Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Miti Hupunguza Uchafuzi wa Hewa Mijini
Gazeti la The Sunday Times la London linasema kwamba “kwa mara ya kwanza wataalamu wameweza kupima jinsi aina mbalimbali za miti zinavyopunguza uchafuzi wa hewa.” Kwa miaka mitatu wanasayansi kutoka Uingereza na Scotland wamechunguza udongo uliochotwa karibu na miti 32,000 hivi ili kuona ni miti gani inayopunguza uchafuzi wa hewa zaidi. Wanasayansi hao walipima vilevile kiwango cha uchafuzi angani na katika tabaka la ozoni. Miti aina ya ash, larch, na msindano wa Scotland iliondoa uchafu hewani zaidi; na muoki, willow, na poplar iliondoa kiwango kidogo zaidi. Uchunguzi huo ulionyesha pia kwamba “miti huondoa uchafu hewani mara tatu zaidi kuliko nyasi.” Maonyesho ya kompyuta yalionyesha kwamba ikiwa miti ingepandwa katika nusu tu ya sehemu zisizo na miti za West Midlands, uchafuzi wa hewa ungepunguzwa kwa asilimia 20.
Kuvumbua Aina Mpya za Wanyama
Mtaalamu wa nyani Marc van Roosmalen amevumbua aina mbili za tumbili katika msitu wa mvua wa Amazon. Aina nyingine nane zimevumbuliwa tangu mwaka wa 1990 katika eneo hilo. Van Roosmalen alipohojiwa na mwandishi wa gazeti la National Geographic Today, alisema hivi: “Sikujua kwamba kuna mambo mengi hivi yasiyojulikana katika msitu wa Amazon mpaka nilipoanza kuvumbua wanyama hao wote.” Van Roosmalen ambaye amevumbua aina tano za tumbili tangu mwaka wa 1996 anasema kwamba kupata wanyama ambao hawajavumbuliwa “hakutegemei ujuzi.” Aina nyingi zimepatikana kwa kutembelea tu vijiji vya mbali vya Wahindi wa Amazon na kuchunguza wanyama walio nao nyumbani kwao. Mtaalamu wa wanyama Anthony Rylands anasema hivi kuhusu uvumbuzi huo wa hivi majuzi katika gazeti la Brazili la Folha de Paulo: “Kwa sababu msitu wa Amazon unaendelea kuharibiwa, inawezekana kwamba wanyama fulani wataangamia kabla hawajavumbuliwa.”
Dini Zinaendelea Kupingwa Nchini Georgia
Gazeti la The New York Times linasema kwamba ‘leo Mashahidi wa Yehova walikuwa wamepanga kufanya kusanyiko kwenye uwanja karibu na mto, lakini watu wenye ghasia walifika usiku uliotangulia. Wanaume 24 wa Kanisa Othodoksi la Georgia, ambao walikuwa wamevaa mavazi yenye misalaba, walifika kwa mabasi na kusaka nyumba ya mwenye uwanja, Ushangi Bunturi. Waliweka Biblia, vichapo vya kidini na vitu vya Bwana Bunturi uwanjani na kuviteketeza. Walijaza kidimbwi cha ubatizo mafuta ya dizeli. Polisi walikuwapo pia, kutia ndani mkuu wa polisi wa eneo hilo. Hakuna yeyote aliyekamatwa. Ni kana kwamba shambulizi hilo lilikuwa limepangwa.’ Gazeti la Times linasema kwamba kumekuwa na chuki ya kidini ‘katika jamhuri nyingi zilizokuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti, kutia ndani Urusi. Lakini huko Georgia chuki hiyo imesababisha jeuri kali zaidi dhidi ya dini ndogo-ndogo na kuna uthibitisho kwamba watu wenye mamlaka wameunga mkono mashambulizi hayo. Uhuru wa kidini ulihakikishwa katika katiba iliyoanza kutumiwa baada ya Georgia kujitenga na Muungano wa Sovieti. Lakini fujo inaongezeka na watu wenye ghasia wamefanya mashambulizi mengi sana, mali zimeteketezwa, na watu wamepigwa.’
Vijana Wamiminika Katika “Kanisa Lenye Raha”
Gazeti la Ujerumani la Nassauische Neue Presse lilizungumzia sherehe ya kwanza ya Siku ya Vijana wa Kanisa iliyopangwa na kanisa la Protestanti huko Hesse na Nassau. Habari hiyo ilikuwa na kichwa “Vijana Walipenda ‘Kanisa Lenye Raha.’” Watu 4,400 hivi walihudhuria sherehe hiyo ya siku tano. Kulikuwa na mikutano na majadiliano, ibada ya usiku na nyimbo, huku mishumaa ikiwaka. Pia kulikuwa na michezo mingi, karamu, na wanamuziki waliotumbuiza watu. Gazeti hilo lilisema pia kwamba “kati ya mambo 220 yaliyofanywa, hakukuwa na mafundisho yoyote ya Biblia wala ibada ya kawaida ya kanisa.” Padri mmoja wa vijana alishangaa kabisa kusikia “vijana fulani wakiomba mafundisho ya Biblia, ambayo huonwa kuwa yenye kuchosha.” Kijana mmoja alisema hivi: “Sherehe hiyo haihusu sana mambo ya kanisa, lakini ni yenye kufurahisha.”
