Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mafuta Hutoka Wapi?

Mafuta Hutoka Wapi?

Mafuta Hutoka Wapi?

“NA KUWE na nuru.” Huko Marekani, katika karne ya 19, chanzo kingine cha nuru kilihitajiwa badala ya mafuta ya wanyama, ya nyangumi, na vitu vingine vilivyotokeza nuru hafifu. Suluhisho likawa nini? Mafuta! Yangepatikana wapi?

Mnamo mwaka wa 1859, kondakta wa gari la moshi aliyestaafu, Edwin L. Drake, alikuwa mtu wa kwanza kuchimba kisima cha mafuta chenye urefu wa meta 22 akitumia injini ya kale ya mvuke karibu na Titusville, Pennsylvania, Marekani. Mafuta yalianza kutumiwa sana wakati huo. Mafuta yalipogunduliwa katika sehemu nyingi za ulimwengu, kukawa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kisiasa. Mafuta yakawa chanzo bora cha nuru kilichokuwa kimetarajiwa kwa hamu ulimwenguni.

Muda si muda, watu walijishughulisha sana na ununuzi wa ardhi na uchimbaji wa visima katika maeneo yenye mafuta nchini Marekani. Wakati huo, lilikuwa jambo la kawaida kusikia juu ya watu waliotajirika haraka na wengine waliofilisika baadaye. Inashangaza kwamba Edwin Drake, aliyechimba kisima cha kwanza huko Pennsylvania, alikuwa miongoni mwa wale waliofilisika.

Licha ya usitawi mkubwa wa biashara ya mafuta, baada ya muda mapato ya wauzaji wa mafuta yalipungua kwa mara ya kwanza huko Pennsylvania. Huenda hilo lilisababishwa pia na usitawi huo. Bei ya mafuta ilishuka kutoka dola 20 hadi senti 10 kwa pipa! Uzalishaji mwingi wa mafuta na kujasiria kulifanya bei zishuke, na baadhi ya visima vilikauka upesi. Mfano mmoja ni jiji la Pithole huko Pennsylvania, ambalo leo ni mahame. Jiji hilo lilianzishwa, lilisitawi, na likaachwa ukiwa baada ya mwaka mmoja na nusu hivi. Mabadiliko hayo yamekuwa ya kawaida katika biashara ya mafuta.

Katika mwaka wa 1870, John D. Rockefeller na washirika wake walianzisha Kampuni ya Mafuta ya Standard. Ilikuwa kampuni pekee iliyouza mafuta ya taa kabla ya kampuni nyingine kutokea, hasa nchini Urusi. Marcus Samuel alianzisha kampuni ambayo leo inaitwa Royal Dutch/Shell Group. Isitoshe, kutokana na maarifa ya jamaa ya Nobel, * biashara kubwa ya mafuta ilianzishwa nchini Urusi, na ilitegemea mafuta yaliyochimbwa huko Baku.

Huo ulikuwa mwanzo wa kampuni za mafuta. Tangu wakati huo, mashirika yameanzishwa kudhibiti uzalishaji na kuzuia bei za mafuta zisishuke kama awali. Moja ni Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta (OPEC), lenye nchi 11 zilizo na hifadhi kubwa zaidi ulimwenguni za mafuta yasiyosafishwa.—Ona sanduku katika ukurasa wa 7.

Mafuta Ni Mengi Kadiri Gani, na Yako Wapi?

Kufikia mwishoni mwa karne ya 19, kampuni za mafuta zingefilisika kwa sababu ya kusambaa kwa umeme. Lakini, kubuniwa kwa injini inayotumiwa hasa kuendesha magari kulibadili jambo hilo sana. Petroli ilihitajiwa ili kuendesha magari katika nchi nyingi zilizoendelea kiviwanda mwishoni mwa miaka ya 1920. Sasa petroli nyingi zaidi ilihitajiwa ili usafiri uendelee ulimwenguni. Lakini ingetoka wapi?

Kadiri miaka inavyopita, biashara ya mafuta imesitawi sana ulimwenguni kwa sababu ya kugunduliwa kwa maeneo mapya ya mafuta katika sehemu mbalimbali za ulimwengu. Maeneo 50,000 hivi yamepatikana! Hata hivyo, kiasi cha mafuta hakitegemei idadi ya maeneo lakini kinategemea ukubwa wa maeneo hayo. Ni makubwa kadiri gani?

