Nyigu Kimelea Mwenye Manufaa
Nyigu Kimelea Mwenye Manufaa
NYIGU aina ya ichneumon ana sura ya ajabu na yenye kutisha. Lakini kwa nini anaonwa kuwa kimelea? Kwa sababu kwa kawaida hutaga mayai yake juu au ndani ya buu la mdudu mwingine au buibui.
Kuna zaidi ya aina 3,000 za nyigu wa ichneumon huko Amerika Kaskazini. Nyigu hao ni sehemu ya jamii kubwa ya nyigu mbalimbali ambao ni vimelea. Wanasayansi wanakadiria kwamba kuna zaidi ya aina 40,000 za wadudu hao ulimwenguni pote.
Nyigu hao wana ukubwa mbalimbali, kuanzia sentimeta 0.3 hadi sentimeta 5 hivi. Tumbo lao jembamba lililojipinda ni refu kuliko kichwa na kifua pamoja. Nyigu hao wana vipapasio virefu tofauti na nyigu wengine.
Kitu kinachomtofautisha zaidi na nyigu wengine ni mrija unaofanana na sindano ulio kwenye ncha ya tumbo lake. Yeye hutaga mayai kwa mrija huo ambao kwa kawaida huwa mrefu kuliko mwili wake. Mrija huo ni mwembamba kama singa ya farasi na una nyuzi tatu zinazosongasonga ambazo husukuma yai kutoka kwenye mrija.
Nyigu hao hutambuaje buu ambapo watatagia mayai? Nyigu wa kike aina ya Megarhyssa, wa jamii ya ichneumon, ameonekana akigongagonga mti kwa kipapasio chake ili kutambua kelele za buu lililo sentimeta mbili au zaidi chini ya gamba la mti. Anapotambua buu, yeye hugongagonga zaidi. Kisha, yeye huanza kutoboa gamba hilo kwa mrija wake.
Watu ambao wamemchunguza wanasema hivi: “Nyigu anapogusa buu kwa ncha ya mrija, yai moja husukumwa nje ya mrija na kutagwa juu ya buu au karibu nalo.” Yai linapoanguliwa, buu jipya hula mafuta na majimaji ya buu la awali. Kisha buu jipya hufanyiza kifuko cha hariri ambapo linakulia na kuwa nyigu aliyekomaa. Nyigu anapotoka nje ya mti, huwa tayari kuvamia wadudu wengine.
Ingawa inaweza kusemwa kwamba nyigu hao ni vimelea hatari, wana kazi muhimu. Mabuu yao hula wadudu ambao huharibu mimea, kama vile aina fulani ya kunguni, mdudu alaye pamba, aina fulani ya nondo, mbawakawa, na kadhalika. Kwa hiyo, yaelekea nyigu hao huzuia ongezeko la wadudu wanaoharibu mazao.
Hata ingawa nyigu hao ni wengi sana, si rahisi kuwaona kwa sababu wao hula, huzaana, na kutaga mayai mbali na wanadamu. Hao ni baadhi tu ya viumbe wengi ambao wanadamu hawajawaelewa kikamili.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Nyigu wa “ichneumon” akijitayarisha kutaga yai
[Hisani]
Scott Bauer/Agricultural Research Service, USDA