Kula Majani Katikati ya Miiba
Kula Majani Katikati ya Miiba
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI
JIUNGE nami ninapotembelea eneo la Afrika Kusini linaloitwa Noorsveld. Jina la eneo hilo kame linatokana na mimea ya miiba yenye majimaji inayoitwa minyara (noors), ambayo inapatikana huko kwa wingi. Kama unavyoona kwenye picha, wakulima katika eneo hilo hufuga mifugo, kama vile mbuzi wa Angora ambao wanapendwa kwa sababu ya manyoya yao meupe. Manyoya hayo hutumiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile nguo maridadi na mazulia. Lakini wanyama hao huwezaje kuishi katika eneo hili kame?
Mahali ambapo unawaona mbuzi hao wakitembea kuna mashina ya miti ya minyara ambayo ni chakula chao muhimu. Zaidi ya asilimia 40 ya chakula cha mbuzi hao katika majira ya baridi kali hutokana na aina hii ya minyara, yaani, Euphorbia coerulescens. Hata hivyo, mbuzi hao wanahitaji kuwa waangalifu wasidungwe na miiba mikali wanapokula mashina ya mimea hiyo. Inakuwa rahisi kwao kula wanapojua kuvunja miiba kwa pembe zao.
Baada ya mvua nyingi kunyesha, mbuzi hao hula mimea inayokua karibu na miti hiyo. Lakini jambo hilo ni hatari pia. Mkulima Jurgen Currie, anaandika hivi katika kitabu chake kuhusu Noorsveld: “Mbuzi wa Angora aliye na manyoya ya kupendeza yaliyojikunja akijaribu kula mimea laini inayokua chini na katikati ya minyara, anaweza kunaswa na miiba.” Hilo linaweza kusababisha kifo. Mkulima huyo wa Noorsveld anaeleza: “Ikiwa jua la wakati wa kiangazi ni kali sana, saa mbili hazitapita kabla ya mbuzi huyo kufa.”
Eneo la Noorsveld hukumbwa na ukame mara kwa mara. Nyakati hizo, majani ya minyara huokoa uhai. Wakulima hutumia mashine zinazounganishwa na trekta kukatakata minyara. Ni salama na rahisi kwa mbuzi hao kula vipande hivyo vya minyara. Wanyama wa mwituni hujiunga pia kufurahia mlo huo. Currie anaeleza hivi: “Wakati wa ukame, tandala [swara wakubwa] huja kula miti hiyo. Utawaona tandala hao kando ya barabara mahali ambapo
minyara imekatwakatwa, na hawaogopi watu kwa sababu wanahangaikia kupata chakula.”Kuna aina nyingine ya mti wa mnyara unaoitwa Euphorbia ferox, ambao ni mdogo lakini huwa na miiba mingi mikali hivi kwamba wanyama wengi hawawezi kufikia mashina yake. Kwa sababu miti hiyo hustahimili ukame, inaokoa uhai pia. Mvua isiponyesha, wakulima na wafanyakazi wao husonga kutoka mti mmoja hadi mwingine wakiteketeza miiba ya minyara kwa kurunzi za aina fulani au kwa njia nyingine. Ni kazi ngumu sana. Kitabu Veld Plants of Southern Africa kinaeleza: “Baada ya miiba kuteketezwa, mifugo hufurahia kula mashina. . . . Aina fulani ya paa hujifunza kula minyara iliyoteketezwa na huzoea sana . . . kuwa karibu na watu wanaoteketeza minyara hiyo.”
Tunastaajabia unamna-namna wa uumbaji wa Yehova tunapowatazama mbuzi hao wakila minyara. Ingawa minyara huonekana kuwa hatari, inategemeza uhai wa wanyama wengi katika eneo hili linalokumbwa na ukame mara kwa mara.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Zaidi ya asilimia 40 ya chakula cha mbuzi katika majira ya baridi kali hutokana na minyara hii
[Picha katika ukurasa wa 25]
Minyara iliyochanua na picha kubwa ya miiba hatari