Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Mafuta Yanayolinda Ngozi ya Kiboko
Gazeti The Independent la London linaripoti kwamba “viboko hulinda ngozi yao isiyo na manyoya isiathiriwe na jua kwa kutokeza mafuta kama yale ambayo wanadamu hutumia.” Wanasayansi fulani huko Kyoto nchini, Japani, walipochunguza umajimaji unaotokezwa na mnyama fulani katika hifadhi ya wanyama ya Tokyo waligundua jinsi umajimaji huo unavyolinda ngozi ya kiboko kutokana na mwangaza wa jua na vumbi katika eneo la tropiki. Umajimaji huo mzito wenye kunata usio na rangi hubadilika polepole na kuwa mwekundu, kisha kahawia, nao hugeuka na kuwa kama plastiki. Unapobadilika kuwa kahawia, unaacha kuwa wa alkali na unakuwa na asidi nyingi, na kwa hiyo unaweza kuua viini. Umajimaji huo wa kahawia pia hulinda ngozi ili isiathiriwe na miale fulani ya jua, kama tu mafuta yanayouzwa madukani. Hata hivyo, gazeti hilo lilimalizia kwa kusema kwamba haielekei kuwa makampuni ya kutokeza vipodozi yataanza kutumia viboko kutokeza mafuta ya kuzuia miale ya jua hivi karibuni, kwani kuna viboko wachache sana ulimwenguni na pia umajimaji huo una harufu mbaya sana.
Kuinua Uzani Hupunguza Mshuko wa Moyo wa Wazee
Gazeti Australian linasema kwamba kulingana na uchunguzi mmoja “kuinua uzani kunaweza kupunguza mshuko wa moyo miongoni mwa wazee kwa asilimia 50.” Kwa hiyo, kulingana na Dakt. Nalin Singh wa Hospitali ya Royal Prince Alfred ya Sydney, kuinua uzani ni sawa na kutumia dawa za kupunguza mshuko wa moyo. Katika uchunguzi huo uliowahusisha wanaume na wanawake 60 ambao kwa wastani wana umri wa miaka 72, hata wale ambao hawakufanya mazoezi ya kuchosha sana “walipunguza mshuko wa moyo kwa asilimia 30, sawa na wale ambao hawakuinua uzani lakini walipata matibabu ya hali ya juu,” linasema gazeti The Australian. Zaidi ya kupunguza mshuko wa moyo, gazeti hilo linasema kwamba kuinua uzani huimarisha “mifupa na misuli inayoendelea kuzeeka na hivyo kuwasaidia wazee wasianguke. Pia husaidia kukabiliana na ugonjwa wa yabisi-kavu, kisukari, na shinikizo la damu.” Dakt. Singh anadokeza kwamba kuinua uzani “kunapaswa kuwa njia ya msingi ya kuwatibu watu walioshuka moyo, hasa wazee.”
Televisheni Hufundisha Ukatili
Kulingana na uchunguzi ulioripotiwa katika gazeti The Times la London, “kutazama vipindi vya televisheni vya mfululizo huwachochea watoto wawe na tabia zisizofaa kama vile kusengenya watu, kupiga porojo, kueneza uvumi, kuvunja mahusiano ya wengine, na kudhulumu watu kwa maneno.” Gazeti hilo linasema kwamba uchunguzi huo, uliotolewa kwa Shirika la Saikolojia la Uingereza, umegundua kwamba kuna “uhusiano mkubwa” kati ya kutazama ukatili huo usio wa moja kwa moja kwenye televisheni na tabia mbaya ya vijana. Vipindi vile vibaya zaidi vilionyesha wastani wa matukio 14 ya kusengenya katika muda wa saa moja. Mhadhiri Sarah Coyne wa Chuo Kikuu cha Central Lancashire nchini Uingereza, anahofu kuwa kuonyesha “tena na tena” kwamba ukatili usio wa moja kwa moja unakubalika, unavutia, au unaleta faida ni mfano mbaya kwa vijana.
Matokeo ya Kula Wanga Kidogo
Ingawa watu wanaweza kupunguza uzito kwa kula chakula chenye kiasi kidogo cha wanga, mambo mengi hayajulikani kuhusu athari za kula chakula hicho kwa muda mrefu. Wachunguzi fulani wanahofia kwamba kula protini nyingi kunaweza kutokeza magonjwa ya ini, ya figo, ya mifupa, na magonjwa mengine makubwa. Gazeti Time linasema kwamba ‘vyakula vingi vitamu kama vile aina fulani za nyama na rojo fulani zilizotengenezwa kwa mayai huwa na mafuta ambayo yanaweza kuziba mishipa, na kutokeza hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa moyo na kiharusi.’ Hata hivyo, Dakt. David Katz wa Chuo Kikuu cha Yale cha Mafunzo ya Afya ya Umma anasema hivi: “Uchunguzi mwingi umeonyesha kwamba vyakula vilivyo na nyuzinyuzi nyingi na kiasi kikubwa cha wanga, ambavyo kwa kawaida hupatikana katika matunda, mboga, maharagwe na nafaka iliyo na maganda, huwafanya watu waishi muda mrefu na wadumishe kiwango kinachofaa cha uzito, hupunguza uwezekano wa kupata kansa, ugonjwa wa moyo, kisukari, magonjwa ya tumbo, na huboresha afya ya watu.”
