Hebu Tujaribu Kuandika Hankul!
Hebu Tujaribu Kuandika Hankul!
NA MWANDISHI WA AMKENI! JAMHURI YA KOREA
KILA MFUMO WA KUANDIKA UNA HISTORIA YAKE, NA MIFUMO MINGI KAMA HIYO ILIANZA ZAMANI SANA. HATA HIVYO, KUNA MFUMO MMOJA WA MAANDISHI ULIOANZISHWA MIAKA 500 TU ILIYOPITA NA ULIBUNIWA ILI MTU AJIFUNZE KUUANDIKA KWA ASUBUHI MOJA! HUO NI MFUMO WA KUANDIKA WA KOREA UNAOITWA HANKUL, AU HANGUL. JINSI ULIVYOANZISHWA NA KUTUMIWA NI JAMBO LENYE KUSISIMUA SANA.
KABLA ya maandishi ya Hankul kuanzishwa, Kikorea hakikuwa na mfumo wa kuandika. Kwa zaidi ya miaka elfu moja, Wakorea wenye elimu waliandika Kikorea wakitumia herufi za Kichina. Hata hivyo, kwa miaka mingi jitihada zilifanywa ili kubuni mfumo bora wa maandishi. Lakini kwa kuwa mifumo yote iliyobuniwa ilitumia herufi za Kichina, ni watu wenye elimu tu ndio wangeweza kutumia maandishi hayo.
Alfabeti Iliamriwa na Mfalme
Katika karne ya 15 W.K., Mfalme Sejong wa ukoo wa wafalme wa Yi nchini Korea, alianza kufikiria kuhusu matatizo ya raia wake wasiojua kusoma au kuandika. Wengi wao hawakuwa na njia nyingine ya kuwasilisha malalamishi yao kwa wenye mamlaka, ila tu kwa kusema. Tatizo hilo lilimtatanisha Mfalme Sejong, anayesemekana kuwa alipenda kuwasikiliza watu wa kawaida.
Kwa hiyo, Mfalme Sejong aliongoza kuanzishwa kwa alfabeti ambayo ilikuwa rahisi kujifunza na kutumia na wakati uleule iliyofaa mazungumzo ya watu wa Korea. Kukamilishwa kwa kazi hiyo kulitangazwa katika mwaka wa 1446. Mfalme Sejong alianza hotuba yake hivi: “Kwa kuwa herufi za Kichina ni za kigeni, haziwezi kueleza maana kwa usahihi katika Kikorea. Kwa hiyo, watu wengi wa kawaida hawawezi kueleza mawazo na hisia zao. Kwa sababu ninajali matatizo yao, nimebuni herufi 28. Ni rahisi sana kujifunza herufi hizo, na nina matumaini makubwa kwamba zitaboresha maisha ya watu wote.”
Kwa kusikitisha, wasomi fulani walipinga Hankul, kwa kuwa ilikuwa rahisi sana kujifunza mfumo huo wa maandishi! Waliuita Amkul, maana yake “herufi za wanawake.” Waliyadharau maandishi hayo ambayo hata wanawake wangeweza kuyajua. Wakati huo wanawake hawakufundishwa kusoma katika shule. Wakorea walioishi maisha ya hali ya juu waliendelea kuwa na maoni hayo mabaya kuelekea Hankul kwa muda fulani. Hata zaidi ya miaka 400 ilipita kabla ya serikali ya Korea kuruhusu Hankul itumiwe katika hati za serikali.
Hankul na Biblia
Biblia ilikuwa na sehemu muhimu katika historia ya Hankul. Ijapokuwa vitabu vingi vya kidini vya Kikorea ambavyo viliandikwa katika herufi za *
Kichina vililetwa nchini Korea, mishonari hawakuleta Biblia za Kichina, hata ingawa zilikuwapo. Hata hivyo, mnamo mwaka wa 1887, Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo (Agano Jipya) yalitafsiriwa katika Kikorea na kuchapishwa katika herufi za Hankul huko Mukden, China.Mwishowe, kukatokea Biblia ya Kikorea ambayo ingeweza kusomwa na karibu kila mtu—hata na wanawake na watoto ambao hawakuwahi kujifunza herufi za Kichina. Leo kuna angalau tafsiri nane za Biblia zilizoandikwa katika herufi za kisasa za Hankul, kutia ndani Tafsiri ya Ulimwengu Mpya ya Maandiko Matakatifu.
Ni Rahisi Kujifunza
Msomi mmoja aliyesaidia kubuni herufi za Kikorea alisema hivi kuhusu Hankul: “Mtu mwerevu anaweza kujifunza herufi hizo kwa asubuhi moja na hata asiye mwerevu anaweza kuzijua kwa siku kumi.” Hata baadhi ya wapinzani wake wa mapema waliziita herufi hizo kwa madharau eti Achimgul, yaani, “herufi za asubuhi.” Waliona herufi za Hankul kuwa rahisi sana kwa sababu mtu angeweza kuzijua kwa asubuhi moja!
Vyovyote vile, urahisi wa kujifunza Hankul umemaliza kwa kadiri kubwa sana tatizo la kutojua kusoma na kuandika nchini Korea. Kwa hakika, kufikia wakati wanapoingia shuleni, watoto wengi huwa tayari wamejua herufi hizo vizuri. Zaidi ya hilo, kuandika herufi za Hankul kwa usahihi si vigumu kwa sababu zinaandikwa kama vile Wakorea wanavyotamka maneno.
