Je, Viatu Vyako Vinakutoshea Vizuri?
Je, Viatu Vyako Vinakutoshea Vizuri?
“Avaaye kiatu ndiye ajuaye mahali kinapomfinya.”—INASEMEKANA NI USEMI WA MROMA MMOJA MWENYE HEKIMA.
MARA yako ya mwisho kununua viatu ilikuwa lini? Je, vilikutoshea? Je, ulijihisi vizuri ulipovivaa? Ulitumia muda mrefu kadiri gani kuvichagua? Je, muuzaji alikusaidia? Je, ulivinunua kwa sababu ya mtindo bila kuzingatia iwapo vinakutoshea vizuri? Baada ya kuvitumia kwa muda fulani, unahisije sasa unapovivaa? Je, vinakufinya?
Kununua viatu si rahisi hata kidogo. Na kupata saizi yako ni kibarua kigumu hata zaidi. Kwa nini?
Kupata Viatu Vinavyokutoshea
Kwanza, ni mguu upi ulio mkubwa zaidi—wa kulia au wa kushoto? Je, unafikiri miguu yote miwili inalingana? Ikiwa ndivyo, chunguza jambo hilo tena! Pia, inafaa uzingatie kwamba vipimo vya kila mguu hubadilika chini ya hali hizi nne: mtu anapoketi, anaposimama, anaposonga, na hali ya hewa inapobadilika. Tofauti ya vipimo hivyo ni nini?
Kitabu Professional Shoe Fitting chasema hivi: ‘Kipimo cha kwanza hubainika miguu inapokuwa imetulia (mteja akiwa ameketi).’ Kipimo cha pili hujulikana mtu anaposimama wakati miguu inapotegemeza uzito wa mwili. Mtu anaposimama, ukubwa na umbo la mguu hubadilika. Kitabu hicho kinasema hivi: “Mguu unapokuwa umetulia, mifupa na nyama hulegea, lakini mtu anaposimama, zinakazika mara moja na kubadili vipimo vya miguu.” Lakini vipimo vya miguu hubadilika pia katika hali nyingine mbili.
Kipimo cha mguu wakati mtu anaposonga kinatia ndani wakati anapotembea, anapokimbia, anaporuka, au anapofanya mazoezi mengine. Utendaji huo “hubadili umbo na ukubwa wa mguu na vilevile jinsi unavyoenea ndani ya kiatu.” Kipimo cha nne hujulikana wakati ukubwa wa mguu unapobadilika kwa sababu ya joto na unyevu. Hilo linaweza kuongeza ukubwa wa mguu kwa asilimia 5. Hiyo ndiyo sababu wewe hujisikia nafuu
unapovua viatu jioni, hasa ikiwa viatu vyako havikutoshei! Na kwa hakika, watu wengi huvaa viatu visivyowatoshea.Miguu Yako Hupimwaje?
Kwa miaka mingi, Eric alikuwa akinunua viatu vya saizi 10 na nusu au saizi 11 vyenye upana wa wastani. Wakati huo, alikuwa akiumia kwa sababu kidole kimoja cha mguu wake kilikuwa kimejikunja na kuota sugu na vilevile kidole kikubwa cha mguu wake wa kushoto kilikuwa na kucha iliyoota kuelekea ndani. Daktari mmoja wa miguu alidokeza kwamba ingefaa aende kupimwa saizi ya miguu yake na mtu aliye na ujuzi huo. Eric alishangaa alipogundua kwamba ili viatu vimtoshee vizuri anapaswa kuvaa viatu vya saizi 12 na nusu vyenye upana wa A! Herufi “A” inaonyesha kwamba mtu ana mguu mwembamba. * Lakini, je, inatosha kujua tu urefu na upana wa viatu unavyostahili kuvaa? Ni njia ipi iliyo bora ya kupima miguu?
