Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kudanganya Ili Kupata Kazi
“Mtu mmoja kati ya watu wanne hudanganya anapojaza fomu ya maombi ya kazi,” laripoti gazeti la Financial Times la London. Kwa muda wa miezi 12, kampuni ya kuchunguza usalama wa kifedha ya Control Risks Group ilifanya uchunguzi kuhusu watu 10,435 waliojaza fomu za maombi ya kazi katika makampuni ya kutoa huduma za kifedha na tekinolojia ya kompyuta na “kugundua kwamba watu walioomba kazi katika nyadhifa mbalimbali walidanganya,” linasema gazeti hilo. “Karibu asilimia 34 ya maombi yote hayakuonyesha kikweli kazi ambazo watu hao walikuwa wakifanya hapo awali, na wakati huohuo asilimia 32 ya watu hao walitia chumvi au kudanganya kuhusu kiwango chao cha elimu. Asilimia 19 walijaribu kuficha kwamba wana madeni au kwamba wamefilisika, na asilimia 11 walikataa kujitambulisha kikamili.” Wale walioishi katika nchi za kigeni walielekea zaidi kudanganya kuhusu madeni yao, labda wakifikiri hawangeweza kujulikana, na wanaume “ndio waliodanganya zaidi kuliko wanawake.” Tim Nicholson, wa Muungano wa Uajiri na Kazi, anathibitisha matokeo ya uchunguzi huo na anaongeza hivi: “Iwapo waajiri wanaamini yale ambayo yameandikwa kwenye fomu za maombi ya kazi, basi hawafanyi kazi yao vizuri.”
Tembo Wanaopenda Mafuta
Tembo katika eneo la Digboi, kaskazini-mashariki mwa India wanapenda mafuta sana. “Tembo hao huzunguka-zunguka karibu na mashimo ya kuchimba mafuta, wakifungua vali muhimu za mabomba yanayosafirisha mafuta hadi mahali yanaposafishwa,”anasema Ramen Chakravarty, mhandisi-mkuu katika kampuni ya Oil India Limited. “Inaelekea tembo hao wanapenda kusikia sauti ya vali hizo wakati zinapofunguliwa, hasa zile zinazopeleka mvuke unaozuia mafuta yasiyosafishwa yasiwe mafuta ya taa.” Tembo hawapendezwi tu na ‘sauti ya mafuta yanayotiririka kasi’ bali yaelekea wanapendezwa pia na visima vya mafuta kwa sababu ya “udongo na maji yanayotoka pamoja na yale mafuta yasiyosafishwa,” laripoti gazeti la Indian Express. “Maji hayo yana chumvi na tembo wanayapenda.” Kwa kupendeza, ni tembo mmoja aliyefanya mafuta yavumbuliwe katika eneo hilo. Tembo huyo alikuwa tu amerejea kutoka safari ya kubeba vyuma ambavyo vingetumiwa kutengeneza reli ya kwanza katika eneo hilo, wakati maofisa Waingereza walipoona mafuta miguuni mwake. Walipofuata nyayo zake walifika kwenye shimo lililobubujika mafuta. Hivyo, kisima cha kwanza cha mafuta huko Asia kikafunguliwa mnamo mwaka wa 1889.
