Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Utumwa Uovu Unaoendelea

Utumwa Uovu Unaoendelea

Utumwa Uovu Unaoendelea

JE, UTUMWA ulikwisha? Watu wengi wangependa kufikiri hivyo. Neno utumwa huleta mawazo yenye kuogopesha, ya ukatili na uonevu. Hata hivyo, wengi huonelea kwamba mambo hayo yalitukia zamani tu. Kwa mfano, wengine hufikiria juu ya meli za mbao kuukuu zilizowasafirisha watumwa katika karne zilizopita, huku zikiwa zimejaa kabisa watu wenye hofu waliosongamana katika uchafu mwingi.

Ni kweli kwamba siku hizi hakuna meli za kuwasafirisha watumwa, na mikataba ya kimataifa imepiga marufuku utumwa wa aina hiyo. Hata hivyo, utumwa haujakwisha. Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa, ambalo linatetea haki za binadamu, linakadiria kwamba watu milioni 200 bado ni watumwa kwa njia fulani. Wanafanya kazi katika mazingira ambayo huenda ni mabaya zaidi kuliko yale ya watumwa wa karne zilizopita. Kwa kweli, wachanganuzi fulani wanasema kwamba “kuna watumwa wengi leo kuliko wakati mwingine wowote.”

Masimulizi kuhusu watumwa hao wa leo yanahuzunisha sana. Kila siku, Kanji, * aliye na umri wa miaka kumi tu, huchunga ng’ombe za mabwana wake wakali ambao humchapa. Anasema hivi: ‘Nikibahatika, mimi hupata mkate mdogo uliokauka, la sivyo mimi hushinda na njaa siku nzima. Sijawahi kulipwa mshahara kwa sababu mimi ni mtumwa na mali yao. Watoto wa rika langu wanacheza pamoja. Ni afadhali nife kuliko kuwa na maisha haya ya taabu.’

Kama Kanji, watumwa wengi leo ni watoto au wanawake. Wao hulazimishwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza mikeka, kujenga barabara, kukata miwa, au hata kuwa makahaba. Na wanaweza kuuzwa kwa dola 10 tu za Marekani. Hata wazazi wengine huwauza watoto wao utumwani ili walipe madeni makubwa.

Je, ripoti hizo zinakuudhi? Basi, si wewe tu unayehisi hivyo. Katika kitabu chake Disposable People, mwandishi Kevin Bales anasema hivi: “Utumwa ni jambo linaloudhi. Utumwa sio tu kumlazimisha mtu kufanya kazi; bali ni kumnyang’anya mtu maisha yake.” Kwa sababu ya ukatili ambao mwanadamu anamtendea mwenzake, je, twaweza kutazamia kwamba siku moja utumwa utakwisha? Swali hilo linakuhusu wewe binafsi.

Kama vile tutakavyoona, kuna aina nyingi za utumwa, na nyingine zinaathiri watu wote walio hai. Kwa hiyo, sote tunahitaji kujua ikiwa wanadamu watapata uhuru wa kweli siku moja. Lakini kwanza, hebu tuchunguze kwa ufupi historia ya biashara ya watumwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Si jina lake halisi.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Kwa muda mrefu, wanawake na watoto maskini wamekuwa watumwa

[Hisani]

Picha ya juu: UN PHOTO 148000/Jean Pierre Laffont

U.S. National Archives photo