Katika nchi fulani, kifaa kinachoitwa Brannock ndicho hutumiwa hasa kupimia miguu. (Ona picha.) Kifaa hicho kinaweza kutumiwa kuonyesha vipimo vitatu muhimu: urefu wa mguu wote, urefu unaoanzia kwenye kisigino hadi kwenye mfupa wa mviringo ulio chini ya kidole kikubwa, na upana unaopimwa kuanzia kwenye mfupa huo hadi kwenye kidole kidogo. Lakini, umbo na ukubwa wa kila mguu hutofautiana. Ndiyo sababu sisi hupima viatu kabla ya kuvinunua. Hata hivyo, kuna hatari fulani. Je, umewahi kupima viatu vilivyokuvutia sana kisha ukagundua kwamba vinakufinya kidogo? Labda vinakufinya kidogo tu au ni vikubwa kidogo. Na duka hilo halina viatu vingine vinavyokutoshea. Kisha muuzaji anakuambia: “Ah! Viatu hivi vitapanuka.” Unavinunua, halafu baada ya kuvitumia kwa siku chache au majuma kadhaa unaanza kujuta. Vidole vinaanza kuota sugu, kucha ya kidole kimoja inaanza kuota kuelekea ndani, au unapata uvimbe kwenye kidole kikubwa!
Je, Wewe Hununua Viatu Vinavyokutoshea Kabisa-Kabisa?
Je, inawezekana kupata viatu vinavyokutoshea kabisa-kabisa? Kitabu Professional Shoe Fitting kinasema kwamba haiwezekani. Kwa nini? “Kwa sababu ya hali fulani zisizoweza kubadilishwa. . . . Hakuna mtu ambaye ana miguu inayolingana kwa ukubwa, umbo, wala miguu inayosonga kwa njia ileile.” Kwa hiyo ikiwa mguu wako mkubwa unatoshea vizuri kabisa ndani ya kiatu, hiyo haimaanishi kwamba ule mguu wako mwingine utatoshea. “Hiyo haimaanishi kwamba mtu hawezi kupata viatu vinavyomtoshea vizuri, bali tunapaswa kufikiri sana kabla hatujasema kwamba viatu vinamtoshea mtu ‘kabisa-kabisa.’”
Ikiwa unataka kujua mahali ambapo miguu yako inasuguana zaidi na viatu, chunguza viatu ambavyo umevitumia tayari. Chunguza kitambaa kilicho ndani ya kiatu. Kimezeeka sana upande gani? Mara nyingi kitambaa hicho huzeeka nyuma ya kisigino na karibu na ule mfupa wa mviringo ulio chini ya kidole kikubwa. Hiyo inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba “sehemu fulani za kiatu hazipatani sawasawa na sehemu mbalimbali za mguu wako. Sehemu fulani za kiatu zinazeeka huku sehemu nyingine zinabaki zikiwa mpya kabisa.”
Hata muundo wa sehemu ya kufungia kamba ni muhimu ili mtu astarehe. Je, unajua kwamba viatu mbalimbali vimeundwa kwa njia tofauti-tofauti kwenye sehemu ya kufungia kamba? Muundo wa bal unakuwezesha kukaza kamba na kuunganisha vile vipande viwili vya mbele. Hata hivyo, ikiwa una miguu minene, basi utastarehe zaidi ukivaa viatu vyenye muundo wa blucher vinavyokuwezesha kulegeza kamba na kutenganisha vile vipande viwili vya mbele. (Ona picha.) Dokezo hilo lina faida gani? Kitabu kilekile kilichonukuliwa awali chasema: “Mara nyingi watu huumizwa na viatu kwa sababu ya kukaza sana shingo ya kiatu, na hilo hufanya kisigino kisugue sehemu ya nyuma ya kiatu.”
Namna Gani Viatu vya Wanawake Vyenye Visigino Virefu?
Wanawake hupenda viatu vyenye visigino virefu, navyo huathiri mwili kwa njia mbalimbali. Viatu vyenye visigino virefu hubadili jinsi mtu anavyosimama. Mara nyingi vinamfanya mtu ainame kidogo na kumlazimu akunje magoti ili asimame wima. Viatu vyenye visigino virefu hukaza misuli iliyo nyuma ya miguu na kuifanya ionekane zaidi.
