Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magna Carta na Jitihada za Wanadamu za Kupata Uhuru

Magna Carta na Jitihada za Wanadamu za Kupata Uhuru

Magna Carta na Jitihada za Wanadamu za Kupata Uhuru

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

MTO Thames unapita kwenye eneo lenye kuvutia la mkoa wa Surrey nchini Uingereza. Katika mojawapo ya makonde yaliyo kwenye kingo za mto huo kuna nguzo ya ukumbusho yenye maandishi yanayoeleza tukio fulani la karne ya 13. Katika konde hilo la Runnymede, Mfalme John wa Uingereza (aliyetawala kuanzia 1199 hadi 1216) alikutana na mabwana waliomiliki mashamba ambao walimpinga kwa sababu walichukizwa na utawala wake mbaya. Mabwana hao walimtaka mfalme huyo aidhinishe haki fulani ili waache kulalamika. Kwa kuwa alishinikizwa sana na mabwana hao, hatimaye mfalme alipiga muhuri hati fulani ambayo baadaye iliitwa Magna Carta (Hati Kuu).

Kwa nini hati hiyo imefafanuliwa kuwa “hati muhimu zaidi ya kisheria katika historia ya Ulaya na Amerika Kaskazini”? Jibu la swali hilo linaonyesha mengi kuhusu jitihada za wanadamu za kupata uhuru.

Matakwa ya Mabwana Hao

Mfalme John alikuwa amekorofishana na Kanisa Katoliki. Alimkaidi Papa Innocent wa Tatu kwa kukataa kumkubali Stephen Langton kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury. Basi, kanisa likaacha kumuunga mkono mfalme na likamtenga. Hata hivyo, Mfalme John alijaribu kupata kibali cha kanisa tena. Alikubali kumpa papa falme za Uingereza na Ireland. Kisha papa akamrudishia John falme hizo kwa kuwa aliapa kwamba angekuwa mwaminifu kwa kanisa na kulipa ushuru kila mwaka. John akawa kibaraka wa papa.

Matatizo ya kifedha yalimlemea mfalme. Wakati wa utawala wake wa miaka 17, John aliongeza kodi ya wenye mashamba mara 11. Kukorofishana kwake na kanisa na matatizo yake ya kifedha yalifanya wengi waamini kwamba mfalme huyo hakuwa mwenye kutegemeka. Na yaelekea utu wake pia ulichangia jambo hilo.

Mwishowe, fujo zikazuka wakati mabwana wa eneo la kaskazini mwa nchi walipokataa kulipa kodi zaidi. Walifanya maandamano katika jiji la London na kutangaza kuwa wameacha kumuunga mkono mfalme. Ugomvi mkali ukazuka kati ya makundi hayo mawili, kati ya mfalme akiwa katika jumba lake huko Windsor na mabwana hao waliokuwa mashariki katika mji wa karibu wa Staines. Mashauriano yalifanywa kichinichini na wakakubali kukutana katikati ya miji hiyo miwili, huko Runnymede. Wakiwa huko, mnamo Jumatatu, Juni 15, 1215, Mfalme John alipiga muhuri hati yenye vifungu 49. Utangulizi wa hati hiyo unasema hivi: ‘Hivi ndivyo vifungu ambavyo mabwana wanataka viidhinishwe na ambavyo mfalme ameidhinisha.’

Uhuru Ulioletwa na Sheria

Hata hivyo, watu walianza kumshuku John. Ijapokuwa watu wengi hawakumpenda mfalme wala papa, mfalme aliwatuma wajumbe wakutane na papa huko Roma. Papa alitoa amri mara moja zilizobatilisha mkataba uliofanywa huko Runnymede. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vikazuka huko Uingereza. Hata hivyo, mwaka uliofuata, John akafa, na mwanawe, Henry, mwenye umri wa miaka tisa akaanza kutawala.

