Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Wazia Poromoko la Maji
Kukosa usingizi ni tatizo la ulimwenguni pote linaloathiri mtu 1 kati ya watu 10, kulingana na gazeti New Scientist. Wanasayansi wanaripoti kwamba nchini Marekani pekee tatizo la kukosa usingizi huwafanya watu kukosa kwenda kazini siku fulani na kusababisha aksidenti, na hivyo kutokeza hasara ya dola bilioni 35 za Marekani kila mwaka. Watu wanawezaje kupata usingizi? Watafiti katika Chuo Kikuu cha Oxford walipendekeza watu katika kikundi kimoja cha wale wenye matatizo ya kupata usingizi watafute mahali pazuri penye kutuliza, karibu na poromoko la maji au waende likizo mahali wanapopenda. Watu wa kikundi cha pili waliambiwa wahesabu kondoo ambao wanaruka uani mmoja baada ya mwingine, na wa kikundi cha tatu wachague njia yao wenyewe ya kutatua tatizo hilo. Watu katika kikundi cha pili na cha tatu walichukua muda mrefu zaidi kupata usingizi, lakini wa kikundi cha kwanza walichukua muda mfupi zaidi, yaani, kwa wastani walilala zaidi ya dakika 20 mapema kuliko wakati wao wa kawaida wa kulala. Allison Harvey, mmoja wa watafiti hao, alisema kwamba kuhesabu kondoo hakumsaidii mtu apate usingizi kwa sababu “hilo ni zoea la kawaida sana ambalo haliwezi kumwondolea mtu mawazo.”
Misitu Inayovuta Mvua
Misitu ya mvua ya maeneo yenye joto ambayo hukua katika maeneo ya urefu wa zaidi ya meta 900 inaweza kuvuta “asilimia 40 hivi ya maji kutoka katika mawingu kuliko kiasi cha mvua inayonyesha,” wanasema wanasayansi wa Australia Dakt. Paul Reddell na Dakt. David McJannet. Kulingana na Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Jumuiya ya Madola, “mawingu na ukungu kila wakati hupiga msitu na kuganda kwenye miti na kuinyeshea,” na hivyo kuongeza maji mengi kwenye mito inayopita katika maeneo hayo. Hata hivyo, “miti inapokatwa, ni maji kidogo sana ambayo huingia katika udongo.”
Matumizi Yasiyosawazika
Asilimia 20 ya watu duniani sasa wanatumia asilimia 86 ya bidhaa na huduma zote ulimwenguni, kulingana na kichapo The State of World Population 2001. Ripoti hiyo, iliyotolewa na Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa, inaonya kuhusu “pengo kubwa la matumizi” lililoko kati ya watu walio katika mataifa yaliyoendelea na wale walio katika mataifa yanayoendelea. Kwa mfano, “mtoto anayezaliwa katika nchi iliyoendelea hutumia bidhaa nyingi zaidi na kuchafua mazingira maishani mwake kuliko watoto 30 hadi 50 wanaozaliwa katika nchi zinazoendelea. Sasa, asilimia 20 ya watu wanaoishi katika mataifa yaliyoendelea huchangia zaidi ya nusu ya gesi ya kaboni-dayoksaidi katika hewa yetu, na asilimia 20 ya watu wanaoishi katika mataifa maskini zaidi hutoa asilimia 3 tu ya gesi hiyo,” ripoti hiyo inasema. Zaidi ya hilo, kutosheleza mahitaji ya mtu mmoja katika nchi tajiri kunahitaji eneo la nchi au la bahari ambalo ni karibu mara nne zaidi ya lile linalohitajiwa kumtosheleza mtu mmoja katika nchi inayoendelea.
Mbawakawa Wenye Akili
Hivi majuzi watafiti wamevumbua jinsi mbawakawa aina ya Stenocara wanavyopata maji yao ya kunywa katika Jangwa la Namib, kusini-magharibi mwa Afrika. Ili waweze kunawiri jangwani, ambako milimeta moja hivi ya mvua hunyesha kwa mwaka, mbawakawa huzoa maji katika ukungu mzito unaotoka Bahari ya Atlantiki. Wanafanyaje hivyo? Kulingana na gazeti Natural History, “mgongo wa mbawakawa una vilima vidogo,” ambavyo, ukivichunguza kwa kutumia darubini, utaona kuwa “vinafanana na milima na mabonde.” Tofauti na mabonde yaliyo na nta ambayo huyasukumia maji mbali, milima hiyo huyavuta. “Mbawakawa huinama kuuelekea upepo na umajimaji unaotokana na ukungu hujikusanya kwenye vilima vilivyoko mgongoni mwake. Tone linapokuwa zito, linavingirika hadi mdomoni pa mdudu huyo,” lasema gazeti hilo.
Dalili za Mapema za Matatizo ya Ulaji
“Wazazi wanaweza kutambua mapema kama watoto wao wana matatizo ya ulaji kutokana na jinsi wanavyokula, kulingana na gazeti The Times la London. Shirika la Matatizo ya Ulaji (EDA) limechapisha mwongozo unaowasaidia wazazi na watunzaji watambue matatizo ya kula mapema. Huenda dalili za mapema zikatia ndani zoea la kupasua-pasua chakula katika vipande vidogo-vidogo au kukawiza chakula mdomoni kufikia muda wa dakika tano. Wengine walio na matatizo ya ulaji huvalia mavazi makubwa kupita kiasi ili wafiche chakula wasichotaka kula. Huenda pia wakaomba picha zao zilizopigwa walipokuwa na afya bora au uzito wa kawaida zisionyeshwe. Mwongozo huo unawashauri wazazi wasipuuze dalili hizo bali wazungumze nao waziwazi.
