Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Umaridadi Uliofichwa Mapangoni

Umaridadi Uliofichwa Mapangoni

Umaridadi Uliofichwa Mapangoni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI SLOVENIA

KULIKUWA na giza totoro. Mtu mmoja aliyeitwa Luka Čeč alitembea polepole chini ya ardhi huku akiwa amebeba taa ndogo. Alipoinuka taratibu juu ya mwamba aliona jambo lenye kustaajabisha sana, nalo lilimshtua kwelikweli. Je, unajua alivumbua nini? Alivumbua kijia kipya katika Mapango ya Postojna nchini Slovenia.

Uvumbuzi huo uliofanywa mwaka wa 1818 ulianzisha biashara ya utalii ambayo imesitawi sana kufikia sasa. Pia, uliwawezesha wanasayansi kufanya uchunguzi zaidi kuhusu miamba. Ili ufahamu zaidi kuhusu mapango hayo ya fahari, jiunge nasi tunapotembelea mji wa Postojna, magharibi mwa Slovenia.

Mahali Penye Mapango Mengi

Eneo la mapango la Postojna ni mojawapo ya maeneo makubwa zaidi ya aina hiyo barani Ulaya kwani lina vijia na mapango mengi ambayo yana urefu wa kilometa 20. Mapango hayo yanapatikana katika eneo la Kras, au Karst, nchini Slovenia, ambalo lina uwanda wa chokaa wenye urefu wa kilometa 50 kutoka Bahari ya Adriatiki, katikati ya Milima ya Alps ya Julian na Dinaric. Mapango yanayopatikana Postojna ni baadhi ya maelfu ya mapango katika eneo hilo.

Leo, neno “karst” hutumiwa kwa njia nyingi. Neno hilo hutumiwa na wataalamu ulimwenguni pote kufafanua maeneo yanayofanana na eneo hilo la Kras. Maeneo kama hayo yanapatikana katika sehemu nyingi ulimwenguni, kama vile Australia, Amerika ya Kati, China, Indochina, Urusi, Karibea, na Mediterania. Kwa kawaida maeneo ya “karst” huwa na udongo mkavu wenye miamba ambayo imemomonyolewa na kufanyiza mapango, mashimo yanayopatikana mapangoni, na vilevile vijito na maziwa chini ya ardhi.

Kwa kuwa sehemu kubwa ya Slovenia ina maeneo ya aina hiyo, kuna mapango na maumbo mengi ya ajabu chini ya ardhi. Mapango ya Postojna yanaweza kulinganishwa na mapango mengine maarufu kama vile Pango la Mammoth huko Kentucky, Marekani, na Pango la Reed Flute huko Kuei-lin, China.

Kuchunguza Mapango

Mapango ya Postojna yalifafanuliwa kwa mara ya kwanza katika karne ya 17, wakati msomi wa Slovenia, Janez Vajkard Valvasor alipoyazungumzia katika kitabu chake The Glory of the Duchy of Carniola. Valvasor alisema kwamba mapango hayo yana “nguzo zenye maumbo ya ajabu.” Alisema kwamba nguzo hizo zinafanana na “wanyama waharibifu wa kila aina, nyoka, na wanyama wengine . . . au viumbe wanaotisha, nyuso zilizoharibika, mizuka, na kadhalika.” Aliongeza hivi: “Vijia vyake vingi, mashimo, na magenge makubwa yaliyo pande zote husababisha hofu hata zaidi.” Si ajabu kwamba baada ya kusoma ufafanuzi kama huo wenye kuogopesha, ni watu wachache tu waliothubutu kuingia ndani sana ya mapango hayo yenye giza!

Hata hivyo, baada ya muda, watu wengi zaidi walianza kutembelea Mapango ya Postojna. Hilo lilitukia hasa baada ya uvumbuzi wa Čeč, mwaka wa 1818. Mwaka uliofuata, watu waliruhusiwa kutembelea mapango hayo. Lakini watu wengi walianza kutembelea mapango hayo yenye kustaajabisha mwaka wa 1872 wakati ambapo reli lilijengwa ndani yake na mwaka wa 1884 wakati taa zilipowekwa ndani. Waliona nini?

Leo, Mapango ya Postojna yanajulikana hasa kwa vijia vyake maridadi. Vijia hivyo huvutia kama vito kwa sababu ya mawe yenye rangi na maumbo mbalimbali ambayo yananing’inia juu na chini ya mapango. Vijia vingine humetameta kana kwamba vimepambwa kwa almasi, hali vingine huwa na rangi nyekundu ya udongo na kutu. Maandishi yaliyo kutani huonyesha kwamba watu wa karne zilizopita walitembelea mapango hayo na kujionea umaridadi wake.

