Mbona Watu Wana Ghadhabu?
Mbona Watu Wana Ghadhabu?
MWANAMUME mmoja auawa kwa kupigwa risasi ndani ya baa huko Prague, katika Jamhuri ya Cheki. Kwa nini? Muuaji alikasirika kwa sababu mtu huyo alikuwa anachezesha muziki kwa sauti kubwa. Dereva mmoja auawa kwa kupigwa na kigoe cha mpira wa magongo kwenye makutano ya barabara huko Cape Town, Afrika Kusini. Mtu aliyempiga alikasirika kwa sababu dereva huyo alikuwa amemmulika kwa taa za gari. Mpenzi wa muuguzi mmoja wa kike Mwingereza anayeishi Australia avunja mlango wa mbele wa nyumba; kisha ammwagia mafuta, awasha moto, na kutoroka.
Je, ripoti kuhusu watu wenye ghadhabu—barabarani, nyumbani, kwenye ndege—zinatiliwa chumvi? Je, ripoti hizo ni ishara za tatizo jingine lisiloonekana wazi? Mambo ya hakika yanaunga mkono swali hilo la mwisho.
Ripoti moja ya hivi karibuni kutoka kwenye Shirika la Magari la Marekani la Usalama Barabarani ilisema kwamba “ripoti kuhusu visa vya ujeuri barabarani zimeongezeka kwa asilimia 7 hivi kila mwaka tangu mwaka wa 1990.”
Ghadhabu imeenea sana nyumbani. Kwa mfano, polisi wa jimbo la New South Wales huko Australia walisema kwamba kulikuwa na ongezeko la asilimia 50 la visa vya ujeuri katika familia mnamo mwaka wa 1998. Robo moja ya wanawake wa nchi hiyo ambao wameolewa au wanaoishi pamoja na wanaume bila kuolewa wametendewa kwa ujeuri na wenzi wao.
Kumekuwa na visa vya ujeuri pia katika ndege. Kwa kuwa abiria fulani wanaosafiri kwa ndege wamewashambulia wafanyakazi wa ndege, abiria wenzao, na hata marubani, makampuni makubwa ya usafiri wa ndege yamewaandalia wafanyakazi wake kamba maalumu za kuwafunga watu wajeuri kwenye viti vyao.
Kwa nini watu wengi wanashindwa kujizuia? Ni nini kinachosababisha matendo hayo ya ghadhabu? Je, inawezekana kudhibiti hisia hizo?
Kwa Nini Ghadhabu Imeongezeka?
Mtu anapoghadhibika yeye huwa na hasira kali au huionyesha. Matendo ya ghadhabu hutokea wakati hasira inaporuhusiwa iongezeke hadi inapolipuka. ‘Ujeuri barabarani hausababishwi na tukio moja. Badala yake, yaonekana ujeuri huo husababishwa na mitazamo ya madereva na misongo mingi maishani mwao,’ ndivyo asemavyo David K. Willis, msimamizi wa Shirika la Magari la Marekani la Usalama Barabarani.
Jambo moja linalochangia misongo hiyo ni habari nyingi tunazopata kila siku. Jalada la nyuma la kitabu Information Overload cha David Lewis, lasema hivi: ‘Wafanyakazi wengi leo wanapata habari nyingi sana. Kwa sababu ya kulemewa na habari hizo, wao hufadhaika, huwa wazembe, na kuvurugika.’ Gazeti moja lilionyesha jinsi ambavyo kuna habari nyingi sana liliposema hivi: “Kiasi cha habari zinazochapishwa katika gazeti la katikati ya juma kinalingana
na kile ambacho mtu wa kawaida aliyeishi katika karne ya 17 alipata katika maisha yake yote.”Vitu tunavyokula au kunywa vyaweza pia kuchangia ghadhabu. Uchunguzi umeonyesha kwamba kuvuta sigara, kunywa vileo, na kula vyakula visivyokuwa na virutubishi huchangia uhasama. Mazoea hayo ya watu wengi huzidisha mfadhaiko. Kisha mfadhaiko huo unafanya watu waropoke matusi, wakose subira na uvumilivu.
Kukosa Adabu na Filamu
Dakt. Adam Graycar, mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Jinai ya Australia alisema hivi alipokuwa akionyesha uhusiano uliopo kati ya ukosefu wa adabu na uhalifu: ‘Huenda njia moja kuu ya kupunguza wizi wa vitu vidogo-vidogo ni kuanza tena kufunza adabu na heshima.’ Taasisi hiyo hukazia kwamba watu wanapaswa kuwa wenye subira, wavumilivu, na waepuke kutumia matusi. Taasisi hiyo yasema kwamba watu wasipofanya hivyo, ukosefu wa adabu unaweza kusababisha uhalifu. Kwa kushangaza, watu wengi huchagua burudani fulani ili kuondoa mfadhaiko na kumbe burudani hiyo inachangia ghadhabu na ukosefu wa uvumilivu. Jinsi gani?
