Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutafuna Chingamu Ni Zoea la Kisasa na la Kale

Kutafuna Chingamu Ni Zoea la Kisasa na la Kale

Kutafuna Chingamu Ni Zoea la Kisasa na la Kale

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

WATU WAMEFURAHIA kutafuna utomvu tangu zamani. Wagiriki wa kale walitafuna utomvu wa mti aina ya mastic. Waazteki walitafuna tzictli, utomvu wa mti wa sapodilla. Na Wahindi Wekundu huko New England waliwafundisha wakoloni kutafuna utomvu wa mti fulani wa aina ya msonobari. Kwa kweli, mapema katika miaka ya 1800, utomvu wa mti huo ukawa chingamu ya kwanza kuuzwa huko Marekani. Baadaye, watu walianza kutafuna nta ya mishumaa iliyoongezwa sukari.

Inasemekana kwamba chingamu ya kisasa ilibuniwa mwishoni mwa miaka ya 1800. Santa Anna, aliyekuwa rais wa Mexico, alipokuwa uhamishoni huko Marekani, alionekana akitafuna vipande vya utomvu wa mti wa sapodilla ambavyo alikuwa ameleta kutoka Mexico. Mbuni mmoja Mmarekani alitambua kwamba watu wangependa utomvu huo kama ungeongezwa utamu na ladha. Kwa hiyo, alianza kuingiza utomvu huo Marekani ili kutengeneza chingamu.

Utomvu wa mti wa sapodilla unafanana na maziwa, na mti huo unaitwa pia mti wa chingamu. Mti huo unapatikana katika msitu wa mvua unaoitwa Gran Petén, kaskazini mwa nchi ya Guatemala, katika nchi ya Belize, na katika Rasi ya Yucatán huko Mexico. Katika maeneo mengine, zaidi ya miti 75 aina ya sapodilla inaweza kukua katika ekari moja tu. Katika majira ya mvua, watu wanaokusanya utomvu huo hukatakata mashina ya miti hiyo ili utomvu utiririke polepole katika chombo kilichowekwa chini ya mti. Kisha utomvu hukusanywa, huchemshwa hadi uwe na ugumu unaotakikana, hufinyangwa na kutengenezwa kuwa vipande, na kuuzwa. Ijapokuwa utomvu huo bado hutumiwa kwa kadiri fulani kutengeneza chingamu, hasa chingamu ya asilia, tangu miaka ya 1940 chingamu nyingi hutengenezwa kwa vitu visivyo vya asili huko Marekani.

Kwa nini chingamu hupendwa sana? Wengi hutafuna chingamu ili kusafisha pumzi na kusafisha meno baada ya kula, wakiwa mahali ambapo hawawezi kutumia mswaki. * Wengine hutafuna chingamu ili kutulia au kukaza fikira kwenye jambo fulani. Kwa kuwa kutafuna chingamu humtuliza mtu na kumsaidia kukaa chonjo, wanajeshi wa Marekani walipewa chingamu wakati wa vita ya kwanza na ya pili ya ulimwengu, na bado ni sehemu ya posho ambayo wanajeshi walio vitani hupewa. Baadhi ya madereva huona kwamba kutafuna chingamu huwasaidia sana kukaa macho kuliko kunywa kahawa. Kutafuna chingamu huwasaidia watu wanaojaribu kuacha kuvuta sigara. Pia inapendwa kama kibadala cha vitafunio, kwa kuwa kipande kimoja cha chingamu kina kalori kumi hivi.

Hata hivyo, zoea hilo huwaudhi watu wengi. Na nyakati nyingine kutafuna chingamu kungekuwa kukosa adabu. Kwa hiyo, ikiwa wewe una zoea hilo la kisasa na la kale la kutafuna chingamu, tumia busara. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kutafuna chingamu huongeza mate, nayo huondoa asidi kwenye meno, na hivyo kudumisha afya bora mdomoni na kuzuia meno yasioze. Madaktari wa meno wanapendekeza kwamba chingamu isiyo na sukari itumiwe kwa kusudi hilo.

^ fu. 7 Tahadhari: Chingamu haipasi kumezwa, kwa kuwa inaweza kufunga koo na matumbo. Pia, kutafuna chingamu hufanya madini mengi ya zebaki yatoke katika risasi iliyotumiwa kujaza mashimo ya meno.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Kukatakata shina la mti unaoitwa “sapodilla”

[Hisani]

Copyright Fulvio Eccardi/vsual.com