Maeneo yenye mafuta yanayoweza kujaza mapipa bilioni tano hivi ndiyo makubwa zaidi, ilhali maeneo yenye kiasi cha mafuta kinachoweza kujaza mapipa milioni mia tano hadi bilioni tano ndiyo ya pili kwa ukubwa. Ingawa “Ripoti ya Marekani ya Nchi Zenye Mafuta Duniani ya Mwaka wa 2000” inaonyesha kwamba nchi 70 zina mafuta, ni chache tu zenye maeneo makubwa zaidi ya mafuta. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 7.) Maeneo makubwa zaidi ya mafuta yanapatikana hasa katika bonde la Arabuni na Iran, katika Ghuba ya Uajemi.

Jitihada za kutafuta maeneo yenye mafuta hazijakoma. Badala yake, teknolojia mpya imeimarisha jitihada hizo. Kwa sasa, eneo la Bahari ya Caspian, linalotia ndani mataifa kama Azerbaijan, Iran, Kazakhstan, Turkmenistan, Urusi, na Uzbekistan, limevutia wachimbaji wa mafuta. Kulingana na Shirika la Marekani Linalosimamia Habari za Nishati, huenda mafuta na gesi ya asili yanapatikana katika eneo hilo. Njia nyingine za kusafirisha mafuta zinachunguzwa, kama vile kuyasafirisha kupitia Afghanistan. Pia kuna uwezekano kwamba kuna mafuta katika Mashariki ya Kati, Greenland, na maeneo fulani ya Afrika. Haidrojeni na kaboni zinaweza kutumiwa kutokeza nishati na bidhaa zinazotumiwa kila siku.

Mafuta Huchimbwaje?

Wanajiolojia na masoroveya hutafuta maeneo ambayo huenda yakawa na mafuta yasiyosafishwa ardhini. Baada ya kuchunguza na kuchukua sampuli, wao huchimba ili wahakikishe kwamba kuna mafuta. Zamani, kisima cha mafuta kilipochimbwa, mchanganyiko wa matope na mafuta ulitoka kwa nguvu na hivyo mafuta mengi yalipotea, na hata kungetokea mlipuko. Hata hivyo, mashine za kuchimba huzuia tatizo hilo kwa sababu zina vali za pekee na vifaa vya kupima. Leo pia inawezekana kuchimba visima vyembamba vyenye kina kirefu.

Hatimaye, mafuta na gesi huibuka kwa utaratibu na hali hiyo hudumishwa kwa kutia maji, kemikali, kaboni-dioksidi, na gesi nyingine kama nitrojeni. Mafuta yanaweza kuwa na uzito mbalimbali ikitegemea eneo. Kwa kawaida, mafuta mepesi yanapendwa sana kwa kuwa ni rahisi kuyachimba na kuyasafisha.

Taasisi ya Mafuta ya Marekani inasema kwamba teknolojia ya kisasa hutumiwa kuchimba mashimo ya mlalo, yaliyo sambamba na miamba ya dunia na hivyo si lazima kuchimba visima vingi. Uchimbaji wa mafuta baharini ulianza katika mwaka wa 1947 katika Ghuba ya Mexico na umeongeza kiasi cha mafuta. Hapana shaka kwamba njia inayotumiwa kuchimba mafuta huathiri bei yake. *

Mafuta Husafirishwaje?

Mnamo mwaka wa 1863, mabomba membamba ya mbao yalitengenezwa ili kusafirisha mafuta, kwa sababu yalipunguza gharama na yalikuwa rahisi kutumia kuliko mapipa ya lita 159 yaliyobebwa kwa magari yaliyokokotwa na farasi. * Leo mabomba mengi tata hutumiwa. Shirika la Mabomba ya Mafuta linasema kwamba mabomba yenye urefu wa kilometa 300,000 hutumiwa kusafirisha mafuta nchini Marekani pekee!

Mabomba, hasa ya chuma, husafirisha mafuta yasiyosafishwa hadi kwenye viwanda vya kusafisha na pia mafuta yaliyosafishwa hadi kwa wauzaji. Mabomba ya kisasa yanaweza kuwa na mifumo ya kompyuta inayochunguza mtiririko na msukumo wa mafuta. Vifaa vya kuchunguza mabomba kwa mamia ya kilometa, vifaa vinavyotumia nguvu za sumaku, na vifaa vinavyotumia mawimbi ya sauti kuchunguza mashimo kwenye mabomba vimebuniwa. Lakini, watu wanaotumia mafuta huona tu ishara inayoonyesha kwamba bomba la mafuta linapita ardhini na onyo la kuwatahadharisha wasilime sehemu hiyo.

