Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, kuna faida Kupunguza Uzito?

Je, kuna faida Kupunguza Uzito?

Je, kuna faida Kupunguza Uzito?

AMKENI! liliwahoji watu kadhaa ambao wamepambana na tatizo la kunenepa kupita kiasi? Je, walifanikiwa? Wanatoa madokezo gani kwa wale wanaokabili tatizo hilo?

▪ Fikiria mfano wa Mike, ambaye ana umri wa miaka 46, kimo cha sentimeta 183, na kilo 130. Uzito wake wa juu zaidi ulikuwa kilo 157.

Mike: “Ama kweli, nilikuwa mnene kupita kiasi. Hata nilipokuwa kijana, nilikuwa mnene sana. Hiyo ni kawaida katika familia yetu, kwani ndugu yangu na dada zangu ni wanene sana. Hatukuwa tukibakisha chakula chochote katika sahani, hata ikiwa ingejazwa sana. Kwa nini nilibadilisha mazoea yangu ya kula? Ni kwa sababu daktari aliniambia kwamba ninakabili hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa kisukari! Niliogopa sana nilipofikiria kwamba nitalazimika kutumia dawa ya insulini katika maisha yangu yote. Pia, nilikuwa na kolesteroli nyingi sana mwilini na ilinibidi nitumie dawa.

“Mimi hufanya kazi inayonilazimu kuketi kwa muda mrefu. Kwa hiyo, nina ratiba ya kufanya mazoezi kwa ukawaida ambayo inahusisha kutumia mashine ya mazoezi ya kutembea kwa nusu saa angalau mara tatu kwa juma. Hatua nyingine muhimu ilikuwa kuandika chakula nilichokula kila siku. Kwa kuwa mtaalamu wa lishe alichunguza orodha hiyo kila juma, hilo lilinisaidia kujizuia. Nilikumbuka jambo hili, ‘Usipokula chakula fulani, hutahitaji kukiandika!’

“Hilo limeniwezesha kupunguza kilo 28 kwa muda wa miezi 15 iliyopita. Hata hivyo, bado ninapaswa kupunguza kilo zaidi hadi nifikie kilo 102. Hivyo, nimeacha kula chipsi na vitafuno vingine. Katika miezi ya karibuni nimekula saladi na mboga nyingi kuliko wakati mwingine wowote!

“Jambo jingine lililonichochea kupunguza uzito ni kwamba, nikiwa dereva wa lori, afya yangu huchunguzwa kila mwaka ili nipate leseni mpya. Karibu nipoteze leseni yangu kwa sababu ya uwezekano wa kupata kisukari. Sasa hali imebadilika. Sihitaji tena kutumia dawa ili kudhibiti kolesteroli. Shinikizo la damu yangu limepungua, nami situmii dawa nyingi kulitibu. Nina nguvu zaidi, na matatizo makubwa ya mgongo wangu yamepungua. Pia, nimepunguza uzito pole kwa pole!”

Amkeni!: “Je, mke anaweza kumsaidia mume wake kupunguza uzito?”

Mike: “Unahitaji mtu wa kukutia moyo unapojitahidi kupunguza uzito. Mke wangu alifikiri kwamba alikuwa akinionyesha upendo kwa kunipa chakula kingi. Lakini sasa ananisaidia kudhibiti kiasi cha chakula ninachokula. Ni muhimu nidumishe jitihada zangu kwa sababu ninapoacha kufanya hivyo mimi huongeza uzito haraka sana.”

▪ Pia, hebu ona mfano wa mtu mwingine anayeitwa Mike, kutoka Kansas, Marekani. Ana umri wa miaka 43 na kimo cha sentimeta 173. Tulimuuliza kuhusu uzito wa juu ambao amewahi kuwa nao na mambo yanayosababisha anenepe.

Mike: “Uzito wangu wa juu zaidi ulikuwa kilo 135 hivi. Kila wakati nilikuwa mchovu na sikuwa na nguvu za kutosha kufanya mambo. Nilishindwa kulala kwa sababu ya matatizo ya kupumua. Kwa hiyo, nilienda kumwona daktari, naye akagundua kwamba kisababishi kimoja cha tatizo langu la kunenepa ni kushindwa kupumua ninapolala. * Pia aligundua kwamba nina shinikizo la juu la damu.”

