Ziwa la Lami la Trinidad na Tobago
Ziwa la Lami la Trinidad na Tobago
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI TRINIDAD
NJIA ya Chini ya Ardhi ya Cross Harbour jijini Hong Kong, Barabara Kuu ya Transalpine huko Austria, na Daraja la Jubilee Way huko Uingereza, zinalingana kwa njia gani? Zote zilijengwa kwa lami * ya pekee inayotoka kwenye Ziwa la Lami la Trinidad na Tobago.
Ziwa la Lami linalojulikana sana lina lami ya asili. Mwaka wa 1814 kamusi moja ya jiografia ilisema kwamba ziwa hilo ni “kitu cha kustaajabisha sana.” Hebu jionee mwenyewe tunapotembelea
ziwa hilo karibu na pwani ya kusini-magharibi ya Trinidad.Kutembea Juu ya Ziwa
Tunapoingia kijiji cha La Brea (yaani, “lami” katika Kihispania), twaona ni kana kwamba vijia vinazama. Hata nyumba fulani zimeinama upande mmoja kana kwamba zinaanguka kwa sababu ya uzito. Hatulifikirii mno jambo hilo, kwani twaona mbele yetu eneo linalofanana na maegesho makubwa yasiyotumiwa. Tumefika kwenye Ziwa la Lami. Yule anayetutembeza anatujulisha kwamba ziwa hilo lina ukubwa wa ekari 115 hivi na kina cha meta 80 hivi katikati. Anatuambia: “Hebu tusonge karibu ili tuone vizuri.”
Twaanza kutembea polepole juu ya ziwa na twagundua kwamba ni gumu lakini si laini. Hata lori kubwa na mashine nyingine nzito zinaweza kusimama juu ya ziwa hilo! (Hata hivyo, zinaweza kuzama polepole zikisimama mahali pamoja kwa muda mrefu.) Lakini, lazima tutembee kwa uangalifu! Sehemu fulani-fulani za lami hiyo ngumu zina bitumeni yenye kunata ambayo inaweza kumtia hofu mgeni asiye na habari kwa kuwa viatu vyake vitakwama.
Tangu tulipowasili, tumekuwa tukipigwa na harufu kali. Twaambiwa, “Ni harufu ya gesi ya hidrojeni-salfaidi.” Ziwa hilo lina kiasi kidogo cha gesi hiyo pamoja na ile ya methani, ethani, na kaboni-dioksidi. Yule anayetutembeza anachota lami kidogo na tunaona kwamba imejaa matundu yaliyofanyizwa na gesi iliyonaswa humo.
Pia kuna wanyama wengi wa pori kwenye Ziwa la Lami. Bata wasiopatikana kwa urahisi wanaoitwa oxyura dominica huishi katika madimbwi ya maji yaliyo juu ya ziwa hilo na kwenye nyasi zilizo kandokando. Huenda hatutamwona ndege huyo mdogo leo, kwa kuwa mara nyingi hubaki tuli au hutumbukia polepole majini mtu anapomkaribia. Tunapopita kati ya nyasi ndefu zinazotufikia kifuani, ndege mwingine aitwaye jacana jacana anatokea ghafula. Ana mwili mweusi na manyoya ya manjano chini ya
mabawa yake. Ndege wa rangi ya zambarau anayeitwa gallinule (Porphyrula martinica) na ndege wengine wanaoishi kwenye sehemu zenye majimaji hupatikana hapa pia. Samaki wadogo huishi kwenye madimbwi yenye maji yasiyo na chumvi, na mamba wa Amerika Kusini huonekana mara kwa mara.Limetumiwa kwa Miaka 400
Yule anayetutembeza anatuonyesha sehemu ya pwani na kusema kwamba mvumbuzi Mwingereza Sir Walter Raleigh alitia nanga katika sehemu hiyo mnamo mwaka wa 1595. Wakati huo, ziwa hilo ambalo sasa liko bondeni lilikuwa eneo tambarare na vijito vya lami vilitiririka kuelekea ufuoni. Raleigh alitumia lami hiyo kuziba mashimo kwenye meli zake zilizovuja na akasema kwamba “ni nzuri sana,” na “haiyeyushwi na jua kama lami ya Norway, hivyo inafaa sana meli zinazokwenda kwenye bandari za kusini.” *
Mnamo mwaka wa 1846, Dakt. Abraham Gesner wa Kanada, ambaye baadaye aliitwa Mwanzilishi wa Viwanda vya Mafuta, alitengeneza mafuta ya taa kutokana na lami ya Trinidad. Aliyaita kerosini. Lakini, mafuta hayo yalikuwa na harufu mbaya kwa sababu ya salfa iliyokuwa kwenye lami. Baadaye, Gesner alivumbua chanzo kingine cha lami ambayo haikuwa na harufu yoyote.
