Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ondol Ni Njia ya Pekee ya Kupasha Nyumba Joto

Ondol Ni Njia ya Pekee ya Kupasha Nyumba Joto

Ondol Ni Njia ya Pekee ya Kupasha Nyumba Joto

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA KOREA

KWA kuwa ni wakati wa baridi kali huku Korea, tunatetemeka tunapokaribishwa na mwenye nyumba mchangamfu. Nyumba ina joto ingawa hatuoni chombo chochote cha kupasha joto. Baada ya kutoa viatu mlangoni, tunakanyaga sakafuni. Kumbe sakafu ina joto! Tunapoketi sakafuni, tunaweka mikono yetu baridi kwenye sakafu. Mikono yetu baridi inaanza kupata joto.

Karibu nyumba zote nchini Korea zina mfumo wa kupasha joto kupitia sakafuni unaoitwa ondol. Mfumo huo wa pekee unafanyaje kazi? Mfumo huo umebadilishaje maisha ya Wakorea? Kabla ya kujibu maswali hayo, hebu tuchunguze jinsi mfumo wa ondol ulivyobuniwa.

Jinsi Mfumo Huo Ulivyobuniwa

Kupasha sakafu joto kulianza zamani sana hata kabla ya Yesu Kristo kuja duniani. Kulingana na uchunguzi wa vitu vya kale na maandishi ya zamani, huenda Waroma wa kale ndio watu wa kwanza kupasha sakafu joto. * Kufikia karne ya nne hadi ya tano W.K., mfumo wa kupasha sakafu joto ulitumiwa sana katika Rasi ya Korea, na hatimaye ukaitwa ondol. Jina hilo linatokana na neno la Kichina linalomaanisha “mitaro yenye joto.” Kitabu cha historia ya China, Books of Old Tang, kinataja mfumo huo kwa kusema hivi: “Wakati wa baridi [nchini Korea] watu walijipasha joto kwa kupitisha mvuke kwenye mitaro waliyokuwa wamechimba.”

Mfumo wa Kale wa Ondol

Joto la ondol lilitoka kwenye joko. Joko hilo lilikuwa kwenye chumba cha kupikia au kwenye ukuta wa nje wa sebule. Chumba cha kupikia chenye meko matatu kiliweza kupasha joto vyumba vitatu vilivyokizunguka. Ikiwa ungeingia katika chumba cha kupikia cha nyumba ya kale ya Kikorea, huenda ungeona chungu kimoja au vyungu viwili vikubwa vya chuma kwenye moto. Hivyo, moto uliotumiwa kupikia wali au mchuzi ulitumiwa pia kupasha joto chumba kilichokuwa karibu na chumba cha kupikia! Mbinu hiyo haikutumia kuni nyingi.

Kwa kawaida chumba cha kupikia kilijengwa meta moja hivi chini ya chumba kilichopashwa joto. Hivyo, iliwezekana kwa moshi na joto kuingia kwenye mitaro iliyokuwa chini ya sakafu. Hivyo ndivyo mfumo huo unavyofanya kazi.

Mitaro ya chini ya ardhi iliyopitisha joto na moshi iliunganisha joko na mabomba ya kutoa moshi. Joto lililopita kwenye mitaro hiyo lilipasha moto mawe na sakafu ya udongo. Jambo hilo halikuwa rahisi sana. Mambo mawili yalihitaji kutimizwa. Ili kuni ziwake vizuri, moshi ulihitaji kupita haraka kwenye mitaro na kutoka nje kupitia mabomba ya moshi bila kuzuiwa. Hivyo, mitaro mifupi iliyonyooka ilifaa zaidi. Lakini ili sakafu iwe moto, joto na moshi ulihitaji kukaa kwenye mitaro kwa muda mrefu iwezekanavyo. Hivyo, mitaro ilichimbwa kotekote chini ya sakafu, na hivyo kuzuia hewa yenye joto isitoke haraka kwenye bomba la moshi. Mambo hayo yalipotimizwa, chumba kiliweza kupashwa joto usiku mzima kwa moto ambao uliwaka kwa saa mbili hivi.

Inasemekana kwamba miaka mingi iliyopita kulikuwa na chumba kilichopashwa joto kwa mfumo wa ondol ambacho kilidumisha joto kwa njia ya ajabu. Kutokana na jinsi mitaro ya moshi ya chumba hicho ilivyojengwa, sakafu yake ilidumisha joto kwa muda wa siku 45 baada ya kupashwa joto mara moja tu! Inasemekana chumba hicho kilibaki na kiasi fulani cha joto kwa muda wa siku 100. Kwa kusikitisha, chumba hicho kiliharibiwa wakati wa vita vya Korea mapema katika miaka ya 1950. Mnamo mwaka wa 1982, wahandisi walikirekebisha, na watalii hutembelea chumba hicho chenye mfumo wa ondol. Mfumo wake wa kupasha joto haulingani na ule wa chumba cha kwanza. Hata hivyo, kikipashwa joto mara moja kinaweza kudumisha joto kwa muda wa siku kumi wakati wa baridi ya wastani, na siku tatu wakati wa baridi kali hata halijoto ikiwa nyuzi kumi za Selsiasi chini ya kipimo cha kuganda.

Jambo lingine linalofanya mfumo wa ondol ufanye kazi vizuri ni muundo wa sakafu. Mitaro ya moshi ilichimbwa kwanza. Kisha mitaro hiyo ilifunikwa kwa mawe membamba yenye kima cha sentimeta 5 hadi 8 hivi. Mawe yenye kima kikubwa zaidi yalitumiwa kutengeneza sakafu karibu na joko ili kuzuia joto lisipotee kwani sakafu ya sehemu hiyo ina joto jingi zaidi. Halafu udongo wa manjano ulitumiwa kufunika mawe na sakafu ilisawazishwa. Hatimaye, karatasi za manjano ziliwekwa sakafuni.

