Kupambana na Maji kwa Muda Mrefu
Kupambana na Maji kwa Muda Mrefu
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UHOLANZI
“Mara mbili kila siku maji ya bahari hufunika nchi kubwa sana hivi kwamba huwezi kujua tofauti kati ya nchi kavu na bahari. Wakaaji wenye kusikitikiwa wa nchi hiyo huishi juu ya vilima virefu walivyojitengenezea, ambavyo haviwezi kufikiwa na maji.”
MAELEZO hayo ya Pliny the Elder, mwandishi Mroma wa karne ya kwanza, yanaonyesha jinsi wakaaji wa maeneo yaliyo chini ya usawa wa Bahari ya Kaskazini walivyopambana na maji. Pambano hilo lingali linaendelea. Kwa kweli, karibu nusu ya wakaaji milioni 16 wa eneo hilo wanaishi na kufanya kazi chini ya usawa wa bahari.
Licha ya pambano hilo linaloendelea, wakaaji wa Uholanzi, au Nchi za Chini, hawajisikitikii. Ni kweli kwamba nchi yao ni ndogo * na iko chini ya usawa wa bahari, lakini ni mojawapo ya nchi tajiri zaidi ulimwenguni. Na inashangaza kwamba nchi ya Uholanzi imepata ufanisi kwa sababu ya maji na pambano hilo dhidi ya maji.
Wakaaji wa Uholanzi waliamua kuishi katika eneo hili hasa kwa sababu lina rutuba. Eneo hili linafaa kwa ukuzaji wa mimea, maua, na matunda, na vilevile ufugaji wa ng’ombe. Pia, eneo
hili ni muhimu kwa uchumi kwa kuwa mito mikubwa ya Ulaya huingia baharini huku. Si ajabu kwamba Uholanzi na bandari kubwa zaidi ulimwenguni ya Rotterdam, zinaonwa kuwa njia ya kuingia Ulaya!Kuta za Kuzuia Maji Zimejengwa kwa Muda Mrefu
Hata hivyo, utajiri haukutokea bila jitihada. Kwa muda wa miaka 900 iliyopita, Waholanzi wamekuwa wakijenga kuta ili kujikinga dhidi ya maji yanayotoka baharini na kwenye mito inayopita nchini. Kwa hiyo, kuta zenye urefu wa maelfu ya kilometa zinakinga nchi ya Uholanzi dhidi ya bahari na mito. Hiyo ni hatua kubwa kwelikweli!
Nchi nyingine pia zina kuta za kuzuia maji. Lakini kuta za maji zinahitajiwa sana kwa sababu ya hali mbalimbali, kama vile urefu juu ya usawa wa bahari. Koos Groen, mwandishi-mshirika wa kitabu Dijken (Kuta za Kuzuia Maji), alisema hivi: “Wakaaji wote wa Uswisi wakienda likizo kwa mwaka mmoja nje ya nchi yao, watapata mashamba yao watakaporudi. Waholanzi wakifanya hivyo, nusu ya mashamba yao na asilimia 75 ya nyumba zao zitakuwa zimefunikwa na maji.” *
Leo mamilioni ya Waholanzi wanaoishi chini ya usawa wa bahari hawaogopi kukumbwa na mafuriko kwa sababu pambano dhidi ya maji linaendelea. Hebu ona jitihada zinazofanywa ili kudumisha fuo na marundo ya mchanga.
Kudumisha Fuo na Marundo ya Mchanga
Katika kipindi cha maelfu ya miaka, fuo na marundo ya mchanga yalisitawi kiasili na kukinga eneo hilo kutokana na maji ya bahari. Lakini wakati wote kizuizi hicho cha asili huathiriwa na mmomonyoko. Ili kurudisha mchanga, meli fulani huzoa mchanga chini ya bahari, kilometa 9 hadi 20 kutoka pwani, na kuuweka kwenye ufuo au karibu nao. Tangu mwaka wa 1970, zaidi ya meta mchemraba milioni 85 za mchanga zimeondolewa ili kuzuia mmomonyoko wa mchanga nchini!
Hata hivyo, kuzuia mmomonyoko wa mchanga hakuwanufaishi wanadamu tu. Kulingana
na gazeti NRC Handelsblad la Uholanzi, “ingawa marundo hayo ya mchanga yanafanyiza asilimia 1 tu ya eneo la Uholanzi, robo tatu ya aina zote za ndege zinazopatikana nchini na thuluthi mbili za aina za pekee za mimea zinapatikana huko.”Kufupisha Fuo
Katika mwaka wa 1932, Waholanzi walijenga ukuta wa kuzuia maji wenye urefu wa kilometa 32 unaoitwa Afsluitdijk. Ukuta huo ulibadili Zuider Zee, yaani, Bahari ya Kusini kuwa ziwa linaloitwa IJsselmeer. Pia, ulifupisha fuo za Uholanzi kutoka kilometa 1,900 hadi kilometa 1,300.
