Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Matineja Walioshuka Moyo Nilifurahia sana kupokea toleo la Amkeni! lenye kichwa “Msaada kwa Matineja Walioshuka Moyo”! (Septemba 8, 2001) Nimeugua ugonjwa huo kwa miaka kadhaa. Asanteni kwa habari hiyo iliyonisaidia katika kipindi cha taabu.
L. D., Ufaransa
Mimi ni mwuguzi wa watoto. Watu wengi hawajui kwamba ugonjwa huo unaathiri watu wengi sana, lakini nyinyi mnatambua jambo hilo. Nimeagiza nakala 100 za gazeti hilo. Ninataka kuyapeleka kwa madaktari wote wa watoto, na watu wote wanaoshughulikia wagonjwa wa akili katika eneo hili.
B. P., Marekani
Nina baadhi ya watu wa ukoo ambao wameshuka moyo au wanatatizwa na hisia zinazobadilika-badilika. Mtu anaweza kusaidiwa kujistahi tena iwapo hali yake itaonwa kuwa ugonjwa badala ya udhaifu. Mapendekezo mliyotoa yatatusaidia sote kuwa wenye huruma na kuwasaidia walioshuka moyo.
C. M., Kanada
Mara tu nilipopata gazeti hilo nilianza kulisoma. Nililia kwa furaha nilipoona kwamba mnawajali na kuwapenda vijana na kwamba mlitumia kurasa 12 kuzungumzia habari hiyo. Asanteni sana!
M. M., Austria
Makala hiyo ilinisaidia kutulia. Pia, ilinisaidia kutambua kwamba si mimi tu ninayeugua ugonjwa huo. Ninamwomba Yehova awafariji na kuwasaidia wote walioshuka moyo.
Y. T., Japani
Nitaweka nakala kadhaa za toleo hilo nyumbani sikuzote. Vijana wetu wanahitaji habari hizi hasa, na ninaamini kwamba litawasaidia wengi wao na wazazi wao kukabiliana vyema na ugonjwa huo. Labda gazeti hilo litaokoa maisha.
R. F., Marekani
Nilifarijika kujua kwamba uchungu huo wa moyoni hautokani na udhaifu wa kiroho. Niliacha kuwa na majonzi na nikalia niliposoma kwamba “BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo.”—Zaburi 34:18.
A. I., Japani
Nina umri wa miaka 16, na nimekuwa nikishuka moyo mara kwa mara kwa miaka kadhaa. Gazeti hilo lilinisaidia sana! Mfululizo huo ulinipa ushauri niliohitaji.
L. B., Australia
Nilipokuwa kijana nilishuka moyo, lakini sikuwaambia wazazi wangu wala mtu mwingine kwamba nilitaka kujiua. Hapo nilikosea sana. Ni muhimu kuomba msaada unaposhuka moyo. Asanteni kwa kuwajali na kuwahangaikia vijana.
S.G.C., Marekani
Chuma cha Pua Ninafanya kazi katika kiwanda cha chuma cha pua, na nilimtolea mkurugenzi wa tekinolojia makala ya “Hutumiwa Kutengeneza Vitu Vigumu na Vyepesi” (Septemba 8, 2001). Alisema kwamba makala hiyo inazungumzia habari ngumu kwa njia inayoeleweka na kwa usahihi bila kutumia maneno mengi magumu. Makala kama hiyo hutuwezesha kuwafanya wengine waanze kusoma Amkeni!
G. B., Italia
Kwa sababu nilimaliza masomo ya ukaguzi wa metali hivi majuzi, sikuwa na hamu nyingi ya kusoma makala hiyo kuhusu kutengeneza chuma cha pua. Lakini nilivutiwa sana na jinsi mlivyoeleza habari hiyo ngumu.
M. F., Ujerumani