Amkeni!: “Ulisuluhishaje tatizo lako?”

Mike: “Daktari alipendekeza nitumie kifaa fulani ambacho huniwezesha kupumua ninapolala. Hivyo, koo langu halizibi na ninaweza kupumua kama kawaida. Kwa hiyo, niliweza kutimiza mengi mchana na kuanza kupunguza uzito. Pia nilianza kutumia mashine ya mazoezi ya kutembea mara tatu kwa juma. Nilibadili mazoea yangu ya kula, na hilo lilitia ndani kudhibiti kiasi cha chakula nilichokula na kuepuka kuongeza-ongeza chakula. Sasa nimepunguza kilo 20 katika muda wa mwaka mmoja tu, na bado ninahitaji kupunguza kilo 20 zaidi. Ijapokuwa ninapunguza uzito polepole, ninajua kwamba ninaweza kufanikiwa.”

Amkeni!: “Ni jambo gani jingine ambalo limekuchochea kupunguza uzito?”

Mike: “Huwezi kufurahi watu wanapokudhihaki na kuchambua sura yako. Huenda wengine wakafikiri kwamba wewe ni mvivu. Hawatambui kuwa kunenepa kupita kiasi kunaweza kusababishwa na mambo mengi. Naamini kwamba huenda kwa kiasi fulani tatizo langu lilisababishwa na urithi, kwa sababu wengi katika familia yetu wana tatizo hilo.

“Hata hivyo, ninatambua kwamba ili nipunguze uzito, ninahitaji kufanya mazoezi na kudhibiti ninachokula.”

▪ Pia, Amkeni! lilimhoji Wayne kutoka Oregon, aliye na umri wa miaka 38. Alipokuwa na umri wa miaka 31, alikuwa na kilo 112.

Wayne: “Nilifanya kazi iliyonilazimu kuketi kwa muda mrefu na sikufanya mazoezi. Nilipomwendea daktari, nilishtuka kujua kwamba nilikuwa na shinikizo la juu la damu na ningepatwa na ugonjwa wa moyo. Alinishauri nimwone mtaalamu wa lishe. Mtaalamu wa lishe alinipa ratiba ya mazoezi na jinsi ya kudhibiti kiasi cha chakula nilichokula. Nilianza kutembea kilometa tano kila siku bila kupumzika, na kuamka mapema kila asubuhi kufanya mazoezi. Ilinibidi kubadili maoni yangu kuhusu mazoea yangu ya kula na kunywa. Niliacha kula vyakula visivyoboresha afya na kupunguza kiasi cha mkate nilichokula na soda nilizokunywa. Badala yake, nilianza kula matunda na mboga nyingi. Sasa uzito wangu umepungua hadi kilo 80!”

Amkeni!: “Umepata faida gani?”

Wayne: “Ninahisi kwamba nina afya nzuri zaidi na kwamba sasa niko hai. Kabla ya hapo, ni kana kwamba nilikuwa nimekufa. Faida nyingine ni kwamba nimeacha kutumia dawa za shinikizo la juu la damu. Sasa ninapokutana na watu siwi na wasiwasi, kwa sababu sitachambuliwa kwa kunenepa kupita kiasi.”

▪ Charles (si jina lake halisi) ana kimo cha sentimeta 196. Uzito wake wa juu zaidi ulikuwa kilo 168.

Charles: “Nilikuwa na matatizo makubwa ya afya, na hali yangu ilikuwa ikizidi kuwa mbaya. Sikuweza kupanda ngazi. Sikuwa na nguvu za kufanya kazi. Kazi yangu hunilazimu niketi kwa muda mrefu na inahusisha utafiti na usimamizi. Nilijua kwamba ninahitaji kupunguza uzito, hasa baada ya kushauriwa na daktari. Alinionya kwamba ninaweza kupata kiharusi. Nimewahi kuona jinsi mtu anavyoathiriwa na ugonjwa huo. Hilo lilinisadikisha kwamba ninahitaji kuchukua hatua. Daktari alipendekeza nifanye mazoezi ya kutembea kwa kutumia mashine huku kukiwa na mtu wa kunichunguza, na alinipa orodha ya vyakula ninavyopaswa kula. Sasa mwaka mmoja hivi umepita na nina kilo 136, lakini ninajua kwamba ninahitaji kupunguza kilo zaidi. Faida ambazo tayari nimepata zinanisadikisha kwamba jitihada zangu si za bure. Sasa ninaweza kupanda ngazi na nina nguvu zaidi.”

