Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Amkeni! Lasifiwa Mnafanya kazi nzuri sana ya kuchapisha Amkeni! Mnawapa watu tumaini. Mume wangu alipokufa, jirani yangu alinipa magazeti mawili ya kwanza ya Amkeni! Nilikuwa nimevunjika moyo na kuhuzunika, sikutaka kumwona mtu yeyote. Lakini niliposoma magazeti yenu, nilifarijiwa na nikatambua kwamba huo haukuwa mwisho wa maisha yangu. Baadaye binti yangu aliniletea magazeti mengine mawili ambayo muuguzi mmoja alimpa alipokuwa hospitalini. Kisha Mashahidi walinipatia mengine machache barabarani. Ingawa nina magazeti machache ya Amkeni!, mimi huyasoma tena na tena ninapohisi nimevunjika moyo. Hayo hufundisha watu mambo mema na kuwasaidia wajue kwa nini sisi hutenda kwa njia fulani.
I.Y.A., Urusi
Udhaifu Asanteni sana kwa kuandika makala “Maoni ya Biblia: Je, Mungu Hupuuza Udhaifu Wetu?” (Novemba 8, 2002) Sina shaka kwamba huo ni msaada bora zaidi niliowahi kupata. Nilifaidika sana kufahamu jinsi Mungu anavyouona udhaifu wetu.
E. C., Marekani
Nimesali kwa Yehova mara nyingi kuhusu tatizo ambalo nimekuwa nalo, nikitumaini kwamba atanijibu. Halafu mkaandika makala hiyo. Nilipomaliza kuisoma, nilitoa sala ya shukrani.
M. S., Japan
Kibodi Ninawaandikia ili niwashukuru kwa makala kuhusu kibodi ya piano inayosema “Je, Unajua Tofauti?” (Novemba 8, 2002) Sikuzote nilipenda muziki, hasa muziki wa piano. Ningependa kujua kucheza baadhi ya nyimbo ambazo sisi huimba katika Jumba la Ufalme. Kwa hiyo nitajaribu kuzicheza nikitumia chombo cha synthesizer ambacho kimekuwa nyumbani kwa miaka kadhaa.
V. T., Marekani
Kwa kuwa ninajua kucheza zumari na ninapenda muziki, nilitaka kufahamu kuhusu vyombo mbalimbali vya muziki vinavyotumia kibodi. Miaka sita iliyopita, nilianza kujifunza kuhusu piano, somo ambalo singeweza kugharimia bila kutumia piano inayotumia kompyuta. Piano hiyo hutoa sauti kama ya piano ya kawaida na pia ya kinubiuzi.
S. T., Scotland
Nimekuwa nikisomea muziki shuleni. Ingawa nilijua mambo machache kuhusu vyombo vya muziki vinavyotumia kibodi, sikuelewa jinsi vilivyoundwa au vilitengenezwa na nini. Makala hiyo, yenye maelezo sahili na picha maridadi, ilinisaidia nifahamu zaidi kuhusu vyombo vya muziki. Asanteni sana.
A. M., Japan
Sanamu ya Ukumbusho Asanteni kwa makala “Mlima Wachongwa Kuwa Sanamu ya Ukumbusho.” (Novemba 8, 2002) Makala hiyo ilikuja wakati nilipokuwa nikijitayarisha kuandika insha kuhusu makabila ya Sioux na Cheyenne na maisha yao. Mwalimu wangu aliisifu insha yangu! Asanteni sana.
F. V., Marekani
Kukutana Tena Nimemaliza tu kusoma makala “Wakutana kwa Njia ya Pekee Baada ya Miaka 30.” (Oktoba 22, 2002) Nimejawa na shukrani, furaha, na huzuni. Ninafurahi kwa kuwa Mark Ruge na Dennis Sheets walipata kumjua Yehova. Hata hivyo, nina huzuni kwa kuwa baadhi ya watoto wangu watano hawajamjua Yehova licha ya kulelewa katika familia ya Kikristo. Wangeepuka maumivu mengi ya moyoni na mateso ikiwa wangejua njia ya Mungu! Ninasali kwamba siku moja wataipata njia hiyo. Asanteni sana kwa makala hiyo. Imeleta manufaa mengi.
M. O., Marekani