Kuishi na Ugonjwa wa Mfumo wa Neva
Kuishi na Ugonjwa wa Mfumo wa Neva
AVIS alikuwa akiendesha gari peke yake kurudi nyumbani alipoanza kuona kiwi. Alisimamisha gari mara moja. Baada ya dakika chache, aliona vizuri tena, na akaendelea na safari yake huku akidhani kwamba jambo hilo lilisababishwa na uchovu. Halafu alipokuwa likizoni miaka minne baadaye, Avis aliamka usiku wa manane akiumwa na kichwa sana. Alienda hospitalini ambako daktari alimpa dawa ya kutuliza maumivu na akamchunguza, akidhani kwamba huenda anaugua ugonjwa wa kuvimba tezi.
Siku iliyofuata maumivu yalikwisha. Hata hivyo, Avis alikuwa dhaifu sana. Hata hangeweza kushika glasi ya maji, na alihisi uchungu na mwasho upande wake wa kulia. Yeye na mume wake walikatisha likizo yao na kurudi nyumbani wakiwa na wasiwasi. Asubuhi iliyofuata, Avis hangeweza kushika uma vizuri wakati wa kiamsha-kinywa, na alijihisi mnyonge upande wa kulia wa mwili wake. Alienda hospitalini na madaktari wakampima, lakini ikaonekana kwamba hakuwa amepata kiharusi. Madaktari hawakujua kisa kilichotukia miaka minne mapema, na vipimo havikuwaonyesha ugonjwa. Baada ya miezi kadhaa, Avis alianza kutumia tena upande wake wa kulia. Alikata kauli kwamba alikuwa amepata virusi fulani visivyojulikana.
Miaka minne ikapita. Kisha Ijumaa moja asubuhi, Avis alipoamka jicho lake la kushoto halikuona vizuri. Daktari alisema kwamba ni kwa sababu ya mfadhaiko. Lakini kufikia Jumapili, jicho hilo lilikuwa limepofuka. Huku akiwa na wasiwasi na akilia, alimpigia daktari simu na daktari akapendekeza achunguzwe mara moja. Alipewa dawa za steroidi ambazo zilimsaidia kuona kidogo. Baada ya kumpima tena, madaktari waligundua ugonjwa wa Avis. Alikuwa anaugua ugonjwa wa mfumo wa neva (multiple sclerosis).
Ugonjwa wa Mfumo wa Neva
Ugonjwa huo hatari husababisha mwasho kwenye mfumo wa neva, yaani ubongo na uti wa mgongo. Madaktari wengi wanaamini kwamba ugonjwa huo hutokea wakati kinga za mwili zinaposhambulia chembe fulani za mwili. Kisababishi cha ugonjwa huo hakijulikani lakini inadhaniwa kwamba huenda unasababishwa na virusi. Kisha sehemu fulani za mfumo wa kinga huvamia utando muhimu wenye mafuta unaofunika nyuzi
za mfumo wa neva, na hivyo kuacha makovu kwenye utando huo.Utando huo hukinga nyuzi fulani za neva. Kwa hiyo unapoharibiwa, mawimbi ya umeme yanaweza kuzuiwa kabisa au yanaweza kupenya kwenye neva zilizo karibu na kutoa ujumbe usiofaa. Kwa kuwa utando wa mfumo wa neva unaweza kuharibika mahali popote, wagonjwa huwa na dalili tofauti. Hata mgonjwa anaweza kuwa na dalili tofauti kila mara anapougua ugonjwa huo, ikitegemea sehemu ya mfumo wa neva iliyoathiriwa. Hata hivyo, kwa kawaida dalili huwa uchovu, unyonge, kufa ganzi kwa mikono na miguu, kushindwa kutembea, kuona kiwi, uchungu, mwasho, matatizo ya kibofu na tumbo, na vilevile kushindwa kukaza fikira na kutofanya maamuzi ifaavyo. Kwa upande mwingine, wagonjwa wengi “hawalemai sana,” chasema Chama cha Kitaifa cha Ugonjwa wa Mfumo wa Neva cha Marekani.—Ona sanduku “Aina Nne Kuu za Ugonjwa wa Mfumo wa Neva.”