Umuhimu mkubwa wa Ziwa la Lami la Trinidad ulianza kuonekana wakati lami yake ilipoanza kutumiwa kutengeneza barabara. Mnamo mwaka wa 1876, wahandisi walipendekeza itumiwe kutengeneza Barabara ya Pennsylvania huko Washington, D.C. Ijapokuwa barabara hiyo ilitumiwa sana, inasemekana kwamba ilidumu katika hali nzuri kwa miaka 11. Hilo lilifanya lami ya Trinidad iwe maarufu.
Katika miaka ya majuzi, makampuni ya mafuta yametengeneza bitumeni ya bei nafuu kutokana na petroli. Hata hivyo, wahandisi wameendelea kutumia lami ya asili ya Trinidad kutengeneza barabara, madaraja, viwanja vya ndege, na bandari. Kwa nini?
Mchanganyiko wa Pekee
Lami hiyo inapochanganywa na vitu vingine, husaidia barabara kuwa imara, kudumu, kuwa thabiti, kutoteleza, na iwe na rangi ya kijivujivu ambayo huwasaidia madereva kuona wanapoendesha gari usiku. Lami hiyo imetumiwa kutengeneza barabara mahali ambapo joto linazidi nyuzi 40 za Selsiasi na mahali penye baridi
kali ya nyuzi 25 za Selsiasi chini ya kipimo cha kuganda. Barabara za ndege zilizotengenezwa kwa lami hiyo zimedumu kwa muda mrefu licha ya kutumiwa mara nyingi wakati ndege kubwa zinaporuka na kutua. Barabara hizo pia hazimomonyolewi na mafuta yaliyovuja au kemikali zinazotumiwa kuondoa barafu katika viwanja vya ndege. Barabara nyingi za lami zimedumu kwa zaidi ya miaka 20 bila kufanyiwa marekebisho makubwa.Lami ya ziwa la Trinidad ni bora kwa sababu ya mchanganyiko wake wa pekee. Lami hiyo ina bitumeni yenye asilimia 63 hadi 67 ya kemikali ya malthene na asilimia 33 hadi 37 ya asphaltene. Malthene ni aina ya kemikali za petroli zenye kunata ambazo hufanya lami ishikamane. Kemikali hizo zimesemwa kuwa “zinanata na kushikamana sana na hazina mafuta mengi kama bitumeni fulani zinazotengenezwa viwandani.” Kemikali za asphaltene zina hidrojeni na kaboni, nazo hufanya bitumeni iyeyuke inapochomwa na kukauka inapopoa. Hali na mchanganyiko wa kemikali hizo hufanya lami hiyo iwe ya pekee sana hivi kwamba haiwezi kutengenezwa viwandani.
Kuchimba na Kusafisha
Tunasikia kelele ya mashine kubwa na twageuka na kuona mashine ya kuchimba ikikaribia. Ni trekta kubwa yenye meno makubwa ya chuma yanayochota lami. Lami iliyokusanywa hupakiwa ndani ya mabehewa maalumu na kupelekwa kwenye kiwanda cha karibu. Zaidi ya tani milioni tisa za lami zimechimbwa kwenye ziwa hili tangu mwishoni mwa miaka ya 1800! Ikiwa lami itaendelea kukusanywa kwa kiwango cha sasa, inakadiriwa kwamba tani milioni kumi zilizosalia zitadumu kwa miaka mingine 400.