Ingawa mabomba ni muhimu, si njia bora ya kusafirisha mafuta mengi katika nchi za mbali, na wauzaji wa mafuta wa hapo kale waliona inafaa kutumia meli kubwa za mafuta. Meli hizo huundwa kwa njia ya pekee na hufikia urefu wa meta 400 hivi. Meli za mafuta ndizo meli kubwa zaidi baharini na zinaweza kubeba mapipa milioni moja au zaidi ya mafuta. Lakini, zijapokuwa kubwa, meli za mafuta hukabili hatari ambayo haijashughulikiwa hadi sasa kama sanduku lenye kichwa “Kumwagika kwa Mafuta” linavyoonyesha. Mashua na magari ya moshi hutumiwa pia kwa ukawaida kusafirisha mafuta mengi. Hata hivyo, kusafirisha mafuta ni sehemu tu ya utaratibu wote wa uzalishaji.

Unaweza kutambua kiwanda cha kusafisha mafuta unapoona mwali mdogo wa moto ukiwaka juu ya mlingoti mrefu. Kwa kawaida mafuta yasiyosafishwa huchemshwa na kuelekezwa kwenye mnara wa kuvukiza, ambako hutenganishwa katika visehemu mbalimbali. Baadhi ya visehemu hivyo huwa vyepesi kama gesi ya butani, na vingine huwa vizito na hutumiwa kutengeneza mafuta ya kulainisha na bidhaa nyingine. (Ona ukurasa wa 8-9.) Lakini kuna swali lingine, Je, mafuta yana faida na hasara?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Mmoja wao, Alfred Bernhard Nobel, baadaye alianzisha Tuzo za Nobeli.

^ fu. 16 “Inakadiriwa kwamba gharama ya uchimbaji wa mafuta kwa kutumia mnara uliojengwa zaidi ya meta 300 [futi 1,000] baharini katika Ghuba ya Mexico ni mara 65 hivi kuliko gharama ya uzalishaji huko Mashariki ya Kati.”—The Encyclopædia Britannica.

^ fu. 18 Zamani, mafuta yalihifadhiwa na kusafirishwa kwa kutumia mapipa ya mbao kama yale yaliyotumiwa kwa ajili ya divai.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 5.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

MAPIPA AU TANI?

Kampuni za kwanza za mafuta huko Pennsylvania zilisafirisha mafuta kwa kutumia mapipa ya divai ya lita 180. Baada ya muda, mapipa hayo yalibeba lita 159 tu ili yasimwagike. Bado kipimo cha pipa (lita 159) hutumiwa leo katika biashara ya mafuta.

Tangu zamani, mafuta yalisafirishwa kwa meli hadi Ulaya na kwa kawaida yalipimwa kwa tani kama leo.

[Hisani]

Chanzo: Taasisi ya Mafuta ya Marekani

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

MAFUTA YALITOKA WAPI?

Tangu miaka ya 1870, wanasayansi wengi husema kwamba mafuta yalitokana na viumbe. Wanadai kwamba “mabaki ya viumbe yaliyozikwa ardhini huoza na kutokeza mafuta na gesi ya asili baada ya muda mrefu na kwamba mafuta na gesi hiyo hujikusanya katika mashimo madogo kwenye tabaka la juu la miamba ya [Dunia].” Utaratibu huo hutokeza mafuta ambayo huwa na haidrojeni na kaboni. Hata hivyo, tangu miaka ya 1970, wanasayansi fulani wametilia shaka madai hayo.

Mnamo Agosti 20, 2002, jarida Proceedings of the National Academy of Sciences lilikuwa na makala yenye kichwa “Mwanzo wa Haidrojeni na Kaboni na Mwanzo wa Mafuta.” Waandishi wa makala hiyo walidai kwamba mafuta yalifanyizwa kwenye mashimo yaliyo “katika tabaka la katikati la Dunia,” wala si katika matabaka ya juu kama wengi wanavyodai.

