Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
Je, Unaweza Kutabasamu na Mamba?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI INDIA
JE, UMEWAHI kuwazia ukitabasamu na mamba? Katika wimbo unaosimulia hadithi ya watoto inayoitwa Peter Pan, mhusika mmoja anayeitwa Captain Hook anasema, “Usitabasamu kamwe na mamba.” Kisha anaeleza hivi kuhusu sababu yake ya kutoa shauri hilo: “Mamba anafikiria jinsi atakavyokumeza”!
Ingawa ni kweli kwamba kati ya aina nyingi za mamba wanaopatikana ulimwenguni kuna wale ambao huwashambulia wanadamu, “hilo hutokea mara chache sana . . . hivi kwamba mamba hawawezi kuorodheshwa kati ya wanyama ambao hula watu.” (Kitabu Encyclopædia Britannica) Ijapokuwa watu fulani huwaona mamba kuwa viumbe wenye sura mbovu na wanaotisha, watu wengine huvutiwa nao. Hebu tuchunguze aina tatu za mamba wanaopatikana nchini India, yaani mamba wa maji ya chumvi, mugger, na gavial.
Mamba wa Maji ya Chumvi
Mamba wa maji ya chumvi ndio wanyama wakubwa zaidi wanaotambaa, kwani wanaweza kufikia urefu wa meta 7 au zaidi, na uzito wa kilo 1,000 hivi. Kwa kuwa wao huishi hasa katika maji ya chumvi, wao hupatikana katika vinamasi vya mikoko kwenye pwani, milango ya mito, na bahari, kuanzia India kuelekea mashariki huko Fiji. Wao hula nyama tu. Mamba hao hula panya, vyura, samaki, nyoka, kaa, kasa, na mbawala kwa kiasi kidogo. Mamba-dume wakubwa hula kati ya gramu 500 na 700 za chakula kwa siku. Hawahitaji nguvu nyingi kwa kuwa wao hutumia muda mrefu wakiota jua na kuelea majini na wana mfumo mzuri wa kusaga chakula. Mara kwa mara mamba hao huwashambulia wanadamu. Wao huogelea kwa kupepesa mkia wao huku wakiwa wamezamisha miili yao isipokuwa pua na macho. Wao hutumia miguu yao mifupi kutembea. Wanaweza kuruka ili kukamata windo, na nyakati nyingine hukimbiza windo lao. Sawa na mamba wengine, mamba hao wana uwezo mzuri wa kunusa, kuona, na kusikia. Wakati wa kujamiiana, mamba-dume hulinda eneo lake kwa ukali, naye mamba-jike huyalinda mayai yake kwa ukali pia.
Mama Wanaojitoa Mhanga
Mamba wa kike hutengeneza mahali pa kutagia karibu na maji, naye hupafanyiza kwa rundo la matope na majani yanayooza. Yeye hutaga karibu mayai 100 magumu, kisha huyafunika na kuyalinda kutokana na wavamizi. Halafu yeye huyamwagilia maji ili kufanya majani yaoze haraka, na hivyo kutokeza joto linalohitajiwa ili yaanguliwe.
Kisha jambo fulani la ajabu hutukia. Jinsia ya mtoto hutegemea joto linalokuwapo wakati yai limefunikwa
kwa majani. Hilo ni jambo la ajabu sana! Kunapokuwa na joto la nyuzi 28 Selsiasi hadi nyuzi 31 Selsiasi mamba-jike hutokezwa baada ya siku 100 hivi, na kunapokuwa na joto la nyuzi 32.5 Selsiasi mamba-dume hutokezwa katika kipindi cha siku 64 hivi. Mayai yanayopata joto la nyuzi 32.5 Selsiasi hadi nyuzi 33 Selsiasi yanaweza kutokeza mamba-dume au mamba-jike. Iwapo upande mmoja wa mahali pa kutagia uko kando ya maji na upande ule mwingine uko upande wa jua, mayai yaliyoko upande wenye joto yatatokeza mamba-dume, huku mayai yaliyoko upande usio na joto yakitokeza mamba-jike.Mamba-jike anaposikia sauti ndogo-ndogo zikitoka mahali hapo pa kutagia, yeye huondoa majani na matope, na nyakati nyingine yeye huyavunja mayai iwapo watoto hawajafanya hivyo kwa kutumia jino lao la kuvunjia yai. Yeye huwainua polepole kwa kutumia mataya yake makubwa na kuwabeba ndani ya kifuko kilicho chini ya ulimi wake hadi kando ya maji. Kwa kuwa watoto wa mamba hujitegemea mara tu wanapoanguliwa, wao huanza kutafuta wadudu, vyura, na samaki wadogo. Hata hivyo, mamba-jike fulani huwalinda watoto wao kwa kukaa karibu nao kwa miezi kadhaa, huku wakitenga sehemu fulani kwenye vinamasi ambako mamba-dume hushiriki kuwatunza na kuwalinda.
