Ni Nani Atakayeokoa Misitu ya Mvua?
Ni Nani Atakayeokoa Misitu ya Mvua?
MTU yeyote anayetaka kutatua matatizo yanayoipata misitu ya mvua lazima kwanza atatue visababishi vyake. Visababishi gani? Tatizo si kuongezeka tu kwa idadi ya watu. Maeneo yenye rutuba duniani yanaweza kuwalisha watu wote ulimwenguni—na hata wengi zaidi.
Katika nchi kadhaa, serikali zinahangaishwa na kuwapo kwa mazao mengi sana mashambani, ambayo yanafanya bei ya chakula ishuke. Serikali fulani huwatia moyo wakulima watumie mashamba yao kwa shughuli za burudani kama vile, maeneo ya kupiga kambi, viwanja vya gofu, au bustani za wanyama-pori.
Basi kwa nini misitu inapungua ulimwenguni? Ni lazima tuchunguze visababishi vingine vikuu zaidi kuliko vile ambavyo tumetaja.
Visababishi Vikuu vya Uharibifu wa Misitu
Miaka mingi kabla ya watu kuongezeka, serikali nyingi ziliharibu misitu ili kupata mamlaka na utajiri. Kwa mfano, Miliki ya Uingereza ilihitaji mbao za kutengeneza meli na hivyo iliharibu misitu ya mialoni ya Uingereza na misitu ya mivule ya Burma na Thailand. Miliki hiyohiyo iliharibu misitu nchini India ili kupata kuni za tanuru za kuyeyusha chuma. Waliharibu misitu mingine ili wapande mashamba ya mipira, kahawa, na kakao.
Hata hivyo, baada ya vita vya pili vya ulimwengu, misumeno ya minyororo na matingatinga yalitumiwa kuharibu misitu mingi kabisa. Misitu mingi zaidi muhimu iliharibiwa ili kujipatia utajiri.
Makampuni makubwa yalinunua mashamba makubwa yenye rutuba na kutumia mashine kuvuna mazao ya kuuza. Maelfu ya watu walihamia majiji baada ya kupoteza kazi zao. Lakini wengine walihimizwa wahamie misitu ya mvua. Nyakati nyingine maeneo hayo yaliitwa “ardhi isiyo na watu kwa ajili ya watu wasio na mashamba.” Watu walipogundua ugumu wa kulima mahali kama hapo, ilikuwa kuchelewa mno—msitu mkubwa ulikuwa umeharibiwa.
Pia ufisadi wa maofisa wa serikali umeangamiza misitu mingi. Kibali cha kukata miti ni ghali sana. Maofisa fulani wasio wanyofu hutoa kibali cha muda mfupi cha kukata miti baada
ya kupokea hongo kutoka kwa makampuni yanayoharibu misitu bila kujali.Hata hivyo, hatari kubwa zaidi kwa wanyama-pori si ukataji wa miti bali ni kubadili misitu kuwa mashamba. Katika visa fulani, jambo hilo laweza kukubalika ikiwa ardhi hiyo ina rutuba. Lakini mara nyingi, ufisadi au maofisa wasiofaa huwaruhusu watu kukata miti isivyo lazima na kuharibu kabisa misitu.
Wahalifu pia huharibu misitu. Wakataji-miti haramu hukata ovyoovyo miti yenye thamani, hata ile iliyo katika mbuga za kitaifa. Nyakati nyingine wao hupasua mbao humohumo msituni—tabia haramu na yenye kuleta hasara. Wanakijiji hulipwa ili kusafirisha mbao hizo kwa baiskeli au hata mgongoni. Kisha, usiku ukiingia, malori makubwa huzisafirisha kupitia barabara za milimani zisizotumiwa mara nyingi ili kuepuka polisi.
Basi uharibifu wa misitu na kuangamia kwa wanyama-pori hakusababishwi na kuongezeka kwa watu. Mara nyingi husababishwa na usimamizi mbaya, biashara yenye pupa, uhalifu, na serikali zenye ufisadi. Hivyo basi, kuna tumaini gani la kuhifadhi viumbe mbalimbali wanaopatikana katika misitu ya mvua?
Kuna Tumaini Gani kwa Misitu ya Mvua?
“Ni sehemu ndogo tu ya misitu ya mvua ulimwenguni pote inayosimamiwa kwa njia inayofaa,” chasema kitabu The Cutting Edge: Conserving Wildlife in Logged Tropical Forest. Chaongezea hivi: “Kwa sasa, ni misitu michache tu (ikiwa ipo) inayosimamiwa kwa njia inayofaa.” Bila shaka misitu inaweza kusimamiwa kwa njia inayofaa, lakini ukweli ni kwamba misitu inaharibiwa kwa kasi ulimwenguni pote.
Inasemekana kwamba hali ni tofauti sana nchini Bolivia kwa sababu asilimia 25 ya misitu yake ya mvua imethibitishwa kuwa inasimamiwa kwa njia inayofaa. Hata hivyo, misitu inayosimamiwa kwa njia ifaayo ulimwenguni pote haizidi asilimia moja—kiasi kidogo sana chenye kusikitisha. Misitu mingi ya mvua inaharibiwa kabisa. Choyo na pupa ndiyo mambo yanayosababisha uharibifu huo. Je, ni jambo la busara kutumaini kwamba wafanyabiashara na wanasiasa wa ulimwengu watakomesha uharibifu huo na badala yake kuwalinda wanyama na misitu?
Kitabu Forests of Hope chamalizia kwa kuwahimiza wanadamu “wajitahidi kuishi kwa njia inayowafaa watu wote ulimwenguni, bila kuharibu dunia na rasilimali zake.” Mradi huo unavutia lakini je, inawezekana?
Muumba wetu alikuwa na kusudi gani kwa dunia na wanadamu? Aliwaamuru hivi wanadamu wawili wa kwanza: “Mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” (Mwanzo 1:28) Kwa hiyo Mungu huwaruhusu wanadamu watumie uumbaji. Lakini ‘kuutiisha’ si kibali cha kuuharibu.
Basi swali ni, Je, wanadamu wanaweza kweli kubadili maisha yao ulimwenguni pote na kuishi “bila kuharibu dunia na rasilimali zake”? Maneno hayo yanaonyesha upendo kwa jirani na staha kwa uumbaji wa Mungu, sifa ambazo ni haba sana katika ulimwengu huu. Kutumaini kwamba viongozi wa kibinadamu wataishi na kuendeleza maisha hayo ni ndoto tu.
Hata hivyo, Neno la Mungu linatabiri wakati ambapo dunia itajaa watu wanaowapenda wanadamu wenzao na Muumba wao. Biblia husema: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.” (Isaya 11:9; Zaburi 37:29; Mathayo 5:5) Ona kwamba watu wa Mungu “hawatadhuru” wala “hawataharibu” kwa sababu wamemjua na kumpenda Yehova, Muumba Mtukufu. Hapana shaka kwamba watu hao wataepuka kuharibu dunia.
Hii si ndoto tu. Hata sasa, Yehova anakusanya watu wanyofu na kuwafundisha. Mamilioni ya watu ulimwenguni pote wamejifunza kutokana na Neno la Mungu kuishi kwa njia inayoonyesha upendo wa kujidhabihu. (Yohana 13:34; 1 Yohana 4:21) Gazeti hili, pamoja na gazeti la Mnara wa Mlinzi, huchapishwa ili kuwasaidia watu wajifunze mengi na kuishi kwa njia hiyo. Twakualika uendelee kujifunza. Ujuzi huo ni wenye kuthawabisha sana.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mwanadamu ataitunza dunia yenye kupendeza badala ya kuiharibu