Michongo Iliyopakwa Rangi
Gazeti la Kijerumani Spektrum der Wissenschaft linasema kwamba “wanaakiolojia na wanahistoria wa sanaa wanasita kubadili maoni waliyokuwa nayo kwamba michongo ya kale iliyofanyizwa kwa marumaru meupe” kama ile ya Wagiriki, “haikupakwa rangi. Ukweli ni kwamba sanamu hizo zilikuwa zimepakwa rangi nyangavu.” Ijapokuwa uthibitisho wa kihistoria unaonyesha kwamba kuna michongo iliyopakwa rangi, wasomi hawajishughulishi na jambo hilo. Hata hivyo, hivi karibuni uchunguzi fulani umethibitisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba michongo ilipakwa rangi. Rangi huchakaa kwa viwango mbalimbali na kubambuka, na hivyo sehemu fulani za mchongo huonekana wazi kabla ya sehemu nyingine. Tofauti iliyopo kati ya sehemu zilizobambuka na zile zenye rangi huonyesha kwamba mchongo umepakwa rangi mbalimbali. Ripoti hiyo inamalizia kwa kusema kuwa inaonekana “Wagiriki na Waroma waliona kwamba mchongo umekamilika baada ya rangi kupakwa.”
Ulimi wa Kinyonga Unaosonga Haraka
Kinyonga huwezaje kuchomoa ulimi wake kwa kasi ili akamate chakula? Gazeti New Scientist linaripoti kwamba kinyonga ana “mfumo fulani katika ulimi ambao huhifadhi nguvu kama zile zinazokuwa katika kifaa cha kurushia mawe kabla tu ya jiwe kurushwa.” Wanasayansi walijua kwamba ulimi wa kinyonga huwa na tishu zilizozungukwa na “msuli wa kuongeza mwendo.” Sasa kwa kutumia video iliyopunguzwa mwendo, wachunguzi Waholanzi wamegundua kwamba muda mfupi sana kabla kinyonga hajarusha ulimi wake ili kunasa chakula, yeye “hutumia msuli huo wa kuongeza mwendo kuhifadhi nguvu ndani ya tishu za ulimi, na kuzipanga kama sehemu za darubini. Wakati kinyonga anapochomoa ulimi wake haraka, nguvu zilizohifadhiwa zinaweza kuachiliwa katika sehemu ya 20 ya sekunde na kuongeza mwendo anaotumia kuurusha” ili kunasa chakula.
Waingereza Wasio na Imani
Kura ya maoni iliyohusisha watu 10,000 katika nchi kumi ilifunua kwamba nchi ya Uingereza ni “kati ya zile zisizomwamini mungu . . . , na zilizo na watu wachache sana walio na imani ya kidini au wanaoshiriki katika mambo ya kidini,” linasema gazeti The Times la London. Ingawa asilimia 46 ya Waingereza walisema kwamba wanamwamini Mungu, ni nchi mbili tu, yaani, Urusi na Jamhuri ya Korea, zilizokuwa na waamini wachache zaidi kuliko Uingereza. Zaidi ya asilimia 90 ya watu huko Nigeria, Indonesia, na Lebanoni, waliamini kwamba mungu wao ndiye Mungu wa pekee wa kweli, lakini ni watu 3 tu kati ya 10 nchini Uingereza walikuwa na maoni hayo. Katika nchi nyingi, zaidi ya watu asilimia 80 walisema kwamba kumwamini Mungu kunamfanya mtu kuwa mzuri zaidi, lakini asilimia 56 tu ya Waingereza ndio waliokubaliana na maoni hayo. Ijapokuwa asilimia 85 nchini Marekani, asilimia 99 nchini Indonesia, na asilimia 83 nchini Mexico wanaamini Mungu aliumba ulimwengu, ni asilimia 52 tu ya Waingereza wanaoamini hivyo. Walipoulizwa ikiwa dunia itakuwa na amani zaidi iwapo dini zikiondolewa, asilimia 6 nchini Marekani, asilimia 9 nchini India na asilimia 11 nchini Israeli walisema ndiyo, lakini nchini Uingereza ni asilimia 29 waliosema kungekuwa na amani zaidi!