Mawaidha Kutoka kwa Rubani Stadi
Mawaidha Kutoka kwa Rubani Stadi
SIKU zote nimefurahia sana kusafiri kwa ndege. Mbali na kumwezesha mtu kusafiri haraka, kunamwezesha mtu apae juu ya mawingu mazito na kusafiri kwenye anga lenye mwangaza wa jua. Nimefurahia kusafiri kwa ndege tangu safari yangu ya kwanza nilipokuwa mvulana mdogo mnamo mwaka wa 1956. Hivyo, nilijifunza kazi ya kuendesha ndege, na pia nimefanya kazi ya kuchunguza misiba ya ndege.
Je, ni salama kusafiri kwa ndege? Unaweza kufanya nini ili upunguze hatari?
Jinsi ya Kupunguza Hatari Unaposafiri kwa Ndege
Kila mwaka ulimwenguni, karibu ndege 18,000 hutua na kupaa kwenye viwanja vingi vya ndege kwa ukawaida, na kusafirisha zaidi ya watu bilioni 1.6, bila kuwa na misiba mingi. Kampuni maarufu ya bima ya Lloyd ya London, inakadiria kwamba ni salama mara 25 zaidi kusafiri kwa ndege kuliko kusafiri kwa gari. Kwa hiyo, hatari kubwa zaidi katika usafiri wa ndege ni wakati ndege inapotua au kupaa kutoka uwanjani. Hata hivyo, kuna mawaidha machache unayoweza kutumia ili kupunguza hatari unapotumia aina hiyo ya usafiri ambayo ni salama kwa kulinganishwa na usafiri mwingine.
● Chagua kampuni ya ndege kwa uangalifu: Si kampuni zote za ndege zinazojulikana kwa kudumisha usalama. Kampuni maarufu za ndege zinajulikana kwa usalama. Zina ndege za kisasa, nazo ni maarufu kwa kudumisha usalama na kuweka ndege katika hali nzuri.
● Fikiria kwa makini mavazi utakayovalia: Manusura wa ndege hukabili hatari ya moto na moshi. Hivyo kuvalia shati zenye mikono mirefu na suruali ndefu kunaweza kukinga ngozi yako kutokana na moto na joto. Mavazi yaliyoundwa kwa nyuzi za asilia yanaweza kukukinga vizuri, lakini mavazi yenye nyuzi zisizo za asilia huyeyuka au kushikamana na mwili kunapokuwa na joto na hivyo kuunguza mwili sana. Mavazi yaliyoundwa kwa ngozi pia hushikamana na mwili yanaposhika moto, kwa hiyo hayapendekezwi. Kuvalia nguo kadhaa juu ya nyingine kunaweza kukukinga kuliko kuvalia nguo moja, na nguo nyeupe ni bora kuliko nguo nyeusi-nyeusi. Viatu vyenye visigino vifupi, hasa vya kamba, vinafaa zaidi kwani vinabaki miguuni na kukuzuia usijeruhiwe au kuungua. Soksi za nyuzi za sufu ni bora kuliko za nyuzi zisizo za asilia.
● Sikiliza matangazo yanayohusu usalama: Kabla ya kuanza safari, wahudumu wa ndege hutoa maelezo mengi kuhusu hatua za kuchukuliwa wakati wa dharura. Iwapo kwa vyovyote msiba fulani unatokea, utahitaji kutoka katika ndege ukitumia madokezo hayo. Kwa hiyo, sikiliza kwa makini. Uchunguzi mmoja kuhusu wasafiri wa ndege nchini Kanada ulionyesha kwamba asilimia 29 tu ya wasafiri ndio waliosoma au kuangalia kadi ya maagizo. Soma maagizo hayo, hasa yale yanayoonyesha jinsi ya kufungua milango na madirisha, kwani huenda ukawa wa kwanza kufika hapo. Fikiria jinsi utakavyofika mlangoni au dirishani kukiwa na giza au moshi. Njia moja ni kuhesabu safu za viti zilivyo kati yako na dirisha au mlango. Hivyo, hata kukiwa na giza, utajua njia ya kutokea.
● Usibebe mizigo mingi mikononi: Gazeti Flight International linasema hivi: “Hatari moja ambayo huwapata wasafiri wengi ni kuangukiwa na mizigo iliyo katika sehemu za kuwekea mizigo, ambazo hazikuwa zimefungwa vizuri au zilifunguliwa na wasafiri wakati wa safari, na kusababisha majeraha mabaya ya kichwa na hata kifo.” Kumbuka kwamba kubeba mizigo mizito mkononi kunaweza kusababisha hatari. Kwa hiyo, wakati wa dharura, acha mizigo YOTE. Zingatia kuokoa uhai wako! Unaweza kupata vitu vingine.
Wakati wa Dharura
Ni vigumu zaidi kutoka kukiwa na moto, moshi, na mvuke. Ripoti moja kuhusu msiba ilisema hivi: “Haikuwezekana kuona kitu chochote ndani ya ndege katika kimo cha zaidi ya sentimeta 30 kutoka sakafuni [kwa sababu ya moshi]. Watu walionusurika katika msiba huo walisema ilikuwa vigumu kujua njia ya kutokea.” Mtu alihitaji kuondoka kwenye ndege haraka ili kunusurika.
Marubani na wahudumu wa ndege wamefundishwa jinsi ya kuwasaidia abiria kutoka kwenye ndege haraka na kwa usalama. Kwa hiyo, fuata maagizo yao upesi. Hata hivyo, siku zote mambo hayaendi kama yalivyopangwa. Kwa sababu ya matatizo katika mfumo wa sauti, wahudumu kujeruhiwa, kuchanganyikiwa, na kelele, joto, na moshi, huenda jitihada za wahudumu zisifanikiwe. Huenda wahudumu wa ndege unayosafiri nayo wanaongea lugha usiyojua na hilo linaweza kutatiza mawasiliano kati yako nao.
Uchunguzi wa misiba unaonyesha kwamba kadiri utakavyojitahidi kuokoka, ndivyo ulivyo na nafasi nzuri ya kunusurika hatari ikitokea. Unahitaji kupanga kihususa vile utakavyotenda na uwe tayari kuchukua jukumu la kujilinda. Pia unapaswa kuwafikiria wale unaosafiri pamoja nao, hasa watoto na wazee, na kuhakikisha hamtaachana wakati wa hatari ili msaidiane. Gazeti Flying Safety linadokeza hivi: “Kukiwa na moshi, shikaneni mikono. Wanaweza kuokoka kwa kuushika mshipi wako.” Mwambie yule au wale unaosafiri pamoja nao jambo unalopanga kufanya dharura yoyote ikitokea.
Njia zote za usafiri ni hatari kwa kiasi fulani, lakini ndege za kisasa za abiria zimetengenezwa kwa njia inayotuwezesha kuepuka hatari nyingi na kuwasili mahali ambapo tunaenda bila kuchoka, tayari kwa ajili ya kazi au likizo. Jitayarishe kwa hali yoyote lakini usiwe na wasiwasi. Starehe na ufurahie safari yako—kama mimi.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Kufundishwa kushughulika na dharura
[Picha katika ukurasa wa 13]
Sikiliza matangazo yanayohusu usalama