Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Je, Ubongo Unatumiwa Kupita Kiasi?

Gazeti Toronto Star la Kanada linaripoti kuwa watafiti fulani wanasema kwamba “kufanya mambo mengi mno kwa wakati mmoja hulemea ubongo.” Uchunguzi unaonyesha kwamba kufanya hivyo kunaweza kusababisha ubongo usifanye kazi vizuri, ukosee mara nyingi, na kunaweza pia kusababisha ugonjwa. Kwa mfano, kunaweza “kudhoofisha uwezo wa mtu wa kukumbuka mambo, kusababisha maumivu ya mgongo, kumfanya mtu aambukizwe mafua kwa urahisi, kuwa na matatizo ya kusaga chakula, na pia kudhuru meno na fizi.” Uchunguzi wa Taasisi za Marekani za Afya huonyesha kwamba sehemu mbalimbali za ubongo huchochewa wakati watu wanapofanya mambo tofauti-tofauti. Hata hivyo, watu wanapojaribu kufanya mambo tofauti-tofauti wakati uleule mmoja, kama vile kutumia simu za mkononi huku wakiendesha gari, “ubongo huacha kutenda kazi, kwani haushindwi tu kufanya mambo yote mawili bali pia hukataa kuyafanya,” anasema Dakt. John Sladky, ambaye ni mtaalamu wa mfumo wa neva katika Chuo Kikuu cha Emory. Watafiti wanasema kwamba watu wanapaswa kuacha kufanya mambo mengi mno na kukubali kwamba ubongo hauwezi kufanya mambo yote ambayo wangetaka.

Aina Mpya za Samaki Zimegunduliwa

Hivi karibuni wanasayansi wanaochunguza bonde la Mto Caura nchini Venezuela, walisema kwamba “aina mpya kumi za samaki zimegunduliwa.” Gazeti El Universal la Venezuela linasema kwamba samaki hao wanatia ndani samaki mdogo “mwenye mkia mwekundu,” “kambare mwenye minyiri kichwani,” na “samaki wa piranha ambaye hula matunda na nyama.” Eneo hilo lenye misitu ya tropiki na vijito linaonwa kuwa mojawapo ya maeneo yenye viumbe wengi sana duniani. Wanasayansi wanaisihi serikali ichukue hatua za kuhifadhi eneo hilo ambalo linaharibiwa na kilimo, uvuvi, ujenzi wa makao, uchimbaji wa migodi, na miradi ya kuzalisha umeme ambayo huenda ikaanzishwa.

Wanachoka Kusubiri

Gazeti Psychologie Heute linasema kwamba “wagonjwa nchini Ujerumani husubiri kwa wastani wa dakika 48 kabla ya kumwona daktari. Wengine husubiri zaidi.” Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na taasisi moja ya usimamizi wa kazi, kuhusu mazoea ya madaktari 610, ulionyesha kwamba “wagonjwa hawafurahii hali hiyo.” Madaktari wa kliniki fulani walipokosa kurekebisha hali hiyo, “idadi ya wagonjwa walioenda kutibiwa kwa ukawaida ilipungua kwa asilimia 19 katika kipindi cha mwaka mmoja,” yasema ripoti hiyo. Madaktari na wasaidizi wao walichoka sana wakati wagonjwa walipokuwa wengi, ingawa hawakufanya kazi nyingi kama kawaida. Pia wasaidizi wengi walikosea mara mbili zaidi ya ilivyo kawaida.

Hawawezi Kutofautisha Jema na Baya

Gazeti The Sun-Herald la Sydney linasema kwamba “mfanyakazi mmoja kati ya kila wafanyakazi wanne nchini Australia, alikubali kuwa amewahi kuiba vifaa vya kuandikia kazini.” Uchunguzi uliohusisha wafanyakazi zaidi ya 2,000 wa ofisini ulionyesha kwamba baadhi ya mazoea ya kawaida ya wafanyakazi hutia ndani kuchunguza habari za kibinafsi za wafanyakazi wenzao, kutumia Intaneti kwa shughuli za kibinafsi wakati wa kazi, kuingiza habari zisizoidhinishwa katika kompyuta, na kutumia vifaa vya ofisini vya kompyuta nyumbani. Garie Dooley, ambaye alisimamia uchunguzi huo anasema kwamba “kuna watu wengi ambao hawajui tofauti kati ya jema na baya.”

Je, Mazishi ya Wanyama-Vipenzi Yanafaa Kutozwa Kodi?

Gazeti la Japani IHT Asahi Shimbun linaripoti kwamba wasimamizi wa hekalu moja la Kibudha nchini Japani, walishtaki idara ya kodi huku wakidai kwamba faida walizopata kutokana na mazishi ya wanyama-vipenzi, kuchoma mizoga, na kuhifadhi majivu, hazipaswi kutozwa kodi. Idara ya kodi ilidai kwamba uchomaji wa mizoga na huduma za kidini kwa ajili ya wanyama-vipenzi ni “mapatano ya kibiashara,” na kwamba kuhifadhi majivu hekaluni hulifanya hekalu kuwa “bohari.” Hata hivyo, wasimamizi wa hekalu hilo wanadai kwamba “huduma ya mazishi ni tendo la kidini ambalo limekusudiwa kuwafariji watu ambao wamefiwa na wanyama-vipenzi na kuzifariji nafsi za wanyama,” bila kutarajia kupata faida yoyote.