Ripoti moja ya Taasisi ya Elimu ya Jinai ya Australia yasema hivi: “Watoto na watu wazima huenda kwenye sinema kutazama filamu za mauaji na uharibifu. Biashara ya kuuza video za ujeuri inasitawi na kuleta mapato mengi. Watoto wengi wanapenda vidude vya kuchezea vya kivita, japo kwa kawaida wazazi wao hawavipendi. Watu wengi, watu wazima kwa watoto, hufurahia kutazama ujeuri kwenye televisheni, na televisheni hutimiza sehemu muhimu katika kufundisha maadili.” Jambo hilo linahusianaje na milipuko ya hasira barabarani na nyumbani? Ripoti hiyo yamalizia hivi: ‘Kadiri jamii inavyopuuza ujeuri, ndivyo watu katika jamii hiyo watakavyokuwa.’
Huenda watu wengi leo wakasema kwamba kuonyesha hasira ni njia ya kawaida tu ya kutenda mtu anapokuwa na mfadhaiko na kwamba ni jambo lisiloepukika katika jamii yetu yenye misongo mingi na ujeuri. Kwa hiyo, je, ni sawa kuonyesha hasira?
Je, Ghadhabu Inapasa Kudhibitiwa?
Kama vile volkeno inayolipuka huwaumiza watu wanaoishi karibu na eneo la mlipuko, ndivyo mtu anayeonyesha hasira kali anavyowaumiza watu walio karibu naye. Pia, yeye hujiumiza sana. Vipi? “Kuonyesha hasira hutokeza ujeuri mwingi hata zaidi,” lasema jarida la The Journal of the American Medical Association (JAMA). Uchunguzi unaonyesha kwamba wanaume wanaoonyesha hasira “wanakabili hatari kubwa ya kufa kufikia wanapokuwa na umri wa miaka 50 kuliko wanaume wasiofanya hivyo.”
Shirika la Marekani la Moyo lasema hivi pia: “Uwezekano wa wanaume wanaoonyesha hasira kali kupata ugonjwa
wa kiharusi ni mara mbili ya ule wa wanaume wanaodhibiti hasira.” Maonyo hayo yanawahusu pia wanawake.Ni ushauri gani unaoleta manufaa? Angalia ufanani uliopo kati ya mashauri ya wataalamu na ule unaopatikana katika kitabu cha mahusiano ya wanadamu ambacho kimesambazwa zaidi ya vingine vyote, Biblia.
Zuia Hasira—Epuka Ghadhabu
Dakt. Redford B. Williams asema hivi katika jarida la JAMA: ‘Kuonyesha hasira hakusaidii kwa vyovyote. Jambo la maana ni kuchunguza hasira yako kisha kuizuia.’ Anadokeza mtu ajiulize hivi: “(1) Je, hali ninayokabili ni muhimu kwangu? (2) Je, ninafikiri na kuhisi ifaavyo? (3) Je, hali hii inaweza kurekebishwa, ili niepuke hasira?”
Mithali 14:29; 29:11 “Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu. Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote; bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.”
Waefeso 4:26 “Iweni na hasira ya kisasi, na bado msifanye dhambi; msiache jua litue mkiwa katika hali ya kuchokozeka.”
Katika kitabu chake Dealing With Anger—Self-Help Solutions for Men, Frank Donovan apendekeza hivi: “Kuepuka hasira—au, kuondoka unapokasirishwa—ni jambo la maana sana wakati mtu anapokuwa na hasira kali.”
Mithali 17:14 “Mwanzo wa ugomvi ni kama kutoboa penye maji; basi acheni ugomvi [“ondoka,” NW] kabla haujafurika.”
Bertram Rothschild alisema hivi katika jarida la The Humanist: ‘Hasira ni daraka la mtu mwenyewe. Sisi wenyewe hujua kwa nini sisi hukasirika. Mara nyingi hasira huleta hasara badala ya kuleta mazuri. Kutokasirika ni bora kuliko kukasirika.’
Zaburi 37:8 “Ukomeshe hasira, uache ghadhabu, usikasirike, mwisho wake ni kutenda mabaya.”
Mithali 15:1 “Jawabu la upole hugeuza hasira; bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.”
Mithali 29:22 “Mtu wa hasira huchochea ugomvi; na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.”
Mamilioni ya Mashahidi wa Yehova ulimwenguni pote hukubaliana na mashauri hayo yaliyo juu. Tunakualika uhudhurie mikutano yao kwenye Jumba la Ufalme lililo katika eneo lenu na ujionee waziwazi jinsi ambavyo kuna faida kufuata shauri la Biblia ijapokuwa tunaishi wakati ambapo watu wengi wana ghadhabu.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kama volkeno inayolipuka, mtu asiyedhibiti ghadhabu husababisha madhara
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kuna faida kufuata shauri la Biblia