Tani kadhaa za lami zikiisha kukusanywa, shimo linalobaki hutoweka baada ya majuma kadhaa, kana kwamba lami inaongezeka. Hata hivyo, kwa kuwa lami hiyo “ngumu” inanata sana, lami iliyo kandokando husonga polepole na kufunika shimo hilo. Hivyo, ziwa lote huwa linasonga daima pasipo kuonekana.
Je, unakumbuka nyumba zilizoinama ambazo tuliona awali? Zimeinama hasa kwa sababu lami imesambaa ardhini. Watu wanaopanga kujenga nyumba katika eneo hili wanapaswa kuchagua kwa busara mahali watakapojenga.
Yule anayetutembeza anatuambia: “Twende kiwandani.” Lami husafishwa kwa njia rahisi sana. Lami isiyosafishwa hutiwa katika mapipa makubwa, na kila pipa linaweza kubeba zaidi ya tani 100. Lami huyeyushwa humo kwa mvuke wenye joto la nyuzi 165 hivi za Selsiasi unaotoka kwenye mabomba. Lami inapoyeyuka, gesi na maji yaliyomo, ambayo hufanyiza asilimia 30 hivi ya uzito wa lami, hutoka. Kisha, lami huchujwa ili kuondoa vipande vya mbao na mimea. Hatimaye, lami hiyo moto humwagwa katika mapipa ya mbao yaliyolainishwa kwa karatasi ya silikoni. Mapipa hayo hutengenezwa mumu humu kiwandani, na kila moja linaweza kubeba kilogramu 240 hivi za lami. Kazi yote ya kusafisha huchukua muda wa saa 18 hivi.
Yule anayetutembeza anatuambia kwamba “lami iliyosafishwa inaitwa Epuré.” Lami hiyo huchanganyika vizuri na bitumeni iliyotengenezwa viwandani na vitu vingine na kufanyiza mchanganyiko bora wa kutengeneza barabara. Katika miaka ya karibuni imetumiwa pia kutengeneza rangi mbalimbali, vifaa vya kuunganisha vitu, vya kuzuia joto, na vile visivyopenya maji. Kwa hiyo, imetumiwa katika nyumba na majengo mengi kotekote ulimwenguni.
Mwandishi mmoja alikata kauli mwafaka alipoandika hivi: ‘Bidhaa hii ya ajabu iliyoumbwa na Mungu hupendeza sana na kumfanya mtu anayechunguza maumbile astaajabu na kuvutiwa.’ Naam, Ziwa la Lami la Trinidad na Tobago ni mahali pazuri sana pa kutembelea!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Maneno bitumeni, lami ya asphalt, na bereu hutumiwa mara nyingi kumaanisha kitu kilekile. Hata hivyo, bitumeni ni mchanganyiko mweusi wa kemikali ya kaboni na hidrojeni ulio katika lami, bereu, na petroli. Lami nayo ni mchanganyiko mweusi unaonata ambao hubaki wakati mbao, makaa ya mawe, na mboji zinapochomwa kwa moto. Lami inapovukizwa zaidi hutokeza mchanganyiko mzito unaoitwa bereu. Lami na bereu zina kiasi kidogo cha bitumeni.
Petroli, au mafuta yasiyosafishwa, yanapovukizwa hutokeza mchanganyiko ulio na bitumeni nyingi. Bitumeni inayotokana na petroli huitwa pia lami ya asphalt. Hata hivyo, katika sehemu nyingi “lami” hiyo huonwa kuwa mchanganyiko wa bitumeni na vitu kama mchanga au changarawe, ambao hasa hutandazwa barabarani. Katika makala hii, neno lami limetumiwa kumaanisha “lami ya asphalt” isiyosafishwa au iliyosafishwa kutoka kwenye Ziwa la Lami.
^ fu. 11 Biblia pia huonyesha umuhimu wa lami isiyopenya maji. Noa alipoagizwa ajenge safina aliambiwa ‘aifunike ndani na nje kwa lami.’ (Mwanzo 6:14) Na kulingana na Kutoka 2:3 NW, kisafina cha mafunjo kilichotumiwa kumficha Musa kilipakwa “lami na bereu.”
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Ziwa la Lami lina lami ya asili
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kiwanda cha kusafisha lami
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kuchimba lami kutoka ziwani