Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mlima Wachongwa Kuwa Sanamu ya Ukumbusho

Mlima Wachongwa Kuwa Sanamu ya Ukumbusho

Mlima Wachongwa Kuwa Sanamu ya Ukumbusho

NI NINI ambacho kingemfanya kijana Mmarekani-Mpolandi aliyejifunza mwenyewe uchongaji, abadili mlima uwe sanamu ya mpiganaji Mhindi aliyeheshimiwa? Mchongaji huyo, Korczak Ziolkowski, hakuamua jambo hilo haraka-haraka. Ilimchukua miaka saba kufanya hivyo.

Mnamo mwaka wa 1939, Korczak alipokea barua kutoka kwa chifu mmoja mzee wa kabila la Kihindi la Lakota, Henry Standing Bear, aliyeishi katika Eneo Lililotengwa la Wahindi la Pine Ridge, Dakota Kusini. Chifu huyo alimwomba achonge sanamu ya chifu mashuhuri wa kale katika Milima Myeusi (Black Hills) huko Dakota Kusini. Walakota huiona Milima Myeusi kuwa eneo takatifu la Wahindi, na hivyo hawakufurahi wakati mchongaji Gutzon Borglum alipochonga sanamu kubwa ya maraisi wanne wa Marekani juu ya Mlima Rushmore ulio katikati ya Milima Myeusi ambayo wao huiona kuwa mitakatifu. Chifu Standing Bear alimwandikia Korczak hivi: “Mimi na machifu wenzangu tungependa kuwajulisha Wazungu kwamba Wahindi wana watu wao mashuhuri pia.”

Kwa Nini Sanamu Hiyo Iliitwa Crazy Horse?

Kwa nini sanamu hiyo iliitwa Crazy Horse? * Robb DeWall aeleza: “Wahindi ndio waliotaka sanamu hiyo iitwe Crazy Horse. Crazy Horse ni jina la Mhindi mashuhuri, aliyekuwa mpiganaji jasiri na mwanajeshi stadi. Alikuwa Mhindi wa kwanza kutumia mitego kuwanasa maadui wakati wa vita. Yeye . . . hakuwahi kutia sahihi mkataba wowote wala kuishi katika eneo lililotengwa la Wahindi.”

Korczak alijuaje picha ambayo angechonga? Kutoka kwa hadithi aliyosikia kumhusu Crazy Horse alipokuwa akimjibu mfanya-biashara Mzungu. Mzungu huyo alimdhihaki Crazy Horse kwa sababu alikataa kuishi katika eneo lililotengwa la Walakota, na watu wengi waliishi huko. Mfanya-biashara huyo alimwuliza: “Mashamba yenu yako wapi?” Crazy Horse “akitazama mbali kwenye upeo wa macho, alimwonyesha kwa kidole, akisema kwa madaha, ‘Mashamba yetu yapo mahali watu wetu walipozikwa.’”

Mahali Ambapo Kumbukumbu Lingejengwa

Kwanza ilikuwa lazima kuchagua mlima ambao ungechongwa na kuwa sanamu kubwa zaidi ulimwenguni, hata kushinda ile ya Mlima Rushmore. Katika mwaka wa 1947, Korczak na Chifu Standing Bear walikubaliana kuhusu mlima ambao ungetumiwa kuchongea kumbukumbu hilo. Lingechongwa juu ya kilele chenye urefu wa meta 200 cha mlima wa meta 2,050. Korczak aliuita mlima huo Thunderhead (Kichwa cha Ngurumo), kwa sababu ya mawingu mengi ambayo hujikusanya nyakati nyingine juu ya mlima huo. Wangepataje kibali cha kuuchonga mlima huo uwe sanamu kubwa ya kumkumbuka Mhindi?

DeWall aeleza katika kitabu Korczak—Storyteller in Stone: “Mtu yeyote angeweza kuomba kibali cha kuruhusiwa kuchimba katika Milima Myeusi, na hivyo ‘angemiliki’ ardhi hiyo iwapo tu angeendelea kulipa ada ya ukaguzi ya dola 100 za Marekani kila mwaka. Korczak alishangaa wakati serikali ilipokubali mlima huo uchongwe na kuwa sanamu ya Mhindi anayepanda farasi, maadamu angeufanyia ukaguzi uliohitajika kila mwaka.”

Mlima Ungechongwa Kiasi Gani?

