Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kuahirisha Mambo na Afya
“Kuahirisha mambo kunaweza kukufanya uwe mgonjwa,” wasema uchunguzi ulioelezwa katika gazeti la Vancouver Sun. Uchunguzi ulifanywa kuhusu wanafunzi 200 wa vyuo vikuu nchini Kanada na kutangazwa kwenye mkutano wa Chama cha Wanasaikolojia cha Marekani hivi majuzi huko Toronto, Kanada. Uchunguzi huo “ulionyesha kwamba wale wanaoahirisha mambo huwa na mfadhaiko mkubwa kwa sababu ya kukawia kutenda, hivyo wao huelekea kupata maradhi yanayosababishwa na mfadhaiko kuliko wengine. . . . Mtihani unapokaribia, wale wanaoahirisha mambo hufadhaika zaidi. Mtazamo wao wa kutojali ulisababisha kuongezeka kwa maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, mafua, kukosa usingizi na mizio. Matatizo ya kupumua, maambukizo na kipandauso yaliongezeka.”
Samaki Anayepanda Miamba!
Kulingana na ripoti ya gazeti la Natural History, kikundi cha wataalamu wa samaki nchini Brazili kimeona aina moja ya samaki wa darter wa Amerika Kusini ambaye kwa kawaida hufanya zoezi gumu la kupanda juu ya mwamba ulio na urefu sawa na orofa tano. Mwamba huo una unyevu na utelezi, na uko chini ya maporomoko ya maji. “Watafiti waliona samaki huyo mwenye urefu wa sentimeta nne akipanda juu ya maji yasiyo na chumvi na yanayoenda kwa kasi ya vijito vya Espírito Santo, mashariki mwa Brazili.” Wakitumia pezi kubwa mbili, samaki hao walijishikilia chini ya maporomoko hayo na kusonga polepole na ‘kwa nguvu huku na huku’ wakipanda juu ya mwamba huo wenye urefu wa meta 15 na kupumzika kila baada ya hatua chache. Ripoti hiyo yasema hivi: “Wanasayansi hao wanaonelea kwamba tabia hiyo husaidia kudumisha samaki hao katika miinuko iliyojitenga.” Hata hivyo, mbali na samaki aina ya darter, samaki wengine wanaweza pia kupanda miamba; kama vile samaki aina ya loach wa Asia na goby wa kitropiki.
Mnyanya Unaoweza Kuhimili Chumvi
“Watafiti wamevumbua mnyanya wa kwanza duniani ambao unaweza kukua katika maji ya chumvi kwa kubadili chembe zake za urithi—uvumbuzi ambao unaweza kusuluhisha mojawapo ya matatizo tata zaidi katika kilimo,” lasema gazeti washingtonpost.com. Aina hiyo ya mnyanya imezalishwa kutokana na chembe ya urithi ya mmea unaohusiana na kabichi. Chembe iliyoongezwa huwezesha mnyanya huo ‘kufyonza chumvi katika sehemu zake za kuhifadhi chakula, na hilo huruhusu mmea huo kunawiri katika eneo ambalo linaruhusu mimea michache tu kukua.’ Kulingana na ripoti hiyo, “mnyanya huo uliotokezwa kwa kubadili chembe za urithi unaweza kukua katika udongo ambao umenyunyiziwa maji yaliyo na kiasi cha chumvi ambacho ni mara 50 hivi kuliko kawaida.” Inatumainiwa kwamba mimea kama hiyo inayoweza kuhimili chumvi itaweza kukua katika maeneo yasiyo na mvua nyingi. Ripoti hiyo yaongeza kuwa “umuhimu mwingine wa mnyanya huo uliobadilishwa maumbile (au mimea mingine ambayo imebadilishwa maumbile ili kuhimili chumvi) ni kuboresha udongo uliojaa chumvi kwa kulowesha chumvi hiyo.”