Mwanafizikia profesa Thomas Gold ametoa hoja ambazo zimezua ubishi na amezifafanua katika kitabu chake The Deep Hot Biosphere—The Myth of Fossil Fuels. Ameandika hivi: “Nadharia ya kwamba haidrojeni na kaboni zilitokana na mabaki ya viumbe waliozikwa ardhini ilipendwa sana Marekani na sehemu nyingi za Ulaya hivi kwamba maoni yaliyo kinyume yalipuuzwa. Haikuwa hivyo katika nchi za ule uliokuwa Muungano wa Sovieti.” Hiyo ni kwa sababu “huenda mwanakemia maarufu Mrusi, Mendeleyev, alikuwa ameunga mkono nadharia ya kwamba mafuta hayakutokana na viumbe. Hoja zake zina nguvu zaidi leo, tukizingatia habari nyingi zinazopatikana.” Nadharia hiyo inasemaje?

Gold anasema hivi: “Nadharia hiyo inasema kwamba haidrojeni na kaboni zilikuwa sehemu ya vitu vilivyorundamana polepole na kuifanyiza dunia miaka bilioni 4.5 hivi iliyopita.” Kulingana na nadharia hiyo, visehemu vinavyofanyiza mafuta vimekuwa ardhini tangu dunia ilipoumbwa. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 37 Gazeti Amkeni! halitetei nadharia zinazotofautiana. Linazifafanua tu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10, 11]

KUMWAGIKA KWA MAFUTA

▪ Kiasi cha mafuta yaliyomwagwa na meli za mafuta kati ya mwaka wa 1970 na 2000 ni tani 5,322,000

▪ Umwagikaji mkubwa zaidi ulitokea katika mwaka wa 1979 wakati meli ya Atlantic Empress ilipogongana na ile ya Aegean Captain huko Karibea, na kumwaga tani 287,000 za mafuta

▪ Ingawa mara nyingi mafuta humwagika wakati yanapopakiwa na kupakuliwa, mafuta mengi zaidi humwagika meli zinapogongana au kuzama

▪ Baadhi ya visa vya kumwagika kwa mafuta ambavyo havikuhusiana na meli:

● Mlipuko wa kisima cha mafuta cha Ixtoc I mnamo mwaka wa 1979, katika Ghuba ya Mexico. Mafuta yaliyomwagika: Lita 500,000,000

● Mlipuko wa jukwaa la kisima cha mafuta katika Ghuba ya Uajemi mnamo mwaka wa 1983. Mafuta yaliyomwagika: Lita 300,000,000

● Mafuta yalimwagwa kimakusudi katika Ghuba ya Uajemi mnamo mwaka wa 1991. Mafuta yaliyomwagwa: Lita 900,000,000

[Picha]

Meli ya mafuta ya “Erika” yazama karibu na Penmarch Point, Ufaransa, Desemba 13, 1999

[Hisani]

Vyanzo: International Tanker Owners Pollution Federation Limited, “Oil Spill Intelligence Report,” “The Encarta Encyclopedia”

© La Marine Nationale, France

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UZALISHAJI WA MAFUTA MAELEZO SAHILI

1KUPIMA

SATELAITI

Mfumo wa Kupokea Habari Kutoka kwa Satelaiti hutoa ishara sahihi ambazo hutumiwa katika uchunguzi

VIKUZA-SAUTI

MALORI YANAYOELEKEZA MAWIMBI YA SAUTI ARDHINI

MELI ZINAZOELEKEZA MAWIMBI YA SAUTI BAHARINI

MABOMBA

Njia moja ni kupima mwangwi wa sauti inayoelekezwa ardhini

2KUCHIMBA

VISIMA VYA NCHI KAVU

JUKWAA LA BAHARINI

KISIMA KILICHO MAJINI

Visima vya mafuta huchimbwa katika nchi kavu, karibu na ufuo, na chini ya bahari. Huenda gesi au kemikali zikatiwa kisimani ili kudumisha msukumo wa mafuta

[Picha]

KISIMA KILICHO MAJINI

Nyambizi zinazoendeshwa kutoka mbali hutumiwa kujenga vifaa vya uzalishaji chini ya bahari

[Picha]

KUCHIMBA KISIMA CHA MLALO

Mashine zinazoendeshwa kutoka mbali na mtaalamu huzungusha mtaimbo wa kuchimba, na vifaa maalumu huchunguza mwamba

3KUSAFIRISHA

MELI YA MAFUTA

Mafuta husafirishwa kwa mabomba yaliyo juu ya ardhi, chini ya ardhi, na baharini. Mafuta husafirishwa pia kwa meli, mashua, na magari ya moshi