▪ Marta, ambaye alizaliwa nchini El Salvador, alikuwa na kilo 83. Hivyo, alikuwa mnene kupita kiasi ukilinganisha na kimo chake cha sentimeta 165.

Marta: “Nilimwona daktari, naye alisisitiza kwamba ninapaswa kupunguza uzito. Nilikubaliana na maoni yake akiwa mtaalamu. Alinishauri nimwone mtaalamu wa lishe. Mtaalamu huyo alinieleza mambo ninayopaswa kufanya. Alinionyesha jinsi ya kupunguza kiasi nilichokula na kuepuka vyakula fulani. Mwanzoni, nilihitaji kumwona kila juma; na baadaye kila mwezi, ili kumwonyesha maendeleo yangu. Daktari wangu na mtaalamu huyo walinipongeza kwa maendeleo niliyofanya. Baada ya muda, nilikuwa nimepunguza kilo 12, na sasa ninadumisha uzito wa kilo 68.”

Amkeni!: “Vipi kufanya mazoezi na kutumia dawa?”

Marta: “Kwa kuwa sikuwa na tatizo la kolesteroli, sikuhitaji kutumia dawa. Lakini nilianza kufanya mazoezi ya kutembea haraka kila siku.”

Amkeni!: “Ulifanya nini ulipowatembelea marafiki ambao walisisitiza ule zaidi ya kiasi chako cha kawaida?”

Marta: “Nilikuwa nikiwaambia hivi, ‘Daktari anataka nifuate mashauri yake kuhusu lishe ili niwe na afya njema,’ na kwa kawaida hawangeendelea kusisitiza.”

Unaweza kufanya nini ikiwa wewe ni mnene sana au ni mnene kupita kiasi? Wahenga walisema, “Penye nia pana njia.” Je, una nia ya kupunguza uzito? Ikiwa wewe ni mtoto au mtu mzima aliyenenepa kupita kiasi, unaweza kuchagua kupunguza uzito au kupunguza maisha yako. Basi, uwe na utendaji mwingi maishani na upate uradhi unaotokana na kufanikiwa—hata katika mambo madogo, kama vile kuvaa nguo za saizi ndogo kwa sababu ya kupunguza uzito!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 11 Kwa habari zaidi kuhusu tatizo la kushindwa kupumua unapolala, ona Amkeni! la Februari 8, 2004, ukurasa wa 10-12.

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Je upasuaji wa kuondoa mafuta ndiyo suluhisho?

Upasuaji huo unahusisha nini? Kamusi moja inasema hivi: “Kwa kawaida upasuaji huo unahusisha kufyonza mafuta ya ziada kutoka sehemu fulani ya mwili kama vile mapajani au tumboni.” (American Heritage Dictionary) Hata hivyo, je, upasuaji huo ni suluhisho la kunenepa kupita kiasi?

Kitabu Mayo Clinic on Healthy Weight kinasema kwamba upasuaji huo huboresha umbo la mtu tu. Si njia ya kupunguza uzito. Chembe za mafuta hufyonzwa kutoka mwilini wakati mrija mwembamba unapopenyezwa chini ya ngozi. Kilo kadhaa zinaweza kufyonzwa kwa wakati mmoja. Hata hivyo, “upasuaji huo si tiba ya kunenepa kupita kiasi.” Je, upasuaji huo ni salama? “Watu walio na magonjwa fulani yanayosababishwa na kunenepa kupita kiasi kama vile kisukari na ugonjwa wa moyo, wanakabili hatari kubwa zaidi wanapofanyiwa upasuaji huo.”