Bado Kuna Tisho la Vita vya Nyuklia?
Bado Kuna Tisho la Vita vya Nyuklia?
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Japan
“Kila mtu mwenye akili anaogopa vita vya nyuklia, na kila nchi iliyoendelea kiteknolojia inavipangia. Kila mtu anajua ni jambo la upumbavu, na kila taifa lina kisingizio cha kutengeneza silaha za nyuklia.”—Carl Sagan, mtaalamu wa elimu ya nyota.
MNAMO AGOSTI 6, 1945, ndege moja ya kivita ya Marekani iliangusha bomu la atomu huko Hiroshima, Japan, na ghafula bin vuu watu wengi walikufa na mali nyingi kuharibiwa. Hilo lilikuwa bomu la kwanza la atomu kutumiwa vitani. Mlipuko huo uliharibu kabisa eneo lenye ukubwa wa kilometa 13 za mraba, lililokuwa na wakazi 343,000. Zaidi ya thuluthi mbili ya majengo ya jiji hilo yaliharibiwa na angalau watu 70,000 walikufa na 69,000 wakajeruhiwa. Siku tatu baadaye, bomu la pili la atomu liliangushwa huko Nagasaki na kuua watu 39,000 na 25,000 wakajeruhiwa. Karibu nusu ya majengo yote ya jiji hilo yaliharibiwa. Silaha yenye nguvu kadiri hiyo haikuwa imetumiwa kabla ya hapo. Ulimwengu ulikuwa umebadilika. Ulikuwa umeingia katika enzi ya nyuklia. Katika kipindi cha miaka michache, Marekani, ule uliokuwa Muungano wa Sovieti, Uingereza, Ufaransa, na China zilitengeneza mabomu makali sana ya hidrojeni.
Vita Baridi, yaani ule uhasama uliokuwapo kati ya mataifa ya Kikomunisti na yasiyo ya Kikomunisti, vilichochea utengenezaji wa silaha za nyuklia za hali ya juu na mifumo tata ya kurusha makombora kutoka mbali. Kukawa na woga ulimwenguni wakati makombora ya masafa marefu yalipotengenezwa, ambayo yangetumiwa kushambulia nchi zilizo umbali wa zaidi ya kilometa 5,600 kwa dakika chache tu. Nyambizi zilibeba makombora ya nyuklia ambayo yangeweza kuharibu maeneo 192 mbalimbali. Wakati mmoja ilikadiriwa kwamba kuna makombora 50,000 katika maghala ya silaha! Wakati wa Vita Baridi, wanadamu walikabili kipindi ambacho watu walikiita Har–Magedoni ya nyuklia, yaani vita visivyo na washindi.
Mwisho wa Vita Baridi
Kulingana na kitabu The Encyclopædia Britannica, katika miaka ya 1970, Vita Baridi vilipungua “kama ilivyoonyeshwa katika mkataba wa 1 na wa 2 wa SALT [Mashauriano ya Kudhibiti Silaha za Nyuklia], wakati mataifa mawili yenye nguvu zaidi yalipokubaliana kupunguza makombora ya masafa marefu na mizinga iliyotegwa ambayo inaweza kurusha makombora ya nyuklia.” Kisha, mwishoni mwa miaka ya 1980, Vita Baridi vikapungua, na hatimaye vikamalizika.
Ripoti ya Shirika la Carnegie la Amani ya Kimataifa ilisema hivi: “Kumalizika kwa Vita Baridi kuliwapa watu tumaini la kwamba mashindano ya kumiliki silaha za nyuklia na mabishano kati ya Marekani na Urusi yalikuwa karibu kwisha.” Kutokana na jitihada za kupunguza silaha za nyuklia, mamia ya silaha za nyuklia zimeharibiwa katika miaka ya karibuni. Katika mwaka wa 1991, Muungano wa Sovieti na Marekani zilitia sahihi Mashauriano ya Kupunguza Silaha za Nyuklia, ambao kwa mara ya kwanza ulishurutisha mataifa hayo yenye silaha nyingi zaidi za nyuklia kudhibiti na pia kupunguza makombora yaliyotegwa hadi 6,000 kwa kila nchi. Mwishoni mwa mwaka wa 2001, nchi zote mbili zilisema kwamba zimetekeleza mkataba huo kwa kupunguza makombora yao ya nyuklia kama walivyokubaliana. Isitoshe, katika mwaka wa 2002, nchi
hizo zilikubali Mkataba wa Moscow uliotaka zipunguze silaha ziwe kati ya 1,700 na 2,200 katika miaka kumi ijayo.Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan alisema kwamba licha ya makubaliano hayo, “huu si wakati wa kupuuza tisho la nyuklia.” Aliongezea hivi: “Kuna uwezekano mkubwa sana kwamba vita vya nyuklia vitatokea mwanzoni mwa karne ya 21 na hilo ni jambo la kuogopesha sana.” Inasikitisha kwamba bado kuna tisho la vita vibaya zaidi vya nyuklia kuliko vile vya Hiroshima na Nagasaki. Tisho hilo linatoka wapi? Swali muhimu zaidi ni, je, vita vya nyuklia vinaweza kuepukwa?