Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mitindo Inayobadilika

Mitindo Inayobadilika

Mitindo Inayobadilika

IWE tunatambua au la, maamuzi yetu ya kila siku kuhusu mavazi tutakayovaa huathiriwa kwa kiasi fulani na mitindo. Kwa hiyo, nguo zinazouzwa madukani hutegemea sana athari zenye nguvu za mitindo.

Hata mavazi tunayoyapuuza sasa yalipendwa sana wakati mmoja. Kwa mfano, shati na tai za wanaume, zilianza kupendwa sana zaidi ya karne moja iliyopita. Na sweta za wanawake zilianza kuvaliwa katika miaka ya 1920.

Mambo mawili ambayo huchochea mitindo ni tamaa ya watu ya kutaka kuwa na vitu vipya na pia kutotaka kuwa tofauti na wengine. Karibu kila mtu anapenda kuvaa kitu kipya. Ndiyo sababu nyakati nyingine tunanunua mavazi, si kwa sababu mavazi tuliyo nayo yamechakaa, bali kwa sababu tunataka mengine. Pia, hatutaki kuonekana tukiwa tofauti na wengine, kwa hiyo tunanunua mavazi ambayo kwa kiasi fulani yanapatana na mitindo inayovaliwa na wenzetu. Kwa karne kadhaa mitindo imetosheleza—na hata wakati mwingine imetumia vibaya—tamaa ya watu ya kutaka kuwa na vitu vipya na pia kutotaka kuwa tofauti na wengine.

Historia Fupi

Ili kuanzisha mtindo fulani, wanaobuni mitindo hutumia mambo matano ya msingi: rangi, maumbo, mikunjo, mifumo, na mapambo ya kitambaa. Kadiri ambavyo miaka imepita, kumekuwa na vitambaa vya rangi, maumbo, mikunjo, mifumo, na mapambo chungu nzima, ambavyo wabuni na washonaji wanaweza kutumia. Kwa mfano, katika Misri ya kale, kitani kinachoonyesha mwili ambacho kilitengenezwa nchini humo ndicho kilichopendwa sana, nacho kilifaa wakati wa joto. Lakini kwa kuwa kitani hakingeweza kutiwa rangi kwa urahisi, kwa kawaida kilikuwa cha rangi moja tu, nyeupe. Hata hivyo, wabuni Wamisri walishona vitambaa na kuvitia mikunjo na maumbo yenye kupendeza. Basi, mojawapo ya mitindo yenye kudumu zaidi ulimwenguni ikabuniwa.

Kufikia karne ya kwanza W.K., vitambaa na rangi mpya zikapatikana. Waroma matajiri walinunua hariri kutoka China au India, ingawa gharama ya kuzisafirisha ilifanya hariri zilizofumwa ziwe ghali kama dhahabu. Sufu iliyotiwa rangi kutoka Tiro ilipendwa sana pia. Kilo moja ya sufu hiyo iligharimu dinari 2,000—mshahara wa miaka sita wa mfanyakazi wa kawaida. Kuwapo kwa rangi hizo mpya pamoja na vitambaa hivyo vipya, kuliwawezesha wanawake Waroma wenye mali kuvaa stola, yaani vazi refu la nje la pamba la bluu kutoka India au hariri ya manjano kutoka China.

Ingawa mitindo mipya ilizuka pindi kwa pindi, katika enzi zilizopita mavazi ya bei ghali yangeweza kudumu kwa muda mrefu. Mitindo hiyo ilibadilika polepole na mara nyingi iliathiri wastaarabu tu. Hata hivyo, mvuvumko wa kiviwanda ulipoanza, mitindo ilianza kuwaathiri hata zaidi watu wa kawaida.

Katika karne ya 19, viwanda vizima-vizima vilianzishwa ili kutengeneza nguo kwa ajili ya matajiri na maskini. Mashine za kufuma pamba na sufu zikawa nyingi, nazo bei za vitambaa zikashuka. Kwa sababu ya mashine za kushona, mavazi yangeweza kutengenezwa kwa bei rahisi zaidi, na rangi mpya za sanisia zikawezesha kuwapo kwa vitambaa vya rangi nyingi.

