Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Adabu Yazorota
“Adabu na tabia za Wajapan zimezorota.” Hayo ni maoni ya asilimia 90 ya watu wapatao 2,000 waliohojiwa na gazeti The Yomiuri Shimbun hivi majuzi. Waliudhiwa na nini? Asilimia 68 kati yao waliudhiwa na “watu ambao hutupa sigara ovyoovyo, chingamu, na mikebe ya vinywaji.” Zaidi ya nusu walisema waliudhiwa na wazazi ambao hukosa kuwatia nidhamu watoto wao ambao hupiga makelele. Wengine walilalamikia utumizi wa simu za mkononi katika mahali pa umma, kukosa kutoa kinyesi cha wanyama vipenzi, na kuegesha magari na pikipiki vibaya. Vijana walilaumiwa zaidi. “Asilimia 66 ya watu waliotoa maoni yao, ambao walikuwa na umri wa kati ya miaka 20 hadi 40, walisema wanafunzi wa shule za msingi na za upili ndio hasa wenye tabia mbaya.”
Mamba Bandia
Ndege aina ya mnandi anayesemekana kwamba hula karibu kilogramu moja ya samaki kila siku, “huwasumbua sana watu wanaovua samaki ili kujistarehesha,” lasema gazeti Calgary Herald la Kanada. Gazeti hilo linasema kwamba wakulima huko Amerika Kaskazini na wasimamizi wa wafugaji wa samaki wanatumia mbinu mpya ya kuzuia mnandi na ndege wengine walao samaki—mamba wa plastiki. Mamba hao wenye urefu wa meta nne “wana macho yanayong’aa, kama ya mamba halisi walio chonjo mwituni,” laeleza gazeti Herald. Mwanabiolojia mmoja aligundua kwamba mamba wa plastiki anayeelea juu ya maji huwazuia ndege kwa mwezi mmoja hivi. Baada ya hapo, ndege hao huanza kumzoea, na hata korongo mmoja alionekana “ametua juu ya mamba huyo bandia.” Lakini wakati mtego huo ulipopelekwa mahali pengine, ndege hao walianza tena kumwogopa.
“Kusumbuliwa” Kazini
Sababu kuu ambayo huwafanya watu wakose kwenda kazini nchini Hispania ni “kusumbuliwa kiakili,” laripoti gazeti El País Semanal. Zaidi ya Wahispania milioni mbili husumbuliwa kwa muda mrefu kazini. Kulingana na mtaalamu wa akili, Iñaki Piñuel, wanaosumbuliwa hasa ni wafanyakazi wenye bidii ambao huonewa wivu kwa sababu ya bidii yao kazini. Wafanyakazi wanaweza kuwanyima kazi, kuacha kuzungumza nao, kuwapuuza, kuwachambua siku zote, kusema uwongo juu yao ili kuwashushia heshima. “Inakadiriwa kwamba mtu 1 kati ya 5 wanaojiua huko Ulaya hufanya kitendo hicho kwa sababu ya kusumbuliwa akiwa kazini,” yasema ripoti hiyo. Wao waweza kufanya nini? Gazeti hilo ladokeza hivi: “Usinyamaze tu. Tafuta mashahidi. Ripoti jambo hilo kwa maafisa wa kampuni. Usijilaumu. Ukisumbuliwa sana, hamia idara nyingine [au] hata ubadili kazi.”
Watoto Wenye Matatizo ya Akili
“Mtoto mmoja kati ya watano ulimwenguni ana matatizo ya akili au ya tabia ambayo inaweza kuathiri maisha yake yote,” lasema gazeti The Independent la London. Ripoti ya pamoja ya Shirika la Afya Ulimwenguni na Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa ilionya kwamba kushuka moyo, kujiua, na kujidhuru kumeongezeka “sana” miongoni mwa vijana. Wanaoathiriwa sana ni wale wanaoishi katika maeneo yenye vita na nchi ambako mifumo ya kijamii na kiuchumi inabadilika haraka. Kulingana na gazeti The Independent, watoto walioshuka moyo “wanaweza kupata magonjwa mengine au kuwa na tabia ambazo zinaweza kufupisha maisha yao.” Pia gazeti hilo lilisema kwamba “karibu asilimia 70 ya watu wazima wanaokufa mapema, hufa kutokana na tabia zilizoanza walipobalehe, kama kuvuta sigara, kunywa pombe na kutumia dawa za kulevya.”