Upande uliokuwa mbali na joko ulikuwa baridi kuliko mwingine. Wazee kama vile babu, nyanya, wazazi, au wageni waliketi kwenye upande uliokuwa na joto jingi zaidi. Hilo lilikuwa tendo la heshima.

Mfumo wa ondol uliotumiwa kusini mwa Rasi ya Korea ulitofautiana kidogo na ule wa kaskazini. Upande wa kaskazini, hakukuwa na ukuta wa kugawanya jikoni na vyumba vingine. Joto kutoka jikoni na kutoka kwenye mfumo wa ondol lilitumiwa kupasha nyumba joto. Upande wa kusini, ukuta ulitumiwa kugawanya sebule na jikoni, na kuzuia moshi usiingie mahali watu walipoketi.

Wakorea walitumia kuni kuwasha moto jikoni. Kwa hiyo, kwanza walipanga rundo la kuni zilizokauka karibu na jiko. Kisha walitumia karatasi na nyasi kavu kuwasha moto. Makaa yalitumiwa pia. Lakini katika karne ya 20, Wakorea walianza kutumia matofali ya makaa. Chumba kilichopashwa joto kwa mfumo wa ondol kilihitaji kutunzwa vizuri. Iwapo mitaro ya moshi ingekuwa na mianya, gesi ya kaboni monoksaidi ingepenya hadi sebuleni kupitia sakafuni, na labda ingesababisha kifo.

Mfumo wa Kisasa wa Ondol

Mfumo wa kale wa ondol hautumiwi sana siku hizi huko Korea. Badala yake, nyumba za kisasa kutia ndani zile zenye ghorofa hupashwa joto kwa mfumo wa kisasa wa ondol ambao hutumia maji badala ya moshi. Hata hivyo, Wakorea hawakuwa watu wa kwanza kutumia mfumo huo wa kisasa.

Mnamo miaka ya 1900, msanifu wa majengo Mmarekani Frank Lloyd Wright alikuwa akijenga hoteli moja huko Japan. Alipoalikwa nyumbani kwa bwana mmoja Mjapani, Wright aliona kwamba chumba chake kimoja kilikuwa tofauti na vingine vya Wajapani. Sakafu yake ilikuwa imefunikwa kwa karatasi ya manjano na ilikuwa na joto. Chumba hicho kilitumia mfumo wa ondol wa Korea! Bwana huyo Mjapani alikuwa ameona mfumo wa ondol huko Korea akapendezwa sana. Hivyo, aliporudi Japan alijenga chumba chenye mfumo huo nyumbani mwake. Wright naye alipendezwa na “starehe isiyo na kifani ya kukaa katika nyumba iliyopashwa joto kupitia sakafuni.” Papo hapo Wright aliona njia hiyo ya kupasha joto ikiwa bora na akaamua kuitumia katika miradi yake yote ya ujenzi. Wright alivumbua mbinu ya kupasha joto kwa kutumia maji ya moto badala ya hewa yenye joto.

Mfumo wa kupasha sakafu joto ulifaana sana na maisha ya Wakorea wakati huo. Punde tu ulipoletwa nchini humo, ulianza kutumiwa na watu wengi. Leo karibu Wakorea wote huutumia.

Mfumo wa Ondol na Maisha ya Wakorea

Mfumo wa ondol umebadili sana maisha ya Wakorea. Kwa mfano, kwa kuwa sakafu ina joto kuliko hewa ya nyumba, watu wanapenda kuketi sakafuni kuliko vitini. Hivyo, Wakorea wanapendelea kuketi, kula, kuzungumza, na kulala sakafuni. Ili kudumisha sakafu ikiwa na joto nyakati nyingine wao huifunika na blanketi nzito inayoitwa ibul. Watu wa familia wanaporudi nyumbani, wao huifunika miguu yao kwa blanketi hiyo ili kufurahia ushirika na joto pamoja. Huo ni muungano wenye joto!

Maisha ya Wakorea yanapozidi kubadilika na kupatana na yale ya nchi za Magharibi, vijana wanapenda kutumia viti na meza na kulala vitandani. Hata hivyo, Wakorea wengi wanapendelea starehe ya sakafu iliyopashwa joto kwa mfumo wa ondol unaotumia maji ya moto. Utakapotembelea Korea, hapana shaka yoyote kwamba utafurahia mfumo huo wa pekee wa kupasha nyumba joto—ondol.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Mfumo wa aina hiyo ulibuniwa na Waroma na ulikuwa na joko la chini ya ardhi na mitaro ya moshi ambayo ilisambaza joto.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mitaro ya kupasha joto ikionekana kutoka juu

Joko

Mitaro

Bomba la moshi

→ → 2 → →

→ → 2 → →

→ → 2 → →

● 1 → → 2 → → ● 3

→ → 2 → →

→ → 2 → →

→ → 2 → →

[Picha]

Joko lilitumiwa kupika chakula na kupasha joto chumba kilicho karibu

Ubora wa mfumo wa kupasha joto wa “ondol” ulitegemea mabomba na mitaro

[Hisani]

Location: Korean Folk Village ▸

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Katika chumba kilichopashwa joto kwa mfumo wa “ondol,” sehemu yenye joto zaidi ilitumiwa na wazee

[Hisani]

Location: Korean Folk Village