“Kito cha Bahari”
“Kito cha Bahari”
Mwani mdogo wa diatom umefunikwa kwa maganda ya gilasi yenye mapambo tata, nao hupatikana kwa wingi katika bahari zote duniani. Mwani huo umewavutia wanasayansi kwa karne nyingi tangu wakati hadubini ilipobuniwa na wanadamu walipoanza kuchora picha zake maridadi. Kwa kufaa, mwani huo unaitwa kito cha bahari.
Alfred Nobel, aliyebuni baruti katika miaka ya 1860, alichanganya silika inayotokana na mwani huo pamoja na nitroglycerin ili aweze kutengeneza vipande vya baruti vinavyoweza kubebeka. Mabaki ya maganda ya mwani huo yaliyobadilika kuwa mawe hutumiwa kwa njia mbalimbali leo, kama vile kutengeneza rangi inayong’aa inayopakwa barabarani na kusafisha divai na maji ya vidimbwi vya kuogelea.
Hata hivyo, jambo muhimu zaidi ni kwamba mimea hiyo midogo yenye chembe moja huhusika kwa asilimia 25 katika usanidimwanga unaotukia duniani. Watafiti Allen Milligan na Francois Morel, wa Chuo Kikuu cha Princeton huko Marekani, wamegundua kwamba silika iliyo katika ganda la gilasi la mwani huo husababisha mabadiliko ya kemikali ndani ya maji yaliyo katika ganda, hivyo kufanyiza hali nzuri kwa ajili ya usanidimwanga. Wanasayansi wanaamini kwamba kinachofanya ganda la gilasi la mwani huo kuwa maridadi sana ni kwamba sehemu yake kubwa hupata maji yaliyomo, hivyo kufanya usanidimwanga kufaulu zaidi. Bado haijulikani jinsi maganda hayo maridadi hutengenezwa kutokana na silikoni iliyoyeyushwa katika maji ya bahari, lakini kile ambacho watafiti wanajua ni kwamba mwani huo hutimiza daraka muhimu katika kuendeleza uhai duniani, labda hata kuliko mimea mingi ya nchi kavu, kwa sababu unafyonza kaboni-dioksidi na kutokeza oksijeni.
Morel anasema kwamba diatom ni “kati ya viumbe vyenye mafanikio zaidi duniani.” Milligan anaongeza kwamba ikiwa mwani huo haungefyonza kaboni-dioksidi, “huenda kungekuwa na ongezeko kubwa zaidi la joto duniani.”
Mwani huo unapokufa, mabaki yake ya kaboni huzama baharini na kugeuka kuwa mawe. Wanasayansi fulani wanaamini kwamba baada ya kugeuka kuwa mawe na kushinikizwa sana, mwani huo umesaidia kutokeza mafuta ulimwenguni. Hata hivyo, kuna wasiwasi mkubwa kwamba joto la maji ya bahari linapoongezeka kwa sababu ya ongezeko la joto duniani, hilo linawezesha bakteria kula mabaki ya mwani huo kabla hayajazama, na kufanya kaboni irudi juu ya maji. Hivyo, huenda ‘kito hicho kidogo cha bahari,’ ambacho ni sehemu ya mfumo wa kuendeleza uhai uliobuniwa kwa njia ya ajabu, kinakabili hatari ya kutoweka.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
© Dr. Stanley Flegler/Visuals Unlimited