Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kunaswa Katika Tone la Manjano

Kunaswa Katika Tone la Manjano

Kunaswa Katika Tone la Manjano

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA DOMINIKA

CHUNGU anapanda shina la mti mbiombio pasipo kujua kwamba kuna hatari mbele yake. Kwa ghafula, mguu wake mmoja unakwama, kisha ule mwingine unakwama pia, halafu chungu huyo ananaswa katika utomvu wa mti huo ulio kama asali. Tone jingine linadondoka na kumfunika kabisa. Hawezi kutoroka. Mwishowe, utomvu huo wenye kunata ambao umemfunika chungu unaanguka chini. Chungu huyo aliyenaswa anapelekwa na maji ya mvua hadi mtoni, ambako anafunikwa na matope. Maelfu ya miaka baadaye, chungu huyo anapatikana tena akiwa amehifadhiwa vizuri katika lile tone la manjano. Utomvu huo umekauka na kuwa kaharabu—mojawapo ya vito vyenye thamani zaidi.

Ni mambo gani yanayojulikana kuhusu kaharabu? Je, tunaweza kujua mambo ya kale kwa kuchunguza kaharabu na wadudu waliomo ndani yake? Je, vitu hivyo vinaweza kusaidia kurudisha viumbe waliotokomea zamani?

Dhahabu ya Kaskazini

Kwa maelfu ya miaka, wanadamu wamestaajabia asili ya kaharabu na muundo wake maridadi wenye rangi ya manjano. Isitoshe, watu waliamini kwamba kaharabu ina uwezo wa kustaajabisha! Wapata mwaka wa 600 K.W.K., mwanasayansi Mgiriki aliyeitwa Thales alitambua kwamba kaharabu inaposuguliwa kwa nguo, inapata nguvu za kuvuta manyoya au vipande vidogo vya nyasi. ‘Uwezo huo wa kustaajabisha’ unaitwa umeme-tuli. Neno “umeme” katika lugha kadhaa limetokana na neno la Kigiriki la kaharabu—elektron. Zaidi ya miaka elfu mbili baadaye, daktari Mwingereza William Gilbert aligundua kwamba mbali na kaharabu kuna vitu vingine pia vinavyoweza kutokeza umeme-tuli.

Kati ya mwaka wa 54 W.K. na mwaka wa 60 W.K., Maliki Nero wa Roma alimtuma mwanajeshi mmoja kutafuta mahali ambapo kitu hicho chenye thamani kinapatikana. Mwanajeshi huyo alisafiri kaskazini, na kugundua mahali hapo—Pwani ya Baltiki—na akarudi na kilogramu nyingi za kaharabu. Huko Roma, kaharabu ilipendwa kwa sababu ya umaridadi wake na kwa kuwa ilidhaniwa kwamba ingeweza kumlinda mtu. Pia, ilitumiwa kutengeneza dawa mbalimbali, kutia ndani zile za kupaka. Mwanahistoria Mroma, Pliny, aliripoti kwamba kaharabu ilipendwa sana hivi kwamba sanamu ya kaharabu ilikuwa na thamani kubwa kuliko mtumwa mwenye afya!

Watu wa maeneo yaliyostaarabika mapema huko kaskazini mwa Ulaya walitumia kaharabu kununua chuma, shaba, na bidhaa nyingine kutoka maeneo ya kusini. Nyakati nyingine kaharabu iliitwa dhahabu ya kaskazini. Katika Zama za Kati, biashara ya kutengeneza na kuuza kaharabu huko Ulaya ilidhibitiwa na kikundi fulani cha mashujaa wa vita wa Ujerumani, ambao walikuwa wamerudi tu kutoka kwenye Vita ya Dini. Mtu yeyote aliyekusanya kaharabu bila idhini aliuawa.