Watoto Wanaotaka Kujiua
Gazeti la The Guardian la London laripoti kwamba simu zilizopigwa na watoto waliotaka kujiua kwa shirika la Uingereza la kusaidia watoto ChildLine, ziliongezeka mara mbili kutoka 346 katika 1990/91 hadi 701 katika 1998/99. “Kuvunjika moyo kupita kiasi kulisababishwa na uchokozi, kusumbuliwa kingono na kimwili, kufiwa na kufadhaika wakati wa mtihani.” Kulingana na shirika hilo, “maoni ya watu wengi kwamba wale wanaojaribu kujiua hufanya hivyo ili tu kujionyesha, ni hatari. Si kweli kwamba wale wanaosema watajiua hawafanyi hivyo. Watoto wengi waliopiga simu kwa shirika la ChildLine walisema msononeko wao uliongezeka wakati wazazi au walezi wao walipoonyesha kutojali.” Baada ya kujaribu kujiua mara ya kwanza, “familia hutulia sana kwa sababu mwana wao amenusurika . . . hivi kwamba wao huwazia kuwa tatizo limekwisha. Halafu, kwa kuhuzunisha, jambo hilo hufanyika tena,” miezi michache tu baada ya jaribio la kwanza. Ingawa idadi ya wasichana waliojaribu kujiua ilikuwa mara nne zaidi ya ile ya wavulana, uwezekano wa wavulana kufaulu kujiua ulikuwa mkubwa zaidi. Watoto wengi waliopiga simu wakitaka kujiua walikuwa kati ya umri wa miaka 13 hadi 18, na wachanga zaidi walikuwa na miaka 6 tu.
Kifaa cha Kunasa Mbu
Kiwanda kimoja huko Singapore kinatengeneza kifaa cha kuua mbu bila kutumia dawa ya kuua wadudu. Gazeti la The Economist la London laripoti kwamba kifaa hicho kimetengenezwa kwa sanduku jeusi la plastiki lenye urefu wa sentimeta 38 “linalotoa joto na gesi ya kaboni dayoksaidi kama mwanadamu.” Mbu hutambua windo lake kwa joto na kwa kaboni dayoksaidi inayomtoka binadamu, na kifaa hicho “humkenga mbu kwamba anakaribia kupata mlo.” Baada ya kupashwa moto kwa umeme, sanduku hilo hutoa kaboni dayoksaidi kutoka kwenye kidude kidogo. Mianga inayometameta huvuta mbu ndani ya shimo lililo katika sanduku, na feni husukuma mbu katika kidimbwi ambamo yeye hufa maji. Kifaa hicho chaweza kunasa mbu 1,200 kwa usiku mmoja na chaweza pia kurekebishwa ili kulenga mbu wa usiku aina ya Anopheles anayeambukiza malaria au yule wa mchana aitwaye Aedes anayebeba viini vya homa ya manjano na kidingapopo. Faida nyingine ni kwamba hakiui wadudu wasiodhuru kama vipepeo.
Wanaume Wanahimizwa Kula Samaki
Wachunguzi katika Taasisi ya Karolinska huko Stockholm wanasema kwamba uwezekano wa kupata kansa ya kibofu kwa wanaume wasiokula samaki sana ni mara mbili au tatu kuliko ule wa wanaume walao kiasi kikubwa sana cha samaki wenye mafuta kama vile salmoni, heringi na kibua. Uchunguzi huo wa miaka 30 uliofanywa kuhusu wanaume 6,272 ulizingatia pia mambo mengine yanayohatarisha, kama vile kuvuta sigara. Wachunguzi walifikia mkataa kwamba “inaonekana kwamba aina ya mafuta omega-3 [ambayo hupatikana hasa katika samaki wenye mafuta] huzuia kuenea kwa kansa ya kibofu.” Ripoti hiyo pia ilisema kwamba omega-3 “hupunguza pia hatari ya mshtuko wa moyo.” Hivyo, wataalamu wanawashauri watu kula samaki “mara moja au mbili kila juma.”