Misiba ya Ndege Yapungua

Gazeti la Flight International linaripoti kwamba idadi ya ndege zilizoanguka mwaka wa 2003 ilikuwa ya chini kuliko wakati wowote tangu 1950 wakati rekodi za misiba ya ndege zilipoanza kuhifadhiwa. Idadi ya vifo 702 ilikuwa ya chini zaidi tangu 1990, ijapokuwa safari za ndege tangu wakati huo zimeongezeka kwa asilimia 40. Gazeti Daily Telegraph la London linasema kwamba jambo moja ambalo limechangia “maendeleo hayo katika usalama ni kule kupungua kwa visa vya ndege kugonga milima, ambavyo husababishwa na makosa ya marubani. Mifumo mipya inayotumiwa kuonyesha urefu wa maeneo ya ardhi imesaidia, hata hivyo, mifumo hiyo ‘inaweza kuwa na kasoro.’” Pia, ndege nyingi za zamani hazina mifumo hiyo.

Chumvi Huokoa Uhai wa Wanawake Wajawazito

Gazeti The Times la London linasema kwamba matibabu rahisi na yasiyogharimu sana ya myeyusho wa chumvi aina ya salfati ya maganesi yanaweza kupunguza kwa asilimia 50 uwezekano wa wanawake wajawazito kupata matatizo hatari yanayoweza kusababisha kifo. Kila mwaka ulimwenguni pote, zaidi ya wanawake 50,000 na watoto wao ambao bado hawajazaliwa, hufa kutokana na aina hatari sana ya shinikizo la damu, ambayo husababisha mpapatiko. Ingawa kwa miaka mingi wanawake nchini Marekani wamekuwa wakitiwa mishipani aina hiyo ya chumvi au kudungwa sindano zake ili kuzuia ugonjwa huo, mbinu hizo hazitumiwi sana katika nchi nyingi. Hivyo, kikundi cha madaktari wa kimataifa katika Taasisi ya Sayansi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Oxford, nchini Uingereza, “kiliamua kuchunguza faida za matibabu hayo kwa kuwafanyia majaribio wanawake 10,000 katika nchi 33,” linasema gazeti The Times. “Miaka mitatu baadaye . . . majaribio hayo yalisimamishwa kabla ya wakati uliopangiwa kwani faida za matibabu hayo zilikuwa zimekwisha kuonekana: kutumia salfati ya maganesi kuwatibu wanawake ambao walikabili uwezekano wa kupata ugonjwa wa shinikizo la damu ambalo husababisha mpapatiko, kulipunguza uwezekano wao wa kupata mpapatiko kwa asilimia 58. Pia kulipunguza hatari ya kufa kwa asilimia 45.” Matibabu hayo “yanagharimu dola 4.50 za Marekani kwa kila mwanamke, hivyo . . . wanawake katika nchi zinazoendelea wanaweza kupata tiba hiyo.”

Mazoea ya Kula ya Vijana

Gazeti Daily Telegraph la London linasema kuwa “inashtua kwamba idadi kubwa ya wasichana wanakosa kula kwa sababu ya kuhangaikia sana umbo lao na kutamani sana kufanana na wanamitindo na watu mashuhuri.” Uchunguzi wa mazoea ya kula ya wanafunzi 300,000 uliofanywa na Idara ya Elimu ya Afya Katika Shule za Uingereza, ulionyesha kwamba zaidi ya asilimia 40 ya wasichana walio na umri wa kati ya miaka 14 na 15 “walienda shuleni bila kula kiamsha-kinywa. Hilo likilinganishwa na takwimu za mwaka wa 1984, inaonekana kwamba idadi ya wale wanaoenda shuleni bila kula kiamsha-kinywa imeongezeka mara mbili hivi.” Vilevile idadi ya wale wanaokosa kula chakula cha mchana imeongezeka kutoka asilimia 2 katika mwaka wa 1984, hadi asilimia 18 katika mwaka wa 2001. Kwa kuhofia kwamba wanafunzi watapata matatizo hatari kama vile ugonjwa wa kujinyima chakula na ule wa kula na kujitapisha, walimu wakuu katika shule za wasichana wameombwa kuchunguza uzito wa wanafunzi katika shule zao. Wavulana pia wameanza kuhangaikia mazoea yao ya kula. Idadi ya wavulana wenye umri wa miaka 12 na 13 wanaotaka kupunguza uzito wao imeongezeka kutoka asilimia 26 hadi 31, huku idadi ya wavulana wenye umri wa miaka 14 na 15 ambao wanataka kufanya hivyo ikiongezeka kutoka asilimia 21 hadi 25.