Kama kisa cha Avis kinavyoonyesha, ni vigumu kutambua ugonjwa huo mapema kwa sababu dalili zinaweza kufanana na za magonjwa mengine. Lakini dalili hizo zinapoonekana mara nyingi, madaktari wanaweza kuutambua kwa usahihi zaidi.—Ona sanduku “Njia za Kupima Ugonjwa wa Mfumo wa Neva.”
Ulimwenguni pote watu milioni 2.5 hivi wanaugua ugonjwa huo. Hiyo inatia ndani Wakanada 50,000 hivi na wakazi 350,000 hivi wa Marekani, ambako karibu watu 200 hugunduliwa kuwa na ugonjwa huo kila juma. Kitabu kimoja cha kitiba kinasema kwamba “mbali na majeraha, ugonjwa wa mfumo wa neva ndicho kisababishi kikuu cha uharibifu wa mfumo wa neva kwa vijana na watu wa umri wa makamo.” Idadi ya wanawake ambao hupata ugonjwa huo ni karibu mara mbili zaidi ya wanaume, na dalili huanza kati ya umri wa miaka 20 na 50.
Kupambana na Ugonjwa Huo
Kwa kuwa kufikia sasa ugonjwa wa mfumo wa neva hauna tiba, madaktari hujaribu kupambana nao na dalili zake au kuuzuia usienee haraka. Dawa zilizotengenezwa kuukomesha au kuuzuia usienee haraka na kupunguza mashambulizi zinatia ndani aina mbili za intaferoni (protini ya kiasili iliyotengenezwa kwa chembe zisizoweza kushambuliwa) na dawa nyingine inayoitwa glatiramer acetate.
Madaktari huwapendekezea wagonjwa wengine dawa zinazoitwa corticosteroid ili kupunguza mwasho na kuwasaidia wapone haraka ugonjwa huo unapoibuka tena. Hata hivyo, kitabu cha kitiba The Merck Manual chasema kwamba “kwa kawaida si vizuri kutumia dawa za corticosteroid kwa muda mrefu kwani hilo linaweza *
kusababisha magonjwa mengine mengi kama vile ugonjwa wa mifupa, vidonda vya tumbo, na kisukari.” Isitoshe, dawa hizo haziwezi kuponya ugonjwa huo kabisa. Hivyo madaktari fulani hawapendi kuzitumia iwapo mgonjwa anaugua kidogo tu.Kwa upande mwingine, wataalamu wanachunguza jinsi wanavyoweza kurekebisha utando wa nyuzi za neva ulioharibiwa. Wamefanya uchunguzi katika maabara na kugundua chembe fulani zinazotokeza chembe zilizokomaa ambazo zinaweza kufanyiza utando huo. Wakivumbua njia ya kuchochea chembe hizo ili zifanyize utando, wanaweza kuufanya mwili urekebishe neva zilizoharibiwa.
Kuishi na Ugonjwa Huo
Zaidi ya asilimia 50 ya watu wanaougua ugonjwa huo wanasema kwamba uchovu ni mojawapo ya matatizo makubwa wanayokabili. Uchovu unaweza kuzidisha dalili za ugonjwa huo na hivyo kuathiri kazi ya mtu na mataraja yake ya kuajiriwa. Uchovu pia unaweza kumfanya mtu ashindwe kustahimili ugonjwa huo. Hivyo watu wengi wanaohisi uchovu alasiri huona inafaa kufanya kazi asubuhi na kulala kidogo alasiri. Kwa mfano, Avis ameweza kuendelea kuwa mhubiri wa kujitolea wa wakati wote kwa kulala kwa saa moja kila alasiri.
