Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Wanaume wa Ulaya Wanatumia Muda Mrefu Kujipamba
Gazeti The Daily Telegraph la London linaripoti kwamba “kwa miaka mitano iliyopita, muda ambao wanaume hutumia kujipamba umeongezeka kufikia wastani wa saa 3.1 kwa juma ikilinganishwa na wastani wa saa 2.5 ambazo wanawake hutumia.” Siku hizi wanaume wengi wanahangaikia sana sura kwani wao hununua kwa wingi bidhaa za kutunza ngozi, nywele, mwili, na marashi yaliyotengenezwa hasa kwa ajili yao. Wanaume walitumia “pauni bilioni 13.6 [dola bilioni 25 za Marekani] mwaka jana na inatarajiwa kwamba kufikia mwaka wa 2008 watatumia pauni bilioni 16.1 [dola bilioni 29 za Marekani]” kununua bidhaa hizo. Msimamizi wa duka moja la kuwapamba wanaume aliwaeleza waandishi wa gazeti hilo hivi: “Biashara imetia fora kwani wateja hutumia pauni 200 [dola 360 za Marekani] ili warembeshwe uso, kucha za mikono, na kucha za miguu.” Isitoshe, gazeti hilo linaongeza kwamba “wanaume ndio wanaojinunulia asilimia 60 ya marashi ya wanaume wala si marafiki zao wa kike au wake zao.”
Wataalamu Wengi Sana
Gazeti El Universal la Mexico City linasema kwamba “siku hizi kupata shahada hakumaanishi kwamba mtu atapata kazi.” Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi huko Mexico ulionyesha kwamba “kati ya mwaka wa 1991 na 2000, asilimia 40 ya wataalamu walilazimika kufanya kazi zisizohusiana na masomo yao ya chuo kikuu.” Hilo linamaanisha kwamba wahitimu 750,000 wa vyuo vikuu wanafanya kazi zisizohitaji kuwa na shahada, kama vile “kupokea simu, kuendesha magari, kufanya viini-macho, kuwa mcheshi, [na] kuwahudumia watu katika baa.” Ripoti hiyo ilikadiria kwamba kufikia mwaka wa 2006, huko Mexico kutakuwa na wasimamizi 131,000 zaidi, wahasibu 100,000 zaidi, wataalamu wa kompyuta 92,000 zaidi, walimu wa shule za msingi 92,000 zaidi, na wanasheria 87,000 zaidi, ikilinganishwa na nafasi za kazi zilizopo.
Magari Yanachukua Mahali pa Baiskeli Nchini China
Uchumi wa China unapozidi kusitawi, watu wanaamua kutumia magari badala ya kuendesha baiskeli. Kwa mfano, sasa asilimia 25 tu ya wakaaji wa Beijing ndio wanaotumia baiskeli, hali miaka kumi iliyopita asilimia 60 ya watu walikuwa wakitumia baiskeli. Gazeti Toronto Star la Kanada linasema: “Huko Beijing, magari zaidi ya 400,000 huongezeka kila mwaka.” Hivyo, katika jiji hilo, “magari husafiri kwa wastani wa kilometa 12 kwa saa.” Gazeti National Geographic linaripoti kwamba katika mwaka wa 2003 huko China, “wafanyakazi waliofanikiwa walinunua zaidi ya magari milioni mbili, na idadi hiyo iliongezeka kwa asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka wa 2002.” Gazeti hilo linaongeza kwamba kwa kuwa watu wanatumia magari kuliko baiskeli, “huenda China imeizidi Japani na kuwa nchi ya pili inayotumia mafuta mengi zaidi ulimwenguni.” Hata hivyo, inakadiriwa kwamba bado kuna baiskeli milioni 470 nchini China.
