“Hatutaki Kusherehekea ‘Halloween!’”
“Hatutaki Kusherehekea ‘Halloween!’”
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UBELGIJI
Huo ndio uliokuwa uamuzi wa wanafunzi wa darasa moja katika shule fulani huko Tienen, Ubelgiji. Kwa nini walifanya uamuzi huo? Nchini Ubelgiji, ni jambo jipya kusherehekea Halloween, ambayo ni sherehe ya mkesha wa Siku ya Watakatifu Wote. Sherehe hiyo ilipaswa kusherehekewa kwa mara ya kwanza katika shule hiyo mnamo Oktoba 31, 2002. Basi kabla ya siku hiyo, mwalimu aliwapa wanafunzi mgawo kuhusu sherehe hiyo. Mwalimu huyo aliwaambia hivi: “Tayarisheni jambo baya sana na lenye kushtua kuhusu sherehe hiyo!”
Matthias, mwenye umri wa miaka kumi, alikuwa miongoni mwa wanafunzi hao. Alikumbuka kwamba pindi moja alisoma kuhusu hatari zilizofichika za Halloween katika gazeti la Amkeni! la Oktoba 8, 2001. Alitambua kwamba sherehe hiyo inahusisha mambo yasiyompendeza Mungu. Basi, Matthias akatumia habari hizo kuandika insha. Mwalimu alipoisoma kwa makini, alikata kauli kwamba sherehe hiyo ni hatari. Kisha akamwambia Matthias awaeleze wanafunzi wenzake darasani kuhusu habari hiyo.
Matthias alipoanza kuzungumzia habari hiyo, ilionekana kwamba baadhi ya wanafunzi hawakuwa wakisikiliza. Hata hivyo, alipoendelea kuzungumza, wote wakamsikiliza kwa makini. Matthias alipomaliza, mwalimu aliwauliza wanafunzi ikiwa bado wanataka kusherehekea Halloween. Wanafunzi wote wakasema: “Hatutaki!” Mwanafunzi mmoja alisema hivi kwa sauti: “Inachukiza!” Mwingine akasema: “Sikujua kwamba Halloween haiwaheshimu wafu.”
Ingawa hapo awali Matthias alikuwa mwanafunzi mwenye haya, tukio hilo lilimwimarisha sana kuendelea kushikamana na mafundisho ya Biblia anayoamini hata anapokabili mkazo. Pia, mwalimu na wanafunzi wenzake wakamheshimu zaidi kwa kuwa Shahidi wa Yehova.