Wakati huohuo, kwenye kisiwa cha Quisqueya huko Karibea, ambacho sasa ni Jamhuri ya Dominika na Haiti, Wahindi Wataino walikuwa pia wamegundua kaharabu. Columbus alipotembelea Quisqueya kwa mara ya kwanza mwaka wa 1492, alimpa kijana mmoja, ambaye alikuwa chifu wa kisiwa hicho, mkufu wenye shanga za kaharabu zenye kumetameta. Yasemekana kwamba Columbus alipigwa na bumbuazi alipopewa viatu vilivyorembwa kwa shanga za kaharabu!

Kaharabu Ni Nini?

Kaharabu ya Jamhuri ya Dominika ni utomvu uliokauka unaotoka kwenye mti mmoja wenye majani mapana, unaopatikana katika maeneo ya joto na ambao sasa umetoweka kabisa. Miti mingine ya aina hiyo, inayoitwa algarroba katika lugha ya wenyeji, bado inapatikana huko Karibea na pia katika Amerika ya Kati na ya Kusini. Hata hivyo, mti unaofanana zaidi na “mti wa kaharabu” wa Dominika unapatikana tu katika Afrika Mashariki. Kaharabu ya eneo la Baltiki huko Ulaya hutokana na msonobari.

Kaharabu hutengenezwaje? Kwanza, ganda la mti hupasuka tawi linapovunjika, shina linapokatwa, au mti huo unapovamiwa na mbawakavu wanaoharibu miti. Kisha utomvu wenye kunata hutiririka ili kuziba shimo hilo. Wadudu au viumbe wengine wadogo hunaswa na hatimaye hufunikwa kabisa na utomvu huo. Kwa kawaida utomvu wa mti huwa na maji na virutubisho, lakini utomvu huo wenye kunata una michanganyiko ya kemikali za tapeni, alkoholi, na esta. Kemikali hizo hukausha na kuua wadudu walionaswa na hata mimea. Kunapokuwa na mazingira yanayofaa, utomvu huo hukauka polepole na kufanyiza kaharabu, kisha huhifadhi vitu vilivyonaswa kwa maelfu ya miaka. Kwa hiyo, kaharabu ni utomvu wenye kunata wa miti ya kale.

Kupata Hazina ya Kale

Ijapokuwa kaharabu inapatikana kotekote ulimwenguni, ni maeneo 20 tu yaliyo na kaharabu ya kutosha kuchimbuliwa. Kwa sasa, kaharabu nyingi huchimbuliwa katika eneo la Baltiki la Ulaya Mashariki, katika Jamhuri ya Dominika, na katika sehemu fulani za Mexico.

Kuchimbua kaharabu ni kazi ngumu. Wanasayansi wengi wanaonelea kwamba ili utomvu uwe kaharabu, inapasa ufukiwe chini ya ardhi, kwa kawaida katika udongo wa kunata wenye unyevu au katika mchanga. Migodi mingi katika Jamhuri ya Dominika iko kwenye sehemu zenye milima-milima na misitu iliyo karibu na maeneo ya joto. Mtu anaweza kufikia sehemu hizo kwa kutembea au kwa kutumia punda huku akipitia vijia vilivyo kwenye miinuko mikali.

Migodi fulani ni mipana na ina kina kirefu. Lakini mingine ina vijia virefu vyembamba vya chini ya ardhi. Vijia vingine vina urefu wa meta 200. Kwa kuwa mashine za kuchimba na vilipukaji vinaweza kuharibu kaharabu, inawabidi wachimbaji wa migodi wapasue mawe magumu ya mchanga na udongo mzito wenye kunata kwa mkono, huku wakitumia patasi, sururu, na sepetu. Mara nyingi, mchimbaji hutumia mshumaa ili kuona.

Kito Kinachong’ara Chatokana na Jiwe Jepesi

Kaharabu ikifukuliwa, mchimbaji huipeleka kwenye mwangaza wa jua, huiosha, na kuondoa sehemu moja ya gamba lake. Kisha yeye hutumia mafuta kufanya sehemu hiyo iwe nyevu ili aweze kutazama ndani ya kaharabu hiyo. Anataka kuona vitu vilivyonaswa ndani—iwe ni wanyama wa kale, wadudu, au viumbe wengine ambao huenda wakawa wamenaswa katika kaharabu hiyo. Kati ya vipande 100 vya kaharabu ya Dominika, unaweza kumwona mdudu 1. Kwa upande mwingine, unaweza kumwona mdudu 1 tu kati ya vipande 1,000 vya kaharabu ya Baltiki. Sababu moja ni kwamba kwa kawaida huwezi kuona kilicho ndani ya kaharabu ya Baltiki, hali zaidi ya asilimia 90 ya kaharabu ya Dominika yaweza kuonekana ndani.

