Samoni wa Atlantiki Yumo Hatarini
Samoni wa Atlantiki Yumo Hatarini
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI IRELAND
SAMONI wanajulikana sana kwa uwezo wao wa kuruka juu ya maporomoko ya maji wanaposafiri kuelekea upande ambao mto unatoka ili kuzalisha. Kulingana na hadithi moja, mvuvi fulani aliona “samoni wengi wakishindwa kuruka [poromoko la maji]” mahali alipokuwa akivua samaki. Baadhi yao walianguka kwenye ukingo wa mto chini ya poromoko hilo. Mvuvi huyo aliwasha moto juu ya mwamba uliokuwa karibu na poromoko hilo na kuweka karai la kukaangia juu ya moto huo. Inasemekana kwamba “samoni wengine waliposhindwa kuruka, walianguka ndani ya karai hilo.” Hivyo, baadaye mvuvi huyo alijivuna kwamba ‘katika nchi yao, kuna samoni wengi sana hivi kwamba wao huruka ndani ya karai kwa hiari yao, na mvuvi hahitaji kutoa jasho kuwavua.’
Huenda hadithi hiyo imetiliwa chumvi. Hata hivyo, samoni huruka juu ya maporomoko ya maji. Ripoti moja ya Shirika la Uchunguzi wa Samoni la Ireland ilionyesha kwamba katika miaka ya karibuni “idadi ya samaki wanaosafiri kuelekea upande ambao mto hutoka ili kuzalisha imepungua sana.” Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba katika mwaka mmoja, kati ya samoni wachanga 44,000 hivi waliotiwa alama na kuachiliwa, ni asilimia 3 tu (karibu 1,300) waliorudi.
Kwa nini samoni wa Atlantiki wamepungua sana? Je, wataongezeka na kuwa wengi kama zamani? Kuelewa mzunguko wa maisha wenye kupendeza na wa pekee wa samaki hao wa ajabu kutatusaidia kufahamu visababishi vya matatizo wanayokabili na jinsi yanavyoweza kusuluhishwa.
Mwanzo wa Maisha
Maisha ya samoni huanza kati ya miezi ya Novemba na Februari kwenye sakafu yenye changarawe ya mto wenye maji yasiyo na chumvi. Samoni wa kiume hufukuza wavamizi huku samoni wa kike akichimba mashimo madogo yenye kina cha sentimeta 30. Samoni wa kike hutaga maelfu ya mayai katika kila shimo, naye wa kiume hupachika mbegu zake juu ya mayai hayo. Kisha samoni wa kike hufunika mayai hayo kwa changarawe ili kuyalinda.
Katika mwezi wa Machi au Aprili, samaki mwenye sura ya ajabu huanguliwa. Samaki huyo, ambaye sasa anaitwa alevin, huwa na urefu wa sentimeta 3, na sehemu yake ya chini huwa na kifuko cha kiini cha yai. Mwanzoni, samaki huyo huishi chini ya changarawe, naye hula kilichomo katika kifuko hicho. Baada ya majuma manne hadi matano kifuko hicho huisha, na samaki huyo mchanga, ambaye kwa sasa anaitwa fry, hutoka kwenye changarawe na kuingia majini. Wakati huo yeye huwa na urefu wa sentimeta tano hivi na huonekana kama samaki wa kawaida. Sasa anahitaji mambo mawili tu. Kwanza, anahitaji kupata chakula, yaani, wadudu wadogo na mimea ya majini. Pili, anahitaji mahali salama pa kuishi. Wakati huo, zaidi ya asilimia 90 ya samoni wachanga huangamia kwa sababu ya kukosa chakula na nafasi, au huliwa na viumbe wengine, kama vile samaki wa trauti, mdiria, korongo, na fisi-maji.
Michael, ambaye amewachunguza samoni na samaki wengine kwa muda fulani, anasema: “Baada ya mwaka mmoja hivi, samoni huwa na urefu wa karibu sentimeta 8 au 10. Wakati huo, samaki huyo, ambaye sasa anaitwa parr, huwa na mabaka meusi kwenye kila upande wa mwili wake. Anapokuwa na urefu wa sentimeta 15 hivi, mabaka hayo huisha na samaki huyo hupata rangi nyangavu ya fedha. Sasa, mabadiliko makubwa hutukia na kufanya samoni atofautiane sana na samaki wengine.”