Hivyo, kisigino ndiyo sehemu muhimu zaidi ya kiatu cha mwanamke, nacho humfanya astarehe au kuumia. Kitabu Professional Shoe Fitting kinasema kwamba kuna sababu tatu za kuweka visigino virefu kwenye viatu: ‘(1) kuongeza “hadhi” ya mtu, kama vile kwa kumfanya aonekane mrefu, (2) ili kuongeza umaridadi wa kiatu, na (3) kuvutia—kwa mfano viatu vya wanawake vyenye visigino virefu huboresha umbo la miguu.’
Wanawake wanapaswa kuzingatia hasa muundo wa kisigino cha kiatu kwani hilo ndilo linaloamua mahali ambapo kisigino kitashinikizwa zaidi na uzito wa mwili. Uzito wa mwili unapolemea sehemu ya nyuma au ya mbele ya kisigino, hilo linaweza kusababisha hatari. Kwa nini? Kwa sababu jambo hilo linaweza kufanya kisigino kikatike na kumfanya aliyevaa viatu hivyo aanguke vibaya sana.
Kupitia mazungumzo haya mafupi, imebainika wazi kwamba ili mtu anunue viatu vinavyomfaa kabisa anahitaji wakati mwingi na labda pesa nyingi zaidi, kwani inachukua muda mrefu zaidi kuunda viatu vizuri. Viatu vyako vinaweza kukustarehesha na kukuwezesha uwe na afya bora. Basi, usinunue viatu mbiombio. Jipime sawasawa. Uwe na subira. Usipumbazwe na mtindo wala muundo wa viatu.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 10 Katika nchi fulani, mbali na kutumia namba, herufi hutumiwa pia kuonyesha upana wa kiatu.
[Sanduku katika ukurasa wa 20]
Mambo Muhimu ya Kuzingatia Unapochagua Viatu
Katika kitabu chao Professional Shoe Fitting, William A. Rossi na Ross Tennant wanatoa madokezo yafuatayo.
“Kusudi la kupima mguu si kumwezesha mtu ajue saizi ambayo itamtoshea, kama vile watu wengine wanavyodhania.” Kwa nini? Kwa sababu saizi ya viatu inategemea mambo mengi kama vile, urefu wa kisigino, mtindo, muundo, vifaa vilivyotumiwa, na kampuni iliyotengeneza viatu hivyo. Jambo hilo ni kweli kwani nchi nyingi sana zinatengeneza viatu kwa kutumia viwango tofauti-tofauti.
Urefu wa mguu wako unapopimwa, vuta soksi mbele ili vidole vyako visijikunje, kwani hilo litafanya vipimo visiwe sahihi.
Unapaswa kupimwa ukiwa umeketi au ukiwa umesimama? “Haifai kumpima mteja akiwa ameketi.” Kufanya hivyo kunatokeza vipimo visivyo sahihi. Basi, simama miguu yako inapopimwa. Naam, si mguu mmoja bali miguu yote miwili. Usifikiri kwamba mguu wako wa kushoto ndio mkubwa zaidi. Unapaswa kupimwa miguu yote miwili!
“Kupima viatu kwa usahihi ni ustadi na ufundi wa watu wenye ujuzi ambao wanafanya kazi katika maduka makubwa na ambao wanaelewa na kutambua umuhimu wa kuwasaidia watu kupata viatu vinavyowatoshea vizuri.”
[Mchoro katika ukurasa wa 19]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Sehemu za kiatu
shingo
kitambaa cha ndani
soli ya kisigino
upande wa ndani wa kisigino
soli
kipande cha mbele
kitambaa cha kisigino
upande wa kiatu
ulimi wa kiatu
kifuniko cha vidole
kisigino
sehemu ya kamba
kipande cha mbele
ngozi inapoungana na soli
soli ya nje
[Picha katika ukurasa wa 20]
Kifaa cha Brannock
[Picha katika ukurasa wa 21]
Mitindo yote ya viatu hutegemea miundo hii saba
[Picha katika ukurasa wa 21]
Miundo ya sehemu za kamba
Muundo wa blucher
Muundo wa bal