Mabadiliko ya kijamii na ya kitekinolojia yalitimiza fungu kubwa hata zaidi katika kutengeneza mavazi kwa ajili ya watu wa kawaida. Katika Ulaya Magharibi na Amerika Kaskazini, watu walikuwa na pesa nyingi zaidi za kutumia. Katika miaka ya 1850, magazeti ya wanawake yakatokea, na punde baadaye maduka makubwa yakaanza kuuza nguo zilizoshonwa tayari za saizi mbalimbali. Pia katika karne ya 19, Charles Frederick Worth alianzisha maonyesho ya mitindo akitumia watu mbalimbali ili kuchochea hamu ya waliotarajiwa kununua mavazi hayo.

Katika karne ya 20, nyuzi mpya za sanisia, kama vile rayoni, nailoni, na poliesta, ziliwawezesha watengenezaji kupata vitambaa vya aina nyingi zaidi. Violezo vilivyohifadhiwa katika kompyuta vilifanya iwe rahisi kubuni mitindo mipya, na kwa sababu ya muungano wa ulimwengu, mitindo mipya ingeweza kutokea karibu wakati uleule katika majiji ya Tokyo, New York, Paris, na São Paulo. Wakati huohuo, wabuni na watengenezaji wamepata njia mpya za kuuza bidhaa zao.

Leo, vijana hasa ndio wanaofuatia sana mitindo hata kuliko matajiri. Mamilioni ya vijana hununua mavazi mapya kila mwezi, na viwanda vya mavazi hutengeneza mavazi yenye thamani ya mamia ya mabilioni ya dola kwa mwaka. * Lakini, je, kuna mitego isiyoonekana?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Katika mwaka mmoja hivi karibuni, thamani ya mavazi yaliyotengenezwa ilikadiriwa kuwa dola bilioni 335.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Waanzilishi wa Mitindo

Kwa karne nyingi wafalme na wastaarabu ndio walioanzisha mitindo ya mavazi. Katika karne ya 17, Mfalme Louis wa 13 wa Ufaransa aliamua kuvaa nywele bandia ili kufunika upara wake. Muda si muda, wastaarabu wengine barani Ulaya wakawa wakinyoa nywele zao na kuvaa nywele bandia—mtindo huo ukadumu kwa zaidi ya karne moja.

Katika karne ya 19, magazeti ya wanawake yakaeneza mitindo na hata yalikuwa na violezo ili wanawake wajitengenezee mavazi yao wenyewe kwa bei rahisi. Katika karne ya 20, kadiri ambavyo sinema na televisheni zilienea, watu ulimwenguni pote walianza kuiga mitindo ya watu maarufu. Wanamuziki mashuhuri pia walivalia mitindo ya kiajabu, ambayo iliigwa upesi na vijana wengi. Leo, mambo hayajabadilika sana, watangazaji hutumia maonyesho ya mitindo, magazeti yenye kuvutia, mabango ya matangazo, madirisha ya maduka, na matangazo ya televisheni ili kuwachochea watu wanunue mavazi mapya.

[Picha]

Mfalme Louis wa 13

[Hisani]

From the book The Historian’s History of the World

[Picha katika ukurasa wa 4]

Vazi hili la kale la kitani la Misri lilikuwa mojawapo ya mitindo iliyodumu zaidi ulimwenguni

[Hisani]

Photograph taken by courtesy of the British Museum

[Picha katika ukurasa wa 4]

Katika Roma ya kale wanawake walivaa stola

[Hisani]

From the book Historia del Traje, 1917

[Picha katika ukurasa wa 4, 5]

Vazi la kimono limekuwapo tangu mwaka wa 650 W.K. hivi

[Hisani]

From the newspaper La Ilustración Artística, Volume X, 1891

[Picha katika ukurasa wa 5]

Katika enzi zilizopita vazi la bei ghali lingeweza kutumiwa kwa muda mrefu

[Hisani]

EclectiCollections

[Picha katika ukurasa wa 5]

Mvuvumko wa kiviwanda uliwawezesha watu wa kawaida kupendezwa zaidi na mitindo

[Hisani]

EclectiCollections