Kuendesha Gari na Uchovu
“Uchovu, hasa unapochanganywa na kileo, husababisha hatari kubwa ya magari kugongana, na watu kupoteza uhai au kuumia vibaya,” laripoti gazeti la British Medical Journal. Watafiti huko Bordeaux, Ufaransa, waligundua kuwa uchovu ulichangia asilimia 20 ya aksidenti katika barabara kuu. Hata kukiwa na hali nzuri, bado asilimia 10 ya aksidenti zilizohusisha gari moja zilisababishwa kwa njia fulani na uchovu. Kulingana na Profesa Jim Horne, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Usingizi katika Chuo Kikuu cha Loughborough, Uingereza, alasiri ni mojawapo ya nyakati hatari zaidi kwa madereva. Yeye anasema: “Tumeumbwa na uhitaji wa kuwa na vipindi viwili vya kulala, kimoja usiku na kingine alasiri, kati ya saa 8 na saa 10 alasiri.” Dereva anapaswa kufanya nini anaposinzia? Anapaswa kuacha kuendesha gari kwa muda mfupi. Horne anasema: “Kufungua kioo au kufungulia redio hakumalizi tatizo hilo kabisa. Jambo linalofaa zaidi ni kuegesha gari mahali palipo salama na kulala kwa dakika 15 hadi 20.” Tatizo ni kwamba madereva wengi huendelea kuendesha gari hata wanapopatwa na usingizi. Gazeti la The Sunday Times la London linasema hivi: “Ukianza kupiga miayo, kufumba-fumba macho au kushindwa kukaza fikira unapoendesha gari, kumbuka kwamba hizo ni ishara ambazo unapaswa kuzingatia, la sivyo unaweza kusababisha kifo.
Mauzo ya Bunduki Yaongezeka Marekani
“Mauzo ya bunduki na risasi kote nchini yameongezeka sana tangu Sept. 11, kwani Wamarekani wengi wamechukua hatua ambayo wengi wanaona kuwa ya kibinafsi zaidi ya kujihisi salama, yaani, kujihami,” lasema gazeti The New York Times. “Watu wengi wanaotaka kujihami wananunua bunduki kwa mara ya kwanza.” Makampuni fulani ya kutengeneza bunduki yametumia msiba huo kuvutia wanunuzi wapya kwa kutumia maneno na picha za kizalendo. Hata hivyo, maafisa wengi wamehofia kuenea huko kwa silaha hatari. William B. Berger, ambaye ndiye mkuu wa polisi huko North Miami Beach, anasema hivi: “Sisi huhofia kiasi kikubwa cha bunduki zilizopo na zinazoweza kupatikana kwa urahisi na mtu yeyote. Jambo hilo linafanya iwe vigumu kwa wale wanaotekeleza sheria kudumisha usalama.” Takwimu zinaonyesha kwamba bunduki zinazonunuliwa na wananchi wanaotii sheria wakati mwingine hutumiwa na wahalifu. Mashirika yanayotetea kupunguzwa kwa idadi ya bunduki yanawasihi watu wafikiri kabla ya kuzinunua.
Wagonjwa wa Akili “Wameongezeka Sana”
“Wagonjwa wa akili wameongezeka sana ulimwenguni pote,” anasema Dakt. Gro Harlem Brundtland, mkurugenzi-mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Ripoti ya hivi majuzi ya WHO ilionyesha kwamba magonjwa ya akili ni “mojawapo ya visababishi vikuu vya kuzorota kwa afya na kulemaa kote ulimwenguni.” Ripoti hiyo inasema kwamba watu wapatao milioni 450 duniani sasa wanaugua magonjwa ya akili au ya mfumo wa neva. Ingawa magonjwa mengi ya mfumo wa neva yanaweza kutibiwa, karibu thuluthi mbili ya wale wanaougua magonjwa ya akili yanayojulikana hawatafuti matibabu kutoka kwa wataalamu kwa sababu ya kubaguliwa, kuona aibu, kukosa pesa, ama kukosa huduma za afya.
Watu Wazima Wanaokufa Kutokana na Tetekuwanga
“Tetekuwanga, mojawapo ya magonjwa yanayoambukiza hasa watoto, sasa unaua idadi inayoongezeka ya watu wazima,” lasema gazeti la Independent la London. Takwimu zilizochapishwa katika kichapo cha British Medical Journal zinaonyesha kwamba mapema katika miaka ya 1970, asilimia 48 ya watu wazima walikufa kutokana na tetekuwanga, na kufikia mwaka wa 2001 idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi kufikia asilimia 81. Profesa Norman Noah, wa Taasisi ya London ya Usafi wa Kiafya na Tiba ya Kitropiki, anaonya hivi: “Uchunguzi huo unathibitisha kwamba ugonjwa wa tetekuwanga unaua watu wengi wazima . . . Huenda ikawa takwimu zetu za vifo 25 kila mwaka [katika Uingereza na Wales] ni za chini sana. . . . Watu wazima wakiugua tetekuwanga wanapaswa kujua kwamba ugonjwa wao ni tofauti na ule wa watoto. Watu wazima wamo katika hatari kubwa zaidi na wanahitaji kumwona daktari bila kukawia.” Wanaume kati ya umri wa miaka 15 hadi 44 wamo katika hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na ugonjwa huo.
