Mafuta Je, Yana Faida na Hasara?
Mafuta Je, Yana Faida na Hasara?
MATAIFA yaliyoendelea kiviwanda yanategemea mafuta na bidhaa zake kwa kadiri gani? Mafuta na gesi ya asili ni muhimu kwa mataifa hayo, na hilo limetokeza “Jamii ya Haidrojeni na Kaboni” kama anavyosema Daniel Yergin katika kitabu chake The Prize. Hebu fikiria vitu kama vile mafuta ya tanuru, grisi, nta, lami, na bidhaa zote zinazotokana na kemikali za mafuta kama vile ndege, magari, mashua, gundi, rangi, nguo za nailoni, viatu, vitu vya watoto vya kuchezea, rangi za nguo, aspirini, marashi, vipodozi, diski za kurekodi, kompyuta, televisheni, na simu. Kila siku watu wengi hutumia baadhi ya bidhaa zaidi ya 4,000 zinazotokana na mafuta ambazo ni muhimu sana maishani. Lakini vipi madhara ambayo mafuta yameleta katika jamii tangu yalipogunduliwa?
Mfalme ‘Anayetawala Vibaya’
Mwishoni mwa mwaka wa 1940, wakati ambapo vita kati ya Rumania na Hungaria ilikuwa karibu kuanza, dikteta Adolf Hitler wa Nazi aliingilia kati haraka akiwa mpatanishi. Je, nia yake ilikuwa kuleta amani? Hitler alitaka tu kuuzuia Muungano wa Sovieti usidhibiti visima vya mafuta vya Rumania. Mafuta yalikuwa sababu kuu iliyofanya Iraki ishambulie Kuwait mnamo mwaka wa 1990 na mataifa mengine yakaingilia vita hivyo. Kuna visa vingi vya aina hiyo. Mara nyingi vita na mateso yamesababishwa na tamaa ya kudhibiti mafuta.
Mafuta si muhimu tu katika maisha ya kila siku, ni muhimu pia katika siasa na watu wachache wenye mamlaka huyatumia kujifaidi. Hivi majuzi Shirika la Nchi Zinazouza Mafuta (OPEC) lilisema kwamba mafuta si bidhaa ya kawaida tu bali “ni bidhaa inayoathiri mikakati ya kisiasa na ya kijeshi.” Mataifa yametumia mafuta kujifaidi kisiasa kwa kuweka vikwazo na vizuizi vya kibiashara. Isitoshe, visima vya mafuta, mitambo ya kusafisha mafuta, na meli za mafuta zimekuwa zikishambuliwa na magaidi na mara nyingi hilo limesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Viwanda vya mafuta vimelaumiwa kwa sababu ya kutokeza hewa ya kaboni-dioksidi inayochafua mazingira ambayo huenda ikabadili hali ya hewa ulimwenguni. Kulingana na shirika la PEMEX (Shirika la Mafuta la Mexico), mojawapo ya mashirika makubwa ya mafuta ulimwenguni, hatua mbalimbali za uzalishaji wa mafuta hutokeza vichafuzi. Ingawa leo vichafuzi vya mafuta vimepungua, miaka sita hivi baada ya Mkataba wa Kyoto, wakati mataifa 161 yalipokutana kuchukua hatua za kupunguza ongezeko la joto duniani, wengi wanahisi kwamba hakuna mabadiliko makubwa. Lakini, shirika la OPEC linasema kwamba “mafuta yameleta utajiri na ufanisi uliopo leo” katika nchi nyingi. Lakini je, inakuwa hivyo nyakati zote?
Huenda watu fulani wakasema kwamba uchimbaji wa visima vya mafuta na ujenzi wa mabomba umeleta hasara. Huenda wengine wakasema kwamba kuna ukosefu mkubwa wa kazi huko Saudi Arabia, nchi yenye mafuta mengi zaidi. Alí Rodríguez Araque, msimamizi wa shirika la OPEC, anasema kwamba “serikali za nchi zilizoendelea kiviwanda zinajifaidi kutokana na jitihada za wazalishaji, wasafishaji, na wanunuzi wa mafuta.”
Shirika la CorpWatch, linalohakikisha kwamba mashirika yanajali mazingira, linasema: “Mafuta yangali yanatawala. Lakini yanatawala vibaya.”
Mafuta yatapatwa na nini wakati ujao?