Makapi ya Mchele Yanaokoa Miti
Gazeti la El Comercio la Peru lasema kwamba makapi ya mchele, yanayotumiwa kama fueli katika viwanda vya kutengeneza matofali, yanasaidia kuzuia mikaruba mingi ambayo iko katika hatari ya kutoweka isikatwe kwa matumizi ya kuni. Makapi hayo, yanayotupwa kutoka mashambani, yalitumiwa na watengenezaji wa matofali 21 na yakasaidia kupunguza kiwango cha gesi ya kaboni dayoksaidi. Kwa kuongezea hilo kukandika kuta za joko kwa mchanganyiko wa mchanga, udongo wa mfinyanzi, na molasi ili kuzuia kupotea kwa joto, kumeboresha utendaji wa joko kwa asilimia 15. Ili kuliongezea nguvu tofali, majaribio yanafanywa kutia majivu ya makapi ya mchele katika mchanganyiko wa tofali. Gazeti la El Comercio lasema hivi: ‘Utumiaji wa makapi ya mchele pia hupunguza uchafuzi na matatizo ya kupata mahali pa kuweka takataka za viwanda.’
Afya ya Akili na Watoto
“Takwimu zinaonyesha kwamba mtoto mmoja kati ya watano atapata ugonjwa wa akili kabla ya kufikia umri wa miaka 11,” lasema gazeti The Gazette la Montreal, Kanada. “Afya bora ya akili humaanisha kusawazisha pande zote za maisha kijamii, kimwili, kiroho, na kihisia.” Kulingana na Sandy Bray, mratibu wa elimu ya kijamii katika Shirika la Kanada la Afya ya Akili, tunapaswa kuhangaikia afya yetu ya akili kama vile sisi hushughulika na afya ya kimwili. Bray anataarifu hivi: “Tukiendelea kupuuza afya ya akili itakuwa rahisi kushuka moyo, kusumbuka na kufadhaika sana.” Wazazi wanatiwa moyo kushughulikia zaidi afya ya akili ya watoto wao, kwa kupanga kuwa pamoja na familia zao na pia kula pamoja. Madokezo mengine ya kusaidia wote kudumisha afya bora ya akili yatia ndani kupata usingizi wa kutosha, kula vizuri, kufanya mazoezi, kuwa na wakati wa kufanya mambo upendayo, kuwa pamoja na marafiki, kucheka, kujitolea, kutoa na kukubali pongezi, kuwasikiliza wengine kwa makini, na kutojilaumu kupita kiasi unapokosea.
Hasara Kubwa ya Uvuvi wa Kupita Kiasi
Gazeti la The Times la London lataarifu hivi: “Uchunguzi mmoja umeonyesha kwamba mwanadamu amesababisha uharibifu katika maji kwa kiwango ambacho hakikufikiriwa awali kwa sababu maelfu ya jamii za viumbe zimeangamia kutokana na uvuvi wa kupita kiasi.” Kulingana na uchunguzi huo, ‘wanadamu wamevua viumbe wakubwa wa majini na hivyo kuharibu chakula cha wanyama na kubadili kabisa mazingira wanayotegemea.’ Ripoti hiyo inataja kuwa wakati Nahodha John Smith aliposafiri kwa meli katika Ghuba ya Chesapeake iliyo katika pwani ya mashariki ya Marekani katika mwaka wa 1607, mzinga ulioanguka kutoka kwa mashua “ulionekana wazi sana hata ulipokuwa zaidi ya meta tisa ndani ya maji.” Watafiti walisema kwamba maji hayo yalikuwa na uangavu hapo zamani kwa sababu “miamba mingi sana ilikuwa na chaza ambao walichuja maji katika ghuba hiyo kila baada ya siku tatu, na hivyo kudhibiti kiasi cha vijidudu na miani.” Wakati huo, “nyangumi wa manjano, pomboo, nguva, fisi-maji, kasa, mamba wa Marekani na sturgeon wakubwa walikuwa wengi” katika eneo hilo. Ghuba hiyo leo ina “jamii chache tu” za viumbe kati ya zile zilizokuwepo.