Michael anaongeza hivi: “Kati ya miezi ya Mei na Juni, samaki huyo [ambaye sasa anaitwa smolt] huongozwa na silika kujiunga na maelfu ya samaki wengine ili kusafiri kwa kufuata mkondo wa maji hadi kwenye milango ya mto.” Lakini je, kiumbe anayeishi katika maji yasiyo na chumvi anaweza kuishi baharini? Michael anajibu swali hilo hivi: “Kwa kawaida hawezi, lakini mabadiliko makubwa hutokea kwenye mashavu yake na kumwezesha kuchuja chumvi inayopatikana baharini. Mabadiliko hayo yanapokamilika, samaki huyo ambaye anaweza kutoshea kwenye mkono wako huwa tayari kufunga safari ndefu.”
Kuishi Baharini
Kwa nini samaki mdogo hivyo huhama kutoka mtoni? Yeye huhamia wapi? Ili akomae, samoni mchanga anahitaji kufika mahali palipo na chakula. Akiepuka wanyama hatari kama vile mnandi, sili, pomboo, na hata nyangumi, atafika baharini naye atakula mikunga, heringi, na samaki wengine. Baada ya mwaka mmoja, uzito wake utakuwa umeongezeka mara 15 kutoka mamia ya gramu hadi kilo tatu hivi. Akiendelea kuishi baharini kwa miaka mitano, uzito wake unaweza kufikia kilo 18 au zaidi. Samoni fulani wamepita uzito wa kilo 45!
Mahali hususa ambapo samoni walipata chakula hapakujulikana hadi kufikia miaka ya 1950, wakati wavuvi wanaouza samaki walipoanza kuvua samoni wengi kwenye ufuo wa Greenland. Mahali pengine kama hapo paligunduliwa karibu na Visiwa vya Faeroe, kaskazini mwa Scotland. Baadaye maeneo mengine kama hayo yaligunduliwa. Pia imeripotiwa kwamba samoni fulani hulisha chini ya barafu ya Aktiki! Maeneo hayo yalipogunduliwa, samoni wa Atlantiki walianza kukabili hatari kubwa. Viwanda vikubwa vya samaki vilijengwa huko Greenland na katika Visiwa vya Faeroe. Samaki wengi sana walivuliwa na wavuvi wanaouza samaki, na idadi ya samaki wanaorudi kwenye mito ili kuzalisha ikapungua sana. Serikali zilipotambua kwamba hilo ni tatizo kubwa, ziliwawekea wavuvi vikwazo. Hatua hiyo imewalinda samoni waliomo baharini.
Kurudi Kutoka Baharini
Hatimaye samoni aliyekomaa hurudi mtoni mahali alipotoka, kisha anatafuta mwenzi, na mzunguko huo wa maisha huanza tena. Michael anaeleza hivi: “Inashangaza kwamba samaki huyo wa ajabu husafiri maelfu ya kilometa katika maeneo ya bahari asiyoyajua bila kupotea! Wanasayansi bado hawafahamu jinsi anavyoweza kufanya hivyo. Wengine husema kwamba samoni husafiri kwa kuongozwa na nguvu za sumaku za dunia, mikondo ya bahari, au hata nyota. Inafikiriwa kwamba anaporudi kwenye mlango wa mto, samoni hutambua mto alimozaliwa kwa ‘harufu’ yake, au kemikali zilizomo.”
Michael anasema: “Kwa mara nyingine tena, samoni hubadilika kulingana na hali ili aishi katika maji yasiyo na chumvi, kisha yeye huingia mtoni. Uwezo wake wa kisilika wa kutambua njia ya kurudi nyumbani ni wenye nguvu sana hivi kwamba hata akikabili maporomoko ya maji au mkondo wenye nguvu, yeye hupambana juu chini na kila moja ya vizuizi hivyo kwa kuwa sasa ni mkubwa na mwenye nguvu zaidi.”
Anapokuwa njiani, samoni hukabili magumu mengine kama vile mabwawa asiyoweza kupanda, mitambo ya nguvu za umeme, au vizuizi vingine vilivyojengwa na mwanadamu. Yeye hufanya nini anapokabili magumu hayo? Deirdre, mtafiti wa samoni, anasema: “Watu wengi wanaohangaikia kuhifadhiwa kwa samoni hutengeneza njia nyingine. Wao hutengeneza vidimbwi mbalimbali vinavyofuatana ili kuwawezesha samaki kuepuka kizuizi hicho kikubwa. Vidimbwi hivyo huitwa ngazi ya samaki au kivukio cha samaki. Kivukio hicho humwezesha samoni kuruka kwa usalama hadi kwenye kidimbwi kilicho juu anaposafiri kurudi kwenye eneo la kuzalisha.”