Kaharabu hupangwa kulingana na ukubwa, umbo, rangi, na kitu kilichonaswa ndani. Idadi kubwa ya vipande vya kaharabu vinavyofukuliwa kila juma huwa vidogo. Lakini vingine ni vikubwa. Kipande kimoja cha kaharabu ya Dominika kina uzito wa kilogramu 8 hivi! Vipande vidogo visivyokuwa na kitu hutumiwa kwa mapambo, na vipande vyenye thamani zaidi hutengwa kwa ajili ya wakusanyaji wa vito na kwa ajili ya majumba ya makumbusho.

Kwa kawaida kaharabu huwa na rangi ya manjano na ya dhahabu. Vipande vichache vya kaharabu ya bluu huchimbuliwa kila mwezi katika Jamhuri ya Dominika. Ni vigumu hata zaidi kupata kaharabu ya kijani. Inadhaniwa kwamba rangi hizo tofauti-tofauti hutokana na kemikali mbalimbali zilizo katika utomvu na madini yaliyo udongoni.

Kuona Msitu wa Kale Akilini

Kwa sababu ya sifa zake za kipekee, kaharabu na vitu vilivyonaswa ndani yake vimedumu kwa muda mrefu kuliko miti iliyotokeza kaharabu yenyewe. Viumbe na mimea mingi ya kale imegeuka kuwa miamba na madini, lakini sivyo ilivyo na wanyama na mimea walionaswa katika kaharabu. Iwapo kaharabu inaweza kuonekana ndani, viumbe walionaswa ndani wanaweza kuchunguzwa na kupigwa picha bila kuwaharibu. Hivyo, kuchunguza kaharabu ni njia bora ya kufahamu vitu vya kale kwa sababu ina habari kuhusu wadudu, wanyama wadogo, mimea, na jinsi hali ya hewa ilivyokuwa zamani sana.

Ni viumbe gani wenye thamani zaidi ambao wamepatikana katika kaharabu? Inategemea maoni ya mkusanyaji wa kaharabu. Wapenzi wa kaharabu wanasema kwamba nge, mijusi, na vyura ndio viumbe watatu wenye thamani zaidi ambao wanapatikana katika kaharabu. Kwa kuwa wao ni wakubwa na wenye nguvu kuliko wadudu wengi, wengi wao wangeweza kujinasua kwa urahisi kutoka kwenye utomvu. Kwa kawaida wale walionaswa walikuwa wadogo sana au labda walidhoofishwa na ugonjwa au kujeruhiwa na wanyama wenye kuwinda. Je, ni rahisi kupata viumbe hao watatu katika kaharabu? Si rahisi hata kidogo! Mkusanyaji mmoja anakadiria kwamba ni nge 30 hadi 40 tu, mijusi 10 hadi 20 tu, na vyura 9 ambao wamewahi kupatikana. Wale wanaopatikana wana thamani kubwa sana. Kipande kimoja cha kaharabu chenye chura mdogo kilipatikana mwaka wa 1997 na kina thamani ya zaidi ya dola 50,000 za Marekani.

Wanasayansi fulani husisimuliwa na vitu vingine vilivyonaswa. Kwa kuwa mara nyingi wadudu walinaswa kwa ghafula, vipande vingi vya kaharabu vina habari za kale. Inawezekana kupata habari kuhusu tabia za wadudu, kama vile wadudu wenye kuwinda na wale waliowindwa. Vipande fulani vilivyo na mayai, viluwiluwi, mayai ya buibui, au buibui wachanga huwawezesha wanasayansi kuchunguza hatua za ukuzi wa wadudu. Kipande kimoja cha kaharabu, kinachohifadhiwa katika jumba la makumbusho huko Stuttgart, Ujerumani, kina kikundi cha chungu 2,000.