Wafuasi wa kijana huyo, Henry, walifanya mpango ili ile hati iliyotayarishwa huko Runnymede itolewe upya. Kulingana na kijitabu Magna Carta, hati hiyo iliyotayarishwa upya ilikuwa “imebadilishwa upesi-upesi kutoka kwenye ile hati iliyozuia uonevu na kuwa hati ambayo ilimwezesha [mfalme] kuungwa mkono na watu wenye maoni ya busara.” Hati hiyo ilitolewa tena mara kadhaa wakati wa utawala wa Henry. Wakati mwandamizi wake, Edward wa Kwanza, alipoitangaza tena rasmi hati ya Magna Carta mnamo Oktoba 12, 1297, nakala moja iliwekwa miongoni mwa zile hati muhimu za serikali ya Uingereza.

Hati hiyo ilidhibiti mamlaka ya mfalme. Ilisema kwamba alikuwa chini ya sheria, sawa na raia wake wote. Kulingana na Winston Churchill, aliyekuwa mwanahistoria maarufu na waziri mkuu wa Uingereza katika karne ya 20, Magna Carta ilileta “mfumo wa kudhibiti mamlaka ambao ungemwezesha mfalme kuwa na mamlaka ya kutosha, lakini ambao ungezuia mamlaka hiyo isitumiwe vibaya na mtawala wa mabavu au mpumbavu.” Hayo ni maneno mwafaka kwelikweli! Lakini hati hiyo ingewafaidije watu wa kawaida? Wakati huo, hawakufaidika sana. Magna Carta iliorodhesha haki za “watu huru” peke yao—ambao wakati huo walikuwa watu wa hali ya juu, nao walikuwa wachache. *

Kitabu Encyclopædia Britannica chasema kwamba “muda mfupi tu baada ya kutolewa kwake,” Magna Carta “ikawa ishara na shime ya kupinga uonevu, na kila kizazi kiliiona kuwa njia ya kulinda haki zake.” Ili kuonyesha umuhimu wa hati hiyo, kila kikao cha Bunge la Uingereza kilifunguliwa baada ya hati ya Magna Carta kusomwa.

Katika karne ya 17, mawakili wa Uingereza walitumia vifungu vya Magna Carta kutetea haki mbalimbali za watu kama vile haki ya kusikilizwa kwa kesi mbele ya jopo la waamuzi, kutumia hati ya habeas corpus, * usawa mbele ya sheria, kuzuia watu wasikamatwe bila msingi, na kudhibitiwa kwa kodi kupitia bunge.

Jitihada Zaendelea

Bwana Bingham ambaye alikuwa hakimu mkuu wa Uingereza na Wales mnamo mwaka 1996 hadi mwaka 2000 alisema hivi: “Katika nyakati zilizopita, hati ya Magna Carta imeonwa kuwa muhimu kwa sababu ya jinsi ambavyo watu wameielewa bali si kwa sababu ya yale inayosema.” Hata hivyo, uhuru ulioletwa na hati hiyo ulienea katika maeneo yote yaliyozungumza Kiingereza.

Wakoloni waliotoka Uingereza mnamo mwaka 1620 ili kuenda Amerika, walibeba nakala ya Magna Carta. Mnamo mwaka 1775, wakazi wa makoloni ya Uingereza huko Amerika walipinga kutozwa kodi ikiwa hawangekuwa na wawakilishi katika serikali. Wakati huo, baraza la kutunga sheria la eneo ambalo sasa linajulikana kama jimbo la Massachusetts lilitangaza kwamba utozaji huo wa kodi ulikuwa kinyume cha hati ya Magna Carta. Ama kweli, muhuri rasmi wa Massachusetts uliotumiwa wakati huo ulikuwa na picha ya mwanamume aliyebeba upanga kwa mkono mmoja na hati ya Magna Carta katika mkono ule mwingine.

Wakati wawakilishi wa taifa hilo jipya walipokutana kutayarisha katiba ya Marekani, waliunga mkono ile kanuni iliyotetea uhuru chini ya sheria. Hati ya Haki za Raia ya Marekani inategemea kanuni hiyo. Hivyo, kwa ukumbusho wa Magna Carta, mnamo mwaka 1957, Shirika la Mawakili la Marekani lilitengeneza nguzo ya ukumbusho huko Runnymede yenye maandishi haya, “Kwa Ukumbusho wa Magna Carta—Ishara ya Uhuru Unaoletwa na Sheria.”