Aina Mpya za Viumbe Zavumbuliwa

Zaidi ya kuvumbua maumbo ya kustaajabisha ndani ya mapango hayo, watu walioyatembelea wamevumbua pia aina mpya za viumbe. Kufikia sasa, zaidi ya aina kumi mpya za viumbe zimepatikana katika mapango hayo ya Postojna.

Kwa mfano, Čeč alivumbua aina moja mpya ya viumbe mwaka wa 1831 na hilo liliwafurahisha sana wachunguzi wa mapango ulimwenguni pote. Čeč alivumbua mbawakawa wa ajabu sana ambaye aliitwa Leptodirus hohenwarti, yaani, “mwenye shingo-nyembamba.” Mbawakawa huyo anaitwa hivyo kwa kuwa ana shingo nyembamba. Isitoshe, ana kichwa kidogo, tumbo kubwa, na vilevile vipapasio vyake na miguu yake ni mirefu sana. Kwa kuwa mbawakawa aliyepatikana mara ya kwanza aliharibiwa bila kukusudia, haikuwezekana kumchunguza kiumbe huyo hadi mbawakawa wa pili alipogunduliwa miaka 14 baadaye.

Kiumbe mwingine wa ajabu aliyepatikana katika eneo hilo ni salamanda kipofu anayeitwa olm. Katika mwaka wa 1689, Valvasor alimfafanua kiumbe huyo kuwa ‘mtoto wa dragoni.’ Uchunguzi mwingi wa kisayansi umefanywa kuhusu kiumbe huyo mdogo.

Mapango Yaliyo Karibu

Mapango yanayopatikana Postojna ni kati ya mapango mengi ya eneo hilo. Pango la Škocjan lililoko karibu linapendeza sana. Tangu mwaka wa 1986, Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa limeliorodhesha kati ya maeneo yanayostahili kuhifadhiwa ulimwenguni. Wageni wanaotembelea huko hustaajabia ukubwa wa mapango yake na wa makorongo yake. Inasemekana kwamba mapango na makorongo hayo ndiyo makubwa zaidi barani Ulaya. Kwa mfano, sehemu moja ya pango hilo ina urefu wa meta 300, upana wa meta 100, na kimo cha meta 110!

Kwenye mlango wa Pango la Predjama kuna ngome kubwa, ambayo hapo kale ilikaliwa na mwanajeshi maarufu Erazem Jamski. Inasemekana kwamba ngome hiyo iliwazuia wavamizi kwa karne nyingi. Vyakula na bidhaa nyingine ziliingizwa ndani kupitia vijia vya chini ya ardhi vilivyoungana na pango hilo chini ya ngome. Inasemekana kwamba Erazem aliwadhihaki wavamizi kwa kuwarushia matunda mabichi au nyama zilizochomwa ili kuwaonyesha kwamba anaishi raha mustarehe ijapokuwa alikuwa amefungiwa ndani ya ngome yake. Haijulikani ikiwa hadithi hiyo ni ya kweli, lakini vijia hivyo vya siri vingalipo.

Inasisimua sana kutembelea eneo hilo lenye mapango ya kustaajabisha. Mchongaji maarufu anayeitwa Henry Moore alisema hivi kuhusu Mapango ya Postojna: “Huu ndio mchongo bora zaidi wa kiasili niliopata kuona.” Yamkini utakubaliana naye utakapopata nafasi ya kutembelea mapango hayo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

“Samaki Mwanadamu”

Kiumbe anayeitwa proteus anguinus huitwa samaki mwanadamu na wenyeji wa eneo hili kwa sababu ya ngozi yake isiyo ya kawaida, ambayo wengine huona inafanana na ngozi ya mwanadamu. Kiumbe huyo aliye na uti wa mgongo hupatikana tu katika maji ya chini ya ardhi ya eneo la kaskazini-mashariki la Italia, Slovenia, na maeneo ya kusini. Kiumbe huyo ana ngozi isiyo na rangi na macho yasiyoweza kuona, lakini hilo halimwathiri kwa njia yoyote kwa sababu anaishi katika giza totoro kuanzia yai linapotagwa hadi anapokufa. Kwa kushangaza, inasemekana kwamba wengine wameishi kwa miaka 100, na samaki hao wanaweza kuishi bila kula kwa miaka kadhaa.

[Hisani]

Arne Hodalic/www.ipak.org

[Picha katika ukurasa wa 24]

1. Kijia kimoja katika mapango ya huko Škocjan kina kimo cha meta 110

2. Ngome iliyo kwenye mlango wa Pango la Predjama

3. Mapango ya Postojna yanajulikana ulimwenguni pote

[Picha katika ukurasa wa 24]

Arne Hodalic/www.ipak.org