Kitabu Harrison’s Principles of Internal Medicine kinakazia kwamba watu wanaougua ugonjwa huo wanapaswa kutunza afya kwa “kupunguza mfadhaiko, kula chakula bora, kupumzika vya kutosha, na kuepuka kupunguza uzito haraka.” Watafiti wengi wanaona kwamba mfadhaiko unaweza kuamsha ugonjwa huo. Hivyo inafaa wagonjwa watambue mambo yanayoweza kuepukwa ambayo yanasababisha mfadhaiko.
Kwa upande mwingine, watu wanaougua ugonjwa huo wanapaswa kuishi maisha ya kawaida kadiri wawezavyo bila kufanya kazi kupita kiasi, kuchoka, au kukaa sana katika joto au baridi kali. Wanapaswa pia kufanya mazoezi yanayofaa. Kitabu The Merck Manual chasema hivi: “Inapendekezwa kwamba wagonjwa, hata wale wanaougua sana, wafanye mazoezi
kwa ukawaida (k.m., kuendesha baiskeli bandia, kutumia kifaa cha mazoezi ya miguu, kuogelea, na kujinyoosha), kwa sababu yanasaidia moyo na misuli, hupunguza mkazo wa misuli, na kufaidi akili.”Avis anasema: “Ni muhimu kuujua mwili wako. Ninapohisi kwamba nimechoka isivyo kawaida au ninapohisi uchungu au kufa ganzi kwenye mikono na miguu, mimi hutambua kwamba ninahitaji kupumzika kwa siku moja au mbili. Hilo limenisaidia kukabiliana na ugonjwa huo.”
Watu wanaougua ugonjwa wa mfumo wa neva wanaweza pia kushuka moyo lakini si kwa sababu ya ugonjwa huo. Baada ya mtu kupimwa na kupatikana na ugonjwa huo, kwa kawaida huhuzunika kwa njia mbalimbali. Anaweza kukataa kwamba anaugua, kukasirika, kufadhaika, kusononeka, na kukosa tumaini. Hiyo ni kawaida na hisia hizo huisha. Hatimaye mgonjwa huwa na maoni mazuri.
Kwa kawaida, watu wa familia na marafiki wanaweza pia kuathiriwa kwa kumsikitikia mgonjwa. Hata hivyo, wanaweza kukabiliana na hali hiyo vizuri zaidi na kumtegemeza mgonjwa kwa kujitahidi kujifunza juu ya ugonjwa huo. Kwa mfano, ni vizuri kufahamu kwamba ugonjwa huo haufupishi sana muda wa maisha, hauambukizwi, na haurithiwi moja kwa moja. Hata hivyo, habari zinaonyesha kwamba uwezekano wa kupata ugonjwa huo hurithiwa.
Wengi wanaougua ugonjwa wa mfumo wa neva huishi maisha yenye furaha na mafanikio. Avis ameimarishwa kwa kuwa na uhusiano mzuri na Mungu na kwa kuwa na tumaini la wakati ujao linaloonyeshwa katika Biblia. Ndiyo, anatarajia kwa hamu wakati ambapo chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu, hakuna mtu atakayesema, “Mimi ni mgonjwa.” (Isaya 33:24; Ufunuo 21:3, 4) Ikiwa unaugua ugonjwa wa mfumo wa neva au ugonjwa mwingine mbaya, acha ‘faraja inayotokana na Maandiko’ ikutegemeze na kukusaidia kukabiliana vizuri zaidi na matatizo yako.—Waroma 15:4.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 12 Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi unaonyesha kwamba asilimia 50 hadi 60 ya watu wanaougua ugonjwa huo hutumia vitamini, madini, mitishamba, na vidonge vingine. Ingawa baadhi ya vitu hivyo haviwezi kuwadhuru, vingine havifaulu au hata ni hatari. Kwa hiyo, kabla ya wagonjwa kutumia njia nyingine za matibabu au kumeza vidonge, wanapaswa kufikiria hatari zake.
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Aina Nne Kuu za Ugonjwa wa Mfumo wa Neva
Aina ya kwanza: Aina hii huwapata watu wengi zaidi, na huathiri asilimia 70 hadi 80 ya wagonjwa dalili zinapoanza kuonekana. Wakati fulani ugonjwa huibuka na nyakati nyingine dalili za ugonjwa hutokomea kabisa au kidogo. Ni rahisi kutambua tofauti hiyo. Ugonjwa unapopungua, dalili zake huwa hazionekani.
