Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Joto Katika Majiji Huathiri Ukuzi wa Mimea
Kulingana na ripoti iliyochapishwa na gazeti Science News, yaelekea uchunguzi wa setilaiti wa eneo la mashariki la Amerika Kaskazini unaonyesha kwamba joto katika majiji huathiri ukuzi wa mimea. Ripoti hiyo inasema kwamba mimea inayokua katika majiji huchipuka mapema katika majira ya kuchipua na majani yake hudumu kwa muda mrefu katika majira ya kupukutika kwa majani kuliko mimea inayokua katika maeneo ya mashambani yaliyo karibu na majiji. Kulingana na gazeti Science News, katika kipindi cha miezi mitano joto la majiji lilikuwa “wastani wa nyuzi 2.28 Selsiasi zaidi ya joto la maeneo yaliyokuwa umbali wa kilometa 10 hivi kutoka katika majiji hayo.” Eneo lililo kati ya kaskazini mwa Florida na kusini mwa Kanada lina majiji 70 hivi yaliyo na ukubwa wa zaidi ya kilometa kumi za mraba. Gazeti Science News linasema: “Habari hizo zinaonyesha kwamba majiji hayo huathiri sana hali ya hewa ya eneo hilo.”
Urafiki Miongoni mwa Wanyama
Kwa muda mrefu wakulima na wachungaji wamedhania kwamba wanyama wenye kwato wanaweza kufanya urafiki na wanyama wengine katika kundi lao, lakini sasa uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na mwanabiolojia Anja Wasilewski unathibitisha jambo hilo. Wasilewski ambaye amewachunguza farasi, punda, ng’ombe, na kondoo, anasema kwamba urafiki kati ya wanyama huonekana wanapokaribiana mara nyingi, wanapogusana wakati wa kupumzika au kula, wanapolisha pamoja, na kusafishana. Kwa mfano, kondoo hutumia kichwa chake kusugua kichwa cha kondoo mwenzake ambaye ametoka kupigana na mnyama mwingine. Gazeti Die Zeit la Ujerumani linaripoti kwamba huenda kufanya hivyo humtuliza na kumfariji kondoo huyo. Kwa kawaida punda huwa na rafiki mmoja, lakini urafiki wao hudumu kwa muda mrefu zaidi. Lakini ili kutowafanya wanyama waonekane kama wanadamu, watafiti huepuka kukisia kusudi na matokeo ya urafiki huo.
Ukataji wa Miti Katika Amerika ya Latini
Ripoti moja iliyochapishwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa inasema kwamba katika kipindi cha miaka 13 tu, eneo la msitu lenye ukubwa wa ekari milioni 125 huko Amerika ya Latini limeharibiwa. Eneo hilo linalingana na eneo lote la Amerika ya Kati. Huko Brazili, eneo la ekari milioni 57 liliharibiwa, hali nchini Mexico eneo la msitu la ekari milioni 16 liliharibiwa kupitia ukataji wa miti na eneo la ekari 990,000 likaharibiwa na mmomonyoko wa udongo. Katika kipindi hichohicho asilimia 46 hadi 49 ya misitu iliharibiwa huko Haiti, El Salvador, na kisiwa cha St. Lucia. Gazeti ¿Cómo Ves? ambalo ni gazeti la sayansi la Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Mexico, linasema kwamba takwimu hizo “zinasikitisha hasa tunapofikiria . . . mamia ya maelfu ya mimea na wanyama ambao wametoweka duniani kwa sababu ya kuongezeka kwa ukame.”
Watu Wanaochoka Daima Wanahitaji Mazoezi
Licha ya uchunguzi mwingi, wanasayansi hawajaweza kugundua visababishi na tiba ya ugonjwa wa kuchoka daima. Ripoti iliyochapishwa katika jarida The Medical Journal of Australia (MJA) inasema kwamba “dawa nyingi za kuua viini, za kuimarisha mfumo wa kinga, za homoni, za kutuliza akili, na dawa nyingine ambazo zimejaribiwa, hazijawa na matokeo makubwa.” Kufanya mazoezi kama vile kutembea, kuendesha baiskeli, au kuogelea kumewafaidi wagonjwa kuliko matibabu mengine. Watu fulani wanaougua ugonjwa wa kuchoka daima huepuka kufanya mazoezi kwa sababu tatizo lao huzidi wanapofanya mazoezi kupita kiasi. Lakini mgonjwa anapaswa kufanya mazoezi kwa kiasi. Kulingana na gazeti MJA, wagonjwa fulani ambao hufanya mazoezi kwa kiasi kupatana na hali zao wanapofanyiwa uchunguzi wa mshuko wa moyo, hali za kihisia, uwezo wa kufanya kazi, na shinikizo la damu, inagunduliwa kwamba afya yao huwa ‘afadhali zaidi.’ Ripoti hiyo inamalizia kwa kusema kwamba “watu wanaochoka daima wanapaswa kufanya mazoezi na kuongeza kiwango cha mazoezi hayo hatua kwa hatua.”