Vivyo hivyo, habari kuhusu mimea ya misitu ya kale inaweza kupatikana kwa kuchunguza vitu vilivyonaswa ndani ya kaharabu. Inawezekana kutambua mimea na miti mingi ya kale kwa kuchunguza maua, viyoga, kuvumwani, majani, na mbegu zilizohifadhiwa katika kaharabu. Isitoshe, wanasayansi wana uhakika kwamba mitini ilikuwepo, hata ingawa hawajawahi kamwe kupata majani wala matawi yake. Kwa nini? Kwa sababu aina kadhaa za nyigu zimepatikana katika kaharabu—nyigu ambao huishi tu katika mitini. Kwa hiyo, ni jambo la akili kukata kauli kwamba mitini ilikuwepo msituni.

Kurudisha Viumbe Waliotokomea?

Miaka kadhaa iliyopita filamu moja ilionyesha kwamba wanyama wakubwa sana wa kale wangeweza kufanyizwa tena kwa kutumia DNA ya damu yao ambayo ilipatikana katika mbu waliokuwa ndani ya kaharabu. Wanasayansi wengi wanasema kwamba hilo haliwezekani. Viumbe wote wana chembe zinazoitwa DNA zinazoamua tabia wanazorithi. Kupitia majaribio ya kisayansi, sehemu ndogo za DNA zimepatikana katika wadudu na mimea kadhaa iliyo ndani ya kaharabu. Hata hivyo, majaribio hayo hayawezi kutokeza tena viumbe waliotokomea.

DNA hiyo imeharibika na pia si kamili. Kulingana na kadirio moja, huenda habari zilizopatikana katika sehemu hizo za DNA hazizidi sehemu moja ya milioni moja ya habari zote zilizo katika msimbo wa chembe za urithi za kiumbe huyo. Yasemekana kwamba kukusanya habari zote hizo kuhusu msimbo wa viumbe hao ni kama kujaribu kuunda tena kitabu chenye maelfu ya kurasa kutoka kwa sentensi moja isiyoeleweka na isiyo kamili. *

Kwa vyovyote vile, dhana ya kufanyiza tena wanyama wakubwa sana wa kale imefanya watu wapendezwe tena na kaharabu, na sasa kuna maonyesho ya kaharabu katika majumba mengi ya makumbusho ulimwenguni. Kwenye Jumba la Makumbusho la Kaharabu huko Santo Domingo, katika Jamhuri ya Dominika, wageni wanaweza kupata habari mbalimbali kwa kompyuta na kuchunguza kaharabu kwa hadubini. Kwenye karakana moja katika jumba hilo, wasanii stadi hutumia kaharabu isiyong’arishwa kutengeneza vito maridadi na mapambo yenye viumbe wa kale.

Kwa karne nyingi, wanadamu wamestaajabishwa na kaharabu. Leo, kaharabu hupendwa sana kwa sababu ya umaridadi wake wa ajabu. Zaidi ya hilo, inatoa habari muhimu kuhusu mambo ya kale.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 28 Kwa habari zaidi kuhusu chembe za urithi, ona gazeti la Amkeni! la Machi 22, 1995, ukurasa wa 3-10.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Wadudu mbalimbali na vilevile vyura wamepatikana ndani ya kaharabu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Vito vinavyong’ara hutengenezwa kwa vipande vidogo vya kaharabu

[Picha katika ukurasa wa 17 zimeandaliwa na]

Wadudu walio ndani ya kaharabu kwenye ukurasa wa 2, 16, na 17 na mapambo kwenye ukurasa wa 18: Cortesía Museo Mundo de Ambar, Santo Domingo RD - Foto Gianfranco Lanzetti; chura kwenye ukurasa wa 17: Cortesía Museo Mundo de Ambar, Santo Domingo RD e Nelson Fulgencio - Foto Gianfranco Lanzetti