Kwa kuwa alikuwa peke yake mwanzoni na alikuwa na pesa kidogo, Korczak alikuwa na kazi kubwa sana ya kufanya. Kilipukaji cha kwanza alichotumia katika Juni 3, 1948, kililipua miamba ya tani kumi tu. Kutoka wakati huo hadi mwaka wa 1994, karibu miamba ya tani milioni 8.4 ililipuliwa kwenye mlima huo. Mamia ya Wahindi walienda kuona ulipuaji wa kwanza, ikiwa ni pamoja na watano kati ya watu tisa waliookoka Mapigano ya Little Bighorn (Juni 25, 1876). *

Korczak alikuwa na moyo mkuu na alijitoa mhanga kwa kazi yake. Alitumia miti aliyokata mwenyewe kujenga ngazi yenye hatua 741 ya kupanda hadi mlimani, ambapo alipanga kulipua na kuchonga kichwa cha farasi. Alihitaji nishati ya kuendesha mtambo wa kuchonga mawe. Nishati hiyo ilitoka kwa mtambo wa zamani uliotumia petroli. Korczak aliweka bomba la kusafirisha petroli lenye kipenyo cha sentimeta 8 na urefu wa meta 620 kupitia mlimani hadi mahali alipokuwa akichimba. Mtambo huo ulipozimika ghafula, yeye alishuka hatua hizo 741 ili kuuwasha tena. Kuna siku alipopanda na kushuka mara tisa! Hakumruhusu mtu yeyote kuugusa mtambo huo. Bila shaka alikuwa mtu mwenye nguvu nyingi na aliyeazimia.

Mnamo mwaka wa 1951, alitumia lita 660 za rangi nyeupe kuchora sanamu hiyo kwenye mlima. Jambo hilo liliwasaidia wageni kuwazia kwa urahisi jinsi ambavyo picha kamili ingekuwa.

Msiba na Tatizo

Katika miaka ya 1970 na mapema katika miaka ya 1980, Korczak aliendelea kulipua miamba zaidi ili aanze kuchonga kichwa cha farasi. Alikuwa amepatwa na mshtuko wa moyo mara mbili (mwaka wa 1968 na 1970). Katika majira ya kiangazi ya mwaka wa 1982, alifanyiwa upasuaji wa moyo. Halafu, katika Oktoba mwaka huo, Korczak alikufa ghafula akiwa na umri wa miaka 74. Je, mradi wake mkubwa ungeendelea? Je, kifo chake kingemaanisha mwisho wa mradi huo?

Korczak hakutarajia kamwe kukamilisha kazi hiyo mwenyewe. Kwa sababu alijua ilihitaji zaidi ya kizazi kimoja kuimaliza, alikuwa amefanya mipango kabambe. Mke wake, Ruth, na watoto wao kumi walijitoa mhanga kama baba yao kukamilisha kumbukumbu hilo. Ruth alikuwa amejihusisha katika kila hatua ya kazi hiyo, akimsaidia kupiga hesabu na kufanya kazi nyingine.

Korczak alitaka kwanza kumaliza kuchonga kichwa cha farasi. Hata hivyo, kufikia wakati wa kifo chake hakuwa amemaliza. Mnamo mwaka wa 1987, mjane wake pamoja na wakurugenzi wa shirika lisilo la kibiashara, waliamua kuchonga uso wa Crazy Horse kwanza. Kwa nini waliamua kufanya hivyo? Kwa sababu uso ni sehemu ndogo kuliko kichwa cha farasi, ungechukua muda mfupi kumalizika na haungegharimu pesa nyingi. Pia, watu wangeona mradi huo ukiwa halisi zaidi, na huenda wengine wangeuunga mkono.

Vipimo Vikubwa Ajabu

Kichwa cha Crazy Horse kingekuwa na urefu wa meta 26.7 na upana wa meta 18. Inasemekana kwamba “vichwa vyote vinne vya sanamu ya Mlima Rushmore vyenye urefu wa meta 20, vinaweza kutoshea ndani ya kichwa cha Crazy Horse pekee, na kuwe na nafasi zaidi!” Kulingana na vyanzo fulani vya habari, sanamu ya Crazy Horse, itakuwa sanamu kubwa zaidi ulimwenguni, yenye kimo cha meta 172 na urefu wa meta 195, kutia ndani mkono wake wa kushoto ulioinuliwa na farasi wake. Mkono huo peke yake utakuwa na urefu wa meta 69, na kidole cha shahada kitakuwa na urefu wa meta 11.4 na upana wa meta 3.

Korczak alikataa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Marekani ili kufadhili mradi wake. Mara mbili serikali hiyo ilitaka kumpa dola milioni 10, lakini alikataa. DeWall asema kwamba Korczak “alishikilia kwa uthabiti msimamo wake wa kufadhili mradi wake mwenyewe. Wakati wa maisha yake, yeye mwenyewe alikusanya na kutumia zaidi ya dola milioni tano kwa ajili ya mradi wa Crazy Horse.” Hakukubali kulipwa wala kuwa na akaunti ya benki kwa ajili ya matumizi ya kibinafsi.