Je, Waumini Wameongezeka Huko Slovakia?
Sensa ya mwaka 2001 huko Slovakia ilionyesha kwamba asilimia 84 ya Waslovaki sasa wanadai kuwa waumini wa dini fulani. Kulingana na mwanasosiolojia Ján Bunčák, jambo hilo linaonyesha kwamba “wanataka sana kukubaliwa na jamii.” Ingawa dini ilipingwa wakati wa Ukomunisti, sasa kufuata dini fulani kunaonwa kuwa jambo “linalofaa” na la “kawaida.” Hata hivyo, Bunčák anasema: “Wengi wao hawaamini kamwe kwamba kuna Mungu.” Akieleza kuhusu hali ya Ulaya kwa ujumla, yeye anaongeza hivi: “Watu wengi wanadai kuwa wafuasi wa dini fulani. . . . Ingawa wanadai hivyo, hawataki dini iingilie sana maisha yao.”
Watu Bilioni Nne Wenye Njaa Kufikia Mwaka wa 2050
Ongezeko kubwa la idadi ya watu katika nchi zinazoendelea linatazamiwa kuongeza idadi ya watu duniani hadi bilioni 9.3 kufikia mwaka wa 2050, kulingana na ripoti ya kila mwaka ya Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa. Inakadiriwa kuwa bilioni 4.2 kati yao watakuwa katika mataifa ambayo hayawezi kupata chakula na maji ya kutosha. Idadi hiyo ni mara mbili ya watu ambao tayari hawana chakula cha kutosha. “Ripoti hiyo inaonyesha kwamba umaskini na kuongezeka haraka kwa idadi ya watu ni mambo mawili hatari,” akaeleza Thoraya Obaid, mkurugenzi-mkuu wa hazina hiyo. “Watu maskini hutegemea sana mali za asili kama vile shamba, mbao na maji, na hivyo huathiriwa vibaya na uharibifu wa mazingira. . . . Wakati wengi wetu tunapotumia mali za asili vibaya, kuna wengine ambao hawawezi kujimudu maishani.”
Kwa Nini Wanaume Hufa Mapema?
“Maisha ya mwanamume ni yenye taabu: wao huugua na kufa mapema.” Hali hiyo ya kusikitisha ilielezwa na watayarishaji wa Mkutano wa kwanza wa Ulimwengu Kuhusu Afya ya Wanaume, uliofanywa Vienna, Austria. Kulingana na gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung, washiriki walishangaa kujua kwamba, kwa wastani, wanaume hufa miaka mitano mapema kuliko wanawake. Kwa nini wanaume hufa mapema? Sababu moja ni kwamba huenda wakavuta sigara au kunywa kileo kupita kiasi. Sababu nyingine ni kula kupita kiasi na kutofanya mazoezi. Inasemekana asilimia 70 ya wanaume wenye umri wa makamo ni wazito kupita kiasi. Zaidi ya hilo, wengi huathiriwa vibaya na mfadhaiko unaosababishwa na kujaribu kusawazisha madaraka ya kazi na jamaa. Wanaume pia huelekea kutomwona daktari wanapokuwa wagonjwa au huenda wasitafute kinga kwa ajili ya magonjwa. Akimalizia, Siegfried Meryn, mmoja wa watayarishaji wa mkutano huo alisema: “Katika mambo ya afya, wanaume kwa kweli wamo katika hali mbaya.”