Mnamo mwaka 1948, mwanasiasa wa kike Eleanor Roosevelt alisaidia kutayarisha Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, akitarajia kwamba azimio hilo lingekuwa “Magna Carta ya kimataifa kwa watu wote kila mahali.” Bila shaka, historia ya hati ya Magna Carta inaonyesha wazi jinsi wanadamu wanavyotamani uhuru. Licha ya matarajio hayo mema, haki za msingi za binadamu zinaendelea kupuuzwa katika nchi nyingi. Serikali za wanadamu zimeonyesha mara nyingi kwamba haziwezi kuwaletea watu wote uhuru. Hiyo ni sababu moja inayowafanya mamilioni ya Mashahidi wa Yehova wathamini uhuru wa hali ya juu zaidi chini ya utawala wa serikali tofauti, Ufalme wa Mungu.

Biblia inasema jambo la kuvutia kumhusu Mungu: “Iliko roho ya Yehova, kuna uhuru.” (2 Wakorintho 3:17) Iwapo unapendezwa kujua juu ya uhuru ambao wanadamu watapata kupitia Ufalme wa Mungu, mbona usiwaulize Mashahidi wa Yehova wakueleze juu yake watakapokutembelea? Jibu la swali hilo linaweza kukusisimua na kukuweka huru.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 “Ijapokuwa katika mwaka 1215 ni wachache tu waliokuwa ‘watu huru,’ kufikia karne ya kumi na saba karibu kila mtu alikuwa mtu huru.”—History of Western Civilization.

^ fu. 14 Hati ya kisheria inayoitwa habeas corpus hutokana na usemi wa Kilatini unaomaanisha “unapaswa kuwa na mwili,” nayo hutumiwa ili kuchunguza iwapo mtu amefungwa gerezani kihalali.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

HATI KUU

Hapo awali Magna Carta (neno la Kilatini linalomaanisha “hati kuu”) iliitwa “Vifungu vya Mabwana.” Mfalme John alipiga muhuri wake kwenye hati hiyo yenye vifungu 49. Siku chache baadaye, vifungu vya mkataba huo viliongezeka kufikia 63, na kwa mara nyingine mfalme huyo akaipiga muhuri hati hiyo. Toleo la mwaka 1217 lilifuatiwa na toleo jingine dogo ambalo lilikuwa na sheria kuhusu misitu. Tangu wakati huo, hati hiyo iliitwa Magna Carta.

Vifungu 63 vya hati hiyo vimegawanywa katika vikundi tisa. Kati ya vifungu hivyo kuna vile vinavyozungumzia malalamiko ya mabwana hao, kurekebishwa kwa sheria na utekelezaji wa hukumu, na uhuru wa kanisa. Kifungu cha 39, ambacho ndiyo msingi wa uhuru wa Waingereza kinasema hivi: “Mtu yeyote aliye huru hapaswi kukamatwa wala kufungwa gerezani, wala kunyimwa haki zake na kunyang’anywa mali zake, wala kutengwa au kufukuzwa nchini, wala kuvunjiwa hadhi yake, hatutatumia nguvu dhidi yake, wala kuwatuma wengine kufanya hivyo, isipokuwa awe amehukumiwa na watu walio sawa naye au na sheria ya nchi.”

[Picha katika ukurasa wa 13]

Nyuma: Toleo la tatu la Magna Carta

[Hisani]

By permission of the British Library, 46144 Exemplification of King Henry III’s reissue of Magna Carta 1225

[Picha katika ukurasa wa 12]

Mfalme John

[Hisani]

From the book Illustrated Notes on English Church History (Vols. I and II)

[Picha katika ukurasa wa 12]

Mfalme John ampa mjumbe wa papa taji lake

[Hisani]

From the book The History of Protestantism (Vol. I)

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mfalme John akutana na mabwana na kukubali kupiga muhuri hati ya Magna Carta, mwaka 1215

[Hisani]

From the book The Story of Liberty, 1878

[Picha katika ukurasa wa 14]

Nguzo ya Ukumbusho ya Magna Carta huko Runnymede, Uingereza

[Hisani]

ABAJ/Stephen Hyde

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

Nyuma upande wa juu: By permission of the British Library, Cotton Augustus II 106 Exemplification of King John’s Magna Carta 1215; King John’s Seal: Public Record Office, London