Panda na Mianzi
Gazeti The Daily Telegraph la London linasema kwamba “panda, ambaye huwakilisha China na jitihada za kuhifadhi wanyama wa pori, hayumo hatarini kama ilivyofikiriwa.” Awali ilifikiriwa kwamba kuna panda wapatao 1,000 hadi 1,100 porini, lakini uchunguzi wa miaka minne uliofanywa na Hazina ya Ulimwenguni Pote ya Vitu vya Asili pamoja na serikali ya China umeonyesha kwamba kuna zaidi ya panda 1,590 porini. Idadi hiyo sahihi ilipatikana kwa kutumia teknolojia iliyoboreshwa, inayohusisha matumizi ya setilaiti kuonyesha maeneo yanayochunguzwa. Ingawa habari hizo zinawafurahisha watu wanaohifadhi mazingira, Kituo cha Kuhifadhi Mazingira Ulimwenguni cha Cambridge, Uingereza, kinaonya kwamba mianzi, ambayo ndiyo chakula kikuu cha panda, inaharibiwa sana. Mianzi inaharibiwa haraka sana kwa sababu, kulingana na gazeti The Guardian la London, “kila mwanzi huchanua mara moja na kwa wakati uleule baada ya miaka 20 hadi 100 halafu hunyauka.”
Hatari ya Kutumia Dawa za Kufukuzia Mbu
Gazeti Down to Earth la India linaripoti kwamba miradi miwili ya uchunguzi imeonyesha kwamba kutumia dawa za kufukuzia mbu kunaweza kusababisha madhara hasa kwa watoto. Dawa hizo hutumiwa sana huko Asia. Kwanza, wanasayansi katika Chuo Kikuu cha California, huko Marekani, wanasema kwamba moshi wa dawa hizo huathiri sana mapafu. Watu wengi katika nchi zinazoendelea hutumia dawa hizo ndani ya nyumba zao ndogo. Pia kulingana na wataalamu waliofanya uchunguzi huo, “madirisha hufungwa watu wanapolala.” Uchunguzi wa pili uliofanywa na wanasayansi kutoka Malaysia na Marekani ulionyesha kwamba ukiwasha dawa ya kufukuzia mbu na kuiacha iwake kwa saa nane “itatoa moshi kama ule unaoweza kutokezwa na sigara 75 hadi 137.” Wataalamu wanapendekeza watu watumie bidhaa zinazotokana na mimea kama vile mwarubaini. Ripoti hiyo inasema kwamba “bidhaa za aina hiyo hazidhuru afya na ni za bei nafuu.”
Kuzorota kwa Viwango vya Kupimia Filamu
“Kwa wastani, filamu zinazoonyeshwa leo zina jeuri, ngono, na lugha chafu kuliko filamu za miaka kumi iliyopita.” Hivyo ndivyo watafiti katika Shule ya Afya ya Umma ya Harvard, huko Marekani, walivyokata kauli baada ya kuchunguza viwango vya kupimia filamu vinavyotumiwa katika nchi fulani. Watafiti hao walichunguza uhusiano kati ya viwango vya kupimia filamu na yaliyomo katika filamu zilizotolewa kati ya mwaka wa 1992 na 2003. Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kwamba viwango ambavyo vimetumiwa kwa muda mrefu vinazidi kulegezwa. Watafiti hao walikata kauli kwamba “ni lazima wazazi watambue kwamba wana daraka la kuwachagulia watoto filamu zinazofaa wakiwa pamoja na watoto, kuzungumza nao kuhusu habari zilizomo katika filamu hizo ili kuwazuia wasiathiriwe na habari zozote zinazoweza kuwadhuru, na kukazia habari zinazoweza kuwanufaisha.”