Aina ya pili: Karibu asilimia 70 ya wagonjwa wa aina ya kwanza hupata aina ya pili. Ugonjwa unaweza kuibuka na kutokomea, lakini mfumo wa neva huharibika polepole.
Aina ya tatu: hupata asilimia 10 ya wagonjwa na huzidi pole kwa pole tangu unapoanza. Ugonjwa huibuka kwa nguvu zaidi na huenda ukadumu. Tofauti na aina ya kwanza, aina hii huendelea hata dalili zinapopungua.
Aina ya nne: Asilimia 10 hadi 15 hupata aina hii nayo huendelea bila kupungua sana. Hata hivyo, ugonjwa huongezeka kwa viwango tofauti na hupungua kidogo sana. Huwapata hasa watu waliozidi umri wa miaka 40.
[Hisani]
Vyanzo: Chama cha Kitaifa cha Ugonjwa wa Mfumo wa Neva cha Marekani na kitabu Multiple Sclerosis in Clinical Practice. Asilimia zinatofautiana kidogo ikitegemea chanzo.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Njia za Kupima Ugonjwa wa Mfumo wa Neva
Kupiga picha kwa nguvu za sumaku: Hii ndiyo mojawapo ya njia bora za kuchunguza viungo na inaweza kuonyesha habari nyingi sana za chembe za ubongo. Picha hizo zinaweza kuonyesha dalili za ugonjwa wa mfumo wa neva au kubainisha kwamba mtu hana magonjwa mengine.
Kuchunguza umajimaji wa uti wa mgongo na ubongo: Umajimaji huo hutolewa kwenye uti wa mgongo. Madaktari huchunguza iwapo vitu fulani vya mfumo wa kinga ni vingi kupita kiasi na vilevile kama kuna vitu ambavyo vimetokana na uharibifu wa utando unaofunika nyuzi za neva.
Kuchochea neva: Mashine zinazoendeshwa na kompyuta hutumiwa kupima muda wa wastani ambao ujumbe hupitia kwenye neva. Neva za asilimia 80 hadi 90 ya watu wanaougua ugonjwa huo hazipitishi ujumbe ipasavyo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]
Kukabiliana na Ugonjwa wa Mfumo wa Neva
Utegemezo: Mtu anapokuwa na uhusiano wa karibu na watu wa ukoo na marafiki wanaojali na wanaomtegemeza, hilo humsaidia awe na furaha. Kwa hiyo, usisite kuomba msaada unapouhitaji na usijitenge.
Zungumza waziwazi: Kuzungumza waziwazi kuhusu ugonjwa huo na magumu yake huwasaidia wengine waelewe hali ya mgonjwa na hilo humsaidia kukabiliana nao. Kwa upande mwingine, kukosa kuzungumza kunaweza kusababisha kutoelewana, mfadhaiko, na kujitenga.
Hali ya kiroho: Uthibitisho mwingi unaonyesha kwamba hali ya kiroho huboresha afya yetu na hutusaidia kuwa na sifa nzuri, na kuwa na matumaini mazuri ya wakati ujao. Hilo linapatana na maneno haya ya Yesu: “Mwanadamu ataishi, si kwa mkate tu, bali kwa kila neno linalotoka katika kinywa cha Yehova.”—Mathayo 4:4.
Kucheka: Ingawa ugonjwa huo haufurahishi, kucheka kunaweza kuboresha mwili na akili.
[Hisani]
Kutoka kwa kitabu Multiple Sclerosis in Clinical Practice.
[Picha katika ukurasa wa 11]
Idadi ya wanawake ambao hupata ugonjwa huo ni mara mbili zaidi ya wanaume
[Picha katika ukurasa wa 13]
Kufanya mazoezi kwa ukawaida hufaidi mwili na akili