Dini na Vita
Gazeti la USA Today linasema kwamba “mizozo hatari zaidi leo na yenye umwagaji mwingi wa damu . . . inahusisha dini.” Ni vigumu sana kutatua mizozo hiyo. Gazeti hilo linaongeza hivi: ‘Mambo yanayotumiwa kwa ukawaida kupatanisha pande zinazopigana kwa mafanikio, yaani utayari wa kuafikiana na kusamehe makosa ya zamani, hayana matokeo sana wakati wale wanaopigana wanapodai kwamba Mungu anawaunga mkono. Hali huwa hivyo hata wakati dini inapotumiwa kuwachochea watu waunge mkono upande fulani wa pambano linalohusu ugomvi juu ya ardhi na utawala.’ Imani mbalimbali za kidini zinafanya iwe vigumu hata kusimamisha mapigano kwa muda. Hivyo ndivyo ilivyokuwa huko Kosovo hivi majuzi. Ingawa ilikuwa imefikiriwa kwamba mapigano yakomeshwe wakati wa Ista, haikuwezekana kwa kuwa tarehe ya sherehe ya Ista ya Kanisa Katoliki inatofautiana na ile ya Kanisa Othodoksi. “Kwa hiyo, mapigano yaliendelea,” gazeti la USA Today lilisema.
Ugonjwa wa UKIMWI “Unaenea Sana”
Gazeti la kitiba la Uingereza, The Lancet, linasema kwamba “ulimwenguni pote watu milioni 40 wameambukizwa virusi vya HIV, watu milioni 20 wameuawa na UKIMWI, na watoto 750,000 huzaliwa wakiwa wameambukizwa virusi vya HIV kila mwaka.” Katika mwaka wa 2001 tu, watu milioni tano waliambukizwa UKIMWI na milioni tatu waliuawa na ugonjwa huo. Kulingana na Peter Piot, mkurugenzi mtendaji wa Mradi wa UKIMWI wa Umoja wa Mataifa, ugonjwa huo “unaenea sana,” na bado ungali katika ‘hatua zake za mwanzo-mwanzo.’ Anakadiria kwamba katika miaka 20 ijayo watu milioni 70 watauawa na UKIMWI. Asilimia 30 hadi 50 ya wakazi wa nchi zilizo kusini ya jangwa la Sahara wameambukizwa virusi vya HIV. Kwa sababu vijana wengi wanauawa na UKIMWI, kuna wasiwasi kwamba kufikia mwaka wa 2020 zaidi ya asilimia 25 ya wafanyakazi watakuwa wamekufa. Gazeti la The Lancet linasema kwamba ‘kwa sababu watoto wengi sana hufa, uchumi utaathiriwa wakati ujao.’ Huko Zimbabwe, “kijana mmoja kati ya watano watapoteza mzazi mmoja au wote wawili.”
Faida za Kuwanyonyesha Watoto
Mpasuaji wa mfumo wa neva, Dakt. Sanjay Gupta anaandika hivi katika gazeti Time: “Chakula bora cha watoto wachanga” ni maziwa ya mama. “Watoto wanaonyonyeshwa hawalazwi hospitalini mara nyingi kwa sababu ya magonjwa ya masikio, kuhara, upele, mizio, na matatizo mengine ya afya kama wale wanaonyonyeshwa kwa chupa.” Kumnyonyesha mtoto humlinda na magonjwa ya mfumo wa kupumua. Uchunguzi uliofanywa huko Denmark unaonyesha kwamba “watu wazima walionyonyeshwa kwa miezi saba hadi tisa walipokuwa watoto wana akili nyingi kuliko wale walionyonyeshwa kwa majuma mawili au chini.” Chuo cha Marekani cha Maradhi ya Watoto kinapendekeza kwamba watoto wanyonyeshwe kwa miezi sita na ikiwezekana kwa mwaka mzima au zaidi. Gazeti U.S. News & World Report linasema kwamba “si watoto tu wanaofaidika wanaponyonyeshwa.” Uchunguzi wa wanawake 150,000 katika nchi 30 ulionyesha kwamba “mwanamke anayenyonyesha mtoto kwa mwaka mmoja hupunguza uwezekano wa kupata saratani (kansa) ya matiti kwa asilimia 4.3.” Hata hivyo, “ni nusu tu ya akina mama Wamarekani ambao huwanyonyesha watoto kwa wastani wa miezi miwili au mitatu.”
Amani Katika Familia Inaweza Kuzuia Matumizi ya Dawa za Kulevya
Mtafiti Dakt. Paul McArdle wa Chuo Kikuu cha Newcastle, Uingereza, alisema kwamba uchunguzi wa vijana uliofanywa huko Ireland, Italia, Uholanzi, Uingereza, na Ujerumani, ‘unaonyesha kwamba kukosa amani ndani ya familia ni sababu kuu inayofanya vijana katika nchi za Magharibi watumie dawa za kulevya.’ Gazeti la The Daily Telegraph la London liliripoti kwamba ni asilimia 16.6 tu ya vijana walioishi na wazazi wawili na waliokuwa na amani katika familia zao, hasa uhusiano mzuri na mama, walioanza kutumia dawa za kulevya. Lakini amani ilipokosekana asilimia 42.3 ya vijana walitumia dawa za kulevya. McArdle alisema hivi: ‘Tunawaambia watoto wazi kuhusu hatari za kutumia dawa za kulevya kwenye televisheni na tunaanzisha miradi ya kuzuia matumizi yake shuleni, lakini inaonekana hakuna anayezungumzia daraka la wazazi. Naamini kwamba tunaweza kufanikiwa kuzuia matumizi ya dawa za kulevya ikiwa kuna amani katika familia.’