidi wa Yehova
Mashahidi wa Yehova wanafundisha kweli safi za Biblia katika nchi zilizo na wakazi wengi Wamaya. Wengi wanaitikia vizuri. Ona mifano miwili tu.
“Nilikuwa na cheo maarufu cha heshima katika jamii yetu, ingawa jambo hilo halikunizuia kutumia mali ovyoovyo na kulewa,” asema Caridad. Sawa na Wamaya wengine wengi, Caridad alikuwa Mkatoliki aliyeamini uwasiliani-roho. “Nilipokuwa mgonjwa, nilimwendea mchawi,” yeye asema. Binti za Caridad walianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova. “Nikaanza kupendezwa pole kwa pole, hasa nilipoona jinsi mwenendo wa binti zangu ulivyobadilika. Punde si punde nikaanza kujifunza pia,” asema Caridad. Matokeo yamekuwa nini? “Ukweli umenisaidia kumjua na kumpenda Yehova,” akiri Caridad. “Nimeacha mazoea na desturi zote zisizompendeza Yehova, na nimewekwa huru kutokana na woga na ushirikina.”
Paula, Mmaya wa kutoka Guatemala, alihuzunishwa sana na vifo vya wana wake wawili. “Niliwajengea madhabahu daima,” yeye aeleza. “Nilikuwa na Biblia ambayo mtawa wa kike Mkatoliki alinipa, na niliisoma kwa muda wa saa mbili kila usiku nikijaribu kupata jibu kwa swali nililokuwa nikijiuliza, ‘Wanangu waliokufa wako wapi?’” Baada ya muda Paula alianza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, na akaanza kuhudhuria mikutano yao mara moja. “Walinifasiria Neno la Mungu waziwazi,” yeye asema. “Nafurahi kujua kwamba Ufalme wa Mungu utakomesha magonjwa na kifo. Sikuzote mimi hufikiria tumaini la ufufuo.” (Yohana 5:28, 29) Sasa Paula anawaambia wengine habari njema za Ufalme wa Mungu. “Bado kuna wengi wanaohitaji msaada,” yeye asema.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 20 Ni kawaida kuona Wamaya wakiashiria alama ya msalaba kama Wakatoliki baada ya kutembea kwa kilometa nyingi ili kutembelea madhabahu ya San Simón, ambamo mna sanamu ya mbao isiyojulikana ilikotoka.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Kalenda ya Wamaya
Wamaya walibuni mfumo wa kalenda sahihi ya kila mwaka ambayo ilitia ndani mwaka mrefu (leap year).
Kulingana na Wamaya mwaka ulikuwa na siku 365. Siku 364 ziligawanywa zikawa na majuma 28, kila juma likiwa na siku 13. Mwaka mpya ulianza siku ya 365, Julai 16. Vipi miezi? Kalenda ya Wamaya, ambayo imeonyeshwa hapo juu, ilikuwa na miezi 18, na kila mwezi ulikuwa na siku 20. Hivyo basi, majuma na miezi haikuenda sambamba isipokuwa pindi moja tu, yaani, mara moja baada ya siku 260 (13 mara 20), majuma na miezi ilianza siku moja. Kichapo kimoja cha marejeo chasema kwamba “ijapokuwa kalenda ya Wamaya ilikuwa tata sana, ilikuwa kalenda sahihi zaidi iliyowahi kubuniwa na wanadamu kabla ya kalenda ya Gregory kubuniwa.”—Funk & Wagnalls New Encyclopedia.
[Grafu/Picha katika ukurasa wa 16, 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Rekodi ya Miaka na Matukio ya Wamaya
Olmec
1000 B.C.E.
500 B.C.E.
Olmec
Zapoteki
Teotihuacan
B.C.E | C.E.
500 C.E.
Teotihuacan
Zapoteki
Toltec
1000 C.E.
Toltec
Aztec
1500 C.E.
Aztec
[Hisani]
Sanaa ya Wamaya: Dover Publications, Inc.
[Ramani katika ukurasa wa 16, 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MEXICO
RASI YA YUCATÁN
BELIZE
GUATEMALA
EL SALVADOR
HONDURAS
[Hisani]
Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mabaki ya piramidi ya hekalu yenye kimo cha futi 75 katika jiji la kale la Wamaya la Palenque
[Picha katika ukurasa wa 16]
Utayarishaji wa “tortilla”
[PPicha katika ukurasa wa 18]
Chichén Itzá
Hekalu la Kukulcán
Sanamu inayolinda mwingilio wa Hekalu la Mashujaa, ikiwa na chombo cha kutolea dhabihu, yaelekea kilitumiwa kupokea mioyo ya wanadamu
[Picha katika ukurasa wa 19]
Caridad akiwa na mkewe na binti zake