Maandishi ya Hankul yanaweza kutumiwa pia kuandika maneno yasiyo ya Kikorea. Je ungependa kujaribu? Chati zifuatazo zinaweza kukusaidia angalau kuandika jina lako kwa kutumia herufi za Hankul, ingawa hazionyeshi mambo yote yanayohusika. Kwa njia hiyo unaweza kujionea jinsi yale maandishi unayoweza kujifunza kwa asubuhi moja yanavyoweza kutumiwa kwa njia nyingi!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 10 Biblia ya kwanza nzima ya Kikorea ilichapishwa mnamo mwaka wa 1911.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
KONSONANTI NA VOKALI ZA HANKUL
KONSONANTI :
ㄱ (g,k)
ㄴ (n)
ㄷ (d,t)
ㄹ (r,l)
ㅁ (m)
ㅂ (b,p)
ㅅ (s)
ㅇ *
ㅈ (ch,j)
ㅊ (ch’)
ㅋ (k’)
ㅌ (t’)
ㅍ (p’)
ㅎ (h)
VOKALI:
ㅏ (ah)
ㅑ (yah)
ㅓ (ǒ)
ㅕ (yǒ)
ㅗ (o)
ㅛ (yo)
ㅜ (u)
ㅠ (yu)
ㅡ (ǔ)
ㅣ (i, as in “machine”)
MFANO WA MCHANGANYIKO WA VOKALI
ㅓ (ǒ) + ㅣ (i) = ㅔ (e)
* Konsonanti ㅇ haitamkwi isipokuwa iwe ndiyo konsonanti ya mwisho, ambapo inatamkwa kama “ng.”
Vokali ǒ, yǒ, na ǔ hutamkwa kwa tabasamu ndogo na mdomo ukiwa umefungwa; o, yo, u, na yu hutamkwa mdomo ukiwa umeviringwa kando. Konsonanti ch,’ k,’ t,’ na p’ huunganishwa na sauti ya h.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
KUANDIKA MANENO YA KIKOREA
Silabi zote za Kikorea zina sehemu mbili au tatu: sauti ya kwanza, sauti ya kati (vokali moja au kadhaa) na, mara nyingi sauti ya kumalizia. Maneno huundwa kwa silabi moja au zaidi. Kila silabi huandikwa ndani ya sanduku la kuwaziwa, kama vile imeonyeshwa hapa chini. Sauti ya kwanza (konsonanti au ㅇ isiyotamkwa) huandikwa upande wa juu ama juu-kushoto. Iwapo vokali ya kati imesimama wima, hiyo huandikwa kwenye mkono wa kulia wa sauti ya kwanza, na vokali zilizolala huandikwa chini yake. Herufi zinaweza kuandikwa zikiwa mbilimbili ili kuongeza mkazo, na vokali nyingi zaweza kuunganishwa na kuandikwa zikifuatana. Iwapo silabi ina konsonanti ya kumalizia, hiyo huandikwa katika sehemu ya chini. Kwa njia hii, maelfu ya silabi mbalimbali zinaweza kuandikwa kwa herufi za Hankul.
MIFANO:
ㅅ (s) + ㅗ (o) = 소 (so) ng’ombe
ㅅ (s) + ㅏ (a) + ㅇ (ng) = 상 (sang) zawadi
ㄱ (k) + ㅗ (o) + ㅁ (m) = 곰 (kom) dubu
ㅁ (m) + ㅗ (o) + ㄱ (k) = 목 (mok) shingo
ㅅ (s) + ㅏ (a),
ㄹ (r) + ㅏ (a) + ㅇ (ng) = 사랑 (sa-rang) upendo
[Sanduku/Mchoro katika ukurasa wa 14]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Alfabeti ya Korea
Katika siku za Mfalme Sejong, alfabeti ya Hankul ilikuwa na herufi 28, na herufi 24 bado zinatumiwa. Kati ya herufi hizo, 14 ni konsonanti na 10 ni vokali. Konsonanti tano za msingi zinafanana na sehemu za mdomo na koo zinazotumiwa kuzitamka: ㄱ (g, k), ulimi uliojipinda ukiwa umegusa upande wa nyuma wa sehemu ya juu ya mdomo; ㄴ (n), ncha ya ulimi uliojipinda kuelekea upande wa mbele wa sehemu ya juu ya mdomo; ㅁ (m), mdomo ukionekana kutoka upande wa mbele; ㅅ (s) meno; ㅇ (ng), koo iliyofunguka. Mistari huongezwa kwenye konsonanti hizo za msingi ili kuwakilisha konsonanti nyingine zinazohusiana nazo—zile ambazo hutamkwa mdomo ukiwa karibu na sehemu ileile.
Vokali huwakilisha anga lililo mviringo kwa kutumia alama ya kituo (•),* nchi iliyo tambarare kwa mstari uliolala (ㅡ), na kumwakilisha mwanamume anayesimama kwa kutumia mstari wima (ㅣ). Hizo ziliwakilisha vokali zilizotamkwa wakati ulimi ulipowekwa upande wa mbele, katikati, na nyuma.
*Herufi hii haitumiki katika maandishi ya Hankul ya kisasa.
[Mchoro]
ㄱ
ㄴ
ㅁ
ㅅ
ㅇ
[Picha katika ukurasa wa 13]
Mfalme Sejong