Miaka 20 hivi baadaye, katika mwaka wa 1953, wajenzi wa kuta za kuzuia maji walianza mradi mkubwa zaidi baada ya furiko moja kusababisha vifo vya watu 1,835. Lengo lao lilikuwa kuziba vijito vyote vilivyoingia baharini katika eneo la kusini-magharibi la nchi ila tu vile vilivyoelekea kwenye bandari za Rotterdam na Antwerp. Hatimaye, mradi huo, ulioitwa Mradi wa Delta, ulifupisha fuo za nchi hii kufikia kilometa 622.
Kinga Dhidi ya Mito
Tatizo la mafuriko halisababishwi tu na bahari bali pia na mito mingine ambayo hupitia Uholanzi kabla ya kuingia baharini. Kuelekea mwishoni mwa majira ya baridi kali, baada ya mvua kunyesha kwa muda mrefu na wakati ambapo theluji inayeyuka, maji mengi kutoka Uswisi, Ujerumani, Ufaransa, na Ubelgiji hupitia mito hiyo na kufika Uholanzi.
Maji mengi jinsi hiyo yanaweza kusababisha matatizo makubwa. Kwa mfano, mnamo Februari 1995, mito iliyo katikati ya nchi ilijaa maji kwelikweli hivi kwamba ilihofiwa kuwa kuta hizo zingeporomoka. Ikiwa ukuta mmoja ungeporomoka, maji yangefunika sehemu iliyo nyuma ya kuta kwa meta nyingi. Uzuri ni kwamba kuta hizo hazikuporomoka. Groen, aliyenukuliwa mapema, anasema: “Ni watu wachache tu wanaojua kile ambacho kingetokea iwapo kuta hizo zingeporomoka.”
“Pipa” Lisilo na Kifuniko
Tofauti na nchi nyingine, nchi ya Uholanzi ina mashamba mengi chini ya usawa wa bahari ambayo yamezungukwa na kuta. Hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 19, kiwango cha maji katika mashamba hayo kilidhibitiwa na vinu vya upepo. Siku hizi, mitambo ya kusukuma maji inayoendeshwa kwa kompyuta hudhibiti kiwango cha maji. Peter Nowak, ambaye hutunza mtambo mmoja kama huo karibu na Amsterdam, alielezea kazi inayohusika.
Nowak alieleza hivi: “Shamba lililo chini ya usawa wa bahari ni kama pipa. Kwa kawaida shamba kama hilo huwa meta kadhaa chini ya usawa wa bahari. Ukuta unaozunguka huzuia shamba hilo lisifurikwe na maji. Lakini ukuta huo si kifuniko. Mvua kubwa inaweza kujaza maji shambani. Maji hayo yanapaswa kusukumwa kwa nguvu ili kuepusha hatari. Lakini maji hayo huenda wapi?”
Shamba lililo chini ya usawa wa bahari huwa na mitaro ambayo hupeleka maji kwenye mtambo wa kusukuma maji. Ili kuzuia mitaro hiyo isizibe, kila mkulima anapaswa kusafisha mitaro iliyo shambani mwake. Kisha, mtambo huo husukuma maji yaliyobaki shambani na kuyaingiza kwenye maziwa na mifereji iliyo nje ya shamba ili yahifadhiwe humo. Maji yanapozidi katika maziwa na mifereji, yanaingizwa baharini wakati ambapo hakuna mawimbi mengi.
Nowak aliongeza hivi: “Kudumisha kiwango kinachofaa cha maji shambani ni muhimu kwa uchumi wa Uholanzi. Katika majira makavu ya kiangazi, maji huingizwa kwenye mashamba kwa kuwa wakulima wanayahitaji katika mitaro yao ili kukuza nyasi au mimea. Maua hukuzwa katika baadhi ya mashamba hayo, nayo ni mojawapo ya mazao muhimu zaidi yanayouzwa katika nchi za nje.”
Kuishi Mahali Bahari Ilipokuwa
Katika karne ya 20, mashamba hayo hayakutumiwa tu kukuza mimea, bali pia nyumba zilijengwa huko. Miaka 50 iliyopita, wakati wapangaji wa miji walipoanza kupanga kujenga miji katika mashamba hayo, hawakujua sana jinsi ya kupangia ujenzi wa maeneo ya makazi. Hata hivyo, ukitembelea mashamba hayo leo, utaona kwamba walifaulu kujenga majengo mahali bahari ilipokuwa! Unakaribishwa huku ujionee mwenyewe.
