Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Faida za Kupiga Mwayo!
Mtoto aliye tumboni mwa mama huanza kupiga mwayo majuma 11 tu baada ya mimba kutungwa, laeleza gazeti la kila juma la Hispania, Salud. Tabia hiyo ya kimaumbile imeonekana pia katika wanyama wengi wanaonyonyesha, aina fulani za ndege, na wanyama fulani watambaazi. Ingawa haijulikani kwa nini sisi hupiga mwayo, watafiti wamegundua kwamba matendo fulani yanahusiana na kupiga mwayo, kama vile kujinyoosha. Wameona kuwa matendo hayo “huongeza shinikizo la damu na mpigo wa moyo, na pia kulegeza misuli na viungo.” Tunapojizuia kupiga mwayo, hatupati faida zake. Kwa hiyo, wachunguzi hao wanapendekeza kwamba ikiwezekana, tunapaswa “kulegeza taya zetu na misuli yetu” tunapopiga mwayo. Huenda kupiga mwayo ifaavyo kukafanya uchangamke!
Maji ya Matunda ya Cranberry Huzuia Ambukizo
“Maji ya matunda ya cranberry yamekuwapo kwa muda mrefu,” lasema gazeti The Times la London. “Wahindi-Waamerika na Waamerika waliosafiri walitumia maji hayo katika tiba na kuyanywa ili kuzuia ugonjwa wa kiseyeye.” Yana vitamini C na madini mengine, “na huzuia viini, hivyo hutumika hasa kuzuia maambukizo ya mfumo wa mkojo.” Tofauti na ilivyodhaniwa awali, kinga hiyo haitokani na athari yake kwa mkojo. Badala yake, lasema gazeti la The Times, inatokana na vitu vilivyo katika maji hayo ambayo “huzuia bakteria za E.coli [kisababishi cha maambukizo mengi, kutia ndani kuvimba kwa kibofu] zisikwame kwenye ukuta wa mfumo wa mkojo kwa kuondoa bakteria hizo kabla ya kusababisha magonjwa.” Pia, watafiti wamegundua kwamba maji hayo hupunguza athari za ugonjwa wa ufizi.
Kinga ya Ubongo kwa Wagonjwa wa Moyo
“Kupunguza kiasi kidogo cha joto mwilini mwa mtu anayeugua mshtuko wa moyo hupunguza hatari ya kupata madhara ya ubongo na kifo kwa kiasi kikubwa, kulingana na matokeo mawili muhimu ya utafiti,” yasema ripoti ya gazeti la Kanada, Toronto Star. Uchunguzi uliofanywa katika mataifa matano ya Ulaya na mwingine mmoja nchini Australia ulionyesha kwamba wagonjwa wa mshtuko wa moyo wanapopunguziwa joto mwilini hupona haraka kiakili na vilevile mfumo wa neva. Joto la wagonjwa waliofikishwa hospitalini bila fahamu lilipunguzwa hadi nyuzi 33 Selsiasi kwa muda wa saa 12 hadi 24 kwa kutumia hewa baridi na madonge ya barafu. Kulingana na mtaalamu wa moyo Beth Abramson, mbinu hiyo ya bei nafuu, na ambayo ni rahisi kutumia hupunguza “kiasi cha oksijeni ambacho ubongo unahitaji na kupunguza utendaji wa kemikali unaoua chembe za ubongo,” lasema gazeti Star. “Mbinu hiyo imefanikiwa sana hivi kwamba madaktari huko Kanada, Marekani, Australia na Ulaya wanahimiza itumiwe kwa ukawaida kuwatibu wagonjwa wa mshtuko wa moyo wanaopelekwa hospitalini.”
Watoto Wapigwa Marufuku Kushiriki Jeshini
“Mkataba unaopiga marufuku watoto kushirikishwa katika shughuli za kijeshi unaanza kutumika leo, na unahitimisha harakati za kimataifa za miaka kumi za kukomesha kisababishi kimoja kikuu cha ukiukaji wa haki za binadamu duniani,” ilisema ripoti ya Umoja wa Mataifa kwa waandishi wa habari iliyotolewa mnamo Februari 12, 2002. Mkataba huo unaoitwa Optional Protocol, uliotiwa sahihi na nchi 96, “unasema kwamba vijana walio chini ya miaka 18 hawatalazimishwa kuingia jeshini, na kwamba Mataifa yanapaswa kuongeza umri wa chini wa wale watakaoruhusiwa kuchagua utumishi wa kijeshi kuwa miaka 16.” Inakadiriwa kuwa “katika nchi 85 ulimwenguni, watoto nusu milioni wanatumika katika majeshi ya serikali, wakiwa wapiganaji na vilevile katika makundi yenye silaha; zaidi ya 300,000 kati yao wanapigana katika nchi zaidi ya 35.” Kulingana na Mtandao wa Habari za Umoja wa Mataifa, wengi wa watoto hao walichukuliwa kwa nguvu na “hupigwa au kuuawa wanapojaribu kutoroka. Wasichana huwa hatarini zaidi kwa sababu mara nyingi wao husumbuliwa kingono.”
