Wewe Huendesha Gari Upande Gani wa Barabara?
Wewe Huendesha Gari Upande Gani wa Barabara?
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Uingereza
Ninamlaki mgeni wangu Mmarekani katika uwanja wa ndege na kuandamana naye hadi kwenye gari langu. Ninamwambia, “Keti kwenye kiti cha mbele,” na mara moja anaelekea upande wa dereva. Kisha anasema, “Ah, nilisahau kwamba ninyi huendesha gari upande usiofaa wa barabara.”
Bila shaka, mimi pia ningesema vivyo hivyo ikiwa ningetembelea Marekani. Tulipokuwa tukielekea nyumbani niliamua kuchunguza sababu inayofanya watu katika nchi nyingine kuendesha gari upande wa kushoto, hali madereva katika nchi nyingi ulimwenguni huendesha magari upande wa kulia.
Upande Ambao Magari Yaliendeshewa Zamani
Hebu tufikirie jinsi hali ilivyokuwa wakati nchi ya Uingereza ilipokuwa ikimilikiwa na Waroma yapata miaka 2,000 iliyopita. Wanaakiolojia wamepata uthibitisho fulani unaoonyesha upande uliotumiwa kuendesha magari enzi hizo. Katika mwaka wa 1998, walipata njia iliyotunzwa vizuri ya kwenda kwenye machimbo ya mawe ya Waroma karibu na jiji la Swindon, nchini Uingereza. Kina cha alama za magurudumu ya magari katika upande mmoja wa barabara hiyo huzidi kina cha alama zilizo upande ule mwingine, na hilo ni jambo linalotazamiwa kwani magari ya kukokotwa yaliingia kwenye machimbo bila mizigo lakini yakatoka yakiwa yamebeba mawe. Alama hizo huonyesha kwamba Waroma waliotumia barabara hiyo waliendesha magari kwenye upande wa kushoto.
Watu fulani huamini kwamba zamani wapanda-farasi walitumia upande wa kushoto. Kwa kuwa watu wengi hutumia mkono wa kulia, wapanda-farasi walishika hatamu kwa mkono wao wa kushoto na kutumia mkono wa kulia kuwasalimu wapanda-farasi wenzao au kubeba upanga ili kupigana ilipohitajiwa.
Magari Yaanza Kuendeshewa Upande wa Kulia
Katika miaka ya 1700, watu katika nchi mbalimbali kama vile Marekani walianza kuendesha magari kwenye upande wa kulia, wakati watu waliotumia wanyama kubeba mizigo walipoanza kutumia magari makubwa ya kukokotwa yaliyovutwa na farasi kadhaa. Magari hayo hayakuwa na kiti cha dereva, hivyo dereva alipanda farasi aliyekuwa nyuma kwenye upande wa kushoto huku akiwa na mjeledi kwenye mkono wake wa kuume. Kwa kuwa dereva aliketi upande wa kushoto, ni wazi kwamba wakati wa kupitana na magari mengine angetaka
yapitie upande wa kushoto ili aone vizuri magurudumu yake na hivyo kuepuka kugongana nayo. Kwa hiyo aliendesha gari lake upande wa kulia wa barabara.Hata hivyo, Waingereza waliendelea kuendesha magari kwenye upande wa kushoto. Walikuwa na magari madogo ya kukokotwa na kwa kawaida dereva aliketi upande wa kulia wa kiti cha mbele cha gari hilo. Akiwa hapo, angeweza kutumia mjeledi wake mrefu bila kutatizwa na mizigo iliyokuwa nyuma. Kwa kuwa dereva aliketi upande wa kulia wa gari la kukokotwa, angeweza kukadiria vizuri nafasi ya kutosha kupishana na magari mengine ikiwa angeendesha gari lake kwenye upande wa kushoto. Nchi ambazo baadaye zilikuwa sehemu ya milki ya Uingereza zilifuata sheria hiyo ya kuendesha magari kwenye upande wa kushoto. Hata hivyo, nchi fulani kati yazo kama vile Kanada, zilibadili sheria hiyo ili iwe rahisi kuvuka mipaka yao na Marekani.
Matukio ya kisiasa yaliathiri sana njia ya kuendesha magari huko Ufaransa. Kabla ya yale Mapinduzi ya mwaka wa 1789, wakuu wa nchi hiyo waliendesha magari ya farasi kwenye upande wa kushoto na kuwalazimisha maskini kupitia upande wa kulia. Hata hivyo, Mapinduzi hayo yalipoanza, wakuu hao walijaribu kuchangamana na maskini waliokuwa wakipitia upande wa kulia ili wasitambuliwe kwa urahisi. Kufikia mwaka wa 1794, serikali ya Ufaransa ilikuwa imeweka sheria ya kuendesha magari kwenye upande wa kulia huko Paris, kisha hatua kwa hatua sheria hiyo ikaanza kutumiwa katika maeneo mengine kadiri majeshi ya Napoléon wa Kwanza yalivyotwaa nchi nyingi za Ulaya. Haishangazi kwamba Napoléon alipendelea kuendesha gari kwenye upande wa kulia. Kitabu kimoja cha marejeo husema kwamba kwa kuwa alikuwa akitumia mkono wa kushoto, “majeshi yake yalilazimika kupitia upande wa kulia ili mkono aliotumia kubeba upanga uwe kati yake na adui zake.”
Huko Ulaya, watu katika nchi zilizompinga Napoléon waliendelea kutumia upande wa kushoto. Mapema katika karne ya 20 watu huko Urusi na Ureno walianza kuendesha magari kwenye upande wa kulia. Mwishoni mwa miaka ya 1930, wakati wa utawala wa Nazi, Ujerumani ilimiliki nchi za Austria na Chekoslovakia nayo magari yalianza kuendeshewa upande wa kulia katika nchi hizo, na baada ya muda magari huko Hungary yakaanza kuendeshwa pia upande wa kulia. Leo, huko Ulaya, magari huendeshewa upande wa kushoto katika nchi nne tu, yaani, Uingereza, Ireland, Saiprasi, na Malta. Inashangaza kwamba, ingawa Japani haikuwa koloni ya Uingereza, watu katika nchi hiyo huendesha magari kwenye upande wa kushoto.
Mashua, Ndege, Magari ya Moshi, na Watu Wanaotembea kwa Miguu
Vipi mashua na ndege? Vyombo vingi vya usafiri wa majini huendeshewa upande wa kulia. Ndege pia huendeshewa kulia. Vipi magari ya moshi? Katika nchi fulani kifaa cha kutoa ishara ndicho huonyesha upande ambao gari la moshi litapitia iwapo kuna reli mbili. Magari ya moshi yanayopitia juu ya reli zinazotumiwa siku hizi huendeshewa upande wowote, lakini vifaa vya zamani vya kutoa ishara vikitumiwa, gari la moshi linapaswa kupitia upande mmoja tu. Nyakati nyingine upande ambao gari la moshi litapitia ulitegemea nchi ambayo ilibuni na kujenga reli hiyo.
Lakini namna gani watu wanaotembea kwa miguu? Ikiwa hakuna kijia cha miguu, ni salama kutembea ukielekeana na magari yanayokuja, haidhuru magari yanapitia upande gani. Ikiwa magari yanaendeshewa upande wa kulia, mtu anapaswa kupitia upande wa kushoto wa barabara akielekeana na magari yanayokuja. Huku Uingereza, sisi hujitahidi kutembea upande wa kulia kwani magari huendeshewa upande wa kushoto. Lakini namna gani rafiki yangu Mmarekani? Yeye hutembea upande wa kushoto!