Je, wewe huogopa kutembea chini ya usawa wa bahari? Hilo linaeleweka, lakini wengi wameshangaa kugundua kwamba tayari wamefanya hivyo bila kujua. Kwa mfano, ikiwa umewahi kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Schiphol, karibu na Amsterdam, ndege uliyosafiri nayo ilitua mahali ziwa lilipokuwa. Kwa kuwa hukutambua kwamba ulikuwa meta nne chini ya usawa wa bahari, hiyo inaonyesha kwamba bado kuta za kuzuia maji za Uholanzi zinafanya kazi!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Nchi ya Uholanzi ina ukubwa wa kilometa 41,500 za mraba.
^ fu. 9 Asilimia 40 ya eneo la Uholanzi liko chini ya usawa wa bahari. Eneo hilo lingefurikwa iwapo kuta za kuzuia maji hazingetunzwa. Nchi zenye milima kama vile Uswisi ziko juu ya usawa wa bahari, hivyo hazikabili tatizo hilo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Kukusanyika CHINI YA USAWA WA BAHARI
Kati ya Majumba mawili ya Kusanyiko ya Mashahidi wa Yehova nchini Uholanzi, jumba moja liko meta 5 chini ya usawa wa bahari. Shahidi mmoja alisema hivi, “Tunaposafiri kuhudhuria makusanyiko yetu yanayofanywa mara mbili kwa mwaka, sisi hukumbuka maneno haya ya Mungu kwenye Ayubu 38:8 na 11: ‘Ni nani aliyeizuia bahari kwa milango na kusema: “Unaweza kufika hapa, na usipite; na hapa mawimbi yako yenye fahari yamewekewa mpaka”?’ Maneno hayo yanatukumbusha kwamba njia ambayo Yehova hutumia kudhibiti nguvu nyingi za maji inapita zile zinazotumiwa na mafundi hata wawe wamebuni mifumo ya ajabu sana.”
[Sanduku katika ukurasa wa 19]
Ni Nani Anayetunza Kuta Hizo?
Kuta za kuzuia maji na mifumo ya kuondoa maji inapaswa kutunzwa na nyakati nyingine kurekebishwa. Tangu Enzi za Kati, kazi hiyo imefanywa na halmashauri za kusimamia kuta za maji. Halmashauri hizo zilianzishwa kwa kutegemea mambo matatu: kufaidika, kulipa, na kuwa na mamlaka ya kufanya maamuzi. Mtu anayetaka kufaidika kutokana na kuta za kuzuia maji zilizo salama anapaswa kulipia gharama za kusimamia na kutunza kuta hizo. Lakini pia anaweza kuamua jinsi kuta hizo zitakavyotunzwa na jinsi pesa zinazokusanywa zitakavyotumiwa.
Halmashauri hizo zimekuwepo nchini Uholanzi tangu karne ya 12. Kwa sasa, kuna zaidi ya halmashauri 30 hivi. Uamuzi wa kuanzisha, kuvunja, na kuelekeza halmashauri hizo hufanywa na mamlaka za mkoa. Mamlaka hizo ndizo huamua ni watu wangapi watakaotunza kuta hizo. Watu hao huishi katika eneo wanalotunza. Wao hufanya kazi kwa bidii kwa sababu usalama wa familia na jamii zao unahusika. Maji yanapoongezeka, wao huzunguka kuta, nao huwa tayari na magunia ya mchanga na vifaa vingine wanavyotumia kuzuia maji yasipenye. Kuwepo kwa halmashauri za kusimamia kuta za maji kwa muda mrefu kumehakikisha kwamba kuta hizo zinatunzwa vizuri.
[Picha katika ukurasa wa 16]
(See publication)
Bila marundo ya mchanga na kuta za kuzuia maji, sehemu hii ya bluu ingefurikwa kila wakati
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kuta kubwa zilijengwa baharini ili kukinga maeneo ya chini yaliyo nyuma yake
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kila mwaka mchanga mwingi sana hurudishwa
[Picha katika ukurasa wa 18]
Magari husafiri chini ya usawa wa bahari
[Picha katika ukurasa wa 18]
Msiba uliotukia wakati ukuta ulipoporomoka mwaka wa 1953
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Both photos: Met vriendelijke toestemming van het Nederlandse Ministerie van Verkeer en Waterstaat
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Top two photos: Met vriendelijke toestemming van het Nederlandse Ministerie van Verkeer en Waterstaat