Mamba Wengine
Mamba aina ya mugger ambaye huishi kwenye vinamasi na mamba aina ya gavial hupatikana India tu. Mamba aina ya mugger ambaye huwa na urefu wa meta nne hivi, hupatikana katika maji yasiyo na chumvi ya vinamasi, maziwa, na mito kotekote nchini India, naye ni mdogo sana kuliko mamba wa maji ya chumvi. Yeye hutumia mataya yake yenye nguvu kuwakamata wanyama wadogo, kisha huwazamisha majini, na kuwatikisa-tikisa ili kuwanyafua.
Mamba hao hukutanaje ili kujamiiana? Mamba-dume hupigapiga maji kwa mataya yake na kunguruma anapotafuta mamba-jike. Baadaye atamsaidia mamba-jike kulinda mayai, kuwasaidia watoto watoke kwenye mayai, na kuwatunza kwa muda.
Mamba aina ya gavial ni tofauti na mamba wengine. Yeye hutambuliwa kwa urahisi kwani mataya yake ni marefu sana na membamba. Mataya hayo yanafaa sana kukamata samaki, ambao ndio chakula chake kikuu. Ijapokuwa anatoshana na mamba wa maji ya chumvi kwa urefu, yeye hawashambulii wanadamu. Mwili wake laini na mwembamba humwezesha kuogelea kasi katika maji yanayotiririka upesi ya mito yenye kina kirefu iliyoko kaskazini mwa India. Mamba-dume wa aina ya gavial hutokeza kinundu kwenye ncha ya mdomo wake katika kipindi cha kujamiiana. Kinundu hicho huongeza mvumo wa sauti yake na hilo huwavutia mamba-jike.
Umuhimu wa Mamba Katika Mazingira
Mamba wana umuhimu gani katika mazingira yetu? Wao hula mizoga ya wanyama na samaki na hivyo kusafisha mito, maziwa, na maeneo yaliyo karibu. Wao hushambulia wanyama walio dhaifu, walioumia, na wagonjwa. Wao hula samaki kama vile kambare, ambao hula samaki wengine wanaovuliwa na kuuzwa kwa wingi.
Jitihada za Kuwaokoa Mamba
Je, umewahi kusikia mtu akiambiwa kwamba anatoa machozi ya mamba? Hilo linamaanisha kwamba anajifanya. Mamba hutoa machozi ili kuondoa chumvi ya ziada iliyo mwilini mwake. Hata hivyo, mwanzoni mwa miaka ya 1970, huenda watu wangetoa machozi ya kweli kwa ajili ya mamba. Wakati huo, kulikuwa na maelfu kadhaa tu ya mamba nchini India, na hiyo ilikuwa asilimia 10 hivi ya idadi yao ya awali. Kwa nini? Kadiri wanadamu walivyozidi kunyakua makao yao, waliwaua mamba kwani walihofia kuwa watahatarisha mifugo wachanga na walio dhaifu. Watu wengi walifurahia sana kula nyama na mayai ya mamba. Tezi fulani za mamba zilitumiwa kutengeneza manukato. Isitoshe, ujenzi wa mabwawa na uchafuzi wa maji umeathiri sana idadi ya mamba. Hata hivyo, inaonekana kwamba uhitaji wa ngozi ya mamba ndio umechangia sana kupungua kwa idadi yao. Viatu, mikoba, masanduku, mishipi, na vitu vingine vinavyotengenezwa kwa ngozi ya mamba huwa maridadi sana, hudumu kwa muda mrefu, na huwavutia watu wengi. Ingawa bado mamba wanakabili matatizo, jitihada za kuwahifadhi zimefanikiwa sana!—Ona sanduku lililo chini.