Deirdre anasema: “Hata hivyo, mbinu hiyo haifanikiwi nyakati zote.” Kisha anaongezea: “Nimeona samoni kadhaa wakiepuka vidimbwi hivyo. Wao hutambua tu njia waliyotumia awali nao hujitahidi
kufa na kupona kuvuka kizuizi hicho kipya kilichotengenezwa na mwanadamu. Wengi wao hufa kwa sababu ya kuchoka sana au kujigonga kwenye kizuizi hicho.”Maeneo ya Kufuga Samoni
Samoni ni chakula kinachofaidi mwili. Kwa sababu ya kupungua kwa samoni wa Atlantiki, samoni hufugwa katika maeneo fulani na kuuzwa. Samoni huhifadhiwa katika vyombo vyenye maji yasiyokuwa na chumvi ambavyo huwekwa ufuoni hadi wanapokua kufikia hatua ya smolt. Kisha wao huhamishiwa baharini kwenye vyombo vilivyo kama vizimba ambako wao hutunzwa hadi wanapokomaa na kuwa tayari kuuzwa kwenye mikahawa na maduka ya vyakula.
Samoni wanaofugwa kwa njia hiyo hukabili matatizo pia. Wafugaji wa samaki huwalisha chakula kilichotengenezewa viwandani. Hilo, pamoja na kufungiwa katika vizimba, hufanya samoni waathiriwe kwa urahisi na magonjwa na wadudu kama vile viroboto wa majini. Baadhi ya dawa zinazonyunyizwa ili kuwalinda ni hatari sana. Ernest, ambaye ni mpiga-mbizi, anasema: “Nilipokuwa nikiogelea chini ya maeneo ya kufugia samaki niliona kwamba hakukuwa na viumbe wowote katika maeneo hayo.”
Samoni wa Atlantiki Yumo Taabani
Samoni wengi hunaswa katika nyavu kabla ya kurudi kwenye mto walimozaliwa. Wavuvi fulani huwavua samoni kinyume cha sheria kwa sababu wana thamani kubwa. Samoni wachache wanaofaulu kurudi katika mto walimozaliwa huhatarishwa pia na wavuvi waliopewa kibali cha kuvua kwa ndoano. Ili kuwalinda samoni, hatua mbalimbali zimechukuliwa kama vile kuwaruhusu watu kuvua samaki katika maeneo hususa tu, kupandisha ada ya kupata leseni ya kuvua samoni, na kuwaruhusu watu kuvua samaki katika kipindi hususa. Hata hivyo, inakadiriwa kwamba samaki mmoja kati ya watano atanaswa anaporudi mtoni.
Isitoshe, samoni wasiofugwa hupata magonjwa, na hilo limepunguza sana idadi yao. Ugonjwa mmoja unaowakumba husababisha vidonda kwenye ngozi yao na mwishowe wanakufa. Pia uchafu unaotoka viwandani na dawa za kuua wadudu huingia kwenye mito na kuhatarisha samoni na viumbe wengine wa majini.
Unapofikiria hatari zote hizo anazokabili, si ajabu kwamba samoni yumo taabani. Anaendelea kukabili matatizo licha ya jitihada bora za mwanadamu. Viumbe wataacha kuangamizwa wakati ambapo Mungu Mweza-Yote, ambaye ni Muumba wa dunia, atakapowazuia wanadamu wasiiharibu dunia.—Isaya 11:9; 65:25.
[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 14, 15]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Samoni wa Atlantiki husafiri kutoka mito ya Marekani, Urusi, na Hispania ili kulisha katika Visiwa vya Faeroe na Greenland kisha wao hurudi kuzalisha
[Ramani]
Marekani
Greenland
Iceland
Visiwa vya Faeroe
Urusi
Ufaransa
Hispania
[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 15]
MZUNGUKO WA MAISHA WA AJABU
Mayai
↓
Mayai yenye macho
↓
Alevin
↓
Fry
↓
Parr
↓
Smolt
↓
Samoni aliyekomaa
↓
Kuzalisha
[Pictures]
Alevin
Parr
[Hisani]
Life cycle: © Atlantic Salmon Federation/J.O. Pennanen; alevin: U.S. Fish & Wildlife Service, Washington, D.C.; parr: © Manu Esteve 2003
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Samoni anayerudi alikotoka anaweza kuruka poromoko hili la maji au avuke kupitia ngazi ya samaki (picha ndogo iliyoongezwa ukubwa upande wa kulia)
[Picha katika ukurasa wa 17]
Hatari ambazo samoni wanakabili zinatia ndani kuvuliwa kupita kiasi na magonjwa wanayopata wanapofugwa
[Hisani]
Photo: Vidar Vassvik
◀ UWPHOTO © Erling Svensen
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]
© Joanna McCarthy/SuperStock ▸