Kuwasomea Watoto Wachanga Kunawanufaisha
Gazeti The Toronto Star linasema hivi: “Kuwasomea watoto wachanga huwanufaisha sana maishani hivi kwamba wataalamu wamependekeza wazazi waanze kuwasomea watoto wao saa chache tu baada ya kuzaliwa.” Dakt. Richard Goldbloom, ambaye miaka miwili iliyopita aliongoza mradi wa kwanza wa kuwasomea watoto waliotoka kuzaliwa huko Kanada, anasema hivi: “Tumegundua kwamba unapowasomea watoto, wao hukaza fikira sana tangu utotoni. Wanasikiliza.” Uchunguzi unaonyesha kwamba kuwapa watoto vitabu katika miaka yao ya mapema huboresha msamiati wao na uwezo wa kusoma. Gazeti hilo linasema kwamba “kusudi la kufanya hivyo si kuwalazimisha watoto wajifunze kusoma, bali ni kuboresha ustadi wao wa lugha na msamiati wao na vilevile kufahamu sauti za maneno, na hatimaye kusitawisha uwezo wa kusoma.”
Jamii za Wanyama Wasiolindwa Zinatoweka
Gazeti El Comercio la Peru linasema kwamba katika miaka ya karibuni watu wanaohifadhi mazingira wamefanikiwa kulinda zaidi ya asilimia 10 ya eneo la dunia. Licha ya mafanikio hayo, miradi ya kuhifadhi mazingira haijaweza kulinda “angalau jamii 300 za ndege, wanyama wanaonyonyesha, kasa, na amfibia, ambao wamo hatarini.” Kulingana na Gustavo Fonseca, makamu-msimamizi wa miradi na sayansi wa Shirika la Kuhifadhi la Kimataifa, miradi ya sasa ya kuhifadhi mazingira “inafaidi kisiasa” lakini haiwezi kufaulu. Anasema kwamba “tunapaswa kuhifadhi hasa maeneo yaliyo na jamii nyingi zilizomo hatarini.” Gazeti hilo linaonyesha hatari nyingine inayokabili jamii zilizomo hatarini. Linaripoti kwamba biashara ya viumbe waliomo hatarini ni mojawapo ya biashara kubwa zilizo haramu, baada ya ulanguzi wa dawa za kulevya na silaha. Karibu nusu ya wanyama wote wanaouzwa kimagendo ulimwenguni pote ni wale wanaotoka katika misitu ya Amerika Kusini.
Jihadhari na Vinywaji Vilivyotiwa Dawa
Gazeti The Australian linasema kwamba huko Australia “kila siku watu watano hivi hudhulumiwa kingono baada ya kutiliwa dawa katika vinywaji vyao wanapokuwa katika baa na karamu.” Dawa hizo au kileo hutiwa katika vinywaji bila wanywaji kujua. Baadhi ya dawa zinazotumiwa hazina rangi, ladha, wala harufu. Watu wanaotendewa hivyo wanaweza kuchanganyikiwa, kushindwa kutembea, au kupoteza fahamu. Baadhi yao wamekufa. Kulingana na gazeti hilo, uchunguzi wa kitaifa uliofanywa na Taasisi ya Uhalifu ya Australia ulionyesha kwamba “inakadiriwa kuwa watu 4500 hutiliwa dawa katika vinywaji vyao kila mwaka, na asilimia 40 kati yao hudhulumiwa kingono.” Baada ya dawa hizo kwisha nguvu, huenda watu waliotendewa hivyo wasikumbuke mambo yaliyowapata.
Je, Kuna Tumaini kwa Tabaka la Ozoni?
Gazeti ECOS linalochapishwa na Shirika la Utafiti wa Sayansi na Viwanda la Australia (CSIRO) linasema kwamba “gesi za chlorofluorocarbon (CFC) zilizo hewani zimeanza kupungua.” Gesi hizo huharibu tabaka la ozoni linalofunika dunia. Kwa zaidi ya miaka 50, gesi za CFC zilizo katika angahewa ziliongezeka hadi mwaka wa 2000. Tangu wakati huo, kiwango cha gesi hizo kimekuwa “kikipungua kwa asilimia moja hivi kwa mwaka,” linasema gazeti ECOS. Ripoti hiyo inasema kwamba kupungua kwa kiwango hicho “kunaonyesha kuwa huenda shimo lililo katika ozoni likazibika kufikia katikati ya karne hii.” Hata hivyo, bado kemikali hizo zinasababisha madhara. Ripoti hiyo inasema: “Licha ya kupungua huko, mwaka huu shimo la tabaka la ozoni lililo juu ya eneo la Antaktika . . . lilikuwa na ukubwa wa kilometa milioni 29 hivi za mraba, ukubwa unaozidi mara tatu eneo lote la Australia.”