4KUSAFISHA

MTAMBO WA KUSAFISHA

Mafuta yasiyosafishwa huchemshwa, huvukizwa, na kutenganishwa katika visehemu vinavyoweza kutumiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali

MNARA WA KUVUKIZA

Mafuta meusi yasiyosafishwa yanayonata huchemshwa katika tanuru, kisha haidrojeni na kaboni huyeyuka na kuwa gesi. Gesi hizo hubadilika na kuwa majimaji katika vipimo mbalimbali vya joto. Hivyo mafuta hutenganishwa katika visehemu kadhaa

68°F. → GESI ZA KUSAFISHA Zinatia ndani methani, ethani,

[20°C] propani, na butani

 

↑ ↑

70°-160°F. → PETROLI Hutumiwa kuendesha magari na

[20°-70°C] kutengeneza plastiki

 

↑ ↑

160°-320°F. → NAFTHA Inaweza kutumiwa kutengeneza

[70°-160°C] plastiki, petroli, na kemikali

nyingine

↑ ↑

320°-480°F. → MAFUTA YA TAA Hutengeneza mafuta ya ndege na [160°-250°C] hutumiwa katika jiko la mafuta oil

 

↑ ↑

480°-660°F. → MAFUTA YA GESI Hutengeneza dizeli na mafuta ya tanuru

[250°-350°C]

 

↑ ↑

750°F. → MABAKI Hutumiwa kutengeneza mafuta ya

↑ ↑ kusafisha, mafuta mazito, nta ya

mishumaa, grisi, na lami

TANURU

MTAMBO WA KUYEYUSHA WENYE KICHOCHEZI

Haidrojeni na kaboni huchomwa kwa mvuke na kuchanganywa na kichochezi moto cha mchanganyiko wa ungaunga wa alumini na silika. Haidrojeni na kaboni huvunjwa na kufanyiza molekuli ndogo muhimu

Kichochezi cha ungaunga huchanganyika na haidrojeni na kaboni katika mvuke

ETHANOLI

Kiyeyusho hiki hutumiwa kutengeneza rangi, vipodozi, marashi, sabuni, na rangi za nguo

PLASTIKI

Kwa mfano, polisterini hutengenezwa kwa kuunganisha molekuli nyingi za sterini

NYONGEZA ZA PETROLI

Oktani huzuia gesi isiwake haraka sana kwenye injini, na hivyo injini hufanya kazi vizuri zaidi

[Hisani]

Photo Courtesy of Phillips Petroleum Company

[Grafu katika ukurasa wa 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

SEHEMU ZENYE MAFUTA MENGI

Idadi zinawakilisha mabilioni ya mapipa. Hazitii ndani mafuta ambayo hayajagunduliwa

▪ Mwanachama wa OPEC

• Nchi yenye angalau eneo moja kubwa zaidi la mafuta

Jumla ya uzalishaji

◆ Hifadhi

▪ • ◆ 332.7 SAUDI ARABIA

• ◆ 216.5 MAREKANI

• ◆ 192.6 URUSI

▪ • ◆ 135.9 IRAN

▪ • ◆ 130.6 VENEZUELA

▪ • ◆ 125.1 KUWAIT

▪ • ◆ 122.8 IRAKI

▪ • ◆ 113.3 MILKI ZA KIARABU

• ◆ 70.9 MEXICO

• ◆ 42.9 CHINA

▪ • ◆ 41.9 LIBYA

▪ ◆ 33.4 NIGERIA

◆ 21.2 KANADA

▪ ◆ 21.0 INDONESIA

◆ 20.5 KAZAKHSTAN

▪ • ◆ 18.3 ALGERIA

◆ 17.6 NORWAY

◆ 16.9 UINGEREZA

[Picha katika ukurasa wa 4]

Kisima cha kwanza cha mafuta yasiyosafishwa huko Titusville, Pennsylvania, mwaka wa 1859

Mafuta yakifoka kutoka kisimani huko Texas

[Hisani]

Brown Brothers

[Picha katika ukurasa wa 5]

Eneo la kale la mafuta, Beaumont, Texas

[Picha katika ukurasa wa 5]

Gari linalokokotwa na farasi likisafirisha mapipa ya mafuta

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kisima cha mafuta kikiteketea huko Kuwait

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 5]

All photos: Brown Brothers