Sumu Inayotokana na Vipima-Joto
“Zebaki inayotoka katika kipima-joto kimoja yaweza kutia sumu ziwa la ukubwa wa ekari 11, na vipima–joto vilivyovunjika huongeza tani 17 za zebaki kwenye mabomba ya maji machafu ya Marekani kila mwaka,” kulingana na gazeti National Geographic. Samaki hufyonza zebaki hiyo, kisha inaingia mwilini mwa watu wanaokula samaki hao. Zebaki inaweza kuharibu mfumo wa neva wa binadamu. Vipima-joto vyenye zebaki vimepigwa marufuku katika majiji mengi kutia ndani Boston, ambako maduka fulani yanabadilisha vipima-joto vyenye zebaki na vile vya elektroniki na vifaa vingine visivyo hatari sana.
Usifanye Mazoezi Kupita Kiasi
“Kufanya mazoezi (kukimbia, kuendesha baiskeli, au kuogelea) kwa dakika 30 au saa moja mara tatu kwa juma hunufaisha,” lasema gazeti L’Express la Ufaransa. Lakini ukitaka kuepuka matatizo makubwa ya afya, usifanye mazoezi kupita kiasi. Mazoezi ya kupita kiasi yaweza kusababisha viungo kudhoofika, gegedu la viungo kupondeka au kuteguka, kuvunjika mifupa, shinikizo la damu, matatizo ya kusaga chakula, mifupa kupungua uzito, na hata mshtuko wa moyo. “Kila mwaka nchini Ufaransa, mazoezi ya mwili huua wanamichezo 1,500 wenye afya bora kabisa,” laripoti gazeti hilo. Daktari wa wanamichezo, Stéphane Cascua wa hospitali ya Pitié-Salpêtrière huko Paris, awashauri hivi watu wengi ambao “hufanya mazoezi mwishoni mwa juma pekee” na ambao huishia hospitalini: Fanya mazoezi kwa ukawaida, lakini usijikaze kupita asilimia 75 ya uwezo wa moyo wako.
Ushirikiano Wenye Faida
Kulingana na gazeti la Sydney The Bulletin, sasa inaaminika kwamba wanyama aina ya potoroos—walio kama panya, wasiopatikana sana—walisaidia kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokea kwa baadhi ya misitu ya mikalitusi ya Australia inayovutia sana. Wanyama hao wanaishi kwenye miti mirefu ya Gippsland katika jimbo la Victoria. Angalau asilimia 90 ya chakula cha wanyama hao hutokana na aina fulani ya kuvu, ambayo huzalisha viazi vyake ndani ya udongo. Mmea huo hushirikiana na miti iliyo karibu kwa kukinga mizizi ya miti hiyo na pia kuelekeza mizizi yake mingi katika udongo ili kufyonza maji na madini muhimu. Miti hufaidi mmea huo kwa kuupatia sukari inayotokana na usanidi-mwanga. Wanyama aina ya potoroos huchangiaje ushirikiano huo? Baada ya kula matunda ya mmea huo, wanyama hao husambaza kinyesi chao chenye kuvu kisichosagwa kotekote msituni. Kwa hiyo, kuvu, miti, na wanyama hao huzidi kunawiri.
Kelele Nyingi Baharini Ni Hatari
“Kelele imeongezeka sana baharini, na kuna hofu kwamba inawatatanisha nyangumi, pomboo na wanyama wengine baharini,” laripoti gazeti la London The Independent. Watafiti waliochunguza kisababishi cha vifo vya nyangumi sita na pomboo mmoja katika pwani ya Bahamas waligundua kwamba walikufa kutokana na ubongo kuvuja damu, hali ambayo huenda ilisababishwa na kelele nyingi kutoka kwa meli za kijeshi za wanamaji zilizokuwa karibu. Sauti kutoka kwa meli za uchukuzi, ujenzi wa maeneo ya pwani, motaboti, na jeti za baharini husumbua wanyama wa baharini, ambao huathiriwa na sauti za aina nyingi kuliko binadamu. “Nyangumi na pomboo wanaporuka majini, hewa kwenye mapafu yao husukumwa kwenye sehemu nyingine za mwili,” inasema makala hiyo. “Mapovu ya hewa yaliyonaswa mwilini hukuza sauti mara 25, na kusababisha . . . uharibifu mkubwa wa viungo vya samaki. Uharibifu huo husababishwa na sauti za chini na unaweza pia kutukia katika eneo kubwa zaidi baharini kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.” Kelele baharini pia “huzuia mawasiliano ya nyangumi na pomboo na hivyo ni lazima wapaze sauti hata zaidi,” anasema mtafiti Doug Nowacek. “Hilo huwafanya wasikutane na kujamiiana, na kama hawasikii hawawezi kuogelea.”