Barabara Kuu Baharini
“Ni njia kubwa zaidi baharini,” laripoti gazeti The Sunday Times la London. “Kuna barabara kuu katika Bahari ya Pasifiki kutoka ufuo wenye joto wa California inayopitia Hawaii hadi kwenye ufuo wenye mawe-mawe wa Japan.” Hivi majuzi, mtaalamu wa viumbe vya baharini huko Hawaii, Jeff Polovina, aligundua barabara hiyo na kuichora kwa kuwatia alama nyangumi, kasa, tuna, pomboo na papa. Barabara hiyo ina mimea na wanyama wengi wadogo ambao huliwa na kaa, yavuyavu, na ngisi. Hao nao huliwa na wanyama wanaosafiri masafa marefu. Kasa wa aina fulani waliotajwa katika gazeti hilo kuwa “watambaazi wanaosafiri masafa marefu zaidi,” hutaga mayai nchini Japan, hukulia karibu na pwani ya California, na kuendelea kusafiri baina ya Japan na California. Katika majira ya baridi kali, barabara hiyo husonga kilometa 1,000 kusini, toka kusini mwa California hadi Bahari ya China Kusini.
Kudumisha Afya Bora
“Mazoezi ya mwili husaidia kupunguza uzito, huzuia maradhi ya sukari na ya mifupa, huchangamsha mtu, na kumsaidia mtu apate usingizi,” lasema gazeti Tufts University Health and Nutrition Letter. Isitoshe, “muda utakaoishi unategemea sana afya yako.” Wanaume wapatao 6,000 wenye umri wa makamo walichunguzwa kwa miaka 13 na watafiti katika Chuo Kikuu cha Stanford na Shirika la Kushughulikia Afya ya Mashujaa wa Vita wa Marekani. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba mtu anayeweza kufanya mazoezi kwa muda mrefu kabla hajachoka anaweza kuishi kwa muda mrefu zaidi. Ingawa uchunguzi mwingine unaonyesha kwamba urithi unachangia kiasi cha mazoezi ambayo mtu anaweza kufanya, hata kufanya mazoezi “mepesi” kila siku, kama kutembea haraka-haraka, husaidia kudumisha afya bora.
Kuwauzia Vijana Pombe
“Karibu kijana mmoja kati ya 10 nchini Australia amezoea kunywa pombe,” lasema gazeti Sunday Telegraph la Australia. Profesa Ian Webster, msimamizi wa Baraza la Australia la Pombe na Dawa za Kulevya, asema vijana wamezoea kunywa pombe sana hivi kwamba wanaona njia bora zaidi ya kutumia siku zao za mwisho wa juma ni “kunywa kupindukia.” Gazeti The Sydney Morning Herald laripoti kwamba wataalamu fulani wana wasiwasi kuhusu “biashara inayoendelea ulimwenguni pote” ya kutangaza bidhaa ya kuwashawishi vijana wanywe pombe. Watafiti waligundua kwamba watangazaji wengi wa pombe wana vituo vya Internet vinavyolenga vijana. “Vituo hivyo hutangaza tiketi za kuingia katika maonyesho ya muziki, uhakiki wa sinema, na habari zinazohusu pombe.” Kulingana na ripoti hiyo, Shirika la Afya Ulimwenguni linahofia kwamba matangazo yote hayo “yatafanya vijana wazoee pombe.”
Kujitenga na Jamii
Tabia mpya inawaathiri vijana walio na umri wa kati ya miaka 13 hadi 20 na kitu nchini Japan. Tabia hiyo inayoitwa hikikomori (kujitenga kabisa na jamii), imedhihirika katika uchunguzi unaohusu baadhi ya uhalifu mbaya uliofanywa na vijana waliojitenga na jamii. “Uchunguzi kuhusu maisha ya wahalifu hao ulionyesha kwamba vijana walizoea kujitenga, kujifungia katika vyumba vyao wakiwa na kompyuta au mchezo wa video pekee,” laripoti gazeti la tiba The Lancet. Uchunguzi mwingine unaonyesha kwamba tabia hiyo inachochewa sanasana na uchovu kuliko jeuri. Hata hivyo, “watu wengi wanafikiri tabia hiyo inasababishwa na utajiri, tekinolojia, na maisha ya starehe ya kisasa ya Wajapan,” lasema gazeti The Lancet. “Vijana wengi wenye tabia hiyo hutumia wakati wao mwingi wa mchana wakitazama Internet au wakicheza michezo ya video, huku wakila vyakula vyepesi wanavyopelekewa nyumbani.” Makadirio fulani yanaonyesha kwamba idadi ya vijana wanaojitenga nchini Japan ni milioni moja.