Leo ada ya mlangoni hutozwa watu wenye magari. Watu wanaotembea kwa miguu na waendeshaji wa pikipiki hulipa kiasi cha chini. Kwa sasa, wageni zaidi ya milioni moja hutembelea mradi huo kila mwaka. Watu wengi wamechanga vifaa na pesa ili kuendeleza mradi huo.

Jumba la Makumbusho la Vitu vya Kale vya Wahindi

Kwenye mradi wa Crazy Horse, kuna Jumba la Makumbusho la kuvutia la Amerika Kaskazini ambalo limejengwa kwa miti ya kiasili. Jumba hilo lina maelfu ya vitu vya kale vya Wahindi. Vitu hivyo vinawakilisha mengi kati ya yale makabila zaidi ya 500 ya Amerika Kaskazini. Pia, lina maktaba kubwa ya vitabu vya marejeo kuhusu Wahindi Waamerika, ambavyo watu wanaweza kusoma.

Priscilla Engen na Freda Goodsell (Walakota Waoglala), ambao ni Wahindi Waamerika huwa tayari kujibu maswali na kueleza kuhusu sanaa na vitu ambavyo vinaonyeshwa. Mlakota wa kabila la Miniconjou, Donovin Sprague, ambaye ni mwalimu wa chuo kikuu, pia huwa tayari kujibu maswali yoyote ya watu wanaotembelea jumba hilo. Yeye ni kilembwe wa Chifu Hump, aliyekuwa katika Pigano la Little Bighorn katika mwaka wa 1876.

Wakati Ujao wa Sanamu ya Crazy Horse

Jumba jipya la makumbusho linapangwa kujengwa. Mwanzoni Korczak aliwazia kujenga jumba la makumbusho lenye muundo wa nyumba za Wanavajo karibu na sehemu ya chini ya sanamu hiyo. Jengo hilo la orofa litakuwa na kipenyo cha meta 110. Pia kuna mipango ya kujenga chuo kikuu na kituo cha elimu ya tiba kwa ajili ya Wahindi Waamerika. Hata hivyo, kabla ya miradi yote hiyo mikubwa kukamilika, ni lazima mradi wa Crazy Horse ukamilike. Utachukua muda gani? Ruth, mke wa Korczak, asema: “Hatuwezi kutaja tarehe hususa ambapo mradi huo utakamilika, kwa sababu mambo mengi huenda yakabadilika, kama vile hali ya hewa, majira ya baridi, hali ya kifedha, na mengineyo. Jambo muhimu zaidi ni kujitahidi kufikia lengo letu.”

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Alipokuwa kijana, Crazy Horse (aliyeishi wapata mwaka wa 1840 hadi 1877) alijulikana kama Farasi Wake Amesimama Karibu. “Huenda aliitwa Crazy Horse [Tasunke Witko, katika Kilakota] kabla ya kufikia umri wa miaka ishirini, hivyo akawa mtu wa tatu, na wa mwisho, katika jamaa yao kuitwa hivyo.” Babake na babu yake waliitwa hivyo pia.—Encyclopedia of North American Indians.

^ fu. 11 Kwenye pigano hilo la kihistoria, jeshi la Walakota na Wacheyene 2,000 hivi liliangamiza Luteni Kanali George Armstrong Custer na kikosi chake cha waendeshaji wa farasi 215, na kumshinda Meja Marcus Reno na Kapteni Frederick Benteen na waendeshaji wa farasi waliokuja kusaidia. Crazy Horse alikuwa mmoja wa viongozi Wahindi katika pigano hilo.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kigezo cha sanamu ya Crazy Horse na mchoro wa kichwa mlimani

[Hisani]

Pages 2 and 15: Korczak, Sculptor © Crazy Horse Memorial Fnd.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Korczak na Chifu Henry Standing Bear mnamo Juni 3, 1948. Nyuma, kigezo cha marumaru cha sanamu hiyo na mlima kabla haujalipuliwa

[Hisani]

Photo: Crazy Horse Memorial archives

[Picha katika ukurasa wa 16]

Jamaa ya Ziolkowski. Ruth, mjane wa Korczak, wa nne kutoka upande wa kulia

[Hisani]

Crazy Horse photo

[Picha katika ukurasa wa 17]

Ndani ya Jumba la Makumbusho la Wahindi

[Picha katika ukurasa wa 17]

Matembezi ya kila mwaka ya kutazama uso wa Crazy Horse

[Hisani]

Photo by Robb DeWall, courtesy Crazy Horse Memorial Foundation (nonprofit)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Photos by Robb DeWall, courtesy Crazy Horse Memorial Foundation (nonprofit)