Dawa na Wazee
“Watu wenye umri unaozidi miaka 60 hutumia wastani wa dawa aina tatu, ambazo ni mara tatu zaidi ya zile zinazotumiwa na wagonjwa wenye umri wa chini,” lasema gazeti la Ujerumani Der Spiegel. “Hata hivyo, athari za [dawa] huongezeka kulingana na kiasi cha dawa zilizotumiwa.” Tatizo jingine ni kwamba “mara nyingi madaktari wa familia . . . hawazingatii utendaji uliopunguka wa mafigo ya wazee.” Kwa hiyo mgonjwa huwa na kiasi kikubwa cha madawa mwilini. Hivyo, “kiasi cha dawa kinachomfaa mgonjwa mwenye umri wa miaka 40 kinaweza kumdhuru mzee mwenye umri wa miaka 70,” laeleza gazeti Der Spiegel. “Wazee wengi hujiongezea matatizo kwa kutokunywa maji ya kutosha.” Ripoti hiyo inaongeza kusema kwamba kukosa maji mwilini pekee kwaweza kuwa na athari sawa na zile za dawa za maumivu, za kuliwaza, na za kudhibiti shinikizo la damu. Dalili zinatia ndani kuchanganyikiwa, kupotewa na akili, na kusinzia, matatizo ambayo mara nyingi hudhaniwa kuwa yanasababishwa na uzee.
Dawa Hatari ya Kusisimua
Watu 9 kati ya 10 ambao hucheza dansi usiku kucha hutumia dawa ya kusisimua inayoitwa ecstasy, laripoti gazeti la Hispania El País. Hivi majuzi, vijana wawili walikufa kwa kutumia kiasi kikubwa cha dawa hiyo katika dansi nchini Hispania. Rafiki wa mmoja wao asema kwamba “mtu hupewa kiasi kikubwa cha dawa hiyo.” Kwa nini vijana wengi huitumia? Wao hushawishiwa na vijana wenzao na wanataka kupata msisimuko na kuhisi kuwa wanajistahi. Mara nyingi, vijana hutumia dawa hiyo pamoja na dawa nyingine hatari za kulevya kama vile hashish na kokeini au hata pombe. Mpango wa Kitaifa wa Kuzuia Utumizi wa Dawa za Kulevya huko Hispania unaonya kwamba licha ya kupoteza kumbukumbu na kushuka moyo, dawa hiyo inaweza kusababisha ‘matatizo ya kupumua, kuvuja damu katika ubongo na hata kifo.’
Matusi Kazini
Matusi yameongezeka kazini, laripoti gazeti The Gazette la Montreal, Kanada. Wataalamu fulani husema kwamba matusi huongeza mkazo kazini. Karen Harlos, profesa wa Chuo Kikuu cha McGill anayeshughulikia tabia ya wafanyakazi katika mashirika, asema: “Kuwachambua wengine kazini kwa matusi kwaweza kupunguza sana uwezo wao wa kufanya kazi, kujistahi au kuathiri afya yao.” Kulingana na gazeti hilo “msimamizi wa kazi ana daraka la kuwawekea wafanyakazi mfano,” halafu wao watamwiga. Iwapo unatatizwa na jambo hilo, gazeti hilo linadokeza umwendee “mtu aliye na tabia hiyo na umwombe kwa heshima akome kutumia usemi kama huo anapozungumza nawe.”
Kazi ya Nyumbani Hutoa Mazoezi Mazuri
Je, kusafisha nyumba kwa kutumia mashine, kuosha madirisha, na kusukuma kigari cha mtoto kunaweza kuandaa mazoezi ya mwili? Jibu ni ndio, kulingana na uchunguzi uliofanywa hivi majuzi katika Chuo Kikuu cha Queensland, Australia. Wachunguzi walitumia kifaa cha kupima kiasi cha oksijeni inayotumika kwa akina mama saba walio na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, walipofanya kazi zao za kawaida, inasema ripoti ya gazeti The Canberra Times. Wachunguzi hao walisema kwamba, “uchunguzi huo ulidokeza kuwa baadhi ya kazi za nyumbani hufanywa kwa nguvu ya kutosha kuboresha afya ya mtu.” Profesa Wendy Brown aligundua kwamba “kazi za akina mama hao zilileta faida kama zile zinazotokana na mazoezi ya kadiri kama kutembea haraka, kuendesha baiskeli, au kuogelea,” inasema ripoti hiyo. Brown alisema: “Ingawa uchunguzi huo uko katika hatua za mwanzo-mwanzo, umeonyesha wazi kuwa ni kosa kudai kwamba eti wanawake hawafanyi kazi wakati wanatembea-tembea hapa na pale siku nzima.”
Makapi ya Mchele Huimarisha Ujenzi
“Watafiti wanatabiri kwamba kutakuwa na badiliko kubwa katika taaluma ya ujenzi,” lasema gazeti la Brazili Jornal da USP. “Majengo yatadumu kwa muda mrefu zaidi na yataweza kuhimili hali ya hewa na mazingira zaidi. Maendeleo hayo yanatokana na uvumbuzi wa aina mpya ya sementi uliofanywa na watafiti katika Taasisi ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha São Paulo,” Brazili. Wanasayansi hao walichanganya silika iliyotokana na majivu ya makapi ya mchele na sementi ya kawaida na kutokeza sementi ya hali ya juu. Saruji inayotokana na sementi hiyo haipenyezi maji kwa urahisi, inahimili uchafuzi wa mazingira na hali mbaya ya hewa, na ina nguvu mara tatu au nne kushinda saruji ya kawaida. Nguzo zinazojengwa kwa mchanganyiko huo zitakuwa ndogo kwa asilimia 30 “lakini zitakuwa imara, [na] matokeo yatakuwa: majengo yenye nafasi kubwa zaidi, yasiyo mazito, yenye kuchukua muda mfupi kukamilika na yenye kugharimu pesa kidogo kwa kuwa hayatahitaji vifaa vingi vya ujenzi, na yanayohitaji wafanyakazi wachache,” lasema gazeti la Jornal da USP. Karibu tani milioni 80 za makapi ya mchele hupatikana kila mwaka ulimwenguni, nazo hutoa tani milioni 3.2 za silika.