Usikose Kutabasamu!
Sasa, baada ya kujifunza kuhusu aina kadhaa za mamba, una maoni gani kuwahusu? Tunatumaini kwamba umebadili maoni yoyote mabaya ambayo huenda ulikuwa nayo kuhusu wanyama hao, na unavutiwa nao sasa. Ulimwenguni pote, watu wengi ambao huvutiwa na wanyama wanatarajia wakati ambapo hawataogopa mnyama yeyote kutia ndani mamba mkubwa wa maji ya chumvi. Muumba wa wanyama wanaotambaa atakapoifanya dunia kuwa mpya, tutaweza kutabasamu na mamba wote.—Isaya 11:8, 9.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]
Eneo la Kuzalishia Mamba la Madras
Katika mwaka wa 1972, mradi wa kuhifadhi mamba kwenye Hifadhi ya Nyoka ya Madras ulianzishwa. Mradi huo ulianzishwa baada ya uchunguzi fulani kuonyesha kwamba kuna mamba wachache sana waliosalia kwenye makao yao ya asili katika maeneo fulani ya Asia. Eneo la kuzalishia mamba la Madras ndiyo hifadhi ya mamba ya zamani zaidi na iliyo kubwa zaidi kati ya hifadhi zaidi ya 30 nchini India. Hifadhi hiyo ilianzishwa na mtaalamu Romulus Whitaker mnamo mwaka wa 1976. Hifadhi hiyo iliyo na ukubwa wa ekari nane na nusu iko katika Ufuo wa Coromandel, nayo ina jamii 150 za miti ambayo huvutia ndege na wadudu maridadi.
Mamba huzalishwa katika hifadhi hiyo, kisha wao hupelekwa kwenye vinamasi na mito, au kwenye hifadhi nyinginezo. Hifadhi hiyo ina sehemu ya kufugia mamba wachanga, ambayo nyakati nyingine huwa na mamba 2,500 hivi. Mamba hao wachanga hufugwa katika vidimbwi, nao hulishwa vipande vya samaki ambavyo huletwa kila siku na wavuvi wa eneo hilo. Nyavu hutumiwa kuwazuia ndege wasiingie kwenye vidimbwi hivyo na kuwala samaki au mamba hao wachanga walio dhaifu. Baada ya kukua kwa kadiri fulani, mamba hao huhamishiwa katika vidimbwi vikubwa nao hulishwa samaki wazima tangu wakati huo hadi wanapokuwa na umri wa miaka mitatu na urefu wa meta 1.25 hadi 1.5. Baada ya hapo, wao huanza kulishwa nyama ya ng’ombe kutoka katika kiwanda fulani cha nyama. Mwanzoni, jamii tatu tu za mamba wanaopatikana huko India ndio waliofugwa katika hifadhi ya Madras, lakini leo kuna jamii nyingine saba za mamba, na mipango inafanywa ili kuhifadhi jamii zote za mamba zinazojulikana. Suala la kufuga mamba wengi ili kuwauza kwa ajili ya nyama na ngozi limejadiliwa sana. Whitaker alimweleza mwandishi wa Amkeni! kwamba nyama ya mamba ni tamu na ina kiasi kidogo cha kolesteroli. Jitihada za kuzalisha mamba na kuwahifadhi zimefanikiwa kuokoa mamba waliokuwa karibu kutoweka na kuongeza sana idadi yao. Hifadhi ya Madras, ambayo hutembelewa sana na watalii, itawawezesha watu kubadili maoni yao yenye kasoro kuhusu mamba na kuwafanya wavutiwe zaidi nao.
[Hisani]
Romulus Whitaker, Madras Crocodile Bank
[Picha katika ukurasa wa 11]
Mamba wa maji ya chumvi
[Picha katika ukurasa wa 12]
Mamba-jike wa maji ya chumvi akimbeba mtoto wake kwa mataya yake
[Hisani]
© Adam Britton, http://crocodilian.com
[Picha katika ukurasa wa 12]
“Mugger”
[Hisani]
© E. Hanumantha Rao/Photo Researchers, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 12]
“Gavial” mwenye pua ndefu