Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Mahakama ya Juu Asanteni kwa makala ya jalada “Mahakama ya Juu ya Marekani Yatetea Uhuru wa Kusema.” (Januari 8, 2003) Makala hizo zilionyesha jinsi ubaguzi wa watu wengi unavyoweza kuonwa kuwa sawa wakati mwingine. Wengi husema kwamba inafaa kuamini kile unachotaka lakini ni mwiko kuongea juu yake. Baada ya kusoma makala hizo, sitaogopa kuwaambia wengine imani yangu ya kidini.
S. O., Japan
Kesi ya Stratton, Ohio, kwa kweli ilikuwa ushindi wa uhuru wa usemi. Uamuzi huo mzuri huenda ukawa na matokeo yenye kushawishi katika sehemu nyingine za ulimwengu kama vile Ufilipino, katika sehemu nyingine ambapo mamlaka imewanyima Mashahidi wa Yehova kibali cha kuhubiri nyumba kwa nyumba. Tunashukuru sana kwa sababu ya ushindi huo muhimu.
N. E., Ufilipino
Chuki Nawashukuru sana kutoka moyoni mwangu kwa ajili ya simulizi la José Gomez, lililokuwa katika makala “Niliwekwa Huru Kutokana na Minyororo Ya Chuki.” (Januari 8, 2003) Kwa miaka mingi, mimi pia nilidhulumiwa. Sasa, simchukii mtu yeyote. Maneno aliyosema José, “Ningekuwa wapi leo iwapo Yehova hangenionyesha rehema?” yananihusu pia. Asanteni kwa ajili ya simulizi hilo zuri linaloonyesha jinsi alivyoshinda chuki aliyokuwa nayo.
N. T., Japan
Mimba Salama Zaidi Nataka kuwashukuru kwa ajili ya makala “Kufanya Mimba Yako Iwe Salama Zaidi.” (Januari 8, 2003) Makala hiyo ilinisaidia kuelewa vizuri mambo yanayohusika wakati wa mimba. Nina umri wa miaka 32, na nilihitaji makala hii kwelikweli. Sasa naelewa kile ambacho lazima nifanye ili kuhakikisha kwamba ninakuwa na mimba salama na kuthamini zawadi hii ya pekee.
B. C., Italia
Makala hiyo inataja kwamba mwanamke anaweza kupimwa kama ana bakteria za kundi la B streptococcus kwenye juma la 26 hadi la 28 la mimba. Pendekezo la kisasa kwa ajili ya kupimwa huko ni kati ya juma la 35 hadi la 37 la mimba wala si juma la 26 hadi la 28. Wasomaji wa makala hiyo huenda wakawauliza madaktari wao kwa nini hawapimwi kwenye juma la 26 hadi la 28. Huenda madaktari wao wakasema kwamba Amkeni! si chanzo kinachotegemeka cha habari kwa ajili ya wagonjwa.
L. S., Marekani
“Amkeni!” linajibu: Matoleo yetu hutayarishwa mapema ili kuwe na wakati wa kutosha wa kuyatafsiri katika zaidi ya lugha 80. Wakati makala hiyo kuhusu mimba salama ilipoandikwa, wengi walikubali kwamba kati ya juma la 26 na la 28 ndio wakati unaofaa wa kupimwa. Hata hivyo, mwezi wa Agosti 2002, American Academy of Pediatrics lilitoa habari iliyorekebishwa ambayo lilipata kutoka kwa U.S. Centers for Disease Control. Kwa sasa, kama vile msomaji huyo anavyosema kwa usahihi, wakati unaopendekezwa wa kupimwa ni kati ya juma la 35 hadi la 37.
Katika ukurasa wa 12, kielezi kinasema kwamba madini ya chuma na vitamini C zaweza kupatikana katika maini na njugu. Hata hivyo, maini huwa na vitamini A nyingi—ambayo, kama makala yenu ilivyosema, yaweza kuwa hatari kwa mtoto.
B. J., Uingereza
“Amkeni!” linajibu: Asante kwa tahadhari hiyo.
Kuathiriwa na Vijana Wengine Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 15 ambaye huona vigumu kukabiliana na msongo wa marika. Nilifurahi sana kuona makala hiyo yenye kichwa “Vijana Huuliza . . . Nawezaje Kuepuka Kuathiriwa na Vijana Wenzangu?” (Desemba 22, 2002) Kusoma juu ya vijana wengine ambao wamekuwa na matatizo kumenihakikishia kwamba siko peke yangu. Tunaweza kushinda msongo wa marika kwa msaada wa Mungu Mweza Yote. Asanteni sana kwa habari hiyo, iliyofika kwa wakati unaofaa.
K. R., Australia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]
Photo by Josh Mathes, Collection of the Supreme Court of the United States